Katika kumuenzi Mwl. Nyerere: Tunaendelea.... kwa kurudi nyuma!

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
705
Tunaendelea…. kwa kurudi nyuma!


NDUGU WATANZANIA, ni jambo ambalo limenishangaza, limenistaajabisha na kunisikitisha, kwamba, baada ya miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, badala ya kusonga mbele na kumuenzi kwa vitendo, bado tunaomboleza.
Katika maisha yake – nasisitiza MAISHA YAKE – Mwalimu alikuwa mtu mwadilifu, aliyependa usawa, aliyepinga ubaguzi, ulaji rushwa, ubinafsi, upendeleo, na kila aina ya ufisadi ambao sasa unatukuzwa na kugeuzwa kuwa “msahafu” maalum wa Kitaifa!
Juzi, Jumatano, 14 Oktoba 2009, Watanzania walipumzika nyumbani kwao, wengine walizuru sehemu mbali mbali, baadhi walikuwa Butiama, nyumbani kwa Mwalimu, wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka kumi ya KIFO cha Mwalimu! Walimkumbuka Mwalimu na yale yote aliyoyafanya wakati wa uhai wake – jambo zuri sana – lakini pia, walisisitiza kwamba hii ilikuwa kumbukumbu ya KIFO cha Mwalimu!
Najiuliza. Utamkumbukaje mtu muhimu kama Mwalimu, kwa yale aliyoyatenda wakati wa MAISHA yake, kwa KIFO chake? Hata kama kuna ulazima wa kumkumbuka, basi, tarehe ile ile ambayo alituaga, tuitumia kwa kukumbuka MAISHA yake, si KIFO chake! Badala ya kusema tunaadhimisha kumbukumbu ya KIFO cha Mwalimu, tuseme, tunaadhimisha kumbukumbu ya MAISHA ya Mwalimu.
Kwa mtazamo wangu, kumbukumbu ya kifo, kwa kweli si jambo zuri hata kidogo. Si jambo chanya, ni jambo hasi. Waislam huwa tunasoma Hitma, lakini si sawa na kumbukumbu, bali ni kuwaombea dua waliotangulia mbele ya haki, Mola awarehemu, awaepushe na adhabu, awalaze pema, awasamehe makosa yao. Unapokuwa unakumbuka kifo cha mtu fulani unakuwa kama hutaki kukubali kwamba, mosi, mtu huyo hayupo duniani, na pili, unakuwa bado unaomboleza, hutaki kumwacha aondoke.
Watanzania wengi bado hawajaamini kwamba Mwalimu hayuko nasi. Hawaamini kwamba – kila wanapomwona akihutubia kwenye picha za kumbukumbu kwenye runinga – hayuko hai. Wanadhani kwamba bado yu nasi.
Tukubali kwamba, mosi, Mwalimu hayuko nasi, na pili, tutamkumbuka tukiyaenzi matendo yake wakati alipokuwa HAI, na si kukumbuka au kuadhimisha KIFO chake! Haya ni makosa!
Ningependa, kuanzia sasa, tuanze kuandika kwenye mabango hayo yetu: Kumbukumbu ya Miaka Kumi na Moja ya Maisha ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nadhani nimeeleweka.
 
Back
Top Bottom