Katiba Ya Tanzania Na Migogoro ya Uongozi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Katiba Ya Tanzania Na Migogoro ya Uongozi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mchambuzi, Jan 13, 2012.

 1. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #1
  Jan 13, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,817
  Likes Received: 1,128
  Trophy Points: 280
  Katiba ya sasa, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejaa mapungufu mengi ambayo, yanapelekea nchi kukosa mwongozo, kila wakati migogoro ya uongozi ndani ya vyama vya siasa, inapojitokeza. Kwa vile tupo katika maandalizi ya kuunda katiba mpya, ni muhimu tukalijadili suala hili. Kwa leo, mjadala utalenga zaidi sakata la kuvuliwa uanachama kwa David Kafulila (NCCR – Mageuzi) na Hamad Rashid (CUF), na pia sakata la kuvuana magamba ndani ya CCM. Ni ndefu kidogo, kwahiyo mniwie radhi.

  Katika taifa, muundo madhubuti wa vyama vya siasa ndio Chapa (TradeMark) ya demokrasia iliyoshamiri. Vyama vya siasa ni moja ya taasisi muhimu katika taifa, za kuimarisha mchakato mzima wa demokrasia, sio tu kwa sababu vyama vinawakilisha sauti na matakwa ya wengi katika chaguzi kuu, lakini pia, vinahamasisha juhudi mbali mbali za kijamii, kupitia mipango na itikadi za vyama, ambazo ni viungo muhimu vya kusisimsha na kuongeza uhai wa demokrasia. Ni dhahiri kwamba vyama vya siasa (duniani kote), vina mapungufu mengi, lakini ukweli unabakia wazi kwamba bila ya vyama vya siasa, wananchi hawana mbadala mwingine wa uhakika kuwakilisha HOFU, MATUMAINI, SHABAHA na KIU zao. Hivyo basi, wanachama wenye nafasi za uongozi/wawakilishi wa wananchi Bungeni, hawana budi kutekeleza wajibu wao kwa kuzingitia Katiba, Kanuni na Taratibu za Chama husika.

  Kuna sababu nyingi kwanini ni muhimu vyama vya siasa kuendeshwa kwa mujibu wa katiba, kanuni, na taratibu, lakini moja ya sababu kubwa ni kwamba, hiyo ni moja ya njia za uhakika za kukipa chama cha siasa, heshima na uhalali mbele ya umma. Ndio maana viongozi wa vyama vya siasa, wakati wote wanatakiwa kuwa na umakini juu ya hili, kwani kinyume cha hayo, ni kukaribisha mifarakano inakayopelekea chama cha siasa, kukosa heshima na uhalali mbele ya umma, na hivyo kupoteza umaarufu katika siasa za ushindani, ndani ya demokrasia ya vyama vingi.

  Je, Katiba ya Tanzania, inatuongozi vipi katika hili?

  Jibu ni kwamba – katiba ya sasa haina mwongozo wa moja kwa moja juu ya suala hili, kwani haitoi maelezo juu ya nini kifanyike iwapo mwanachama wa chama cha siasa 'anafukuzwa' au ‘anaachishwa' uanachama. Badala yake, katiba inatoa mwongozo pale tu mwanachama anapoamua ‘kujiuzulu' kwa hiyari yake mwenyewe au kwa njia nyingine, mbali ya ile ya kufukuzwa au kuachishwa uanachama. Pamoja na ukweli kwamba vyama vya siasa vina uhalali wa kufukuza watu unachamana kwa mujibu wa katiba zao, Katiba ya Tanzania haitoi kinga hiyo kwa vyama vya siasa, sana sana juu ya nini kifuate iwapo mwanachama huyo pia ana nafasi ya ‘ubunge'. Hii inapelekea Katiba ya Tanzania kuwa na migongano na Katiba za vyama vya siasa. Kwa mfano:

  Kwa mujibu wa IBARA YA 71 ya KATIBA YA TANZANIA, mtu atakoma kuwa Mbunge na ataacha kitichake katika Bunge litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo:

  (a) Ikiwa litatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Mbunge lingemfanya asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi au asiweze kuchaguliwa au kuteuliwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii;

  (b) Ikiwa Mbunge huyo atachaguliwa kuwa Rais;

  (c) Ikiwa Mbunge atakosa kuhudhuria vikao vya Mikutano ya Bunge Mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika;

  (d) Ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma;

  (e) Ikiwa Mbunge "ataacha" kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge;

  (f) Iwapo Mbunge anachaguliwa au anateuliwa kuwa Makamu wa Rais;

  (g) Kwa Mbunge ambaye anatakiwa kutoa taarifa rasmi ya mali kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 70, ikiwa atashindwa kutoa hilo tamko rasmi kwa mujibu wa masharti ya hiyo ibara ya 70 katika muda uliowekwa mahususi kwa ajili hiyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, lakini iwapo Mbunge hatakoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa jambo lolote kati ya mambo hayo yaliyotajwa na kama hatajiuzulu au kufariki mapema zaidi, basi Mbunge ataendelea kushika madaraka yake kama Mbunge "mpaka wakati Bunge litakapovunjwa kwa mujibu wa ibara ya 90, bila ya kuathiri haki na stahili zinazotokana na ubunge wake."

  Mapungufu haya katika katiba ya sasa, pia yanatoa mwanya kwa mwanachama yeyote aliyefukuzwa uanachama kuendelea kuwa mwanachama mpaka pale atakapojiunga na chama kingine cha siasa.

  Je, mtu anapotezaje sifa za kuwa mwanachama wa chama cha Siasa?

  Kwa ujumla wake, uanachama wa mtu utakwisha kwa:

  1. Kujiuzulu mwenyewe.
  2. Kuachishwa kwa mujibu wa katiba.
  3. Kufukuzwa kwa mujibu wa katiba.
  4. Kutotimiza masharti ya uanachama.
  5. Kujiunga na chama kingine cha siasa.

  Ni dhahiri kwamba pamoja na vyama vya siasa kuwa na uwezo na uhalali wa kutekeleza maamuzi haya kwa mujibu wa katiba za vyama vyao, Katiba ya sasa ya Tanzania haivipi meno vyama vya siasa kutekeleza majukumu yake haya. Na ni hali hii ndio inayopelekea sakata la David Kafulila na Hamad Rashid, kuendelea, licha ya vyama vyao kutanganza rasmi kuwavua uanachama. Uwezekano mkubwa ni kwamba wataendelea kuwa wabunge mpaka 2015, vinginevyo wao wenyewe waamume ‘kujiuzulu', au kujiunga na vyama vingine, au kutokee sababu zozote nyingine, mbali ya kufukuzwa/kuachishwa uanachama. Ni dhahiri kwamba, wakimua kuendelea na nafasi zao, katiba na kanuni za vyama vyao vitawakosesha faida, fursa, marupurupu na ushirikiano kwa mujibu wa katiba za vyama vyao, lakini kutokana na mapungufu ya Katiba Tanzania, Bunge, Mahakama, na Msajili wa Vyama vya siasa, hawana budi kuendelea kuwapa heshima zao ‘kikatiba', pamoja na ushirikiano, fursa, faida, na marupurupu yote yanayoendana na nafasi ya ‘ubunge'. Hili ni suala ambalo inaonekana, Mbatia, Seif, Mtatiro na wengine bado hawalielewi vizuri.

  Mbali ya sakata la CUF na NCCR, hizi pia ni sababu kubwa kwanini wabunge wa CCM (iwapo watavuliwa magamba), wana uwezo wa kuendelea na nafasi zao za ubunge, hadi pale watakapoamua aidha: Kujizulu kwa hiyari yao; Kujiunga na Vyama vingine vya siasa; Au kupoteza uanachama wa CCM kwa sababu nyingine zozote, nje ya ile ya kufukuzwa/kuachishwa uanachama. Kwa maana nyingine, iwapo wanachama hawa watafukuzwa CCM, watapoteza fursa, faida, marupurupu na ushirikiano kutoka kwa viongozi na wanachama wengine wa CCM, kwa mujibu wa katiba ya CCM, lakini kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kitendo hicho hakina maana kwamba watapoteza ubunge ‘automatically'. Na ni muhimu nisisitize hapa kwamba - ukweli huu hautokani na nguvu zao kisiasa ndani ya CCM, bali ni kutokana na mapungufu tuliyokwisha yaona ndani ya Katiba ya nchi (Tanzania). Ni Mbunge wa Zamani wa Igunga peke yake ambaye katiba inatambua sakata lake, kutokana na kitendo chake cha kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi CCM, huku AKIAMUA kubakia mwanachama, ingawa nia ya CCM ilikuwa ni pamoja na kumfukuza uanachama. Kwa hali ya sasa, Katiba yaTanzania bado inalinda uanachama wake mpaka aamue vinginevyo.

  Tujikite kwenye mjadala zaidi kwa kuangalia katiba za vyama vyetu vya siasa ili tuelewe suala hili kwa mapana zaidi.

  Nitatumia mfano wa katiba ya CCM kwasababu, Vyama vingi vya siasa Tanzania, vimechukua mawazo mengi kutoka kwenye katiba ya CCM, bila ya kuelewa kwamba na wao wanarithi migogoro na migongano na katiba ya Tanzania. Lakini vilevile nitaizungumzia CCM zaidi kwa sababu CCM ndio iliyotufikisha katika hali hii ya uwepo wa migogoro baina ya katiba ya nchi na ile ya vyama vya siasa.

  Katiba ya CCM inatoa masharti ya uanachama, ambayo yakikiukwa, yanapelekea mtu kupoteza uanachama. Lakini kabla hatujaendelea, tujikumbushe mambo makuu matatu kuhusu mfumo wa zamani wa siasa, kabla ya ujio wa vyama vingi na ule wa soko huria. Moja, pamoja na marekebisho kadhaa ndani ya katiba ya sasa ya CCM, katiba hii ni zao la mazingira ya mfumo wa chama kimoja, ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipiga marufuku mfumo wa vyama vingi vya siasa, na pia ilikataza wagombea binafsi. Kwa hiyo, katika kipindi kile, ili mtu aweze kuwa Mbunge, ilikuwa hana budi awe kwanza mwanachama wa chama cha siasa - CCM ikiwa ndio chama pekee miaka ile. Pili, katika kipindi kile, ili mtanzania apate ajira ya aina yoyote katika sekta yoyote ya uchumi/nchi, ilikuwa ni lazima kwanza awe mwanachama wa CCM, na ambae amelipia ada zake zote za uanachama. Na ndio maana ofisi zote za serikali pamoja na taasisi za umma zilijaa matawi ya CCM. Na tatu, Tanzania ilikuwa ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. Ili mtu afanikishe shughuli zake Kama mkulima au mfanyakazi, ilimlazima mtu huyo, si kuwa tu Mwanachama hai (aliyelipia ada zake zote za CCM), bali pia ilimlazimu kuwa mtiifu kwa Katiba ya CCM. Kwa mfano, tofauti na sasa ambapo ukiukwaji masharti ya uanachama ni jambo la kawaida, miaka ile, masharti ya uanachama yalikuwa yanatekelezwa kwa vitendo.

  Yafuatayo ni Masharti ya uanachama ndani ya katiba ya Sasa ya CCM:
  1. Mwanachama lazima awe mtu anayeheshimu watu.
  2. Awe mtu anayefanya juhudi ya kuelewa, kuielezea, kuitetea na kuitekeleza itikadi na siasa ya CCM.
  3. Awe mtu mwenye kuamini kuwa kazi ni kipimo cha utu, na kutekeleza imani hiyo kwa vitendo.
  4. Awe mtu anayependa kushirikiana na wenzake.
  5. Awe mtu ambae siku zote yuko mstari wa mbele katika utekelezaji wa mambo yote ya umma, kulingana na muongozo wa CCM.
  6. Awe ni mfano, wakati wote, wa tabia nzuri kwa vitendo vyake na kauli zake, awe mwaminifu na kutokuwa mlevi na mzururaji.
  7. Awe ama mkulima na mfanyakazi, au mwenye shughuli nyingine yoyote halali ya kujitegemea.
  ​

  Sharti la saba (7) la uanachama, lilifanyiwa marekebisho baada ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa soko huria, ambapo sasa wanachama wanaruhusiwa pia kuwa wafanyabiashara, na wakati mwingine kupewa kipaumbele kuliko wakulima na wafanyakazi.

  Je, Kwa Sasa, Masharti ya Uanachama yanatekelezwa CCM?

  Ni dhahiri kwamba, tofauti na miaka ya nyuma, CCM imeacha kutekeleza kanuni zake, kwani nyingi zimebakia katika hali ya ‘nadharia'. Imekuwa jadi kwa wanachama na viongozi wengi kukiuka masharti ya uanachama, bila ya kuhojiwa au kupewa adhabu yoyote ile. Kwa mfano:

  · Sharti la kwanza la uanachama (rejea juu), huwa linavunjwa mara kwa mara, kwani, tofauti na zamani, leo hii, viongozi wengi hawa heshimiani tena ndani na nje ya vikao vya chama; Tumeona mara kadhaa jinsi gani "MEZA KUU" inavyodhalilishwa.

  · Sharti la pili pia linavunjwa mara kwa mara kwani, tofauti na zamani, hakuna juhudi za dhati miongoni mwa wanachama na viongozi wengi, kuitetea itikadi na siasa za CCM. Kwanza itikadi ya sasa ya CCM, haieleweki kama ni ya siasa ya ujamaa na kujitegemea au ni ya soko huria. Vilevile tunashuhudia mara kwa mara, jinsi gani viongozi wa CCM wanavyotofautiana juu ya siasa ipi ya CCM ndio ya kuitetea (mfano sakata la gamba), lakini vile vile misimamo ipi ya CCM ndiyo ya kuitetea (mfano Magufuli dhidi ya kina Mtemvu, Zungu, Ndugulile, Guninita...)

  · Sharti la tatu kuhusu kazi ni kipimo cha utu, hili halipo tena kwani pesa ndio utu. Vile vile mara nyingi, kazi hupatikana kwa kupitia rushwa au kwa kujuana, sio kwa vigezo na sifa za mtu. Kwa kifupi, utu unaheshimika zaidi, iwapo tu mhusika ana uwezo wa fedha, au ana ukaribu na walio madarakani.

  · Sharti la nne linalohimiza ushirikiano - viongozi wengi ndani ya CCM ya sasa hawatekelezi sharti hili tena, kwani kuanzia kwenye matawi, kata, wilaya, hadi Taifa, CCM kwa inaendeshwa kwa makundi. Hata nyakati muhimu kama za chaguzi kuu, nikiwa mwanachama wa CCM, hivyo kuwa na wajibu wa kushiriki katika kampeni za 2010, wengi wetu tulikumbana na wakati mgumu sana pale ambapo, baadhi ya wanachama wenzetu walipokuwa wanaendesha kampni za Urais, ubunge na Diwani, kwa mitazamo na mbinu tofauti. kama vile CCM imegawanyika katika vyama viwili tofauti.

  · Sharti la tano linalohimiza umuhimu wa viongozi kuwa mstari wa mbele kukitetea chama, leo viongozi wengi hatekelezi kazi zao kwa mujibu wa mwongozo wa CCM, bali kwa maslahi binafsi au ya kundi fulani ndani ya chama. Wengine ni wanafiki. Na mbaya zaidi ni kwamba, kwenye matawi ya CCM ambapo ndiko wanaishi wanachama, viongozi huko wameishiwa ‘agenda', hawana silaha za kupambana na upinzani, kwani CCM haina tena Dira. Wamebakia kuduwaa wanapoona upinzani ukizidi kuimarika katika maeneo yao.

  · Sharti la sita linalohimiza viongozi kuwa kioo cha jamii - tofauti na zamani, viongozi wengi wa CCM ya leo sio mfano wa kuigwa, kwani wanatia aibu mbele ya jamii. Ni mafisadi na ni watu wa madharau na kauli za ovyo ovyo. Pia viongozi wengi wa CCM ni wazururaji kwa maana ya kwamba - ni mara chache sana kukuta viongozi wa CCM wakiwa maofisini. Wengi pia ni walevi, wa vilevi vya aina mbalimbali.

  · Na Sharti la saba kuhusu chama kuwa cha wakulima na wafanyakazi, CCM ya leo sio chama cha wakulima na wafanyakazi tena, kwani kimetekwa na wafanyabiashara.

  Kwanini Naiongelea CCM Zaidi ya Vyama Vingine?

  Ni kwa sababu, CCM ndio imetufikisha katika hali ya leo ambapo viongozi wanakosa maadili, lakini katiba ya nchi inashindwa kuwashughulikia. Isitoshe, Katiba ya sasa ya Tanzania ni zao la CCM, katiba iliyojaa migogoro ya kila aina. Baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia nchini, CCM ilikuwa na muda na nafasi nyingi za kubadilisha Katiba mbovu ya sasa, lakini haikuona umuhimu huo, pengine kwa sababu kwa miaka mingi – ni Katiba ya CCM ndiyo ilikuwa inaendesha nchi, sio Katiba ya Tanzania, kwani mara nyingi viongozi walikuwa wanashughulikiana kwa kuvunja katiba ya CCM, lakini sio kwa kuvunja katiba ya Tanzania.

  Mimi ni mwanachama ‘hai' wa CCM, na hivyo, wakati wote, nalindwa na kauli kuu ndani ya Mwongozo wa CCM (1981) kwamba Kukosolewa na kukosoana ndio silaha ya Mapinduzi. Lakini vile vile, kanuni ya CCM inasema hivi: Nitasema Ukweli Daima, Fitina Kwangu Mwiko.

  Ni CCM pekee ndiyo yenye uwezo wa kurudisha hali kuwa shwari, kwani kama alivyowahi kusema Mwalimu Nyerere – CCM ni chama kikubwa na chenye nguvu, na kikiyumba, lazima nchi itayumba. Ni muhimu kwa CCM kurudisha uhalali wake mbele ya umma, uhalali wa ridhaa ya umma, sio uhalali wa kulazimisha. Ni muhimu CCM ikarudi kuwa Chama cha kuonyesha vyama vingine njia, tofauti na hali ya sasa ambapo vyama vingine ndio vinaionyesha CCM njia. Na njia mojawapo kuu ya kufanikisha ili ni kwa serikali ya CCM kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kwamba katiba mpya ya Tanzania, inapatikana kwa kushirikisha wananchi, na kwa njia ya uwazi (transparency). Vinginevyo CCM itazidi kujichimbia kaburi.

  Enzi za Mwalimu (chini ya mfumo wa Chama Kimoja), kulikuwa na nidhamu ya hali ya juu, na chama kilikuwa na heshima kubwa sana mbele ya umma. Ilikuwa ni kawaida kwa viongozi wa ngazi mbali mbali kuachishwa kazi au uanachama kwa kukiuka maadili na masharti mbalimbali. Kwa mfano, kuna Mkuu wa Mkoa mmoja aliyekuwa mlevi kupindukia, hadi kufikia hali ya kujisaidia kitandani, ambae Mwalimu alimfukuza kazi. Kuna mifano mingine mingi. Ndio maana ilikuwa ni vigumu sana kwa viongozi kukiuka masharti ya uanachama kwani kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kujiandikia leseni ya kifo, kutokana na ukweli kwamba ilikuwa ni vigumu kujikimu nje ya kuwa mfanyakazi na mkulima.

  Nini ilikuwa uhusiano baina ya katiba ya Tanzania na katiba ya CCM?

  Kinadharia, katiba ya Tanzania ilikuwa ndiyo yenye mamlaka makubwa kuliko chombo kingine chochote katika Ardhi ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Lakini kivitendo, hapakuwa na chombo chenye mamlaka ya juu kuliko CCM. Kwa maana nyingine, kivitendo, Katiba ya CCM ilikuwa na mamlaka makubwa Kuliko katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uongozi wa nchi. CCM ilishika hatamu, na ilitawala mihimili yote mikuu. Rais, Jaji Mkuu, Spika, Wakuu wa Vyombo vya ulinzi na usalama, wote walitakiwa kuwa watiifu kwa Katiba ya CCM kwanza, hata ikibidi kuvunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni kutokana na ukweli huu ndio maana ilikuwa ni rahisi kuwavua uanachama viongozi waliokuwa wanakwenda kinyume na kanuni za CCM. Kwa mfano, katika miaka ya 80, Maalim Seif Sheriff Hamad alifukuzwa uanachama wa CCM, hivyo kupoteza nafasi yake ya ubunge na Waziri Kiongozi. Pamoja na yeye, pia Hamad Rashid Mohamed (Mbunge wa sasa wa Wawi), alivuliwa uanachama wa CCM, na hivyo kupoteza nafasi yake ya ubunge, na U-Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia nchini, ndipo Seif na Hamad, kwa pamoja wakaunda chama cha wananchi - CUF.

  Lakini mazingira ya sasa yamebadilika. Mamlaka ya CCM hayapo juu zaidi ya yale ya katiba ya nchi, na ndio maana nchi inapata misukosuko kila mara. Uhalisia wa mambo unakilazimisha CCM kuongoza kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, lakini kwa vile katiba hiyo ina mapungufu mengi, utawala chini ya serikali ya CCM umekuwa wa taabu sana. Ndio maana, tofauti na miaka ya nyuma, ni vigumu kwa CCM leo, kuwafukuza wanachama wake, kama ilivyofanya kwa Seif na Hamad kipindi kile, haswa wale waliopo kwenye nafasi zao za uongozi Ubunge, kwani madhara yake Kikatiba, na hivyo kisiasa, ni makubwa kuliko enzi zile Katiba ya CCM ilipokuwa inaongoza nchi. Kwa nyakazi hizi za sasa, inakuwa rahisi zaidi pale tu mwanachama anapoamua kujiuzulu mwenyewe, kwa mfano ‘Mbunge wa Zamani wa Igunga'. Vinginevyo, uwezo wa kuwafukuza wanachama wenye nafasi za ubunge, haupo kikatiba (ya nchi). Kinachobakia ni kutoleana vitisho, na kuambiana kwenye vikao kwamba kina ‘fulani', hawakubaliki tena/hawana mvuto mbele ya umma, hivyo tuwavue magamba.

  Sote tunakumbuka kwa mfano, Mbunge wa zamani wa Igunga alipojiuzulu, Ofisi ya spika ilitoa tamko kwamba haijapata uthibitisho kwa maandishi kwahivyo itaendelea kumtambua mhusika kama ndiye Mbunge. Ni muhimu tukatambua kwamba ofisi ya Spika haikutoa kauli hii kwa sababu tu Mhusika ni kiongozi mwenye nguvu katika chama, bali ni kwa sababu enzi za CCM kuwa juu ya katiba ya Tanzania, na kuamua kukiuka katiba hiyo kwa jinsi inavyotaka, kama ilivyofanya wakati Seif na Hamad wapo CCM miaka ya 80, imepitwa na wakati. Hivyo suala la kufukuzana ovyo ovyo ni kutafuta mgogoro mkubwa zaidi Kikatiba kwani - kutokana na mapungufu tuliyo kwisha yaona katika Katiba ya sasa ya nchi, mwanachama wa wa chama chochote cha siasa anaweza kufukuzwa uanachama kwa mujibu wa katiba ya chama chake, lakini haina maana kwamba moja moja katiba ya nchi inasema kitendo cha kufukuzwa au kuachishwa kinampotezea mwanachama huyo nafasi ya ubunge, ni halali. Pia katiba ya Tanzania iliyopo, haielezei iwapo mtu anakoma kuwa mwanachama wa chama cha siasa kabla ya kujiunga na chama kingine cha siasa. Kwa maana nyingine, haielezei nini kinatokea in between. Be what it may, haya yote ni matokea ya migongano liyopo sasa baina ya Katiba ya Tanzania na Katiba ya Vyama vyote vya Siasa – CCM, Chadema, NCCR, CUF, TLP, n.k.

  Hitimisho:

  Ni umuhimu kwa viongozi/wanasiasa kuwa watiifu kwa vyama vyao ili kuvijengea heshima na uhalali mbele ya umma, kwani kinyume cha hayo, ni halali kuvuliwa uanachama. Lakini kutokana na migogoro ambayo tumeijadili, ni muhimu sana kwa viongozi wa vyama hivi, kupitia nafasi zao kwenye bunge na kwingineko, kuelekeza jitihada zao kurekebisha mapungufu haya kwenye katiba ya sasa ya nchi, kitu ambacho kitavipa vyama vya siasa meno ya kutekeleza maamuzi yao ya kuwashughulikia kikamilifu, wanachama na viongozi wote wanaokiuka katiba na kanuni za vyama vyao. Vinginevyo, kitendo cha viongozi wa vyama vya siasa kutoshughulikia tatizo hili la Kikatiba, na badala yake kujikita zaidi kushughulikia wanachama hawa, kutazidi kuongeza migongano baina ya Katiba ya nchi na katiba za vyama vyao, huku watanzania wakiendelea kuangalia ‘Sinema' isiyokwisha utamu.

  Ni muhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa (CUF na NCCR) wakubali kwamba, kwa hali ya sasa, hawana la kufanya zaidi ya kukubali kwa shingo upande kwamba, kuwafukuza uanachama Kafulila na Hamad, haina maana kwamba automatically wanapoteza ubunge, kwani Katiba ya nchi haisemi hivyo. Viongozi hawa wataendelea kuwa wabunge mpaka uchaguzi mkuu ujao - 2015, au mpaka pale watakapopoteza nafasi hizo kwa sababu nyingine, nje ya ile ‘kufukuzwa' uanachama. Hili pia liwe angalizo kwa CCM katika sakata la sasa la kuvuana magamba.

  Vinginevyo, chini ya katiba ya sasa ya Tanzania, wananchi tutaendelea kutizama sinema iliyojaa vituko vya watu wazima ya kuvunjiana heshima na kuaibishana mbele ya umma, kwani zao la sinema hii, ni Katiba hiyo hiyo iliyopo, ambayo wote, katika nyakati tofauti, Maalim Seif na James Mbatia, kwa nafasi zao za ubunge huko nyuma, hawakuwa makini kuhoji mapungufu haya, ukitilia maanani kwamba bunge sio tu kwamba ni chombo cha kutunga sheria, lakini pia ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kufanyia marekebisho katiba ya nchi iliyopo (sio kutunga upya). Na mwisho, ni muhimu Julius Mtatiro, Naibu Katiba Mkuu wa CUF bara akaelewa kwamba, kauli yake kwamba Hamad si Mbunge wa CUF, bali wa mahakama, sio sahihi kwani ukweli ni kwamba Hamad bado ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kupitia Chama Cha CUF, kwa mujibu wa Katiba mbovu ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na hii ndio sheria mama, ambayo sheria nyingine zote zinazotumika katika mahakama, huizingatia.
   
 2. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #2
  Jan 13, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,817
  Likes Received: 1,128
  Trophy Points: 280
  Ni bahati iliyoje kwamba muda mfupi baada ya mimi kuweka hii thread, ITV wakarusha kipindi kinachigusia mambo haya haya. Mnyika amejieleza vizuri sana, hongera sana Mh. Mnyika.
   
 3. k

  kicha JF-Expert Member

  #3
  Jan 14, 2012
  Joined: Jul 13, 2011
  Messages: 503
  Likes Received: 531
  Trophy Points: 180
  mimi mara nyingi napenda thread na koment zako ambazo unapenda sana kuuhubiri ukweli, lkn inabidi uwe na free time ya kutosha mana sio siri kaka thread zako zinakuaga ndefu sn
   
 4. SOBY

  SOBY JF-Expert Member

  #4
  Jan 14, 2012
  Joined: Sep 19, 2011
  Messages: 1,265
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Camarada,
  Hakuna aliyejieleza vizuri kwenye huo mjadala. Wote bado wana dhana ya Chama kushika hatamu.
  Kinachonisikitisha ni kuwafukuza uanachama viongozi wa wananchi, ambao wamepewa ridhaa na wananchi kuwawakilisha simply because hawakutii amri ya baraza kuu, au kamati kuu ya chama.
   
 5. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #5
  Jan 14, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,817
  Likes Received: 1,128
  Trophy Points: 280
  Ni kweli, kwani kwa upande mmoja wanahimiza umuhimu wa nguvu ya umma - ambao ndio huwa unazaa viongozi, lakini viongozi hao hao wakiwa na tofauti ndogo tu, wananyukana na kusahau kwamba wote wametokana na umma.
   
 6. Mchambuzi

  Mchambuzi JF-Expert Member

  #6
  Jan 14, 2012
  Joined: Aug 24, 2007
  Messages: 4,817
  Likes Received: 1,128
  Trophy Points: 280
  Asante Mkuu,
  nitajitahidi kuzingatia hilo next time.
   
Loading...