Katiba ya sasa hivi inayoruhusu demokrasia kubakwa, haitufai

Mag3

Platinum Member
May 31, 2008
13,060
22,755
Duh, Katiba inayotoa mwanya kwa viongozi kufanya uhuni kama huu hapa chini haitufai. Hebu shuhudieni wenyewe:
CCM yabaka demokrasia, Mbeya.
Na Felix Mwakyembe, Raia Mwema toleo Na. 165
UCHAGUZI wa kumpata Meya wa Jiji la Mbeya umekamilika kwa Athanas Kapunga wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchaguliwa kwa mara nyingine kuendelea na nafasi huo. Hata hivyo, huu ni uchaguzi ulioweka historia ya aina yake katika siasa za jiji hilo na Taifa kwa ujumla.

Katika uchaguzi huo, Kapunga alipata kura 30 dhidi ya 18 za mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Boyd Mwabulanga huku mshindi wa tatu akiwa George Mwakabaya wa NCCR-Mageuzi.

Katika nafasi ya naibu meya kura ziligawanyika kama ilivyokuwa kwenye umeya kwa Frank Mayemba (CCM) kuongoza akifuatiwa na Albert Kilato wa CHADEMA na Ngao Mwenibanga wa NCCR-Mageuzi.

Uchaguzi huo ulioshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evans Balama, ulitawaliwa na ubabe na ukandamizaji wa demokrasia kwa kiwango kikubwa kwa kulazimisha matokeo yenye kuwafurahisha zaidi wakubwa na kukandamiza fikra huru za baadhi ya madiwani wa CCM.


Ni uchaguzi uliodhihirisha kushamiri kwa unafiki miongoni mwa viongozi wa chama hicho na serikali yake pamoja, na umeongeza mpasuko ndani ya chama hicho unaoendelea kimya kimya badala ya kuimarisha umoja miongoni mwa madiwani wake.


Lakini pia ni uchaguzi ulioweka wazi unafiki ndani ya vyama vya upinzani kwa kutokuwa tayari kushirikiana hata katika masuala ya msingi yenye maslahi kwa umma, na badala yake maslahi binafsi ndiyo yenye kupewa kipaumbele, kwani pamoja na uchache wao, madiwani wa NCCR Mageuzi hawakuwa tayari kushirikiana na wenzao wa CHADEMA pamoja na fununu za wale 10 wa CCM waliohitaji mabadiliko kuwa tayari kuwaunga mkono.


Katika kuhakikisha kinawadhibiti madiwani wake 10 walioaminika kutokubaliana na uteuzi wa Kapunga chama hicho kilitumia vitisho na hadaa ya wazi kwa wananchi wa jiji hilo.


Lakini ni hadaa iliyotumika wakati wa uchaguzi pale katika ukumbi wa Mkapa, Jumamosi ya Desemba 17, mwaka huu, ambapo baadhi ya madiwani hao walionekana kuwa nuksi kwa chama hicho kupiga kura zao chini ya ulinzi wa wanachama wenzao.


CCM ilitumia hadaa ya madai kwamba baadhi ya madiwani wake hao kukabiliwa na tatizo la macho, hivyo walihitaji msaada wakati wa kupiga kura.


Alikuwa Diwani Syzia Mwakatundu aliyeanza kwa kuomba msaada wa kupigiwa kura yake na Mbunge Viti Maalumu (CCM), Mary Mwanjelwa, akafuatia Joyce Bilali aliyepigiwa na diwani mwenzake wa CCM, Godon Malema.


Ni hadaa iliyobainika wazi kuwa ilikuwa hatua ya chama hicho kuhakikisha kuwa hakuna diwani wake anayempigia kura mgombea kutoka CHADEMA, Mwabulanga ambaye taarifa zilikwishakuvuja kwamba angeungwa mkono na madiwani hao 10 kutoka CCM hivyo kujinyakulia kiti cha umeya wa jiji hilo kiulaini.


Upigaji kura siku hiyo ulifanyika kwa diwani mmoja mmoja kuitwa mbele, kwenye meza kuu kisha anapatiwa karatasi ya kupigia kura na kuingia kwenye chumba maalumu kwa ajili ya kupiga kura, na ilipofika zamu ya madiwani hao, kila mmoja alimwita mtu wa kumpigia kwa madai kwamba walikuwa na matatizo ya macho.


Diwani wa Kata ya Sinde (CHADEMA ), Fanuel Kyanula, aliitilia shaka njama hiyo hivyo kuhoji hatua hiyo ya baadhi madiwani kutoka CCM kupigiwa kura.


“Tuna wasiwasi kwamba kuna mchezo wa makusudi umefanywa na hao madiwani waliopigiwa kura kwa sababu fomu za kiapo wamepewa na wakazijaza, mbona hawakuomba kujaziwa na watu wengine,” alihoji Kyanula.


Hata hivyo, hoja ya diwani huyo ilitupiliwa mbali na msimamizi wa uchaguzi huo, Mkurugezi wa Jiji hilo, Juma Iddi aliyesema kuwa utaratibu wa kupigiwa kura upo iwapo mtu anajisikia vibaya kwa hiyo anaweza akamchagua mtu wa kumpigia.

Taarifa zilikwishakuvuja kabla ya kuanza upigaji kura kwa baadhi ya madiwani waliokuwa wakitiliwa shaka kuweka wazi kuwa hawatapiga kura hivyo wangeteua watu wa kuwapigia kwa sababu wenzao wameonyesha kutowaamini wakiwashutumu kuwa wamejiandaa kumpigia mgombea wa CHADEMA.

Tangu kuanza kwa mchakato wa kumtafuta Meya wa Jiji la Mbeya ndani ya CCM, madiwani hao 10 walidaiwa kumpinga Kapunga na inaelezwa kuwa kutoelewana kwao kulianzia katika Baraza la Madiwani lililopita na msimamo wao ulikuwa wazi ukifahamika na takribani kila mtu jijini hapo, wanaelezwa kutokubaliana na utendaji wake, wakimuona kuwa chanzo kikuu cha kudumaa kwa maendelo ya jiji hilo.

Ufa kati ya madiwani hao na Kapunga ulidhihirika katika uchaguzi wa ndani pale ilipodaiwa kuwa kura 10 alizopata Diwani wa Kata ya Isanga Dul Mohamed Issa katika uchaguzi wa ndani zilikuwa ni za hao madiwani 10 na inabainishwa zaidi kwamba mara baada ya uchaguzi huo wa ndani madiwani waliokuwa wakishukiwa kutomhitaji Kapunga waliitwa na uongozi wa CCM Wilaya katika kikao kilichoelezwa kujaa ubabe dhidi ya madiwani hao wakitishiwa kuvuliwa uanachama.


“Zile kura 10 alizopata Dul zilisababisha hali kuwa tete zaidi ndani ya chama, madiwani 10 walioshukiwa kumkataa Kapunga waliitwa na viongozi, walitishiwa kunyang’anywa uanachama endapo kura hizo 10 zitaenda kwa mgombea wa CHADEMA, ” anaeleza mtoa habari wetu aliyeomba asitajwe.

Hofu ya CCM ilikuwa halali kabisa kutokana na karata zilivyojichanga, kwani hao madiwani 10 waliompinga Kapunga ndio walikuwa na turufu ya ushindi kwa wagombea wa CCM na CHADEMA kwamba upande ambao wangepeleka kura zao ndio ulioibuka mshindi.

Katika Baraza la Madiwani wa Jiji hilo, CCM ilikuwa na kura 30, CHADEMA 18 na NCCR-Mageuzi tatu, hivyo iwapo zile 10 zingehamia CHADEMA ni wazi Mwabulanga angeibuka mshindi kwa kura 28 huku Kapunga akibakiwa na 20. CCM wakifahamu fika ufa uliokuwapo walielewa uwezekano ulikuwa mkubwa kura 10 kuwaponyoka.

Akionyesha chuki dhidi ya wakosoaji wake, mara baada ya kuteuliwa na chama chake Kapunga alimshambulia kwa maneno mwandishi mmoja wa habari akidai kuwa kwamba amekuwa akiwagawa madiwani kutokana na habari anazoandika.

Hatua ya Meya huyo ilisababisha viongozi wa CCM Wilaya ya Mbeya kumwita mwandishi huyo kisha pamoja na Kapunga mwenyewe, walimwomba msamaha kwa niaba ya chama, huku Kapunga akisema kwamba mashambulizi yake yalisukumwa na hasira.

Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Mbeya uliibua swali la msingi kuhusu nafasi za viongozi mbalimbali wa serikali nchini, hii ni kutokana na hatua ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, Iddi kukiri wazi kuhusu uchafu wa jiji hilo alioukuta, barabara mbovu na jiji kukosa taa za barabarani lakini wakati huo huo akibariki hadaa ya madiwani wa CCM waliodhibitiana hadi kwenye sanduku la kura mradi tu mgombea wao apite hata kama hawamkubali.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa uchaguzi, Mkurugenzi huyo alisema ya kuwa Mbeya ni jiji chafu lakini wamejipanga kukabiliana na tatizo hilo, kwamba tayari wamenunua magari sita ya takataka, na kisha akazungumzia kuhusu taa za barabarani akisema: “Hili ni jiji pekee la ajabu lisilokuwa na taa za barabarani.”

Uchaguzi umekwisha, wananchi wanachosubiri ni mabadiliko, ni kuliona jiji hilo likibadilika na kupata sura ya kweli ya kuitwa jiji, linaingia katika kipindi ambacho umma hauhitaji unafiki wa madiwani, kuja nje ya vikao vyao wakijifanya wenye uchungu na maendeleo ya jiji hilo na lawama lukuki kwa Meya wao wanayedai kuwa mbabe kisha hao hao wakikutwa wakipongezana kwenye vikao vyao vya siri vya matanuzi.

Ukweli utabaki katika mioyo ya umma, wakiwamo viongozi wa CCM wenyewe, Meya Kapunga na madiwani walio mashabiki wake pamoja na wale 10 waliolazimishwa kutofuata dhamira zao, kwamba wamenajisi demokrasia, na kila siku wataishi wakisutwa na nadhiri zao kwamba walichokifanya si kwa maslahi ya jiji bali maslahi binafsi ya na chama chao.
Watanzania hakika tunachezeshwa mdundiko na genge la wahuni wakijiita viongozi wa serikali. Na hapo thubutu Mbunge wetu alalamike kama bado hajapata mkong'oto kutoka kwa vijibwa vyao vikijiita polisi. Hili halina jina jingine lolote lile, ni laana.
 
Back
Top Bottom