Katiba: Tumeanza Na Mguu Mbaya! ( Makala, RAIA MWEMA)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Na Maggid Mjengwa,


NAUONA mwelekeo mbaya wa upepo wa kisiasa nchini mwetu. Nina shaka kubwa, naamini, tuko wengi wenye shaka na mwelekeo wa nchi yetu tunayoipenda.


Prince Bagenda, Mwakilishi wa CCM kwenye Kongamano la Katiba amekaririwa na gazeti la Mwananchi akitamka; ” Msifikiri kila kitu mnapewa tu, lazima mdai”. (Mwananchi Aprili 3, 2011). Ndio, Prince Bagenda anasema; kuwa hoja ya Katiba haikuwa ya CCM. Kwamba CCM ilikubali kwa kuwa Serikali huongozwa kwa maoni ya wananchi.


Afrika safari ndefu huamuliwa na hatua ya mguu wa kwanza. Ukiianza safari na ’ mguu mbaya’, basi , hiyo haitakuwa safari njema. Ina maana moja kubwa, namna ulivyojipanga na safari yako kuanzia mwanzo. Nilivyofuatilia Kongamano lile la Katiba pale Chuo Kikuu Mlimani, nasikitika kusema, tumeianza safari yetu na mguu mbaya.


Tafsiri yangu juu ya alichokitamka Bagenda ni hii; Katiba ni suala la ’ Sisi na Wao’. Ni mapambano. Hapa kuna tatizo kubwa. Maana, kuna hali ya kutafuta mshindi na mshindwa. Ndio, unatafutwa ushindi na ufahari, le prestige, kama wasemavyo Wafaransa. Ninachokiona, kama tutachagua njia ya kushindana katika kuifanyia marekebisho katiba yetu, basi, hakutakuwa na mshindi. Sote tutashindwa.


Hakika, pale Chuo Kikuu Cha Mlimani ndio tulianza rasmi safari hii ya mchakato wa Katiba kwa wadau kuutolea maoni Muswaada wa Katiba ulio Bungeni sasa. Nionavyo, kama Serikali yetu ni sikivu kweli, na imefuatilia kile kilichoongelewa pale Chuo Kikuu Mlimani, basi, haina kingine, bali kuahirisha safari hii.


Serikali irudi na kutafakari kwa kina. Ndio, safari hii ya kuitafuta Katiba yetu ipangwe upya kwa kuwashirikisha wadau muhimu katika nchi . Na wadau hao tunao. Nayasema haya kama Mtanzania ninayeiangalia na kuitafakari nchi yetu na bendera ya taifa letu . Si chama cha siasa wala bendera yake.


Katika dunia hii, chama na bendera yake huja na kupotea. Nchi na wananchi hubaki pale pale. Si kuna Msajili wa vyama, na anaweza kukifuta chama? Kikapotea chama na wanachama wake. Lakini, duniani hakuna Msajili wa Nchi wala wanachama wake. Ukizaliwa kwenye nchi tayari umeshapata usajili wa kudumu kama mwananchi. Ndio maana, katika nchi za wenzetu, hata raia wao akijiandikisha uraia wa nchi nyingine, bado nchi aliyozaliwa haiwezi kuufuta uraia wa nchi yake aliyozaliwa. Siku yeyote anaweza kurudi nyumbani alikozaliwa na kukaribishwa, awe na hati ya kusafiria ya nchi yake au ameipoteza.


Katika hili la mchakato wa Katiba hii ni rai yangu; ” Tutangulize Maslahi Ya Taifa.” Mifano mingine ni hai na tunaishi nayo. Si tunayaona yanayotokea Ivory Coast? Ni matokeo ya wanasiasa kutotanguliza maslahi ya taifa. Na tumeyaona Misri, Tunisia na kwingineko. Ivory Coast watu wanapoteza uhai kutokana na utata wa matokeo ya Uchaguzi. Chanzo hasa ni mapungufu ya Katiba ya nchi hiyo. Na tuliyaona hayo kwa jirani zetu wa Kenya. Sababu hasa ni wanasiasa wetu kutanguliza maslahi binafsi, ya vyama na makundi yao. Wanasiasa wetu si wepesi wa kujifunza. Ni jukumu letu kuweka shinikizo. Tuweke wazi tunayoyataka kwa nchi yetu. Tusikubali kupitishwa kwenye njia yenye maafa na kubaki kimya. Tuanze kupiga kelele, sasa.


Ni vema na ni busara, kwa kazi ya kuandaa Katiba ya nchi ikaridhiwa na wadau muhimu katika nchi. Inahusu imani. Kukosekana kwa imani kwa maana ya wadau wa Katiba wasipokuwa na imani na dhamira za walioandaa Katiba, basi, hicho huwa ni chanzo cha kinyongo, chuki na machafuko katika nchi.


Haiyumkini mechi ya kandanda ikawa na matokeo ya haki pale timu moja inapojibebesha jukumu la kuamua uwanja, mwamuzi na taratibu za mchezo. Mwamuzi wa kandanda anaweza kuwa chanzo cha wachezaji kupigana uwanjani na hata mashabiki kupigana pia. Mara nyingi chanzo ni upande mmoja kukosa imani na mwamuzi. Kinyume chake, timu zote mbili zikiwa na imani na mwamuzi, basi, mara nyingi mechi humalizika kwa hata aliyeshindwa kutangulia kumpa mkono mshindi na mwamuzi pia. Katiba, mbali ya mambo mengine, iwe pia msingi wa chaguzi za kiungwana ili, kama taifa, tuepukane na yaliyotokea Kenya na yanayotokea Ivory Coast na kwingineko.


Tumedhamiria kuifanyia marekebisho makubwa Katiba yetu. Tufanye hivyo tukiwa na dhamira njema na mapenzi kwa nchi yetu. Nimepata kuandika, kuwa katika hili la Katiba tujiulize; Je, Katiba yetu ya sasa, na kwa wakati uliopo, inakidhi matakwa ya shabaha na malengo yetu kama taifa? Jibu langu ni HAPANA.


Na katika hili hatuna sababu za kugombania fito ilihali nyumba tunayojenga ni moja na ni yetu sote. Ieleweke, kuwa huko nyuma, madai ya Watanzania kupata Katiba mpya yamekuwa ni madai ya haki, muhimu na ya kihistoria. Tumewasikia hata wanaojidanganya, wakiandika, kuwa madai hayo yalitokana na ‘ Njama za Mabeberu!’. Hizi ni propaganda za miaka ya 70, zimepitwa na wakati.


Ni busara kutambua, kuwa wakati umebadilika. Mtanzania wa mwaka 1977 si Mtanzania wa mwaka 2011. Hoja hii ya Katiba si kama nzi anayetua na kuruka. Hoja ya Katiba kwa sasa inaongozwa na kundi kubwa la vijana wanaotaka mabadiliko. Hawa si nzi wanaotua na kuruka, ni siafu wanaokuja kwa kuongezeka idadi yao.


Na harakati za Watanzania kutaka marekebisho ya Katiba zina muda mref. Hizi si harakati mpya. Si harakati za chama au kikundi kidogo cha ’wapinzani’ wasioitakia mema nchi hii. Siku zote, yamekuwa ni madai ya msingi ya Watanzania, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini, rangi na makabila.


Kama ni shauri mahakamani, basi, lilishafunguliwa zamani. Kinachofanyika sasa ni mwendelezo wa shauri. Si wengi, miongoni mwa vijana wa sasa, wenye kumbukumbu ya ukweli huu. Kuwa tayari mwaka 1991 vuguvugu la kudai vyama vingi na Katiba mpya lilishaanza. Wakati huo madai makubwa yalikuwa mawili; vyama vingi na Marekebisho ya Katiba. Kuna mnaokumbuka ’ KAMAKA’- Kamati ya Marekebisho ya Katiba iliyoundwa na wanaharakati. Ikumbukwe, kuwa hayo yalikuwa ni madai ya Watanzania ndani ya mfumo wa chama kimoja.


Marehemu Chifu Abdalah Fundikira aliongoza Kamati iliyoundwa, si na Serikali, bali wanaharakati, kuratibu mchakato wa kudai vyama vingi na Katiba mpya.


Hata wakati huo, Mzee Mwinyi, kama Rais, aliweka ‘ mkwara’, kuwa madai hayo yasiendeshwe na watu au makundi ya watu bila kibali cha Serikali. Presha ya madai ilipoongezeka, tunakumbuka, kuwa Mzee Mwinyi aliweza kusoma alama za nyakati. Aliongea pale Chuo Kikuu Mlimani na kuweka bayana dhamira ya Serikali ya kuunda ‘ Tume ya Nyalali’ . Tume hiyo ilizunguka nchi nzima kuwauliza Watanzania kama wanataka kuendelea na Chama kimoja au Vyama vingi.


Itakumbukwa, Chifu Fundikira alipata kutamka; kuwa huko ni kupoteza muda na fedha za wananchi. Itakumbukwa pia, Mabere Marando alikuwa Katibu wa Kamati ile ya wanaharakati ya kuratibu mchakato wa madai ya kuwepo na vyama vingi na marekebisho ya Katiba. Marando alipata kutamka na kunukuliwa na Daily News, April, 12, 1991; “ We have a bad political system because our Constitution embraces political discrimination. What we want is that all of us should shout out that our Constitution is bad.” ( Mabere Marando, Daily News, April 12, 1991)


Tafsiri; “ Tuna mfumo mbaya wa kisiasa kwa sababu Katiba yetu ina ubaguzi wa kisiasa. Tunachotaka, ni sote, tupige kelele, kwamba katiba yetu ni mbaya.”)


Marando aliyasema hayo katika Semina ya kwanza ya Kamati ya kuratibu mchakato wa madai ya vyama vingi na Katiba mpya iliyoongozwa na Chifu Fundikira. Semina hiyo iliudhuriwa na watu wapatao 800 kwa mujibu wa taarifa ya Daily News la April 12, 1991.


Na akina Chifu Fundikira waliandamwa sana na Serikali na Chama Tawala. Kwa mujibu wa Daily News la April 26, 1991, Mbunge wa Shinyanga, Ndugu Paulo Makolo alimshambulia Fundikira kwa kusema kuwa , katika hilo la kuwa na vyama vingi na katiba mpya , Chifu Fundikira hakuwakilisha mawazo ya Wasukuma na Wanyamwezi wenzake; “ This is not a Wanyamwezi and Wasukuma movement. It is the selfish interests of Fundikira and his ten colleagues. Our people are not after parties. They want food, water, education and health care.” ( Paulo Makolo, MP, Shinyanga, Daily News, April 26, 1991).


Mwenyezi Mungu umrehemu Chifu Abdalah Fundikira. Nahitimisha.

MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo




 
Nadhani ni wakati wa kujipanga kuangalia muundo wa tume ya kutunga katiba na vile vile wengine waende mbali na kuangalia nini kiko dhahifu katika katiba ya sasa na kinatakiwa kubadilishwa .Nadhani Tanzania tunatakiwa tuwe mfano wa mabadiliko ya katiba kwa amani na bila za zengwe la aina yeyote ile. Daima tungependa tume itayoundwa ichukue mawazo ya wananchi na si waandike fikra za wanatume

Mungu ibariki Tanzania
 
je, wanachama wa kawaida wa CCM nao hawataki mabadiliko ya katiba kama wanachama wenzao wenye hamu na ndoto za kushikilia madaraka? maana sioni kama kuna juhudi za wazi kutoka kwa wanachama wa CCM katika kuhakikisha kuwa viongozi wao wanafanya maamuzi kwa maslahi ya taifa zima badala ya chama. wapo wapi wana-CCM?
 
Back
Top Bottom