Katiba Mpya ni msingi wa maendeleo ya jamii tukiipata tumepata mkombozi

Jec 2411

New Member
Aug 3, 2021
3
45

Na Chu Joe

Leo nataka tuzungumze kuhusu umuhimu wa katiba mpya lakini kabla ya kuelezea kuzungumzia hilo ngoja nikueleze maana ya katiba ambayo ni mkusanyiko wa sheria mama inayoainisha misingi mikuu ya kisiasa na kuonyesha madaraka na majukumu ya serikali.

Baada ya kipindi kirefu kupita tukishuhudia vyama vya siasa vya upinzani kikiwemo CHADEMA pamoja na baadhi ya wananchi wakidai katiba mpya leo nimeona niweke hapa umuhimu na faida za katiba mpya kama itapatikana.

Uwajibikaji kwa viongozi, jambo la kwanza la muhimu ambalo tutanufaika nalo ikiwa tutaipata katiba mpya ni viongozi kuwajibika pale ambapo wanakuwa wameenda kinyume na taratibu kwasababu itatungwa sheria itayowabana kwa manufaa ya wananchi kwa ujumla, kwa mfano viongozi waliokwapua pesa za Escrow hawakuwajibishwa kwasababu hakuna kifungu kinachotaka wawajibishwe kwahiyo tukipata katiba mpya tutakuwa tumepata mkombozi.

Huduma bora za kijamii, kwasasa wananchi wengi hasa wa hali ya chini wanashindwa kupata elimu bora, huduma za afya, na maji ya kutosha, na hiyo inatokana na kukosekana kwa sheria rafiki yenye misingi ya kuleta haki na usawa kwa jamii nzima, kwahiyo kama tukipata katiba mpya itakayowalazimisha viongozi kujenga shule, vituo vya afya, na kuanzisha miradi ya maji itasaidia kuondokana na tatizo la ukosefu wa huduma bora za kijamii pamoja na kupunguza gharama za huduma hizo ili kila mmoja aweze kumudu.

Uhuru wa vyombo vya habari, kwa muda mrefu sasa waandishi wa habari na wadau wa sekta hiyo wamekuwa wakipigania uhuru wa vyombo hivyo, licha ya serikali kusema upo lakini ukilitazama hilo kwa undani utagundua kuwa hakuna uhuru kamili, kwasababu redio na magazeti ambayo yamekuwa yakiikosoa serikali yamekuwa yakifungiwa mfano radio five ya Arusha na gazeti la Mwanahalisi, kwahiyo ili hilo liweze kutimia ni lazima ipatikane katiba mpya itayokuwa na sheria ya kuvilinda vyombo vya habari visifungiwe hata vikitangaza au kuandika maovu yanayofanywa na serikali.

Uhuru wa mihimili ya serikali, wengi wetu tunafahamu kwamba serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inaendeshwa na mihimili mitatu ambayo ni bunge chini ya spika wa bunge, mahakama chini ya jaji mkuu, na serikali kuu chini ya rais, lakini licha ya uwepo wa mihimili hii mitatu bado kumekuwa na muingiliano wa majukumu baina ya muhimili mmoja na mwingine hali inayosababisha kazi kutofanyika kama inavyotakiwa, kwa mfano rais anauwezo wa kumuamrisha spika wa bunge kufanya jambo fulani na spika akalifanya kitu ambacho ni kinyume na sheria kwahiyo ili hilo lisijitokeze tena ni lazima iwepo sheria inayombana rais au kiongozi yeyote kuingilia majukumu ya muhimili mwingine wa serikali.

Demokrasia makini, kwasasa tunaambiwa kuwa nchi yetu ni ya kidemokrasia na lakini ukilitazama hilo na hali ambayo tunaipitia utagundua kuwa bado Tanzania haina demokrasia makini kwasababu watu tofauti wamekuwa wakifunguliwa mashitaka na kupewa kesi za uongo kisa wanausema vibaya uongozi uliopo madarakani kwa mfano Mdude Nyagali aliyepewa kesi ya kusafirisha madawa ya kulevya wakati hajawahi kufanya hivyo na kilichosababisha hayo kumtokea ni kuikosoa serikali pale inapoenda kinyume kwahiyo ili haya yasitokee ni lazima tuipate katiba mpya itakayobeba maana halisi ya demokrasia.

Hayo ni kwa uchache tu kati ya mengi ambayo jamii itanufaika nayo ikiwa tutaipata katiba mpya ambayo itazingatia utu, haki, utawala bora, na maendeleo ya jamii kiujumla kwahiyo tuendelee kupaza sauti zetu ili tuweze kuipata katiba bora itayosaidia kuijenga Tanzania imara.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom