Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi

ACT Wazalendo

Verified Member
May 5, 2014
490
1,000
UMUHIMU NA ULAZIMA WA KUWA NA TUME HURU ZA UCHAGUZI, MAPITIO YA SHERIA ZA UCHAGUZI NA KATIBA MPYA YA JMT;

UCHAMBUZI (CASE STUDY) KWA MUKHTASARI;

IDARA imekusanya taarifa za kutosha na kufanya uchambuzi wa matukio 9 Makubwa (Case Study) ya uvunjifu na ukiukwaji wa Haki za Binaadamu yaliyofanywa dhidi ya Viongozi Wakuu wa Chama, Viongozi wa ngazi za chini, Wagombea na wanachama wengine;


1. TUKIO LA MAUAJI, KUKAMATWA KWA WANACHAMA NA KUFUNGULIWA KESI ZA UHARIBIFU WA MALI NA UHUJUMU UCHUMI JIMBO LA LIWALE, MKOANI LINDI;

Pamoja na hujuma mbalimbali zilizojitokeza wakati wa uchukuaji wa fomu mwezi Agosti na baadae kampeni za uchaguzi mkuu Agosti-Oktoba, 2020 wananchi wa Jimbo la Liwale walijiandaa vyema kuingia katika uchaguzi mkuu Tarehe 28/10/2020. Kutokana na hujuma zilizojitokeza siku ya Uchaguzi na kupora ushindi waziwazi usiku wa siku hiyo zilianza vurugu zilizoambatana na kubomolewa kwa nyumba mbalimbali na baadhi yake kuchomwa moto, magari binafsi na ya serikali yalichomwa moto. Katika kadhia hiyo uporaji na uharibifu wa mali ulitokea bila kujali itikadi za kisiasa za wahusika.

Kwa kiasi kikubwa vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa CUF, CHADEMA na Polisi. Siku iliyofuata Tarehe 29/10/2020 kamata kamata ilianza kwa Jeshi la Polisi kukamata watu kwa maelekezo ya wana-CCM. Wananchi wengi walikamatwa na kufikishwa kituoni polisi Liwale, takribani wananchi 36 walikamatwa na baadhi yao waliachiwa na kutakiwa kuripoti kituoni Polisi Liwale kila wiki. WanaACT wawili (2) na wanachama wa CUF na CHADEMA 12 walifkishwa mahakamani Lindi na baadae Mahakama Kuu Mtwara walipokata rufaa ya kuomba kupatiwa dhamana. Watuhumiwa wote wanashtakiwa kwa kosa la Uhujumu Uchumi. Shtaka ambalo halina dhamana, na mpaka sasa wapo mahabusu gerezani Lindi. Mahakama ya Mkoa/wilaya Lindi haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kisheria. Huenda ikasubiriwa kupangwa ‘session’ ya majaji kwenda kusikiliza shauri hilo pale ushahidi utakapokamilika.

Wana-ACT ni Ndugu Mohamed Nganogeta (Katibu wa Ngome ya Vijana Jimbo la Liwale) na Ndugu Mikidadi Abdallah Mchiriri (aliyekuwa Mgombea wa Udiwani Kata ya Likongowere) Rejea ripoti ya kesi namba 6/2020 hapa chini. Mwanachama wa ACT-Wazalendo Ndugu Kudra Ally Bilinji (Mjumbe wa Kamati ya Uongozi tawi la Likongowere) nyumba yake ilichomwa moto na kutokana na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa wana-CCM na Jeshi la Polisi alilazimika kukimbia na kutafuta hifadhi nje ya Liwale. Kutokana na hofu ya kukamatwa wananchi wengi walikimbia majumba yao na kuishi maporini na mpaka sasa hali hiyo inaendelea kwa baadhi ya watu.

KIFO CHA MTOTO OMARY ABBAS LIPONDA;

Kutokana na Wananchi kukimbilia kujificha maporini kwa kuhofia usalama kwa mateso na vipigo toka Jeshi la Polisi Omary Abbas Liponda alikufa akiwa porini kutokana na kugongwa na nyoka wakati akiwa amejificha na wazazi wake.

MAUAJI YA NDUGU AZIZA CHANDE KIBOU YALIYOFANYIKA TAREHE 19/12/2020;

Katika muendelezo wa madai ya kuendelea kuwatafuta watu wanaodaiwa kufanya vurugu Tarehe 28/10/2020 mara baada ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi lilivamia kijiji cha Kibutuka Kata ya Kibutuka usiku wa Tarehe 19/12/2020 wakiwa katika gari pick-up Toyota Land-cruser. Walifanya uvamizi katika nyumba ya Ndugu Mawazo Magumba kwa kuvunja mlango kwa nia ya kumkamata, kabla ya Ndugu Mawazo Magumba kutoka chumbani mkewe Ndugu Aziza Chande alitoka chumbani kuja kuangalia nani anagonga mlangoni na kuna nini, ndipo Polisi akafyatua risasi iliyompiga kifuani upande wa ziwa la kushoto na kutokea upande wa pili mgongoni na akaanguka chini akiwa nusu ya mwili wake umeangukia chumbani na sehemu ipo sebuleni.

Baadae wakamkama Ndugu Mawazo na kuanza kumpiga na kumuumiza vibaya sana. Ndani ya nyumba hiyo walikuwepo mume na mke na watoto wao wawili wenye umri wa miaka 7 na mwingine mwaka mmoja. Mtoto huyo na mdogo wake walifanikiwa kutoroka eneo la tukio na kukimbilia kwa bibi yao na kutoa taarifa kuwa mama yao ameanguka amezirai amepigwa na Polisi. Baada ya tukio hilo Polisi walikwenda nyumbani kwa Nassoro Pingili na kisha wakaelekea Liwale Mjini wakiwa na watuhumiwa hao na mwili wa marehemu Aziza. Operesheni hiyo ilikuwa ikiongozwa na muelekezaji wao kada wa CCM Ndugu Ally Kilete mkaazi wa kijiji hicho cha Kibutuka.

Baada ya tukio hilo baba wa Marehemu Aziza Ndugu Yassin Kijumba akifuatana na ndugu wa marehemu aitwae Furaha Yassin Kijumba walianza kufuatilia kujua ndugu zao wamepelekwa wapi na walipofika Polisi walifanikiwa kuupata mwili wa marehemu Tarehe 20/12/2020 saa 5 asubuhi na kwenda kuuzika siku hiyo hiyo saa 9 alasiri. Kisha walirejea Polisi kwa ajili ya kujua kuhusu malezi ya watoto wa marehemu kutokana na mauaji hayo yaliyosababishwa na Jeshi la Polisi na huku Baba yao wakiwa wanamshikilia wao (Polisi). Baada ya kuzungurushwa kwa takribani siku 4 Jeshi la Polisi Liwale walidai hawahusiki na walijiondoa katika suala hilo na kusema hawana uwezo wa kuwalea watoto hao wa marehemu. Baba wa watoto hao baadae amefikishwa mahakamani Lindi na kufunguliwa shtaka la “Kuharibu mali” akiwa na wenzake wawili, rejea kesi namba 32/2020 hapa chini.

Katika tukio hilo risasi moja iliokotwa ndani ya nyumba ya marehemu na kukabidhiwa mtendaji wa Kijiji. Kutokana na familia hii kuwa katika hali ya umasikini na wazazi wao ndio haya yaliyotokea wanahitaji msaada wa hali na mali ili wapate matumaini ya maisha ikiwemo msaada wa kisheria kwa baba yao na pili mahitaji muhimu ya kibinaadamu kwa watoto hawa na masomo. Kutokana na matukio haya hali ya kisiasa Liwale imekuwa mbaya sana kwani viongozi wa CUF na CHADEMA wamekimbia makazi yao hawajulikani walipo, viongozi wa ACT Wazalendo wachache wananendelea kuishi kwa hofu na wananchi wamekata tamaa sana kwa dhulma hii iliyofanyika kwa marehemu Aziza na mumewe, pamoja na uharibifu wa mali uliotokea. Wanahitaji kutembelewa na kufarijiwa.

TAARIFA YA RPC LINDI;
Akizungumza mbele ya Vyombo vya habari; Mkuu wa Polisi Mkoa wa Lindi amedai kuwa mauaji ya Aziza Chande yametokea kwa bahati mbaya wakati Jeshi la Polisi likitekeleza majukumu yake. Na polisi walikuwa wakijilinda kutokana na panga aliloshika mumewe Aziza akitaka kuwadhuru maafisa wa Polisi. Taarifa hii si ya kweli na inapingana na ukweli wa tukio hilo tulioueleza hapo juu.

#acthumanrightsviolationreport-2020/2021

Sehemu ya Ripoti ya ACT Wazalendo juu ya Ukiukwaji na Uvunjifu
wa Haki za Binaadamu nchini-2020/2021
 

Trillion

JF-Expert Member
Apr 24, 2018
1,989
2,000
Nitoke vipi na CCM B yangu, Zito nimekuzarau sana kiongozi.. maneno mengi ili upozwe na cheo, kizamani sana.
 

Man Mvua

JF-Expert Member
Apr 12, 2016
1,950
2,000
Unakuta mbunge anajisifia kusema watu wangu. Huku hao watu wakiteseka, fukara. Shule majengo shida, huduma za afya tabu. Mtu mmoja analipwa mamilioni.

Hakuna haki. Wabunge wenyewe majimboni hawaonekani. Wakienda Bungeni maswali ni yale yale toka nazaliwa hakuna linalo badilika. Utasikia korosho, Pamba, ufugaji, madini, elimu. Hivi haya yote hayajapata ufumbuzi toka wakati wa Nyerere hadi Leo! Miaka 60 tunaongelea jambo lile lile!

Ulaya ya miaka ya hamsini na tisini ilikuwa masikini si kama ya Leo. China, Malyasia, India, Korea na nyinginezo walikuwa masikini.
Je sisi watanzania tumelaniwa nini? Nyerere alitupatia viwanda leo vyote hakuna.

Shida ni nini? Nilibahatika kufanya kazi serikalini, nilipo ingia nilishangaa mengi. Hapo nikajua Tanzania kwendelea ni kazi. Tutapiga mark time.

Tunahitaji kubadili mfumo wa kiutumishi. Tunahitaji kubadili matumizi ya fedha na mshahara. Tunahitaji kubadili mfumo wa utekelezaji wa miradi.

Pia kubadili mfumo wa Bunge. Na kuwa na wabunge wachache. Kufuta viti maalum. Na wabunge wawajibishwe mara wanapokuwa si wawajibikaji.

Hivyo tunahitaji muundo mpya wa serikali. Hata baraza la mawaziri hatuhitaji utitiri wa mawaziri.

Kuna mtaalamu wa ujenzi ni Afisa mkubwa walijenga barabara isiyo na kiwango ktk kumhoji akanambia akijenga ya kiwango yeye na familia yake watakula nini?

Anajua hyo isiyo na kiwango baada ya muda itahitaji matengenezo hivyo atapata fedha. Nilichoka!

Afisa mmoja mkubwa anateuliwa na Rais akanambia usipo kula fedha ya serikali wengine wanakula. Usiangalie kuendeleza nchi. Jiendeleze mwenyewe.

Baada ya muda niliona niache kazi ya serikali na kufanya kazi katika mashirika ya kimataifa.

Tuombeni na kudai Katiba mpya. La sivyo hata vyama shindani vikiingia bado ni yale yale.
 

Faana

JF-Expert Member
Dec 12, 2011
17,534
2,000
kabla ya Ndugu Mawazo Magumba kutoka chumbani mkewe Ndugu Aziza Chande alitoka chumbani kuja kuangalia nani anagonga mlangoni na kuna nini, ndipo Polisi akafyatua risasi iliyompiga kifuani upande wa ziwa la kushoto na kutokea upande wa pili mgongoni na akaanguka chini akiwa nusu ya mwili wake umeangukia chumbani na sehemu ipo sebuleni. Baadae wakamkama Ndugu Mawazo na kuanza kumpiga na kumuumiza vibaya sana
Kuna mambo ukisoma huwezi kuamini kama yanatokea kwenye ardhi aliyoiacha mwanamapinduzi Hayati Baba wa Taifa Mwl J K Nyerere
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom