KATIBA MPYA kama inavyotazamwa na CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

KATIBA MPYA kama inavyotazamwa na CCM

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by charityboy, Jan 7, 2011.

 1. c

  charityboy Senior Member

  #1
  Jan 7, 2011
  Joined: Nov 11, 2010
  Messages: 138
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Katiba Mpya

  SOURCE: Website Rasmi ya Chama Cha Mapinduzi - CCM


  BAADA ya malumbano, mijadala, maandamano na kauli za hapa na pale kudai uundwaji wa Katiba Mpya, hatimaye Rais Jakaya Kikwete amesikia na ameunda Tume maalumu ya Katiba.

  Tume hiyo kwa mujibu wa Rais, itaongozwa na mwanasheria aliyebobea na kuwa na wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya jamii za pande zote mbili za Muungano.

  Hayo yamo katika hotuba ya salamu za Rais Kikwete aliyoitoa jana kwa Taifa katika kuaga mwaka 2010 na kukaribisha mwaka mpya wa 2011.

  “Jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaoshirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya yatakayohusu Katiba ya nchi yao,” alisema Rais katika hotuba yake.

  Alisema baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya kikatiba kwa kufanyiwa uamuzi.

  “Baada ya makubaliano kufikiwa, Taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika,” alisema Rais.

  Alieleza matumaini yake kwamba mchakato huo utaendeshwa vizuri, kwa amani na utulivu kama ilivyo sifa ya nchi na mazoea ya kujadiliana bila kugombana, ambapo wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na kwa uvumilivu wa hali ya juu pale watu wanapotofautiana kwa mawazo.

  “Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana.

  Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema.

  “Na inapohusu Katiba ya nchi, itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.

  Nawaomba Watanzania wenzangu wenye maoni yao, wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato huu,” alisema.

  Rais alisema uamuzi huo unatokana na makubaliano yaliyofikiwa kati yake na viongozi wenzake kufanywa, hili la Katiba likiwa ni moja miongoni mwa mambo manne yaliyokubaliwa.

  Aliyataja mengine kuwa ni kuutangaza mwaka 2011 kuwa wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambayo kilele chake kitakuwa Desemba 9, ambapo kutafanyika sherehe kubwa na za aina yake nchi nzima na wananchi kushirikishwa kwa ukamilifu.

  Pili, kufanyika tathmini ya kina ya mafanikio yaliyopatikana nchini, katika juhudi za wananchi kujiletea maendeleo katika miaka hiyo 50.

  “Kila wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi, zifanye tathmini ya eneo lake. Tathmini hizo ziandikwe katika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo,” aliagiza.

  Alisema vitabu na nyaraka hizo vitakuwa kumbukumbu zenye manufaa makubwa kwa watakaokuwapo mwaka 2061 wakati wa kusherehekea miaka 100 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

  Pia ilikubalika yafanyike maonesho maalumu katika Uwanja wa Maonesho wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na mikoani, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara.

  Na lingine ndilo la mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye kuwa na Katiba inayoendana na Taifa lenye umri wa nusu karne.

  “Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo.

  “Tuna nchi moja huru, ya kidemokrasia na inayoendesha mambo yake kwa kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya Dola.

  Nchi yenye amani, utulivu na watu wake ni wamoja, wanaopendana na kushirikiana na maendeleo yanazidi kupatikana,” alisema.

  Hata hivyo, aliwahadharisha Watanzania kuacha kupoteza muda muhimu wa kujiendeleza na badala yake kugeuzwa ‘mbuzi wa kafara’ kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani.

  “Najua wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa ambavyo vimepanga mikakati ya kuendeleza malumbano ya uchaguzi na kutaka Watanzania waishi kama vile nchi ipo kwenye kampeni za uchaguzi.

  “Wamepanga wakati wote kutafuta jambo au hata kuzua jambo, ili kuwachochea wananchi waichukie Serikali.

  Wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara. Kwao huo ndiyo mkakati wa kujijenga kisiasa, ili kujiandalia ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015,” alisema.

  Alikumbusha kuwa uchaguzi ulishaisha Oktoba 31, na malumbano ya kampeni za uchaguzi yalimalizika wakati huo. Sasa ni wakati wa kuendelea kufanya shughuli za kawaida za kujiletea maendeleo.

  “Kuendeleza malumbano na kuendelea kuishi kama vile kampeni za uchaguzi bado zinaendelea si sahihi hata kidogo.

  Kwa jinsi watu hao walivyokuwa wabinafsi na wasivyokuwa na huruma na wenzao, wako tayari kuchochea ghasia bila kujali madhara yatakayowakuta watu watakaoshiriki,” alisema.

  Alisema wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya Dola kuingilia kati ili waiambie Jumuiya ya Kimataifa jinsi Serikali ilivyo katili.

  “Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hawa. “Nawaomba, wakiwafuata wakumbusheni kuwa wao wana fursa nyingi za kusema wayatakayo bungeni na kwingineko, waache kuwatumia kama chambo au wahanga wa maslahi yao,” alisisitiza.

  Akifafanua kuhusu uchaguzi, alisema ulikuwa na ushindani mkali na nguvu ya vyama vya upinzani iliongezeka na kwamba ni jambo jema kwa utawala bora na uwajibikaji nchini.

  “Bila shaka Bunge litachangamka kama tunavyotarajia sote. Nimewakumbusha mawaziri wajibu wao wa kuwa makini na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi bungeni.

  Kwa upande wa Chama tawala, hatuna budi kujipanga na kujijenga upya kwa kuzingatia mazingira mapya ya kisiasa nchini,” alisema.
   
Loading...