Katiba Iruhusu Wagombea Binafsi Kwenye Vyaa Vya Siasa ( Makala, Mwananchi, Jumapili) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Katiba Iruhusu Wagombea Binafsi Kwenye Vyaa Vya Siasa ( Makala, Mwananchi, Jumapili)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Aug 19, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Aug 19, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,057
  Likes Received: 320
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,  Ndugu zangu,


  KATIKA suala la mchakato wa Katiba mpya, nitajadili dhana ya kuwa na wagombea huru katika nafasi za uongozi.

  Mahakama Kuu ilipata kutoa hukumu kuwa wagombea binafsi waliruhusiwe katika chaguzi zetu. Labda hapa kuna haja ya kuchukua tahadhari, kwamba huenda si jambo zuri kwa yeyote yule kugombea bila kuwa na chama nyuma yake.


  Kutoruhusu uwepo wa wagombea binafsi kama ilivyo sasa ni upungufu. Na kuruhusu uwepo wa wagombea binafsi bila hata kuwa na vyama ni upungufu pia. Badala yake, wagombea binafsi waruhusiwe kugombania nafasi za uongozi wakiwa ndani ya vyama.
  Ni wakati sasa wa Katiba yetu mpya nafasi katika chaguzi zetu, kuwepo kwa wagombea binafsi wanaotokana na vyama vya siasa.


  Kwa bahati mbaya , jambo hilo kwa sasa litakutana na vipingamizi vingi kwa vile, ingawa inawezekana, lakini, hakuna dhamira ya kisiasa ya kufanikisha jambo hilo. Na kama jambo kama hilo lingefanyika, basi, Serikali ingekuwa imetengeneza njia ya tatu iliyo salama zaidi na yenye kulinda maslahi ya taifa.


  Kwanini tunafikiri hivi? Wagombea binafsi wanaotokana na vyama wangesaidia kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama (Intra-party democracy). Njia hii itavinusuru pia vyama vya siasa katika hatari ya kusambaratika zaidi. Kimsingi, kwa kuruhusu wagombea binafsi kuwania nafasi za uongozi nje ya vyama kutawafanya wagombea hao wasione umuhimu wa kushiriki katika siasa za vyama.
  Kuna umuhimu pia wa mgombea kuwa na utambulisho wa chama. Mgombea anawayewakilisha wananchi bungeni au kwenye baraza la madiwani anafanya shughuli ya siasa. Hivyo basi, ni vema mtu huyu nyuma yake akawa na chama ambacho itikadi, madhumuni, malengo na sera zake anakubaliana nazo.


  Asipokiona chama chenye itikadi, sera na malengo yanayomridhisha yeye, basi mtu huyu apewe uhuru wa kushirikiana na wenzake wenye mawazo yenye kufanana ili aanzishe chama chake cha siasa.
  Tusikubali kujenga utaratibu utakaoruhusu wagombea binafsi waharibu dhana nzima ya siasa na itikadi za vyama vya siasa. Kama taifa, tumeazimia kujenga na kuimarisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Hata tukiwa na wagombea wengi, basi, watokane na vyama vingi.


  Kuruhusu wagombea binafsi bila sharti la ushiriki wa siasa za vyama sio tu ni kukaribisha vurugu za kisiasa, bali pia tunawaweka wananchi kwa maana ya wapiga kura wetu katika wakati mgumu.
  Badala ya kuangalia mgombea na sera za chama chake, wengi wa wapiga kura watajikita zaidi katika kumwangalia mgombea, umaarufu wake, sura yake, namna anavyosaidia kutoa michango ya hapa na pale na kadhalika.  Umaarufu wa mtu na kwa kusaidiwa na fedha na labda vyombo vya habari unaweza kutangulizwa mbele badala ya kuangalia umahiri wake ikiwemo sera na misingi ya kiitikadi aliyosimamia mgombea husika.
  Utaratibu wa mgombea binafsi ndani ya chama umwezeshe mgombea aliye mwanachama wa chama cha siasa kupewa haki ya kisheria. Haki ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uongozi wa kuchaguliwa na wananchi hata kama hakupitishwa na vikao halali vya chama husika.

  Kwa mfano: mgombea X ni mwanachama wa chama Y. Amechukua fomu ya kugombea ubunge kwa tiketi ya chama chake Y. Lakini chama chake hakikumpitisha kuwania nafasi anayoitaka ya kuwatumikia wananchi. Basi, mgombea X awe na haki ya kikatiba na kisheria ya kuchukua foimu ya kugombea kama mgombea binafsi kwa tiketi ya chama Y .
  Mgombea huyu X akiwa majukwaani aonekane kuwa ni mgombea binafsi lakini ni mfuasi na mwanachama wa chama Y.  Hata akiingia bungeni atatetea sera na itikadi za chama Y. Endapo ikitokea katika kipindi chake cha ubunge mgombea X atadhani ameshindwa kubaki bungeni kutetea sera na itikadi za chama hicho, basi anaweza kufikia uamuzi wa kujivua unachama. Inawezekana pia mgombea X akavuliwa uanachama na chama chake. Basi, mgombea X abaki 
kikatiba na kisheria, kuwa ”Mbunge pori” hadi kipindi cha uwakilishi wake wa wananchi bungeni kitakapofikia ukomo.


  Endapo mgombea X atapenda tena kutetea kiti chake cha ubunge katika uchaguzi utakaofuatia, basi, atalazimika kujiunga na chama kingine cha siasa au kujiundia chama chake cha siasa.
Maana, katika hili la wagombea binafsi tusije tukatoka kwenye dhana nzima ya Chama na umuhimu wake.
  Tukumbuke, mojawapo ya tafsiri ya chama cha siasa ni kama hii ifuatayo; Chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye itikadi, madhumuni, shabaha na malengo yenye kufanana. Ni chama kilichojiwekea kanuni za kufuatwa kwa viongozi na wanachama wake.


  Katika hilo la hapo juu ni vigumu kukawa na chama cha siasa kitakachodumu muda mrefu kikiundwa na watu wenye itikadi tofauti na wasiokubaliana katika madhumuni na malengo ya msingi.
  Kikishindwa kuwa na hivyo muhimu, hakiwezi kuwa na kanuni zitakazofuatwa. Hicho ni chama kwa nadharia, lakini kimatendo, ni mkusanyiko wa vikundi vya watu wenye malengo, 
madhumuni na shabaha tofauti chini ya kivuli cha “chama nadharia”. Nahitimisha. ( MWANANCHI, Leo Jumapili)
  0788 111 768
  Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
Loading...