Kati ya Serikali na Q net nani wa kulaumu

sweettablet

JF-Expert Member
Nov 16, 2014
7,704
2,000
JE KATI YA QNet NA SERIKALI NANI AMEMTAPELI MWANANCHI?

Habari kubwa Tanzania kwenye ulimwengu wa biashara ya mtandao Juma hili ni QNet!

Wengi wanaifananisha QNet na DECI hii ni makosa sana! QNet ni kampuni ya biashara iliyosajiliwa kisheria hapa Tanzania, inalipa kodi na jengo la makao makuu huko Darisalama lilizinduliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya wakati huo Hamisi Kigwangala pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara! DECI haikuwahi kusajiliwa popote na mamlaka za Tanzania.

Je kampuni inayofanya biashara haramu ya upatu haramu iliwezaje kuzinduliwa na Waziri huyu sambamba na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara?

Binafsi nimewahi kuingia kwenye ofisi za QNet pale Mjini Darisalama. Ndani ya afisi hii kuna kila nyaraka na vyeti vinavyohitajika na serikali ili kukidhi matakwa ya kisheria ya kampuni yoyote ile ya biashara. Pia kuna picha mbili za viongozi wa nchi hii ambazo moja ni ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na nyingine ni picha ya Rais aliyepo madarakani John Pombe Magufuli na wamesajiliwa kama MULTI- LEVEL-MARKETING (MLM).

Ukifuatilia nyaraka za kampuni hii hususani za uanachama kuna watumishi wengi sana wa umma pamoja na wastaafu wengi tu walioekeza pesa zao pia wamo wastaafu wa jeshi, polisi, viongozi wastaafu wa serikali wakiwemo miongoni mwa Mawaziri Wakuu wastaafu!

Iko namna hii. Watanzania waliowekeza mitaji yao katika kampuni hii baada ya kuona kuna viashiria vya kutapeliwa pesa zao wakapiga yowe ili atakayesikia yowe awasaidie wasipoteze mamilioni yao ya fedha na mitaji yao!

Well Serikali "sikivu" ikasikia yowe la Wananchi wake "wanyonge" ikamkamata anayelalamikiwa "kutapeli" Wananchi bahati nzuri wakamkuta "tapeli"akiwa akiwa na bilioni za Wananchi mfukoni kwake " alizotapeli" kama ambavyo serikali ya wanyonge inadai wanyonge wamelalamika.

Baada ya Serikali kumtia mbaroni tapeli akiwa na kibunda cha mabilioni ya pesa za Wananchi wanyonge serikali ya wanyonge inawaambia wanyonge kuwa hawana HAKI na hizo pesa kwa kuwa zilipatikana kwa njia ya upatu haramu!

Kwamba yale mabilioni ya Wananchi waliyowekeza QNet ni haramu, na QNet ni haramu na pesa zote zile ni pesa haramu ni pesa chafu sasa inabidi zitaifishwe ziwekwe kwenye akaunti ya aliyesikia yowe la WANYONGE sasa sijui kuwa fedha haramu na chafu kwake anaenda kuihalalisha na kuitakatisha ama namna gani.

Hapa kumbuka siyo Serikali iliyoweza kubaini kuwa QNet ni biashara haramu. Bali wanyonge waliowekeza huko ndio wanadaiwa kwenda kulalamika kuwa wana hofu watatapeliwa wasaidiwe kupata pesa zao, serikali ikasema inawasaidia matokeo yake pesa ilipopatikana serikali ikawachinjia baharini wanyonge kuwa hawana HAKI kwa kuwa pesa zile ni haramu!

Hebu tuiulize serikali maswali:

1. Ni nani aliyewahakikishia wanyonge kuwa QNet ni biashara halali na ni fursa ya kupata utajiri wa chapuchapu?

Bila shaka ni serikali hihii. Ni serikali hihii ambapo Waziri wake mdogo wa Afya Hamisi Kigwangala akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara walienda kuzindua makao makuu ya QNet na kuwataka wanyonge waachane na unyonge wafikiri nje ya box na kuchangamkia fursa hii adhimu ulioletwa na mabeberu kumkomboa Mnyonge!

Hivyo kama biashara hii ni haramu ni serikali ya wanyonge iliyowadanganya wananchi wake kuwa ni biashara halali.

Hivi Mnyonge, kabwela na mlalahoi anahitaji vidhibitisho gani zaidi ili kubaini kitu halali baada ya kumuona Naibu Waziri wa Afya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara wakizindua miradi ya QNet?

Hivi kama Waziri na Katibu Mkuu wanakuja wanazindua kiwanda changu cha kuchakata bangi na gongo kisha Wananchi wanabaini fursa zilizopo wanawekeza mitaji na hisa zao kwenye kiwanda changu kilichozinduliwa na Waziri na kimesajiliwa na kulipa kodi leo unawezaje kutuambia sisi wana hisa kuwa hii ni biashara haramu?

2. Je QNet haijasajiliwa hapa Tanzania?

Bila shaka imesajiliwa na mamlaka husika na imekuwa ikilipa kodi na gharama mbali mbali kwa mujibu wa Sheria za usajili wa makampuni ya kibiashara.

3. Je serikali ya wanyonge imefahamu leo kuwa kuna kampuni inaitwa QNet na inafanya biashara haramu?

Bila shaka ni HAPANA. Kama ni HAPANA kwa nini miaka yote hiyo QNet imeendelea kuachwa itapeli na kufanya biashara haramu?

4. Je serikali ya wanyonge hajawahi kumuona Waziri wake Hamisi Kigwangala akizindua makao makuu ya QNet? Je imewahi kumhoji kwamba kwa nini alizindua jengo lile la kufanya biashara haramu? Je kuna Sheria yoyote ile amechukuliwa?

Maswali ni mengi sana!

Binafsi mimi sio muhanga wa QNet licha ya kuifahamu kuwepo nchini kwa takribani miaka 6 na ushee sasa. Niseme bayana kwamba sijawahi kuitilia shaka QNet kuwa inaweza kuwa ni kampuni ya kitapeli na hadi naandika hapa huenda nikawa wa mwisho kuamini hivyo.

Unaweza ukajiuliza kwa nini sikujiunga nayo ikiwa naifahamu vema. Kilichonifanya nisijiunge hadi leo ni ukosefu wa mtaji wa kuweza kuwekeza huko na niwe mkweli ningekuwa na hiyo fedha ningewekeza! Ndio ningewekeza! Nawezaje kupuuzia fursa ambayo hadi mawaziri wanaonekana kuichangamkia? Ningewezaje kupuuza fursa ambayo hata Mzee wa nje ya box ameichangamkia?

Mimi simlaumu mnyonge yeyote aliyewekeza katika kampuni hii. Kila Mnyonge aliyejiunga na QNet ni mpambanaji anayejitafutia mafanikio kwa faida yake, nduguze na Taifa kwa ujumla. Naamini hakuna Mnyonge aliyejiunga na QNet kwa makusudio ya kupoteza pesa au kutapeliwa sio na QNet wala serikali.

Kinachoniumiza kichwa ni kwamba QNet hapa nchini imekuwepo kwa zaidi ya miaka 6. Je! Serikali ndio imegundua leo kwamba QNet ni biashara haramu ya upatu unaotapeli wanyonge?

Kwa nini QNet inafungiwa 'miaka sita' baadae na mabilioni ya shilingi za walalahoi waliodunduliza humo ili watusue maisha waachane na unyonge zinaambiwa sio za wanyonge tena bali sasa ni za Serikali? Au hiki pia ni chanzo kingine cha mapato ya serikali hii ya wanyonge?

Poleni mliowekeza QNet. Maumivu yenu ni maumivu yetu sote, machozi yenu ni machozi yetu sote, tunaomboleza pamoja nanyi.

Wanyonge wamekuwa ni watu wa kupigwa nje ndani wakilima korosho wanapigwa, wakilima mbaazi wanapigwa, wakinunua nyavu wavue zinachomwa Moto.

Wanyonge wamepigwa sana, hadi Wachungaji nao wameona wakuwapiga ni wanyonge si mnakumbuka mabilioni ya DECI wanyonge si walikufa kwa presha, sukari na mshtuko wa moyo? Wanyonge wakapigwa kwenye RIFARO, wanyonge wakapigwa kwenye D9, wanyonge tukapigwa kwenye Bitclub Advantage leo wanyonge tumepigwa kwenye QNet. Nani ajuaye kesho Mnyonge kwamba hatopigwa kwenye Aim Global n.k.

Juzijuzi tulisikia na kuona hapa Benki kadhaa zikifungwa na kufilisiwa Wananchi waliowekeza na kuhifadhi pesa zao huko sijui kama hadi leo walipata HAKI stahiki zao. Mambo ya ajabu sana haya. Huku kukubali kuendelea tuitwe WANYONGE kutatugharimu sana na bado tunawasifu wanaotutendea haya tukiwaomba watutawale milele! Unyonge wetu umetufanya hadi AKILI na FIKRA zetu zimekuwa za kinyonge na MATOPE!
Mkuu ebu tembelea Qnet - Wikipedia uijue vizuri.
 

mkorinto

JF-Expert Member
Jun 11, 2014
24,581
2,000
serikali haijawahi kukosea,kuchelewa,wala kukawia kuchukua maamuzi.

Qnet ni wahuni na matapeli wanaojua kuishi kijanja.
 

Mr muhuni

JF-Expert Member
May 26, 2014
1,117
2,000
seriously kweli jf inakosa mdau alie nufaika na Qnet wakati ukienda ofisin kwao una kuta picha za watu waliopiga hela nakununua gari za maana mijengo pia

msiniulize nilienda kufanya nini ofisin kwao na ikawaje
ova
 

LESIRIAMU

JF-Expert Member
Feb 12, 2008
7,160
2,000
Kama unailaumu serikali basi na wewe inafaa uwekeze Qnet
Huwa sichezi upatu. Ila kabla ya kiipa taasisi kama hiyo vibali, serikali makini ilitakiwa kujiridhisha. Na sio Dpp kuja na kusema walio wekeza hawastahili kurudishiwa pesa. It does not sound kama serikali walikuwa na uhakika na biashara ya hawa wahuni.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom