Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Wengi wetu tumefungwa sana na jamii kiasi kwamba kuwa sisi siyo jambo rahisi kiasi hicho. Kinachokubaliwa na jamii ndiyo sahihi hata kama kinanuka kiasi gani. Hivyo ndivyo tunavyotakiwa kuwa kwa sababu sisi ni jamii na tunatakiwa kuishi kwa matakwa ya jamii na siyo tutakavyo sisi.
Ukweli tunatakiwa tuwe nao sisi na siyo jamii. Lakini kwa bahati mbaya hatujawahi kuwa sisi, siku zote tumekuwa jamii, hivyo tunasikiliza jamii inasemaje kuhusu sisi na inatutaka tuishi vipi. Tukiwa sisi jamii itaona tumeasi au tumekuwa vichaa.
Jamii haitaki tujitambue (tujue sisi ni nani). tukijitambua tutakoma kuwa jamii na jamii haiko tayari kutupoteza maana tayari tumeshakuwa watumwa wa jamii.
Kama tukiwa sisi jamii haiwezi kututumia itakavyo. Tukifanya jambo zuri tunapendwa na kusifiwa; na tukifanya kinyume na matakwa ya jamii tunachukiwa na kubezwa. Hii hujenga choyo cha kujipenda zaidi ambacho hutaka kushibishwa kila siku.
Mtu anajitahidi kufanya kile ambacho jamii inampangia ili kushibisha choyo alichopewa na jamii husika. Atataka gari na nyumba kwa sababu jamii imemwambia ni vya maana na vinampa thamani siyo kwa sababu yeye anavitaka. Atataka asome sana ajikusanyie digrii nyingi sana, aoe mke mzuri sana, awe tajiri sana, apate umaarufu sana, yote ikiwa ni choyo alichopewa na jamii. Kila siku tunatafuta sisi ni akina nani kupitia kwa watu wengine, kwamba, wakituona, kututambua na kutusifia ndipo tunahisi kuwa sisi.
Jamii inayumba kila siku kuhusu kipi ni kipi na hivyo na sisi tunayumba kila siku kwa sababu hatuishi kama sisi bali tunaishi vile jamii itakavyo. Maamuzi yetu na mitazamo yetu inategemea tu namna itakavyopokelewa na jamii. Na ndio maana unaweza kushangaa mtu anasema, "Hivi nikiolewa na fulani au nikimuoa fulani watu watanionaje?" Yaani si kwamba yeye hampendi huyo anayetaka kumuoa au anayetaka kuolewa naye bali anaogopa namna jamii itakavyomuona na kumhukumu kwa sababu tu huyo anayetaka kumuoa au kuolewa naye amepachikwa sifa mbaya na jamii, na yeye hayuko tayari kwenda kinyume na jamii…. Ajabu eh!
Kumbuka wakati unazaliwa ulishakuwa wewe na uwewe wako bado unao. Lakini kwa sababu umepewa uwewe mwingine na jamii ndiyo maana kuchanganyikiwa na kujuta ni kwingi sana. Ni hadi hapo utakapovua uwewe uliopewa na jamii na kubaki na uwewe uliozaliwa nao (kuwa wewe halisi) , ndipo kuchanganyikiwa na kujuta kutaisha. Inawezekana!!!
Jitambue…………….
@Lara1, King'asti, snowhite, gfsonwin, AshaDii, Fixed Point, miss neddy, miss chagga, Karucee, Chocs, Neylu, Lady doctor, Lisa, Nivea, charminglady, Heaven on Earth, Munkari, MankaM, BADILI TABIA, Kongosho, The Boss, Asprin, Nyani Ngabu, Bujibuji, Nicas Mtei, Mwita Maranya, Kiranga, Zinduna, Ruttashobolwa, Kaizer, Husninyo, MwanajamiiOne, DEMBA, Preta, marejesho, Nyamayao