Kasi ya ongezeko la Saratani za Kirusi cha HPV nchini yashtua

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,117
Kirusi cha HPV (Human Papilloma Virus) kimetajwa kuwa hatari kwa kusababisha saratani za aina mbili zinazokua kwa kasi ikiwemo inayoathiri koo na shingo ya kizazi aina inayoongoza kwa asilimia 36 kati ya saratani zote zinazoshambuliwa nchini.

Wataalamu wamesema asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi hupata maambukizi kwa njia ya ngono huku saratani ya koo ikishika nafasi ya saba na mojawapo ya chanzo kikitajwa kuwa ngono ya kinywa.

Pamoja na visababishi vingine, saratani ya shingo ya kizazi inatokana na aina 40 ya virusi, aina mbili ikiwa ni vinavyosambaa kwa njia ya ngono ikiwemo ‘Squamos cell carcinoma’ kirusi namba 16 na ‘Adenocarcinoma’ namba 18.

Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya AgaKhan ambaye pia ni Meneja mradi mtambuka wa saratani Tanzania (TCCP), Dk Harrison Chuwa alisema saratani ya koo kisababishi kikuu ni kirusi cha HPV namba 9 na 11.

“Saratani ya koo la hewa au koromeo pale juu ambapo sauti ndiyo inatengenezwa inaweza kuanza kwa kutoa uvimbe juu yake, katikati au chini yake na yote hiyo inategemea jinsi gani ya kuitibu.

“Kirusi hiki kinahamishika kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kujamiiana kwa kinywa, mara nyingi kinajificha ama kimejihifadhi kwenye mfumo wa uzazi kwa mwanamke na mwanaume,” alisema.

Dk Chuwa ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya saratani, alisema iwapo mtu atajamiiana na mwenza kwa njia ya kinywa ndipo kirusi hupata nafasi ya kuingia na kushuka kwenye koromeo na kuanza kuleta athari na kwamba mabadiliko huchukua zaidi ya miaka 15 kujitokeza saratani.

Alitoa angalizo kwa wale wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja kwamba wanaathirika zaidi na aina hiyo ya saratani.

“Tunaamini mataifa ya magharibi yanafanya mambo mengi yanayoleta maendeleo lakini si kila kitu ni cha kuiga ni muhimu kuendelea kutunza mila na desturi za kiafrika na naamini zilitulinda na magonjwa mengi,” alisisitiza.

Dk Chuwa alisema mara nyingi saratani za kichwa, kinywa au shingo hujumuishwa zote kwa pamoja, “Kwa hiyo tunajaribu kuzinyumbulisha na kuzitenga ukijumlisha aina zote hizi mbili zinashika namba saba kwa kusababisha saratani.”


Kinga

Wakati kukiwa na hatari hiyo, Dk Chuwa alisema watu wengi hupata virusi vya HPV, lakini si wote huwaathiri kwani kuna kundi la watu wenye kinga imara ambayo virusi hivyo vinapofika kwenye koromeo hupoteza uhai na visisababishe maambukizi.

“Mara nyingi wengi tunapata haya maambukizi, kwa hiyo kinga yetu ikiwa vizuri kirusi kinapambana kinakufa, lakini afya ikiyumba kidogo ndiyo unaanza kuumwa na ndiyo maana ukichunguza inawapata zaidi watu wenye umri mkubwa miaka 45 na kuendelea pale kinga zao zinapoanza kushuka, hivyo huwa rahisi mabadiliko kutokea na kuwa saratani,” alisema.

Ili kujikinga na kirusi hicho, Dk Chuwa alishauri kuwapa chanjo mabinti wenye umri mdogo pamoja na kuangalia namna ya kutoa chanjo kwa vijana wadogo wa kiume, ili kuwalinda dhidi ya saratani ya koo.

Kirusi cha HPV

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Hospitali ya Aga Khan, Aleesha Adatia alisema kila kirusi kina namba na vinagawanywa katika pande mbili, kwani vipo vyenye hatari zaidi na visivyo vya hatari.

Virusi visivyo na hatari vinaweza kusababisha maudhi madogo madogo kama vivimbe sehemu za siri, huku vile vyenye hatari vipatavyo 13 vikisababisha saratani.

Alipoulizwa iwapo matumizi ya kondomu yanaweza kusaidia mhusika kutokupata maambukizi ya virusi hivyo, Dk Aleesha alisema yanaweza kupunguza hatari za kupata maambukizi kwa kiasi fulani.

Alisema mwanamume akipata virusi hivi atamwambukiza kila mwanamke anayekutana naye kimwili na mwanamke akivipata huchukua kati ya miaka 15 hadi 20 kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Taasisi ya saratani Ocean Road, Crispin Kahesa alisema takwimu za mwaka hadi mwaka zinaonyesha ongezeko la aina za saratani zinazosababishwa na kirusi hicho.

Alisema kwa miaka 10 iliyopita saratani zinazosababishwa na maambukizi ndio zilikuwa zinaongoza ikianza saratani ya shingo ya kizazi, karposis sarcoma, kibofu, shingo na kichwa.

“Saratani zinazosababishwa na mfumo wa maisha usio bora, tabia, mazingira na maambukizi ndio zinaongezeka kwa kasi ,lakini pia idadi ya wagonjwa wanohudhuria hospitali imeongezeka kutoka asilimia 10 kwa miaka 12 iliyopita na kwa sasa ni zaidi ya asilimia 30,” alisema Dk Kahesa.

MWANANCHI
 
Uwaambie nini vijana wa bongo na kulambana uchi wakuelewe
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom