Kasi mpya, ari mpya kwa wawekezaji wa nje au wazawa? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kasi mpya, ari mpya kwa wawekezaji wa nje au wazawa?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sulphadoxine, Mar 9, 2012.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Mar 9, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  KAULI mbiu ya “Ari, Nguvu na Kasi Mpya” ilioasisiwa na Rais Jakaya Kikwete ilikuwa na lengo linalofanana na ule msemo maarufu wa Kichina unaosema: “Usijali rangi ya paka, iwe nyeusi au nyeupe, alimradi anakamata panya”


  Msemo huo wa Kichina uliasisiwa na Hayati Mao Tse-tung na ulilenga kuhimiza Wachina kuchapa kazi kwa bidii na kuacha tabia ya kuchagua ajira, ilihali mradi kazi wafanyazo ni halali na zinakidhi mahitaji matatu muhimu ya binadamu; mavazi, chakula na malazi.

  Mao (1893-1976), aliongoza mapinduzi nchini China na kuunda Jamhuri ya Kijamaa ya Watu wa China mwaka 1949. Alitawala nchi hiyo kwa miaka 25 kama mwenyekiti wa chama tawala na rais hadi alipofariki dunia mwaka 1976.

  Kauli-mbiu ya “Ari, Nguvu na Kasi Mpya” kwa upande mwingine inalenga kuhimiza vijana wa Tanzania kusahau makosa au kasoro zilizopita, ulalamishi na uvivu na badala yake kuchapa kazi kwa bidii ili kuliletea taifa lao maendeleo haraka.

  Ingawa Wachina wameshaweka kando au kubadilisha sehemu kubwa ya mafundisho yaliyotokana na filosofia ya Ujamaa wa MaoTseTung, lakini msemo wa “usijali rangi ya paka…” bado inaendelezwa kwa mtazamo mpya.

  Wachina wanachapa kazi sana na hawajali wanashirikiana na binadamu wa aina gani ili mradi hawadhuru na wanafikia malengo yao. Awe mweusi au mweupe, ana dini au mpagani, Wachina wanashirikiana na mteja au mfanyabiashara yeyote anayeweza kuwaletea neema.

  Wachina wanauza na kununua bidhaa mahali popote wanapoona pana unafuu kwao. Wanatafuta na kuuza elimu na maarifa popote duniani kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo.

  Mataifa yaliyoendelea huko Ulaya, Marekani na Japan tayari yameshaanza kuhofia kasi ya maendeleo huko China na kuanza ushirikiano mpya ili kukabiliana na tishio la China kuwa taifa kubwa na lenye nguvu zaidi duniani.

  Inakadiriwa kwamba kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi inayofanywa na China, taifa hilo litakuwa limefikia kiwango cha maendeleo sawa au kupita kiwango cha sasa cha Marekani miaka 25 tu ijayo.

  Viwanda vingi vya China vilivyokuwa vinamikiwa na dola ya kijamaa enzi za Mao hivi sasa vinamilikiwa na wafanyabiashara binafsi wa Kichina wakishirikiana na wabia toka nchi zilizoendelea, hususan Japan, Korea ya Kusini, Ulaya na Marekani.

  Wachina wamebadili sera za kijamaa lakini kabla ya kufanya hivyo walihakikisha ubinafsishaji unarudisha rasilimali za taifa (umma) toka kwenye umiliki wa dola na kwenda katika umiliki Wachina binafsi na sio umiliki wa wawekezaji wa kigeni. Wawekezaji wa nje waliuziwa sehemu ya hisa tu za mali za umma ili wavutiwe kuleta mitaji na maarifa mapya katika uzalishaji viwandani.

  Tofauti na Watanzania, Wachina hawakufanya ubinafsishaji kutokana na shinikizo la wafadhili wa nje bali kutokana na utashi wao wenyewe baada ya kubaini kwamba sera za kijamaa hazitaweza tena kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kasi kubwa katika mfumo wa sasa wa uchumi wa dunia.

  Kwa bahati mbaya Tanzania haikuweza kubinafsisha rasilimali za taifa kwa Watanzania binafsi kwa sababu serikali ilikuwa inashinikizwa kutekeleza masharti ya wafadhili wa nje haraka kabla ya kutafakari kwa kina.

  Wafadhili hao ndio wanataka wawekezaji wa kigeni wamiliki uchumi. Hivi leo Watanzania wanaohubiriwa kauli-mbiu ya “Ari, Nguvu na Kasi-Mpya” hawamiliki tena sehemu kubwa na muhimu ya uchumi wa taifa lao.

  Watanzania ni kama wamiliki wa bodi ya gari ambalo injini yake ni mali ya wageni ambao pia ndio madereva wa gari hilo. Ndani ya gari hilo, Watanzania ni kama abiria wenye tiketi halali lakini hawana uwezo wa kumwamuru dereva apite njia gani au aendeshe gari kwa kasi gani ya mwendo.

  Kauli-mbiu ya “Ari, Nguvu na Kasi-Mpya” inahubiriwa kwa Watanzania wakati kwa hakika ilistahili kuhubiriwa kwa wageni wawekezaji wanaomiliki sehemu nyeti ya uchumi wa taifa. Lakini bila shaka viongozi wa serikali wanatambua fika kwamba kuhubiria wawekezaji kauli-mbiu hiyo ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. “Mbuzi” kwani hataweza kucheza muziki wao. “Mbuzi” hao wana aina tofauti ya muziki wanaopenda na ambao unapigwa nje ya nchi na viongozi na tasisi za kimataifa za nchi tajiri wanakotoka.
  Mifano halisi ya kudhihirisha ukweli huo ipo mingi. Miaka ya 1970, serikali iliwekeza rasilimali nyingi kujenga viwanda vikubwa vitatu vya kuhifadhi ngozi kwa chemikali (tanneries) katika miji ya Moshi, Mwanza na Morogoro. Serikali pia ilijenga viwanda vikubwa viwili vya kutengeneza viatu - Tanzania Shoe (Bora) mjini Dar es Salaam na Morogoro.
  “Bora” ilikuwa inatengeneza viatu imara na maarufu sana kabla ya kubinafsishwa. Serikali ya Mwalimu Nyerere ilitambua ukweli kwamba Tanzania ni nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo katika Afrika baada ya Sudan na Ethiopia hivyo mifugo na ngozi zake zinaweza kutumika kujenga uchumi. Viwanda vya ngozi (tanneries) na viatu (Bora) vilikuwa vinatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya watu 5,200 na ajira za pembeni zaidi ya 10,000.

  Bora pia ilikuwa imeshaanza uzalishaji wa mipira ya magurudumu ya baiskeli lakini leo hii inatengeneza kandambili tu. Maduka yamejaa viatu vya mitumba au viatu hafifu toka viwanda vya China, Japan, Korea, Singapore, Malaysia, Taiwan, Dubai na kadhalika.

  Maonesho ya Sabasaba ya kila Julai katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam ni kielelezo halisi. Maonesho haya yana bidhaa nyingi za plastiki na ngozi toka nje kuliko bidhaa za nchini.

  Ukiachilia mbali Sabasaba, kumekuwepo usafirishaji wa ngozi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi na nyingi zikiwa bado mbichi kiasi kwamba hata ajira za kuziweka kemikali ili zisivunde na kuoza nazo zimefutwa kwa Watanzania na sasa ni ajira za “wajanja” walio nje ya nchi.

  Tani za magogo ya miti ya asili licha ya kuwepo udhibiti wa hapa na pale zimekuwa zinasafirishwa nje ya nchi. Magogo hayo hutumika kutengeneza samani nzuri zinazouzwa kwa matajiri wa ng’ambo kwa bei ‘mbaya’.

  Mabaki ya magogo hayo husagwa, kuungwa kwa gundi na hatimaye kutengeneza mbao za samani hafifu zinazoletwa Tanzania na kuuzwa kwa bei ‘mbaya’ tena kwa ofisi za serikali na hata binafsi. Samani hizo hafifu hudumu kwa muda mfupi na huharibika na hivyo kulazimu kuagiza nyingine hali inayosababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma. Hata hivyo hivi karibuni serikali ilipiga marufuku uagizaji wa samani kutoka nje. Hivyo ni vema na haki.

  Hakuna mwekezaji anayetaka kuanzisha tena upya uchinjaji wa ng’ombe na usindikaji wa nyama katika kiwanda cha Tanganyika Packers kilichokuwa Kawe jijini Dar es Salaam na badala yake mwekezaji mpya anataka kujenga majumba eneo lote la kiwanda.

  Hakuna mwekezaji aliye tayari kujenga kiwanda bora cha kutengeneza mbao na kutumia mabaki ya mbao na taka za magogo kutengeneza samani hapa nchini. Wakishauriwa hivyo wanasema umeme wa Tanzania ni ghali na hivyo wakizalisha mbao hapa hawatapata faida kama wanayopata wakibeba magogo na kuyauza nje. Hata ajira na kupasua mbao zinahamia nje!

  Kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Mgororo huko Mufindi - Southern Paper Mills (SPM) - kilichoanzishwa na serikali mwaka 1985 hivi sasa ni mali ya wawekezaji wapya toka nje baada kusitisha uzalishaji kwa muda mrefu na hatimaye kubinafsishwa Januari 2004.

  Hadi sasa imeshapita miaka nane toka SPM kibinafsishwe rasmi na kuitwa Mufindi Paper Mills Limited lakini wawekezaji wapya (M/S Rai Group ya Kenya) wanauza magogo tu toka katika mashamba ya miti waliyokuta badala ya kuyatumia kutengeneza karatasi.

  Wawekezaji walinunua hisa za Serikali kwa Dola za Kimarekani 1,000, 000 na kuahidi kuwekeza dola nyingine milioni 25 kufufua kiwanda hicho na kuanza uzalishaji upya. Lakini kwa zaidi ya miaka 20 hadi sasa bado viwanda vya ndani vya magazeti, vitabu na madaftari vinaendelea kuagiza karatasi toka nje kwa sababu hazizalishwi nchini.

  Wakati Tanzania inaendelea kugeuzwa gulio la bidhaa za hafifu toka nje Serikali inaongeza juhudi katika kupanua nafasi za wanafunzi katika vyuo vikuu. Katika kipindi hicho hicho ambacho uzalishaji wa viwanda vya ndani unapungua kutokana na wingi wa bidhaa toka nje, idadi ya vyuo inaongezeka na ajira hazipo.

  Mwaka 1990, Tanzania ilikuwa na vyuo vikuu viwili tu vilivyokuwa vinatoa wahitimu ambao ni chini ya 4,000. Tena awali (kabla ya 1985) vyuo hivyo, University of Dar (UDSM) na Sokoine University of Agriculture (SUA) vilikuwa chuo kimoja.

  Baada tu ya kipindi kifupi cha miaka 17 (1990-2007) hivi sasa Tanzania ina vyuo vikuu takribani 18 vilivyosajiliwa na Tanzania Commission for Universities (TCU) na inatarajia kusajili vyuo vingine zaidi kutokana na maombi iliyopokea.

  Katika hafla ya kuchangia Chuo cha Sebastian Kolowa University College (SEKUCo), miaka ya hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alisema ingawa idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu inaongezeka lakini idadi ya wahitimu wa masomo ya sayansi ya teknolojia hapa Tanzania ni asilimia 30 tu.

  Aliongeza kwamba maendeleo endelevu yanaletwa na maendeleo katika sayansi na teknolojia hivyo kuna haja ya kutilia mkazo masomo hayo ambayo yanakwepwa na wanafunzi wengi kwa sababu ambazo hazielewi.


  Pengine Rais Kikwete aliona vibaya kusema ukweli kuwa wanafunzi wengi wanakataa masomo ya sayansi na teknolojia kwa sababu hayana ajira hapa nchi kutokana na uchache wa viwanda vya uzalishaji.


  Ongezeko la wasomi wa fani nyingine zisizokuwa za sayansi na teknolojia watakuja pia kukosa ajira wakiwa wengi bila kuwepo na maendeleo ya viwanda vya ndani. Kuendelea kuongeza vyuo vikuu na idadi ya wahitimu kwa matarajio kuwa nchi itaendelea bila juhudi za kujenga viwanda endelevu ndani ya nchi ni sawa na kutamani kuonja pepo kabla ya kufa
   
 2. Anheuser

  Anheuser JF-Expert Member

  #2
  Mar 9, 2012
  Joined: Mar 23, 2011
  Messages: 1,962
  Likes Received: 46
  Trophy Points: 145
  Article inatia uchungu kweli kweli, hatuna kiwanda cha makaratasi? Tuna export magogo tuna import makaratasi?

  Hata makaratasi?
   
Loading...