Kashfa ya UDA ina mizizi ya ‘ukada wa CCM’ ; nani hawa Simon Group LA? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kashfa ya UDA ina mizizi ya ‘ukada wa CCM’ ; nani hawa Simon Group LA?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, Aug 13, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Aug 13, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145

  Waandishi WetuToleo na 198


  [​IMG]
  • Ni nani hawa Simon Group LA?
  • Walilivamiaje Jiji la Dar kutoka Mwanza?
  KATI ya mijadala iliyozua hisia kali hivi karibuni katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma, ni ule wa juu ya kuuzwa kinyemela kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa kampuni ya Simon Group ya jijini Mwanza.
  Kama ambavyo karibu mashirika yote ya umma yalivyoweza kuuzwa kinyemela miaka ya karibuni, uuzwaji wa UDA unadhihirisha jinsi ufisadi ulivyokithiri miongoni mwa watendaji wakuu serikalini na makada wa chama tawala Chama cha Mapunduzi (CCM) ‘waliofunga ndoa' na wafanyabiashara wasio na uchungu na nchi hii na jasho la umma kwa ujumla.

  Kwa ilivyodhihirika Bungeni, unaweza kusema, pasi shaka yoyote, kwamba UDA na mali zake imeuzwa kihuni; tena kupitia katika akaunti za watu binafsi.
  Akiuelezea kwa waandishi wa habari ufisadi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Deo Filikunjombe, alionyesha jinsi sehemu ya malipo hayo yalivyolipwa kupitia akaunti ya mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya UDA, kuanzia Septemba 2, 2009, ambapo Sh. milioni 250 zililipwa, Septemba 26, Sh. milioni 20; na Desemba 9, 2009 Sh. milioni 30.
  Inashangaza kidogo ni vipi Sh. milioni 30 ziliweza kulipwa kwenye akaunti ya kigogo huyo Desemba 9, 2009 ambayo ilikuwa ni siku ya mapumziko ya sherehe za Uhuru!

  Lakini pengine hilo si la kushangaza sana kwa mitandao ya kifisadi ilivyo hapa nchini; kwani hata baadhi ya akaunti za kashfa nyingine kubwa kama zile za Kagoda, Deep Green, Tangold na nyingine zilizohusishwa na kashfa ya EPA, nazo zilifunguliwa na kuingiza fedha siku za sikukuu za Taifa na za Jumapili!

  Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe anasema, taratibu za kuuza UDA hazikufuatwa, na hivyo uamuzi wowote ni batili.

  "Kilichofanyika ndani ya mkataba huo ni ufisadi mtupu", anasema Kabwe, na kuongeza kwamba mwekezaji huyo (Simon Group) "ameingia choo cha kike"; kwa maana kwamba ameingia pasipostahili na hivyo hawezi kukwepa aibu kwa "jeuri" yake hiyo.


  Maeneo ya UDA yaliyouzwa kinyemela ni pamoja na eneo la kuegesha magari Kurasini, kiwanja kilichopo "Railway Station", nyumba na mali nyingine, pamoja na hisa zaidi ya 7,700,000 ambazo zimenunuliwa kwa thamani chini ya senti moja kila moja.


  Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Simon Group, Robert Kisena, ni kwamba tayari amekwishalipa Sh. milioni 760 na kiasi cha Sh. milioni 500 kilichobaki atakamilisha baadaye; licha ya kwamba thamani halisi ya kampuni hiyo ya umma haijafahamika.


  Utata unaongezeka pale kigogo aliyewekewa fedha za manunuzi ya UDA kwenye akaunti yake anapokana na kudai kuwa fedha zinazodaiwa kuingia kwenye akaunti yake ni mali yake halali kutoka vyanzo vingine; wakati huo huo uongozi wa Simon Group nao unadai kuwa hayo ndiyo sehemu ya malipo kwa ununuzi wa UDA.

  Kama madai ya kigogo huyo ni sahihi, basi, UDA imekabidhiwa kwa mwekezaji bila kulipiwa chochote. Na kama maelezo ya mwekezaji ni sahihi, basi, malipo ya UDA yameporwa na kigogo huyo kwa njama za pamoja na mwekezaji.
  Lakini tujiulize; je, mwekezaji alipata stakabadhi ya malipo yake? Kutoka kwa nani? Je, anaamini huo ndio utaratibu wa kununua mali ya umma, na ndio uwekaji sahihi wa kumbukumbu za ununuzi kama huo?

  Kuzinduka kwa Serikali Bungeni juu ya ufisadi huu kumefanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aagize ufanyike uchunguzi ukihusisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB); wakati huo huo umma, pamoja na wabunge wote wa Mkoa wa Dar es Salaam (bila kujali tofauti za itikadi za vyama vyao) wakitaka Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Iddi Simba wakamatwe na au kusimamishwa kazi.


  Wengine ni Mkurugenzi wa Jiji, Bakari Kingobi na watendaji wote waliohusika katika mchakato mzima wa kuuza mali za shirika hilo kinyemela.


  Jambo moja linalokera pia ni kuundwa kwa Kamati ndogo ya Kamati ya Bunge kufuatilia sakata hilo, ambayo inajumuisha Mheshimiwa Juma Kapuya anayehusishwa na umiliki wa Simon Group Ltd, na ambaye ametajwa pia katika nyaraka za wanahisa wa kampuni hiyo. Je, huu ni mkakati wa kufifisha juhudi za kuibua ufisadi huu?


  Lakini ni nani hawa, Simon Group LA na wamevamiaje jiji la Dar kutokea Mwanza na Shinyanga?

  Simon Group ni kampuni iliyozaliwa na kampuni ya Simon Agency iliyoanzishwa mkoani Shinyanga na Robert Kisena, kushughulika na ununuzi na uchambuaji wa pamba karibu miaka minane iliyopita.

  Kampuni hiyo ina historia ya kuingia kwenye migogoro mikubwa ya kibiashara na Vyama Vikuu vya Ushirika vya Kanda ya Ziwa, vikiwamo Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (NCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), ambavyo vinaidai mamilioni ya fedha kwa kukiuka mikataba mbalimbali, ikiwamo ya kukodi vinu vya kuchambulia pamba na ununuzi wa rasilimali.


  Simon Agency inahusishwa pia na kununua kiwanda cha kusindika mafuta cha NCU kijulikanacho kama "New Era", na nyumba za ushirika huo kwa bei ya kutupa.

  Inadaiwa kuwa, wakati kampuni hiyo iliweza kununua kiwanda hicho kwa Sh. milioni 700 tu, bei halisi ya kiwanda hicho na miundombinu yake ilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 2.5.

  Mheshimiwa Kapuya anaingiaje?

  Kutokana na kuzongwa na mitafaruku mingi ya kibiashara dhidi ya vyama vya ushirika, kampuni ya Simon Agency ilianza kujivua gamba kwa kuunda kampuni tanzu iliyofahamika kama Robersika, yenye makao makuu yake Urambo, Tabora kwa ajili ya kuendesha viwanda vya kusindika mafuta ya pamba.

  Inaaminika hapa ndipo Mheshimiwa Kapuya alipoingia ubia na kampuni hiyo tanzu, au alikuwa mwanzilishi kama ambavyo jina la kampuni hiyo linavyoashiria; yaani ROBERSIKA, kifupi cha "Robert Simon" [Robersi] na "Kapuya".


  Hata hivyo, kampuni hiyo haikudumu, na imeacha mlolongo wa malalamiko mengi kwa waliofanyanayo biashara.


  Ukitaka mambo yakunyokee jiunge na CCM

  Robert Simon Kisena, kwa kutaka mambo yamnyokee, mwaka 2008 alijaribu bahati yake kwa kugombea ujumbe wa Halmashauri ya Mkoa (CCM) kuwakilisha Wilaya ya Maswa, lakini hakubahatika kuchaguliwa.

  Kuanzia hapo alijipambanua kama kada wa CCM na tajiri anayeibukia. Kipindi hiki kilishuhudia wafanyabiashara wengi nchini wakifadhili au wakiteuliwa kuwa makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM ili wasiweze kuguswa na kwa biashara zao zinawiri.


  Mwaka 2010, Robert Kisena, alijitosa kugombea ubunge Jimbo la Maswa Magharibi kwa tiketi ya CCM, lakini akashindwa na John Magalle Shibuda wa CHADEMA, katika uchaguzi uliojaa fujo za kila aina na umwagaji damu.


  Katika hali iliyoashiria kwamba alikuwa tayari ameingia katika "pepo ya wasioguswa", alidiriki kumkata "mtama" (kumpiga ngwala hadi chini) Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Maswa, kofia na "crown" yake ikabwagwa chini na kuchaniwa sare, kwa sababu tu alitaka kumhoji kuhusiana na ghasia za uchaguzi.


  Kwa dhambi hiyo kuu ya kudhalilisha dola, Robert Simon aliachwa huru bila kukamatwa wala kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu alikuwa na kinga ya wakubwa, wakati Shibuda akisota mahabusu kwa kugeuziwa kibao.


  Ni baada ya uchaguzi huo, Robert Kisena alipohamia Dar es Salaam kutafuta "malisho mapya", kwa wito au kwa kubebwa na "makada" wenzake wa CCM, baada ya kuthibitika anao ujasiri wa kutosha kuweza kuingia kambi ya "makada wa zama hizi wa CCM."


  Kuundwa kwa Simon Group

  Kampuni ya Simon Group Ltd iliundwa katika kipindi cha vuguvugu la maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, kati ya mwaka 2009 na 2010, na wakurugenzi ambao wengi wao ni wenye ushawishi wa kisiasa.

  Kufuatia kuundwa kwa kampuni hiyo, mali nyingi ambazo kabla ya hapo zilimilikiwa kwa jina la Simon Agency, kikiwamo kiwanda cha mafuta cha New Era kilichonunuliwa kutoka NCU, zilihamishiwa kwenye miliki ya Simon Group.


  Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Kapuya anatajwa kuwa Mkurugenzi mwenye hisa katika Simon Group, basi, inawezekana kabisa kuwa [yeye na vigogo wengine] alikuwa tangu mwanzo Mkurugenzi katika Kampuni ya Simon Agency, kama alivyokuwa kwa kampuni tanzu ya ROBERSIKA.


  Kwa sababu hii, kuna sababu za kuamini kwamba kupaa kwa kampuni hiyo hadi kufikia uwezo wa kununua UDA, kunaweza kuwa na mkono wa Kapuya.


  Simon Group yatanua mbawa jijini Dar

  Raia Mwema limebaini ya kuwa Simon Group iliingia anga za Dar es Salaam kwa kuanza na ununuzi wa kiwanda kikubwa cha unga kwa kushirikiana na mtoto wa kigogo mmoja mzito wa CCM na Serikali.

  Kwa hiyo, kwa kufumba na kufumbua, kampuni ikawa inamiliki idadi kubwa ya magari (zaidi ya 100) ya mizigo na ya kubeba mafuta yanayosafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na nchi za DRC, Rwanda, Burundi na Zambia.


  Haiingii akilini kwamba, kampuni changa ya Simon Agency ingeweza kupata ukwasi mkubwa wa haraka kiasi hicho bila kushirikisha makada wazito wa CCM.


  Kuhusishwa kwa makada wa CCM na kampuni hii hakushangazi, kwa kuwa michirizi ya damu ya sakata hili inaonyesha wana uhusiano wa kibiashara, uliojengeka kwa misingi ya nasaba ya kichama (CCM) tangu harakati za Uchaguzi Mkuu wa 2010.


  Kwa kifupi, tunaweza kusema kwamba kashfa ya UDA ni moja ya kashfa nyingi nchini zinazobuniwa na kulitesa Taifa hili kila mwaka wa Uchaguzi Mkuu, kuanzia na kashfa ya TANESCO/IPTL (1995), Meremeta, EPA, Deep Green (2000) na sasa UDA na nyinginezo (2010).


  Kama utamaduni wa kujitajirisha miongoni mwetu kwa kuwapiga Watanzania "changa la jicho" kwa kaulimbiu za Uchaguzi ndio huu, basi, kazi ya "kujivua gamba" itakuwa ngumu; kwa maana huenda asipatikane wa kumfunga paka kengele miongoni mwa "Waarabu wa Pemba" wajuanao kwa vilemba vyao.
   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Aug 13, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Kweli CCM imebadilika sasa ngao yao ni Uma na Kisu; Lasima tuwe Makini wanakula zaidi ya ilivyokuwa KANU ya Kenya?
   
 3. pcman

  pcman JF-Expert Member

  #3
  Aug 13, 2011
  Joined: Oct 9, 2008
  Messages: 744
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 45
  machozi yana nidondoka
   
Loading...