Kashfa ya mgodi wa dhahabu Buhemba, bilioni 30/- `zaliwa`

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,098
Kashfa ya mgodi wa dhahabu Buhemba, bilioni 30/- `zaliwa`

2008-05-11 12:06:39
Na Mwandishi Wetu

Kashfa ya ufisadi katika mgodi wa dhahabu wa Buhemba ulioko mkoani Mara, umesababisha mapato ya nchi yenye thamani ya Sh. bilioni 30 `kuliwa` na wajanja.

Fedha hizo `zilitafunwa ` katika Awamu ya Rais Benjamin Mkapa, kuanzia 2003 hadi 2006 kupitia wawekezaji wa kampuni ya Tangold `iliyojimilikisha` mgodi huo kinyemela.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka Benki Kuu (BoT), jijini Dar es Salaam, Tangold ilichukua mgodi wa Buhemba ambao kuanzia mwaka 1997 ulikuwa ukiendeshwa kwa ubia na kampuni ya MEREMETA, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Triennex Properietary Limited ya Afrika Kusini.

Nyaraka nyeti kutoka BoT zilisema kuwa JWTZ na mbia huyo walianza kuchimba dhahabu Oktoba 1997 na baadaye mkataba ulimalizika na Tangold ilijimilikisha mgodi huo kuanzia mwaka 2003 hadi 2006.

Ziliibua kuwa mambo ya MEREMETA hayakwenda vizuri kwani miradi yote iliyoanzishwa ilitumia fedha za mikopo kutoka Benki ya Nedcor ya Afrika Kusini ambayo ilichukuliwa na kampuni ya Triennex Properietary kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.

``Kwa kuhofia athari za mkopo huo kwa uchumi wa nchi, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, aliunda Kamati maalum (task force) mwaka 2003 kwa ajili ya kuhakikisha mkopo unalipwa , kusimamia uendeshaji wa miradi ya MEREMETA na kuchunguza matatizo ya kampuni hiyo ya JWTZ na wawekezaji kutoka Afrika Kusini``, kilisema chanzo cha BoT.

Wajumbe wa kamati ya kuchunguza matatizo ya MEREMETA walikuwa ni Gavana wa BoT aliyefutwa kazi Dk. Daudi Balali, aliyekuwa Mwenyekiti.

Wengine ni Makatibu Wakuu Bw. Gray Mgonja wa Wizara ya Fedha, Bw. Patrick Rutabanzibwa -Madini na Nishati, (sasa Wizara ya Maji na Umwagiliaji), Bw. Vincent Mrisho aliyekuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (sasa Ofisi ya Waziri Mkuu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya awamu ya tatu, Bw. Andrew Chenge.

Bw. Chenge mwezi uliopita alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu kufuatia tuhuma za kuhifadhi zaidi ya shilingi bilini moja zinazodaiwa kuwa ni rushwa aliyopewa katika ununuzi wa rada iliyogharimu bilioni 70/-

Baada ya Tangold kuchukua Buhemba, ilichimba dhahabu yenye thamani ya Dola milioni 121.3 sawa na Sh. bilioni 147.

Dhahabu iliyochimbwa kwa kipindi hicho ni mali ya serikali kwani mgodi huo ulikuwa ni mali ya umma na ilikuwa na thamani ya Dola.

Taarifa zilizoifikia Nipashe Jumapili zilieleza kuwa katika kipindi hicho cha miaka minne, Tangold ilichimba karibu kilo 10,000 za dhahabu kutoka mgodi huo na kupata faida ya bilioni 30/-.

Tangold ilionyesha kuwa ililipa mrahaba wa Dola milioni 3.6 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini ambao ni sawa na Sh. bilioni 4.36 kwa muda wote.

Takwimu za uchimbaji zilionyesha kuwa mwaka 2003 zilichimba kilo 2,848. 874, wakati mwaka uliofuata zilipatikana kilo 291.290. Mapato yanaonyesha kuwa mwaka 2005 ilipata kilo 2,220. 560 na mwaka 2006 ilipata kilo 1,890.934 na kwa jumla zilipatikana kilo 9, 941.658.

Hata hivyo, baada ya kupata kiasi hicho BoT ilionyesha kuwa Tangold iliilipa kampuni moja ya Afrika ya Kusini gharama za kuendesha mgodi ambazo ni kati ya Dola milioni 80 na 90 kwa miaka minne ambazo ni sawa na Sh. bilioni 100 mpaka 116.3.

Hata hivyo, licha ya kupata mabilioni hayo Tangold haikuwasilisha fedha hizo serikalini.

``Taarifa za Tangold haziko Wizara ya Fedha-Msajili wa Hazina , wala kwa Msajili wa Biashara (BRELA) hata BoT hazikuwahi kuwasilishwa,`` kilisema chanzo cha BoT.

Pesa hizo bilioni 30 ni mali ya umma lakini hazijulikani zilipo na swali linaloendelea kuulizwa ni wamiliki wa kampuni hiyo ni akina nani?

Katika Mkutano wa Bunge wa mwezi uliopita Mbunge wa Musoma Vijini Bw. Nimrod Mukono, alitaka kufahamishwa wamiliki wa mgodi wa Buhemba.

SOURCE: Nipashe


Nani mmiliki wa Mgodi wa Buhemba? see here
 
Vigogo Tangold walikodi kampuni Afrika...

2008-05-12 09:10:18
Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya Tangold inayohusishwa na uchimbaji wa dhahabu katika mgodi wa Buhemba mkoani Mara, inadaiwa kukodisha kampuni ya Afrika ya Kusini ya Time Mining Limited `kiujanjaujanja` kwa ajili ya kuisaidia kusimamia na kuratibu shughuli za uendeshaji.

Habari zinasema kuwa Tangold ilisajiliwa `kisanii` nchini Mauritius na kuingizwa nchini kama kampuni ya kigeni `off-shore company` na kisha kusajiliwa ambapo ilipewa hati ya kukubalika ya certificate of compliance iliyotolewa na Wakala wa Serikali wa Kusajili na Kutoa Leseni za Biashara kwa Makampuni (BRELA), mwaka 2004, habari za ndani kutoka Benki Kuu (BoT), jijini Dar es Salaam, ambayo ndiyo iliyokuwa inasimamia biashara ya dhahabu zilidokeza.

Habari zimezidi kudai kwamba kupitia kampuni ya Time, Tangold ilisafirisha dhahabu kutoka Tanzania hadi kiwanda cha Rand nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuongezea thamani, kama vile kusafishwa, kuchujwa na kupangwa kwenye madaraja tayari kwa hatua nyingine na kuuzwa.

Kampuni hiyo ya Time Mining ilielezwa kuwa kila mwezi ilikuwa inalipwa wastani wa Dola milioni mbili, zaidi ya Shilingi bilioni mbili, na katika kipindi hicho cha miaka minne ya uzalishaji, yaani kuanzia 2003 hadi 2006 ilipata zaidi ya Dola milioni 95. Kiasi hicho ni zaidi ya Sh. bilioni 116.

Habari zaidi zilisema kuwa kampuni hiyo iliyokuwa inasimamia gharama za mradi huo ilikuwa inaweka fedha za mapato za Tangold katika Benki ya Nedcor ya Afrika Kusini na hivyo utajiri huo haukuzalisha faida kwa ajili ya Tanzania bali kwa nchi hiyo.

Benki hiyo ndiyo iliyokuwa imeikopesha kampuni ya MEREMETA iliyoundwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuingia ubia na kampuni ya Triennex Properietary Limited ya Afrika Kusini ili kuchimba dhahabu katika mgodi wa Buhemba.

Tangold ambayo imekuwa ikizua utata umiliki wake kama ni ya serikali ama la kiasi cha kumfanya Mbunge wa Musoma Vijijini, Bw. Nimrod Mkono kuchachamaa Bungeni akitaka kujua ni ya nani, ni kampuni ilioanza kuchimba dhahabu Buhemba kuanzia mwaka 2003 hadi mgodi huo ulipofungwa na serikali mwaka 2006.

Habari zilizoifikia Nipashe zilidai kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na vigogo kadhaa ambao hata leo wako madarakani na kwamba walisaidia kuilinda na kusimamia uendeshaji wa kampuni hiyo kwa kutoa maagizo ili isiingiliwe wala kuhojiwa na asasi za umma.

Wawekezaji wa kampuni hiyo wanadaiwa kuvuna `vijisenti` zaidi ya Sh. bilioni 30 katika kipindi cha miaka minne tangu ilipoanza kuchota dhahabu katika mgodi huo ulioko Wilaya ya Musoma Vijijini, wakati wa serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa.

Dhahabu iliyochimbwa kwa kipindi hicho ilikuwa na thamani ya zaidi ya Dola milioni 121.3, sawa na zaidi ya Sh. bilioni 147 ambazo ni fedha za serikali kwa vile mgodi huo ni mali ya umma.

Hata hivyo, zilitafunwa na wajanja hao na serikali haikuambulia chochote mbali na mrahaba wa Dola milioni 3.6 (zaidi ya Sh. bilioni 4.5) zilizoelezwa kwamba zililipwa.

Kuanzia mwaka 2003 hadi 2006 kampuni hiyo ilichimba karibu kilo 10,000 (tani 10) za dhahabu kutoka mgodi huo na kujipatia zaidi ya Sh. bilioni 30 baada ya kuondoa gharama za uendeshaji.

Tangold ilichukua mgodi wa Buhemba kuanzia 2003 ambao tangu mwaka 1997 uliendeshwa na kampuni ya MEREMETA iliyoundwa na JWTZ na Triennex Properietary Limited ya Afrika Kusini.

Hata hivyo JWTZ na mbia wake walioanza kuchimba dhahabu Oktoba 1997, walisimamisha uchimbaji mwaka 2003.

Ilielezwa kuwa miradi yote iliyoanzishwa na kampuni hiyo ilikopa fedha kutoka Benki ya Nedcor ya Afrika Kusini na zilichukuliwa na kampuni ya Triennex kwa niaba ya Tanzania.

``Kwa kuhofia athari za mkopo huo kwa uchumi wa nchi, Rais mstaafu Mkapa, aliunda kamati maalumu (task force) mwaka 2003 kwa ajili ya kuhakikisha mkopo unalipwa, kusimamia uendeshaji wa miradi ya MEREMETA na kuchunguza matatizo ya kampuni hiyo ya JWTZ na wawekezaji kutoka Afrika Kusini,`` kiliongeza chanzo cha BoT.

Wajumbe wa kamati walikuwa ni Gavana wa BoT aliyefukuzwa kazi, Dk. Daudi Balali, aliyekuwa Mwenyekiti.

Wengine ni Makatibu Wakuu Bw. Gray Mgonja wa Wizara ya Fedha, Bw. Patrick Rutabanzibwa -Madini na Nishati, sasa yuko Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Bw. Vincent Mrisho aliyekuwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya awamu ya tatu, Bw. Andrew Chenge `Mzee wa Vijisenti`.

Akiongea na Nipashe kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa alisema kwamba wajumbe wa kamati hiyo ndio wanamjua mmiliki wa Tangold.

``Kwa kuwa wao ndio wanajua habari za MEREMETA na wanajua kilichotokea Buhemba baada ya MEREMETA basi ilikuwa ni vyema wakamatwe waseme mmiliki wa Tangold ni nani,`` alisema.

Jitihada za kuwapata wajumbe wa kamati hiyo maalum zinaendelea.

SOURCE: Nipashe
 
na bado hapa hayajaanza kuandikwa madhambi waliyofanyiwa wakazi wa Buhemba wakati wakitolewa kwa nguvu toka kwenye vishimo vya jirani na mgodi wa buhemba (ambao kwa muda mrefu ulikuwa umezikwa na kambi ya jeshi la kujenga taifa).

Na hivi ni nani atafukia lile bonde la ufa lililoachwa na mafisadi huko Buhemba?
 
Back
Top Bottom