Kashfa ya Escrow iwe ya mwisho serikalini

Mapengo 17

R I P
Mar 28, 2014
1,232
0
Karibu dunia nzima hivi sasa inasubiri kwa hamu na shauku kubwa kuona Rais Jakaya Kikwete na mamlaka nyingine za uteuzi wakiwawajibisha vigogo wa serikali na watu wengine wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha uporaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).


Hilo linasubiriwa baada ya Bunge, ambalo lina dhamana kubwa ya kusimamia utekelezaji wa serikali, kupitisha maazimio kadhaa Novemba 29, mwaka huu, likitaka serikali pamoja na mamlaka nyingine za uteuzi ziyatekeleze.


Bunge lilifikia uamuzi huo baada ya Kamati yake ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya uongozi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuwasilisha bungeni Novemba 26, mwaka huu, taarifa maalumu yenye mapendekezo kadhaa, likiwamo la kutaka wahusika wa kashfa hiyo kuwajibishwa.


Taarifa hiyo ya PAC ilifuatia ripoti za ukaguzi maalumu wa malipo yaliyofanyika katika akaunti hiyo.


Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), ambazo zimethibitisha pasi na tone la shaka kwamba, fedha hizo zilikuwa ni za serikali (umma).


Kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, ukaguzi wa taasisi hizo mbili za serikali umeonyesha kwamba, kuna waliohusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miala haramu ya fedha za akaunti hiyo kwenda kwa Pan African Power Solutions Limited (PAP) na VIP.


Hao ni pamoja na 'mmiliki' wa kampuni ya kufua umeme ya IndependentTanzania Power Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi, na aliyekuwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering & Marketing, James ugemalira.


Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi; Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.


Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).


Wamo pia wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, akiwamo William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo.


Katika maazimio yake, Bunge limeziagiza kamati husika za kudumu za Bunge kuchukua hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge kuwavua nyadhifa zao Ngeleja na Mwambalaswa.


Kuhusika kwa vigogo hao katika kashfa hiyo, kumeelezwa kuwa kumeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma.


Fedha hizo zinatokana na kutolipwa kwa kodi mbalimbali za serikali na kushindwa kwa Tanesco kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (capacity charge) wa IPTL.


Pia inaelezwa kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilitumika kuwapa kile kinachooonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maofisa wa serikali, kama vile mawaziri, majaji na wabunge.


Wengine ni wenyeviti wa kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.


Azimio la kutaka watu hao wawajibishwe lilizingatia ukweli kwamba, vitendo, ambavyo Bunge limejiridhidha kwamba, wamevifanya, vinaashiria uzembe na makosa mbalimbali ya jinai.


Makosa hayo ni kama vile wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali za wizi.


Mbali na kuazimia mamlaka za uteuzi ziwawajibishe, Bunge pia liliazimia kwamba, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama zichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na vitendo vya kijinai katika kashfa hiyo.


Pia vyombo hivyo vichukue hatua stahiki dhidi ya watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali, ambao vinaendelea kuufanya.


Vilevile, Bunge liliazimia kwamba, Rais Kikwete aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.


Kadhalika, liliazimia kuwa mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic Tanzania Limited na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.


Kama nilivyotangulia kusema hapo juu, kila kitu hivi sasa ni bayana. Mamlaka za uteuzi, akiwamo Rais Kikwete ndiyo wanaosubiriwa na karibu dunia yote.


Linalotia faraja ni kauli za matumaini kwa serikali kutekeleza maazimio hayo ya Bunge, ambazo zimekwishatolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kwa nyakati tofauti, kuhusiana na hilo.


Kwa mfano, muda mfupi baada ya Bunge kupitisha maazimio hayo, Pinda akitoa hoja ya kuliahirisha Bunge, alisema serikali inaheshimu mawazo ya wabunge na kwa hiyo, itayafanyia kazi.


Kauli hiyo ilisisitizwa baadaye na Balozi Sefue, kwa kuwahakikishia Watanzania kuwa serikali itatekeleza maazimio hayo ya Bunge mara baada ya kupata taarifa rasmi.


Pamoja na hivyo, inasikitisha kuona hadi sasa serikali imeshindwa kujifunza kutokana na kashfa nyingi, ikiwamo ile iliyohusisha kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond iliyosababisha serikali yote kuanguka na kulazimika kuundwa upya baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu!


Bado pia ile kashfa ya uporaji wa zaidi ya Sh. bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya BoT) iliyohusisha kampuni mbalimbali, ikiwamo ya Kagoda Agriculture inayodaiwa kuchota Sh.bilioni 40 kutoka akaunti hiyo, haijasahaulika Kashfa nyingine, ambazo nazo bado hazijasahaulika masikioni mwa Watanzania ni ile inayohusisha kampuni ya Tangold, Deep Green, Meremeta, Buzwagi, Kiwira nakadhalika.


Mbali na kuiangusha serikali, kashfa ya Richmond pia imekuwa ikiisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kila uchao.


Hivi sasa serikali inalazimika kuilipa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans/Richmond zaidi ya Sh. bilioni 100 kutokana na uzembe na ufisadi uliofanywa na genge la watu wachache. Kwa lugha nyingine, uchumi wa nchi umehujumiwa na watu hao.


Hiyo ni kutokana na kuiruhusu Richmond, ambayo ni kampuni ya mfukoni, kupewa zabuni ya kufua umeme wa dharura, huku ikijulikana dhahiri shahiri kuwa haikuwa na sifa wala uwezo wowote ule; uwe wa kitaalamu, kifedha na kadhalika pia.


Hali hiyo ilichafua heshima, hadhi, sifa na taswira nzima ya nchi. Nchi ilifikia kuonekana kana kwamba vile haina uongozi wala vyombo vya ulinzi na usalama kiasi cha wajanja wachache kufanikiwa kujipenyeza ndani ya mfumo na kupata zabuni ya kushughulikia jambo nyeti kama la nishati ya umeme!


Hali hiyo haina tofauti kabisa na kashfa ya akaunti hiyo. Mtu mmoja, ambaye ana rekodi nyingi zilizogubikwa na utata mwingi ndani na nje ya nchi, ameweza kupenya na kuingia kwenye mfumo na kuutumia na kufanikisha matakwa yake haramu dhidi ya nchi na Watanzania kwa jumla.


Kwa hali hiyo, ni matumaini ya wengi kuwa somo lililopatikana safari hii katika kashfa ya sasa ya akaunti ya Tegeta Escrow, serikali na vyombo vyake watakuwa wamejifunza.


MY TAKE: Wenzetu watakuwa macho na makini ili kujua kama kashfa hii itakuwa ya mwisho kusikika serikalini au la!.

 

Lizaboni

JF-Expert Member
Feb 21, 2013
33,871
2,000
Kwani escrow ni kashfa? Au na wewe upo kwenye kampuni ya Udalali ya Reginald Mengi?
 

Mapengo 17

R I P
Mar 28, 2014
1,232
0
Kwani escrow ni kashfa? Au na wewe upo kwenye kampuni ya Udalali ya Reginald Mengi?
Kumbe akili yako ni changa namna hiyo? Hivi Lizaboni unafikiri waliohusika kuiba hizo fedha ni sawa na mtu kuchukuliwa fedha kwenye nyumba ya wazazi wako?acha siasa za kupapatika tulia kwanza ili unapoongea uongee kwa panching sio blaa blaa zako za kitoto.
 

Abunuas

JF-Expert Member
Apr 8, 2011
8,726
1,500
kama kutakuwa na utawala wa uwazi kama wa Kikwete basi kashfa kama hizi zitaongezeka maradufu.
kwa taarifa yako kashfa za aina hii ziko nyingi sana lakini kwa marais madikteta kama alivyokuwa mkapa nani angethubutu kwenda kumfunga paka kengele?
kashfa hizi zipo mpaka dunia iliyoendelea itakuwa Tanzania?
la muhimu ni uwajibishwaji, namaanisha kulipa walichoiba na kwenda jela.
 

Mapengo 17

R I P
Mar 28, 2014
1,232
0
kama kutakuwa na utawala wa uwazi kama wa Kikwete basi kashfa kama hizi zitaongezeka maradufu.

kwa taarifa yako kashfa za aina hii ziko nyingi sana lakini kwa marais madikteta kama alivyokuwa mkapa nani angethubutu kwenda kumfunga paka kengele?

kashfa hizi zipo mpaka dunia iliyoendelea itakuwa Tanzania? la muhimu ni uwajibishwaji, namaanisha kulipa walichoiba na kwenda jela.

Sasa mzee anaachia kiti mda sio mrefu, nimeshindwa kupata picha kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo kama hivi sasa mambo yako hivi itakuaje?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom