Kashfa ya BOT: Mawaziri wa sasa na wa zamani wahojiwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Mawaziri wahojiwa

Mwandishi Wetu Januari, 16, 2008
Raia Mwema

HALI si shwari ndani na nje ya Serikali kuhusiana na matukio ya Benku Kuu (BoT) na sasa imebainika kwamba baadhi ya wanasiasa, wakiwamo mawaziri, wa sasa na wa zamani, wanatuhumiwa kuhusika na ufisadi ndani ya benki hiyo.

Habari za ndani ya Serikali zinaeleza kwamba tuhuma hizo zimetokana na ukweli kwamba baadhi ya wanasiasa na watendaji waliojificha nyuma ya wafanyabiashara, wamenufaika na fedha zilizopotea ndani ya BoT.

Habari zinasema kati ya watuhumiwa hao, ni mawaziri wawili, ambao wamewahi kuwa karibu na aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk Daudi Ballali, ambaye wiki iliyopita alitangazwa kufukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete.

Mawaziri hao waliopata kufanya kazi na Dk. Ballali, taarifa zinasema, kwa muda sasa, wamekua wakichunguzwa na vyombo vya dola na siku za karibuni walihojiwa kwa mara kadhaa na vyombo hivyo.

Raia Mwema imetajiwa majina ya mawaziri hao lakini kwa kuwa haikufanikiwa kuwapata waeleze undani wa tuhuma hizo, haitawataja.

Lakini vyanzo kadhaa vya habari vinasema wenyewe walishitushwa sana na hatua hiyo ya kuhojiwa hasa ikizingatiwa kwamba mmoja wao ana nguvu kubwa ndani na nje ya Serikali na ilibidi ahakikishiwe kwamba uchunguzi huwa unafanywa kujiridhisha, hata kama mtuhumiwa anajiamini kuwa si mhalifu.

"Ni kweli wazee hao wamekuwa wakichunguzwa kwa muda mrefu hasa baada ya nyaraka nyingi kuwagusa moja kwa moja. Baada uchunguzi kufikia hatua muhimu ndipo walipoitwa kuandika maelezo yao, jambo ambalo wahusika wanasema halijawapendeza kabisa," anasema kiongozi mmoja serikalini.

Pamoja na wanasiasa hao, vyombo vya dola vimekuwa vikiimulika Wizara ya Fedha na Waziri wa Wizara hiyo, Zakia Meghji, ameelezwa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye amepania kusafisha maeneo nyeti ya uchumi.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba kabla hata ya kutolewa kwa ripoti ya wakaguzi wa nje wa kampuni ya Ernst and Young, Rais Kikwete, alikwisha kujulishwa kuhusiana na hali ilivyo ndani ya taasisi za fedha na idara za Serikali zinazohusika na uchumi wa Taifa.

"Rais aliamua tu kuanzia na BoT ambayo ndio mhimili mkuu wa uchumi wa Taifa, lakini anafahamu kwa undani kila eneo la kiuchumi na anafahamu kwa kila kitu kuhusu watendaji wanaohusika katika kuhujumu uchumi wa Taifa," anaeleza mtoa habari wetu ndani ya Serikali.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, muda si mrefu Rais Kikwete atafanya mabadiliko mengine ndani ya taasisi kadhaa zinazohusiana na uchumi, kazi ambayo anaifanyia utafiti wa kina kabla ya kufanya maamuzi ili kuepuka kinachoelezwa kuwa ni "kutopenda kufanya makosa ama kumuonea mtu".

Pamoja na kuwa ni hivi karibuni tu Rais Kikwete aliagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, kuongoza timu ya wataalamu akisaidiwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea, kulikuwa na kazi iliyokwisha kuwa imeanza kufanywa na vyombo hivyo ndani ya BoT na maeneo mengine nyeti kiuchumi.

"Kabla hata ya Rais kutoa maagizo hayo, alikuwa anafahamu kwamba vyombo vyake vilikuwa vimekwisha kuanza kazi ya kuchunguza kwa makini maeneo yote yanayogusa uchumi na kinachosubiriwa sasa ni hatua dhidi ya wahusika na miezi sita aliyoitoa kwa wahusika kuchukuliwa hatua ni mingi mno kwani wako watakaofikishwa mahakamani hivi karibuni," anasema ofisa huyo.

Wiki iliyopita maofisa wa idara mbalimbali za Serikali walikuwa makini zaidi katika kuchunguza viongozi na watendaji wa zamani na wa sasa katika Serikali na asasi zake ikiwamo BoT na baadhi wameonyesha mwanga mkubwa wa kupatikana ushahidi dhidi yao.

Mbali ya mawaziri hao, maofisa waandamizi wa asasi kadhaa za Serikali ikiwamo BoT, nao wamekwisha kufanyiwa mahojiano ya kina na vyombo hivyo vya Serikali ikiwa ni miezi kadhaa baada ya Gavana Ballali kuhojiwa kwa nyakati tofauti kabla ya kusafiri kwenda Marekani kwa matibabu na hatimaye kudaiwa kujiuzulu kabla ya Rais Kikwete kumuondoa madarakani.

Imeelezwa kwamba baadhi ya wanasiasa mwanzoni hawakufurahishwa na hatua hiyo ya Gavana Ballali kuhojiwa kiasi cha kutaka hatua hiyo isitishwe lakini mahojiano hayo yakaendelea baada ya kupata kibali kutoka kwa Rais Kikwete akiwataka watendaji ndani vyombo vya upelelezi kuendelea bila "kuogopa ama kumuonea yeyote."

"Wanasiasa hao walihojiwa na kwa kweli wana taarifa muhimu sana zinazoweza kusaidia kutoa fundisho kwa wanasiasa kuacha kabisa kuchezea fedha za umma kwa kutumia vibaya madaraka wanayopewa na sheria ama kanuni," kinaeleza chanzo chetu cha habari.

Habari zaidi zinaeleza kwamba Mkurugenzi mmoja wa BoT, amekua akichunguzwa na kwa sasa amekwisha kufanyiwa mahojiano mara kadhaa na sasa huenda akachukuliwa hatua za kiutawala ama kufikishwa mahakamani na pengine vyote kwa pamoja.

Sakata la BoT lilianza kufukuta kwa muda mrefu kupitia vyombo vya habari vilivyokua vikihoji hasa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo na matumizi mabaya ya fedha za umma kupitia mifuko na dhamana kwa wakopaji wakubwa ambao walianza kuonyesha dhahiri kuwa ukopaji wao ulikuwa wenye shaka kubwa.

Baada ya kujadiliwa kwa muda na vyombo vya habari, jina la BoT lilianza kuingia pole pole ndani ya vikao rasmi ikiwa ni pamoja na vikao vya Bunge ambako Mbunge wa Karatu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, aliongeza kasi ya waandishi wa habari kujua undani wa matumizi mabaya kupita kiasi ya fedha ndani ya Serikali kupitia Benki Kuu na Hazina.

Dk. Slaa alifikia hatua ya kutaka kuwasilisha hoja binafsi akitaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza matumizi mabaya ya kutisha ndani ya BoT, hoja ambayo iligonga mwamba hata kabla ya kuwasilishwa na badala yake kambi nzima ya Upinzani kuamua kuanza kutoa baadhi ya vipengele katika mikutano ya hadhara.

Hata hivyo, wakati Dk. Slaa akizungumzia BoT ndani ya Bunge, tayari Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Zakia, ilikwisha kutangaza kufanya uchunguzi wa kuhusu matumizi ya fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) lakini bila kufanya uchunguzi katika maeneo mengine pamoja na kuwa maeneo hayo yamekuwa yakichunguzwa na vyombo vya dola.

Baada ya kauli ya Meghji, Serikali kupitia ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali Ludovic Uttouh (CAG) iliajiri mkaguzi wa nje, kampuni ya Ernst and Young, ambayo ilianza kazi Septemba, 2007 na kukamilisha Desemba, 2007. CAG aliikabidhi ripoti ya wakaguzi hao kwa Rais Kikwete Januari 7, 2008.

Anaeleza Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo kuhusu maoni ya Rais Kikwete juu ya ripoti hiyo: " Amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwapo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile BoT."

Rais Kikwete alimuondoa madarakani Dk. Ballali na kuagiza kwamba hatua za kisheria na kiutawala zichukuliwe dhidi ya makampuni na watu waliohusika na upotevu huo.

Rais Kikwete alimteua Profesa Benno Ndulu, ambaye Raia Mwema lilimtaja mara kadhaa kuwa mmoja wa waliokuwa wakitajwa akiwatangulia wengine, kuchukua nafasi ya Dk. Ballali.

Rais Kikwete aliagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ikutane mara moja kujadili taarifa ya ukaguzi na kuchukua hatua zipasazo za kinidhamu dhidi ya maofisa wote wa benki, walio chini ya mamlaka yake waliohusika na kusababisha hasara kwa taifa.

Mbali ya kusitisha shughuli za EPA na kuagiza vyombo vya dola kuwashughulikia wahusika, Rais Kikwete alimuagiza Mwanasheria Mkuu kuhakikisha kwamba fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa na Luhanjo alisema kwa wale ambao wamezibadilisha fedha hizo katika rasilimali, serikali itachukua rasilimali hizo kufidia fedha.

Makampuni 22 yametajwa kuhusika na upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 133, kutokana na ama kutokuwapo kumbukumbu za kuonyesha makampuni hayo ama kuwapo kwa nyaraka za kughushi na mengine kukosa uhalali wa kulipwa fedha hizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ukaguzi katika mwaka wa fedha wa 2005/2006 uliochunguzwa, katika mwaka 2005 yalifanywa malipo ya jumla ya Shilingi 133,015,186,220.74 kwa Makampuni 22 ya hapa nchini. Makampuni hayo ni: Bencon International Ltd., VB & Associates Company Ltd., Bina Resorts Ltd., Venus Hotel Ltd., Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd., Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd., Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd., G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KARNEL Ltd.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kwamba ukaguzi umebaini kwamba kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi 90,359,078,804.00 zililipwa kwa makampuni 13 ambayo yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kugushi na hivyo makampuni hayo hayakustahili kulipwa chochote.

Makampuni hayo yametajwa kuwa ni: Bencon International Ltd., VB & Associates Company Ltd., Bina Resorts Ltd. of Tanzania, Venus Hotel Ltd., Njake Hotel & Tours Ltd., Maltan Mining Company Ltd., Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd., B. V. Holdings Ltd., Ndovu Soaps Ltd., Navy Cut Tobacco (T) Ltd., Changanyikeni Residential Complex Ltd., Kagoda Agriculture Ltd.

Ukaguzi umeendelea kubaini kuwa makampuni tisa ambayo yalilipwa jumla ya Sh. 42,656,107,417.00 hayakuwa na nyaraka za kuonyesha stahili ya malipo na hivyo kuwafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wa malipo hayo.

Makampuni hayo yalitajwa kuwa ni: G&T International Ltd., Excellent Services Ltd., Mibale Farm, Liquidity Service Ltd., Clayton Marketing Ltd., M/S Rashtas (T) Ltd., Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na KERNEL Ltd.

Wakati huo huo Makampuni mawili, yaani, Rashtas (T) Ltd na G&T International Ltd., kumbukumbu zake za usajili katika daftari la Msajili wa Makampuni nchini hazikuweza kupatikana.





 
Back
Top Bottom