Kashfa nzito ofisi ya DPP Moshi

John Kisii

Member
Nov 27, 2013
7
0
Kashfa nzito ofisi ya DPP Moshi

Mwandishi Wetu,Moshi

Ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP) imelaumiwa na baadhi ya Polisi kuwa ndio kiini cha kuibuka upya kwa wimbi jipya la wizi wa vifaa vya magari mjini Moshi.

Kwa wiki moja , gazeti hili lilikuwa likipokea simu nyingi kutoka mjini Moshi za wamiliki wa magari wakilituhumu Jeshi la Polisi kuhusika kukilea kikundi kinachoendesha wizi huo.

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zimedokeza kikundi kinachoendesha wizi huo kilikamatwa Desemba mwaka jana lakini mawakili wawili wa Serikali walishinikiza watu hao kufutiwa mashitaka.

“Tuliwakamata ‘red handed’ lakini mmoja ni ndugu na wakili mmoja wa Serikali kule Arusha akaja hapa Moshi akatufokea kwanini tunaendelea kuwashikilia watuhumiwa hao”alidokeza polisi mmoja.

Polisi huyo alifafanua hata baada ya mkuu wa upelelezi mkoa wa Kilimanjaro (RCO), Ramadhan Ng’anzi kueleza sababu za kuwashikilia bado wakili huyo alitoa lugha za kibabe akitaka waachiwe.

Inadaiwa kuwa baada ya Polisi kushikilia msimamo wa kutowaachia, wakili huyo alikwenda ofisi ya DPP Moshi na kula njama na wakili mwingine ambaye alitumia ubabe kuitisha jalada la kesi hiyo.

“Baada ya kuliitisha akatoa maelekezo yake tukayafanyia kazi na kumrudishia jalada lakini huwezi kuamini yule wakili wa Moshi aliturudishia tena akitoa maelekezo yasiyo na msingi”alidai polisi huyo.

Polisi wanadai kuwa, baada ya polisi kugundua mawakili hao wawili wa Serikali wana maslahi katika kesi hiyo waliamua kuifungua mahakama ya mwanzo ambako kisheria mawakili hawaendeshi kesi.

Habari zinadai kuwa kuona njama zao za kuwatoa watuhumiwa hao zimegonga mwamba, wakili wa serikali wa Moshi alikwenda mahakama ya mwanzo na kisha kumfokea hakimu na kuifuta kesi hiyo.

“Tunashangaa tunalaumiwa kurejea kwa wimbi hili wakati huyu wakili (jina tunalo) aliandika nolle (hati ya kufuta mashitaka) na wala hakuifungua tena kesi hiyo”wamedokeza Polisi.

Kwa wiki nzima ya jana, mji wa Moshi ulitingishwa na wizi wa vifaa vya magari na Polisi wanadai kundi hilo ndilo lile lile ambalo walilikamata desemba mwaka jana lakini likaachiliwa na DPP.

Kwa uchache, magari yapatayo 12 yalivunjwa kioo cha nyuma kwa kutumia kemikali na kisha kufunguliwa vifaa vyenye thamani kubwa huku mengine yakiibiwa vifaa vya hadi Sh8 milioni.

Kufuatia kurejea kwa wizi huo, wamiliki wa magari wanalinyooshea kidole Jeshi la Polisi kwamba ndilo linalokilea kikundi hicho kwa kuwa kilikamatwa mwaka jana na kuachiwa bila kushitakiwa.

Lakini polisi kadhaa waliopiga simu chumba cha habari Rai, walimtaka DPP aanzishe uchunguzi kuchunguza mazingira ya tukio zima la kukamatwa watu hao na kufutiwa mashitaka.

“Uone Mungu alivyo mkubwa miongoni mwa walioibiwa safari hii ni pamoja na Hakimu aliyesikiliza ile kesi mahakama ya mwanzo kabla ya kufutwa na wakili mmoja wa Serikali”alidokeza Polisi mmoja.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kuwapo kwa wimbi hilo na kusema tayari watu kadhaa wamekamatwa.

Alisema watu hao wamekuwa wakiiba vifaa mbalimbali kwenye magari kama vile kompyuta mpakato(laptop), redio na vifaa vingine.


Source: Rai Desemba 6,2013
 
Back
Top Bottom