Kashfa Manispaa ya Ilala

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,006
Kashfa Manispaa ya Ilala

na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima

BAADHI ya watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wamedaiwa kuwa katika orodha ya watu wanaolipwa mishahara na kundi la Watanzania wenye asili ya Kiasia kwa ajili ya kutekeleza matakwa yao.

Habari zilizoifikia Tanzania Daima Jumapili zilieleza kuwa watendaji hao wanalipwa kwa ajili ya kutoa vibali bandia vya ujenzi na kuuza maeneo ya wazi katika eneo ya Upanga, jijini Dar es Salaam.

Eneo linalodaiwa kuathirika zaidi na ujenzi holela kupitia vibali bandia ni la barabara ya Alykhan ambako baadhi ya barabara zimezibwa kwa kuta zinazojengwa na wakazi wa eneo hilo.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo anayedaiwa kujenga ukuta katikati ya barabara alilieleza gazeti hili kuwa kibali chake kilitengenezwa na maofisa ardhi wa Manispaa ya Ilala baada ya kuwaomba wamsadie kufanikisha ujenzi wa ukuta huo.

Mkazi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Walji Sachejina, alisema alifahamishwa kwa maofisa hao na viongozi wa msikiti wao ambao hakuutaja jina na alipoomba msaada walikubali kwa heshima na uhusiano walionao na viongozi wa msikiti huo.

“Mimi ni mtu mwema, ninaongea vizuri na watu, nina uhusiano mzuri na maofisa wa Manispaa ya Ilala, wamenisaidia sana, kama hati hii ina kasoro basi mimi sihusiki, niliwaomba wanisaidie wakanitengenezea hii hapa,” alisema Sachejina ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mgogoro ulioibuka kati yake na majirani kuhusu kujenga ukuta unaoziba sehemu ya barabara inayotumiwa na watembea kwa miguu na magari iliyo katika eneo la kiwanja namba 283, 284 na 285. Alisema jirani zake wanamuonea wivu kwa vile ana uhusiano mzuri na wakubwa.

Alisema aliamua kujenga ukuta kuziba sehemu hiyo ya barabara kutokana na usumbufu wa kelele anazozipata kutoka kwa majirani wanaopita karibu na dirisha lake.

Alisema kabla ya kuanza ujenzi wa ukuta huo aliwasiliana na wakubwa wake wa dini ambao walimpatia msaada wa fedha zilizomwezesha kuwahonga baadhi ya maofisa ya Idara ya Ardhi wa Manispaa ya Ilala waliompatia kibali cha kujenga eneo hilo.

“Mimi sina fedha, najua hii ni barabara, lakini napata shida na kelele, nililieleza hili kwa wakubwa wangu msikitini, wakanipatia fedha, nikamfuata mtu wetu Manispaa ya Ilala, akanipatia kibali, sasa mkiniuliza kwa nini najenga barabarani nawashangaa, kwa sababu nina kibali, tena kina muhuri wa manispaa,” alisema.

Kibali hicho ambacho gazeti hili lilikiona, kinaonyesha kilitolewa Julai 10, 1987 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kikiruhusu ujenzi wa ukuta katika viwanja namba 283,284 na 285.

Kibali hicho kwa nyuma kimesainiwa na Mhandisi wa Manispaa ya Ilala Septemba 4, 2007 kikiwa na maelezo kuwa kimeongezwa muda kama mchoro ulivyoidhinishwa.

Nakala nyingine ya kibali hicho ambayo pia ina muhuri wa Mhandisi wa Manispaa ya Ilala, inatoa maelekezo kwa Ofisa Mkaguzi Majengo wa Manispaa ya Ilala, (jina tunalo) kumsaidia Sachejina kwa vile ni maskini sana.

Alipoulizwa kuhusu uhalali wa vibali hivyo, ofisa huyo alisema ana shaka navyo na alitoa vivuli vyake kwa ajili kuvifanyia uchunguzi zaidi.

Alisema mgogoro wa ujenzi wa ukuta katika eneo hili ni wa muda mrefu na ameukuta na aliahidi kufuatilia na kuupatia ufumbuzi.

Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Mohammed Yakub, ambaye alifika eneo hilo akiwa ameandamana na waandishi wa habari, alisema ameshtushwa na vibali hivyo na kwamba suala hilo atalifikisha katika vikao vya juu vya manispaa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema atawaagiza wataalamu wa ardhi wa manispaa kukagua ramani ya eneo hilo ili kubomoa sehemu zote zilizojengwa kinyume cha taratibu.

Kuhusu kauli ya Sachejina kuwa amewaweka baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo mfukoni, alisema hilo pia litajadiliwa katika vikao vya juu. Hata hivyo alishindwa kukutana na Sachejina ambaye alikimbia na kwenda kujificha baada ya kumuona naibu meya.

Alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, John Lubuva, alisema hawezi kulizungumzia suala hili kwa vile yuko safari. Alilitaka gazeti hili kuwasiliana na mtu aliyemwachia ofisi na kumtaja kwa jina moja la Kisisa. Pia alitoa namba ya simu ya mkononi ya ofisa huyo.

Hata simu ilipokewa na mtu mwingine ambaye alikataa kujitambulisha jina lake na kueleza kuwa hamjui Kisisa wala namba iliyopigwa haihusiani na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, bali ni yake binafsi.
 
Back
Top Bottom