BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,117
Karume amkwaza Kikwete
John Bwire, Butiama Aprili 2, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
CUF yadai Kikwete dhaifu, haitashiriki tena majadiliano
Wajumbe NEC Zanzibar wakumbuka ASP yao

WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM/NEC) kutoka Zanzibar, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, wamemkwamisha Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, katika azma yake ya kutibu mpasuko wa kisiasa Zanzibar kupitia Mwafaka na Chama cha Wananchi (CUF), imefahamika.
Karume ambaye aliingia madarakani mwaka 2000 akionekana kuwa mpole kuliko Dk. Salmin Amour, aliyempokea urais, ndiye ambaye amekuwa akikwamisha mambo, na safari hii, katika mkutano wa NEC uliofanyika Butiama dhahiri aliwaongoza wenzake kukwamisha Mwafaka na CUF.
Habari kutoka ndani ya CCM na kutoka kwa watu mbalimbali Bara na Visiwani zinaeleza kwamba hata pale Rais Karume alipotaka kulegeza kamba kuruhusu kukamilika kwa mazungumzo ya Mwafaka, alijikuta akibanwa na wana CCM wenye msimamo mkali kwa upande wa Zanzibar na hivyo kuendeleza ugumu wa kufikiwa kwa Mwafaka kati ya chama hicho na CUF.
Hiyo ni pamoja na ukweli kwamba taarifa ya Kamati ya Mwafaka ya CCM iliyowasilishwa na kupitishwa na Kamati Kuu kwa kufanyiwa marekebisho madogo, inaonyesha kwamba Rais Kikwete na Rais Karume walikuwa wakishirikishwa katika kutoa ushauri kwa kila hatua ya mazungumzo ya Mwafaka na ushauri wao kuzingatiwa na hivyo kukwama kwa Mwafaka huo safari hii kunaibua maswali mengi zaidi ya majibu.
Suala la Mwafaka ndilo lililokuwa likitarajiwa kufikia hatua nzuri katika kikao cha NEC cha Butiama ambacho kilikuwa kianze Ijumaa iliyopita kijijini Butiama, lakini baada ya kufika katika eneo la mkutano wajumbe wake walikabidhiwa makabrasha ya nyaraka za Mwafaka na wakarejea Musoma, umbali wa zaidi ya kilometa 40, kwa maelezo kwamba wapate muda wa kutosha kuyapitia makabrasha hayo kabla ya kukutana siku iliyofuata.
Hali kama hiyo ilijitokeza pia siku iliyofuata baada ya Kamati Kuu kukutana mjini Musoma kwa takriban saa sita na kusababisha kuchelewa kuanza kwa kikao cha NEC kijijini Butiama siku ya Jumamosi, kikao ambacho nacho hakikufanyika kwa maelezo kwamba wajumbe walikua wamechoka na walihitaji kupitia kwanza waraka wa Mwafaka waliokabidhiwa siku hiyo.
Kuchelewa na baadaye kuahirishwa kwa vikao vya Kamati Kuu na NEC kwa sababu zinazofanana, ilikua ni ishara ya kuibuka kwa utata wa mjadala wa mazungumzo ya Mwafaka kati ya CCM na CUF.
Raia Mwema imedokezwa kwamba ni misimamo mikali ya kundi la Zanzibar iliyochelewesha vikao vya Kamati Kuu na NEC na hatimaye kushindikikana kupitishwa kwa mapendekezo ya timu ya wajumbe sita wa CCM katika Kamati ya Mwafaka.
Wajumbe wa CCM katika Kamati ya Mwafaka wanaongozwa na Katibu Mkuu wake, Yussuf Makamba akisaidiwa na Kingunge Ngombale Mwiru ambaye ni Mwenyekiti Mwenza. Wajumbe wengine ni Ali Ameir Mohamed, Zainab Omar Mohamed, Vuai Ali Vuai (Katibu) na Mwanasheria Dk. Masumbuko Lamwai.
Kwa upande wa CUF, wajumbe ni Seif Sharif Hamad (Mwenyekiti), Hamad Rashid Mohamed (Mwenyekiti Mwenza), Juma Duni Haji, Abubakar Khamis Bakary, Ismail Jussa Ladhu (Katibu) na Joram Bashange.
Kabla hata ya kikao cha NEC kuanza kijijini Butiama, wajumbe kutoka Zanzibar ambao baadhi walifika dakika za mwisho kuongeza nguvu, walikua wakiimba nyimbo zilizoashiria kwamba wasingeruhusu mapendekezo ya Mwafaka yenye kulenga kuwa na Serikali ya mseto (shirikishi) kupita. Nyimbo hjizo ni kama: Mapinduzi daima milele na hatutaki mseto, kauli ambazo zilirudiwa pia katika mjadala juu ya Mwafaka ndani ya kikao cha NEC.
Baadhi ya wajumbe walionekana dhahiri kuwa na jazba na wengi walionyesha wazi kutokuwa tayari kushirikiana na CUF wakirejea historia ya kisiasa Zanzibar na wakimtupia lawama Seif Sharif Hamad, wakidai kwamba amekuwa akipotosha historia ya kisiasa Zanzibar.
Raia Mwema imeambiwa kwamba akichangia kwenye mjadala, mjumbe mmoja ambaye yuko karibu na Rais Karume alitaka CUF wamtambue kwanza Karume na kuitambua Serikali yake kabla ya kufikia maamuzi yoyote akieleza kwamba CUF ni chama kinachoendekeza shari na kwamba kuwakubalia CUF ingekuwa ni sawa na kuisaliti Serikali ya Zanzibar aliyosema ilishinda kwa kishindo uchaguzi wa mwaka 2005.
.
Kama tunaambiwa kwamba mazungumzo yalifanyika kwa mtindo wa nipe nikupe sasa tujiulize CUF wametupa nini? Sisi CCM tumeambiwa tunataka kuwapa Serikali yetu. Hivi sasa Zanzibar ya leo si ya zamani, hali ni shwari kabisa wananchi wana matumaini. Hivi Kamati Kuu haitambui mchango wa Rais Karume katika maendeleo ya Zanzibar? Wahenga wamesema heri hutafutwa kwa heri haitafutwi kwa shari. CUF wamtambue Karume na waitambue Serikali yetu, alisema mjumbe huyo.
Mjumbe mwingine akishangiliwa na wenzake, alisema Seif alikwisha kufukuzwa na CCM, hivyo hawezi kushirikiana na chama ambacho kilimfukuza.
Katika kuhalalisha maelezo yake, mjumbe huyo anaelezwa na vyanzo vyetu vya habari akidai kwamba CUF walitoa kauli ya kwamba uchaguzi wa mwaka 2000 ilikuwa mwisho wa serikali ya mtu mweusi, kauli ambayo ilionyesha wazi kuibua hisia za ubaguzi, huku baadhi wakiapa kwamba kama ikibidi itabidi Afro Shiraz Party (ASP), kilichoungana na TANU kuunda CCM, kirejee.
Viongozi wetu mnaijua historia ya Zanzibar? Mnataka kutupeleka wapi? Wenzetu CUF wanasema eti wamekwisha kupata wanachokitaka na kwamba sisi hatuna letu na kwamba wamekwisha kuwaweza wahafidhina Mnaturudisha nyuma, watu hawa wamefika kusema kwamba hata wakipewa utume hawawezi kushirikiana na ASP kwa hiyo hawa watu hawatashirikiana na CCM Nasema hapa hakuna cha Serikali ya mseto wala nini, alisema mjumbe mmoja wa Zanzibar.
Kwa kiasi kikubwa wajumbe kutoka Zanzibar walionekana wazi kushikilia karata ya kukumbushia ASP ikiwa ni ishara kwamba wanataka kuachiwa kuamua mambo yao wenyewe yanayohusu siasa za Visiwani na wengi walihoji ushirikishwaji wa Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, ambayo walisisitiza ipewe nafasi ya kujadili na kufanya maamuzi kabla ya kujadiliwa na pande zote.
Baada ya mwelekeo kuonekana wazi kuwa wajumbe wengi waliochangia hawakutaka kabisa kujadili taarifa ya mazungumzo ya Mwafaka, Mwenyekiti wa CCM Kikwete, alilazimika kutoa maelezo ya ziada kuwataka wajumbe kujadili yaliyomo katika taarifa hiyo ikiwamo muundo wa serikali ya pamoja.
Habari zinasema kwamba Rais Kikwete aliwaeleza wajumbe wazi kwamba hata kama wakiamua kupeleka suala hilo kwa wananchi ni lazima wawe na jambo wanalopelekewa na akasisitiza kujadiliwa kwa waraka huo na kutoa mapendekezo kabla ya kuyafikisha kwa wananchi.
Hata kule kwa wananchi si kuna jambo utakalolipeleka? Si ndilo hili? Sasa kwa mazungumzo haya yalikuja na mapendekezo, tunachotakiwa ni kutizama haya mapendekezo na katika haya tujadili haya yaliyopendekezwa na Kamati Kuu, haya ambayo tumeyarekebisha na yale tuliyoyakataa tunawatuma (wajumbe wa kamati ya Mwafaka) wakawaambie wenzao (CUF), alisema Rais Kikwete kama alivyokaririwa na vyanzo kadhaa vya habari.
Rais Kikwete alisema baada ya majadiliano uamuzi wowote utakaotolewa utapelekwa katika vikao vya CCM upande wa Zanzibar ikiwamo Kamati Maalumu ya NEC na baadaye kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.
Katika kujaribu kuwakumbusha, Rais Kikwete alisema yanayojadiliwa katika Mwafaka wa sasa ni yale yale yaliyojadiliwa na kusainiwa mwaka 2001 ikiwamo uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya pamoja huku akirejea yaliyopitishwa na Kamati Kuu ikiwamo muundo wa serikali shirikishi.
Hata hivyo, wajumbe kutoka Zanzibar, wanadaiwa waliendelea kujadili kwa jazba hoja hiyo na wengi wakielekeza mashambulizi yao kwa Seif Sharif Hamad.
Mjumbe mmoja mwanamke alisema CUF imekwisha kupoteza mwelekeo, ni sawa na mgonjwa mahututi na kwamba kukubali serikali ya mseto ni sawa na kumrudishia uhai akisisitiza: hili suala la serikali shirikishi au sijui serikali ya mseto wananchi wa Zanzibar hawalitaki kabisa.
Baada ya kikao hicho kumalizika huku viongozi wote wa juu wa CCM wakionekana kuchoka kutokana na ugumu wa vikao vyote viwili vya Kamati Kuu na NEC, lilitolewa tamko kuonyesha kwamba waraka wa Mwafaka unahitaji kufanyiwa marekebisho ambayo hayakutajwa bayana na baadaye kuitishwe kura ya maoni.
Akisoma maazimio ya NEC, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, alisema wajumbe wote wamekubali kimsingi mapendekezo ya kamati ya mazungumzo lakini wametaka kufanyika kwa marekebisho katika mambo kadhaa na baadaye kuwashirikisha wananchi kupitia kura ya maoni.
Katika mapendekezo ya kamati ya Mwafaka yaliyopitishwa na Kamati Kuu, ilipendekezwa kuwapo kwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais itakayochukuliwa na chama cha upinzani kitakachokua kimepata kura nyingi za urais na Makamu wa Pili wa Rais angeteuliwa na Rais Mtendaji kutoka katika chama chake.
Uteuzi wa Baraza la Mawaziri unaelezwa kufanywa na Rais Mtendaji kwa uwiano wa matokeo ya uchaguzi baada ya kushauriana na wakuu wa vyama husika na kwamba vyama husika vitashiriki katika Baraza la Mawaziri iwapo tu vitapata zaidi ya asilimia tano ya kura za Rais.
Katika kutatua tofauti ambazo zinaweza kutokea ndani ya serikali ya pamoja, imependekezwa kuundwa kwa Baraza la Usuluhishi na pia serikali hiyo shirikishi ya kitaifa ingetokana na uchaguzi mkuu ulio huru na wa haki kwa nia ya kupata viongozi watakaopatikana kidemokrasia.
Mazungumzo kati ya CCM na CUF yalilenga kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar, kama alivyoahidi Rais Kikwete katika vikao mbalimbali na ndani na nje ya CCM, ikiwamo siku alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza mjini Dodoma mapema mwaka 2006.
Baada ya tamko hilo la CCM kuhusu Mwafaka yamekuwapo maoni kwamba kilichofanyika ni kuahirisha tu tatizo na kwamba katika mazingira ya siasa za leo, Zanzibar haiyatulia mpaka kuwe na serikali ya mseto.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Joseph Warioba ameiambia Raia Mwema katika mahojiano juu ya hatua hiyo kwamba tatizo analoliona yeye ni kwamba viongozi hawataki kuwajibika ili kumaliza mpasuko wa Zanzibar.
Alisema Warioba: Kama wamekubali waendelee kuboresha ni jambo zuri kwa sababu ni lazima waelewane vizuri ili kuwa na utekelezaji mzuri.
Lakini jambo hili limechukua muda mrefu na katika muda huo mpasuko nao umekuwa ukiimarika. Sasa kuna haja bada ya muda wote huo kufikia maamuzi.
Alisema hata hivyo kwamba hatua ya kupeleka suala hilo kwa wananchi itakuwa ni sawa na kufanya uchaguzi mwingine, na kwa maana ya chaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika Zanzibar, matokeo yatakuwa ni yaleyale.
Chanzo cha mpasuko wa Zanzibar ni uchaguzi. Ukilipeleka tena kwa wananchi utapata matokeo yaleyale na mpasuko utakuwa mkubwa zaidi, isipokuwa kama vyama vyote husika vitahimiza wananchi wakubali mseto. Ukweli hili si suala ambalo unahitaji kura ya maoni. Ni suala lililo ndani ya uwezo wa viongozio kulimaliza.
Kusema unalirudisha kwa wananchi, kuwatupia wananchi waliamue ni kushindwa kwa viongozi kufanya maamuzi yaliyo ndani ya uwezo wao. Matatizo ya aina hii hutatuliwa na viongozi kwa niaba ya umma.
Madhumuni hapa ni kupigania umoja wa wananchi. Na mifano ya aina hii duniani iko. ANC cha Afrika Kusini tangu wka 1994 kimekuwa kinapata viti vingi bungeni. Katika uchaguzi uliopita kilipata zaidi ya theluthi mbili, lakini wakati wote kimekuwa kikiunda serikali ya umoja wa kitaifa. Madhumuni ni kuwaunganisha raia baada ya siasa za ubaguzi.
Lakini mfano wa karibuni zaidi ni wa Kenya. Zote Kenya na Zanzibar zina matatizo yanayotokana na uchaguzi. Kwa juhudi za Umoja wa Afrika wamekubaliana kuunda serikali ya pamoja ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kubwa kwa upinzani.
Japo matatizo hayajaisha, makubaliano yale yanafanya nchi itulie. Bila hivyo Kenya ingekuwa pabaya. Na Rais Jakaya amesaidia sana Kenya. Kama tunaweza kusaidia nchi jirani kupata suluhisho kwa nini sisi tunashindwa? Tofauti zetu si za kiitikadi, ni za kikabila, kuna Unguja na Pemba. Hatutaweza kumaliza tofauti hizo kama viongozi hawashirikiani, alisema Jaji Warioba.
Imani yangu ni kwamba serikali ya mseto ingesaidia sana na hasa kama tungefikia makubaliano kabla ya 2010, vinginevyo matatizo haya yatakuwa makubwa zaidi, alisema Warioba.
Wakati huo huo Aristariko Konga anaripoti kutoka mjini Dar es Salaam kwamba Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, amesema kuwa hatua ya CCM kuweka masharti mapya nje ya makubaliano ya mwafaka kinaonyesha mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, amekuwa akifanya usanii wa kisiasa au ni kiongozi dhaifu asiye na udhibiti na chama chake.
CUF imevunjwa moyo sana na Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM. Imani tuliyokuwa nayo kwake kama kiongozi wa nchi na ambayo tulibaki nayo hadi CCM inaelekea katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa imetetereka sana, alisema Seif.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam, ili kujibu tamko la Halmashauri Kuu ya CCM, iliyoketi Butiama kuhusu marekebisho mapya ya mwafaka baina ya vyama hivyo viwili kuhusu mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Kitendo cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, chini ya uenyekiti wake, kukataa kupitisha makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya CCM na CUF, na badala yake kuja na hoja mpya za ajabu ajabu, zenye lengo la kuipiku CUF kisiasa, kinamwonyesha Rais Kikwete ama hakuwa mkweli na mwaminifu tokea mwanzoni.
Kwamba alikuwa akifanya usanii wa kisiasa wakati alipotangaza kuwa anasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa Zanzibar, au ni kiongozi dhaifu asiye na udhibiti wa chama anachokiongoza. Yote mawili hayampi sifa za kuwa kiongozi ambaye nchi inamhitaji inapopita katika vipindi vigumu, alisema Seif, ambaye ndiye aliongoza ujumbe wa CUF katika mazungumzo ya mwafaka.
Seif alisema kwamba ni bahati mbaya Rais Kikwete ameyaangusha matumaini ya Watanzania kama ambavyo ameyaangusha matumaini yao katika masuala mengine yote aliyowaahidi wakati anaomba kura na kuingia madarakani.
Maeneo ambayo CUF inaona kwamba CCM imefanya usanii wa kisiasa ni pamoja na CCM kutamka kuyakubali kimsingi mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati ya chama hicho, inayoshiriki mazungumzo, lakini wakati huo inazungumzia marekebisho ambayo inataka yafanywe na hivyo kuiagiza kamati yake kukutana na wajumbe wa CUF, ili kujadilimarekebisho hayo.
Kwanza, CCM haikutaja ni maeneo gani yafanyiwe marekebisho. Pili hoja hii inashangaza kwa sababu wajumbe wa kamati ya mazungumzo kutoka upande wa CCM walikuwa wakiwaarifu wajumbe wa kamati kutoka upande wa CUF, kwamba wao walikuwa wakiwasilisha taarifa kwa kila hatua, inayofikiwa katika vikao vya chama, vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na pia kwa viongozi wao wa juu, Rais Jakaya Kikwete na Amani Karume, alisema.
Hoja nyingine inayolalamikiwa na CUF, ni kwamba CCM imekuja na hoja mpya kwamba iwapo mapendekezo haya yatakubaliwa, yatakuwa yanaleta mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala kwa Zanzibar na hivyo yanapaswa kuridhiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya kura ya maoni.
CCM kuleta hoja hii ni kulifanyia mzaha jambo kubwa linalohitaji umakini wa hali ya juu kwani linagusa mustakabali wa taifa letu. Muda wote wa mazungumzo ambayo yamechukua miezi 14 na yakiwa yamehusisha vikao 21, wajumbe wa kamati ya CCM hawakuleta hoja hii ya kura ya maoni.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa, tofauti na ilivyoelezwa, pendekezo la kutaka kura ya maoni halikuwa limeibuliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, bali lilikuwemo katika taarifa ya Kamati ya CCM likiwa ni pendekezo walilotaka liridhiwe. Hivyo, ni wazi liliandaliwa mapema kutokana na kile ilichokiita kuipiku CUF katika ubunifu wa kujenga, alisema Seif.
Wasiwasi wa CUF pia upo kwenye vyombo ambavyo vitaendesha kura ya maoni na utaratibu wake, kwa kuwa CCM na CUF tayari wamekubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vina matatizo ya msingi, ambayo yanahitaji kurekebishwa.
Kutokana na hali hiyo, Seif akiwa na wajumbe wengine wa Kamati ya Mwafaka ya CUF, alitangaza kwamba chama chake hakiko tayari kushirikiana na CCM kuwafanyia Watanzania usanii wa kisiasa, na kwamba hawatakuwa tayari kurejea katika mazungumzo kwa utaratibu inaoutaka CCM.