Karibu Kwenye Chuo Kikuu Kinachotembea (University On Wheels), jifunze popote ulipo

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Moja ya hitaji la msingi sana kwenye maisha yako, kama unataka kuishi maisha bora na ya mafanikio ni kujifunza. Na kujifunza huku sio kama kule kwa shuleni kwamba ukishahitimu unaweka vitabu pembeni, badala yake unahitaji kujifunza kila siku, yaani KILA SIKU.

Unahitaji kujifunza kila siku katika maeneo mbalimbali ya maisha yako, ikianzia kuhusu kuongeza ubora kwenye kazi au biashara yako, kuboresha maisha yako binafsi, kuwa na mtizamo chanya, kushawishi na mengine mengi ambayo ni muhimu sana kwenye maisha ya mafanikio.

Lakini changamoto inakuja moja, sina muda wa kujifunza kila siku, ratiba zangu zimebana sana, kazi au biashara zangu zinanichukua muda mrefu wa siku, nikitoka nimechoka na siwezi kushika kitabu nisome. Hii ni sababu ambayo imewafanya wengi kushindwa kujijengea tabia ya kujifunza kila siku.

Leo nina habari njema kwako, ya kwamba licha ya kukosa muda wa kukaa na kusoma kitabu, bado unaweza kujifunza kila siku, tena kwa muda w akutosha tu. Na habari hii njema ni kuhusu kujiunga na CHUO KIKUU KINACHOTEMBEA, yaani ulipo na chuo chako kipi.

Chuo kikuu kinachotembea ni nini?

Kama unakaa maeneo ya mijini, na nina hakika wengi hapa tunakaa maeneo hayo, usafiri kwenda kwenye shughuli zako mbalimbali ni kitu ambacho unafanya kila siku, au karibu kila siku. Mimi binafsi natumia muda usiopungua masaa mawili kwenye usafiri, kila siku, hasa siku za wiki. Asubuhi naendesha gari kwa muda usiopungua saa moja, na jioni naendesha muda usiopungua saa moja. Na siku nyingine uwepo wa foleni ndefu naweza kukaa barabarani hata masaa mawili au matatu kwa safari moja tu ya kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.

Huu ni muda ambao ungeweza kuwa unapotea bila ya kufanya chochote, au kama ukiamua kuutumia Kitanzania basi utaishia kumlaumu kila unayeweza kumlaumu kuhusu uwepo wa foleni ndefu. Lakini hilo halitakusaidia kwa sababu bado utaendelea kuwa kwenye foleni, na sio siku hiyo tu, na kesho yake tena na tena.

Badala ya kulalamikia muda unaopoteza kwenye foleni wakati unatoka sehemu moja kwenda nyingine, iwe kwenye usafiri wako binafsi au usafiri wa umma, unaweza kugeuza muda huu kuwa muda wa kujifunza. Na hapa ndio dhana ya CHUO KIKUU KINACHOTEMBEA inapokuja.

Unajifunzaje wakati upo kwenye usafiri?

Kushika kitabu na kuanza kusoma inaweza isiwe rahisi sana, hasa kama wewe ndio unaendesha usafiri binafsi, au umepanda kwenye usafiri wa umma ambao umejaza watu wengi na huenda wewe mwenyewe umesimama. Hivyo njia bora kabisa ya kujifunza katika hali hizi ni kusikiliza vitabu vilivyo somwa, kwa kiingereza vinajulikana kama AUDIO BOOKS.

Audio books hivi ni vitabu ambavyo vimesomwa na unachofanya wewe ni kusikiliza tu. Uzuri wa Audio books ni kwamba unaweza kusikiliza popote pale ulipo, kama unaendesha unaweka kwenye redio yako ya gari, kama upo kwenye daladala unaweka kwenye simu yako na unasikiliza kwa spika za masikioni, kama upo nyumbani unaweza kuweka kwenye redio au kompyuta na kama unafanya mazoezi unaweza kuweka kwenye kitu cha kusikilizia masikioni. Uzuri ni kwamba unaendelea na kile unachofanya na huku ukiendelea kupata maarifa mbalimbali ya kufanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Kwa mtu ambaye unaenda kwenye shughuli zako za kila siku kwa usafiri, kama ukijiwekea utaratibu wa kusikiliza kila siku, utashangaa baada ya muda mtazamo wako unabadilika kabisa. Utashangaa unaanza kuziona fursa zaidi, unapata hamasa ya kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya. Na pia utaanza kupata maarifa zaidi ya kufanikiwa kwenye kazi au biashara. Haya yatategemea na vitabu gani unasikiliza katika muda wako.

Na ili kujijengea tabia nzuri ya kujifunza kwa kusikiliza vitabu, jiwekee utaratibu kwamba unapopata dakika zaidi ya kumi za kusubiri kitu, basi sikiliza kitabu, na unapoingia kwenye chombo cha usafiri iwe binafsi au cha umma, sikiliza kitabu. Mimi nimejiwekea utaratibu nikiwasha tu gari basi kitabu kinaendelea kusomwa. Kwa njia hii sisikilizi kitu kingine kwenye gari zaidi ya vitabu.
Kwa taarifa zaidi kuhusu AUDIO BOOKS, bonyeza maandishi haya.
Nakutakia kila la kheri katika kutumia muda kujifunza zaidi.
TUPO PAMOJA.
 
Mkuu nashukuru kwa ushauri mzuri wa kujiongezea maarifa kwa kadri tupatapo wasaa...Nitoke nje ya mada kidogo ni jinsi gani naweza ku-access uchambuzi wa vitabu unaoufanya na je ni free ama kuna michango?
 
Back
Top Bottom