Kardinali Pengo, JPM waliteta jambo gani?

HNIC

JF-Expert Member
Sep 6, 2011
1,898
2,195
Magufuli.jpg


Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amedokeza sehemu ya mazungumzo yake na Rais John Magufuli, yanayoonyesha mkuu huyo wa nchi anapitia katika kipindi kigumu hivi sasa.

Kadinali Pengo alidokeza hayo juzi wakati wa misa maalumu ya kumuombea aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Sokoine iliyofanyika kwenye kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye misa hiyo, Kardinali Pengo alisema waliwasiliana na Dk Magufuli kwa simu wakati akiwa mapumzikoni Chato mkoani Geita na Rais alimueleza maneno ambayo yanaonyesha kuwa kazi ya urais si rahisi, na jinsi kiongozi huyo wa kiroho alivyompa moyo.

“Sijui ni vizuri nikisema Mheshimiwa Rais, lakini kwa vile uliyataja maneno hayohayo hata kule Chato. Napenda kusema yale uliyosema kwangu binafsi kwa njia ya simu,” alisema Kadinali Pengo.

“Ulisema ‘ningelijua kwamba kuwa Rais ndiyo hivi, wala nisingeligombea urais’ … na mimi nilisema afadhali mtu mmoja afe kuliko Taifa liteketee. Kwa hiyo endelea mbele.”

Kadinali Pengo, aliyeonekana awali kusita kuweka bayana mazungumzo hayo, alisema kwa kuwa Rais Magufuli alishaeleza hayo akiwa Chato, basi angependa aeleze sehemu ya mambo aliyowahi kuzungumza naye kwa simu.

Ingawa Kadinali Pengo hakueleza kile alichozungumza Rais akiwa Geita, Dk Magufuli amekuwa akieleza jinsi kazi ya urais ilivyo ngumu na kila mara kuomba wananchi wamuombee na kumsaidia kutekeleza majukumu yake.

Akiwa kwenye ibada iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria, Parokia ya Chato, Rais aliwataka Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.

“Niwaombe Watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana kwa umoja wetu na siku zote tumtangulize Mungu mbele. Wakati tunaadhimisha wiki moja baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo,” alisema Rais Magufuli katika ibada hiyo.

“Yesu Kristo alikufa kwa sababu ya dhambi zetu. Sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane.”

Hata hivyo, haijaeleweka mazungumzo hayo baina ya Rais na mtumishi huyo wa Mungu yalifikia hatua gani kiasi cha Kadinali Pengo kumtuliza kwa kumwambia “ni afadhali mtu mmoja afe kuliko Taifa zima liteketee”.

Akiwa Chato, Rais Magufuli pia alitangaza kwamba atapunguza mishahara ya watendaji wakuu wote wa Serikali wanaolipwa hadi Sh40 milioni, akisema chini ya utawala wake hakuna mtu atakayelipwa zaidi ya Sh15 milioni.

Rais Magufuli amejikita katika kupambana na ufisadi, ukwepaji kodi, matumizi mabaya ya fedha za umma, uzembe na wizi, huku akisimamisha kazi, kutengua uteuzi na kutimua watumishi wa umma wanaotuhumiwa au kujihusisha na wizi wa fedha za umma.

Zaidi ya watumishi 160 wa umma wameshasimamishwa au kutenguliwa uteuzi wao tangu Rais Magufuli aapishwe Novemba 5, 2015, huku akinasa wafanyabiashara wakubwa na wadogo waliokuwa wakipitisha bidhaa bandarini bila ya kulipa kodi na ushuru.

Kadinali Pengo alitoa dokezo hilo siku ya kukumbuka kifo cha Sokoine, ambaye amejijengea sifa ya kuwa mpambanaji katika vita dhidi ya uhujumu uchumi, uvivu, wizi wa fedha za umma na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

Alieleza katika misa hiyo kuwa watu wanamfananisha Rais Magufuli na waziri mkuu huyo wa tatu tangu nchi ipate uhuru.

Alisema kuna ming’ono kuwa sura ya Rais Magufuli inafanana na ya Sokoine, akisema maneno mengi ya mtaani ni ya ukweli zaidi ya yale yanayoandikwa na vyombo vya habari.

Sasa kadinali anataka nani afe? Mbona hajatoa list ya hao wanaotakiwa kufa?


Chanzo:
Mwananchi
 
Kadinali Pengo aliongea kiroho zaidi kuliko kimwili.

Yohana 11:50

47 kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. 48 Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!" 49 Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu! 50 Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?" 51 Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao; 52 na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika. 53 Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu.
 
Back
Top Bottom