Karamagi na wanasheria wake watupiana mpira kuhusu tuhuma za ufisadi.

Lawson

Member
Sep 25, 2007
69
4
Waziri aliyetuhumiwa ufisadi adai fidia ya Sh10bilioni

Muhibu Said said:


WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ametoa siku mbili kwa Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, wamwombe radhi na kumlipa Sh10 bilioni zikiwa ni fidia ya kuchafuliwa jina kwa kuhusishwa na ufisadi. Hata hivyo, kumbukumbu za notisi ya kusudio la kufungua mashtaka iliyoandikwa na mawakili wa Kampuni ya FK Law Chambers ya jijini Dar es Salaam wanaomwakilisha Waziri Karamagi, zinaonyesha kuwa muda ambao waziri huyo ametaka aombwe radhi na Dk Slaa na Lissu ulishapita tangu Septemba 26, wakati ule wa kulipwa kiasi hicho cha fedha uliisha Oktoba Mosi, mwaka huu.

Notisi hiyo yenye Kumbukumbu Na. FK/CF/NMK/DN/, iliyosainiwa na mwanasheria wa kampuni hiyo, Joseph Ndazi, iliandikwa Septemba 24, mwaka huu na kumtaka Dk Slaa na Lissu kuomba radhi kwa maandishi ndani ya siku mbili na kumlipa kiasi hicho cha fedha ndani ya siku saba, kuanzia tarehe ya notisi hiyo.

Mbali na kuwataka kutekeleza mambo hayo, mawakili hao wamewataka Dk Slaa na Lissu katika notisi hiyo, kukiri kwamba tuhuma walizozitoa dhidi ya mteja wao hazikuwa sahihi na hazikuwa na ukweli wowote na wakiri hivyo kwa kuchapisha kwenye magazeti yenye mtandao mkubwa wa usambazaji. Pia watoe ahadi ya maandishi kwenye magazeti kwamba, wataacha mara moja kuchapisha taarifa zenye maneno yasiyokuwa ya kweli au yenye kashfa dhidi ya Karamagi, familia na washirika wake na walipe Sh10 bilioni kwake, au kupitia kwa mawakili wake, kama fidia ya madhara yote waliyomsababishia mteja wao.

Vilevile, mawakili hao wamemtaka Dk Slaa na Lissu wamlipe Karamagi gharama zote ambazo tayari ameshaingia na anazotazamia kuingia kuhusiana na suala hilo. "Kwa vile (Dk Slaa na Lissu) wamezungumza mambo yanayohusu jinai dhidi ya mteja wetu ambayo si sahihi na ya kweli, mteja wetu anayo haki ya kufungua malalamiko ya jinai dhidi yao katika vyombo vinavyohusika," ilieleza sehemu ya notisi hiyo ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Mawakili hao wamedai kuwa kutokana na Dk Slaa na Lissu kutaja hadharani tuhuma hizo dhidi yake (Karamagi), wamemsababishia madhara mbalimbali, ikiwamo kudhoofisha heshima yake ya kitaaluma na nafasi yake ya kisiasa kwa viongozi wa serikali ya Tanzania na wa kisiasa, maafisa wa ngazi za juu wa serikali, marafiki, washirika wake na jamii kwa ujumla.

Wamedai pia wamesababisha aonekane vibaya kwa washirika wake wa ndani na nje ya nchi ambao sasa wanamkwepa. "Kutokana na madhara waliyomsababishia mteja wetu, katika muda usiozidi siku mbili, kuanzia Septemba 24, wamwandikie barua ya kumwomba msamaha, pia wamwandikie barua ya kukiri kwamba tuhuma walizozitoa dhidi ya mteja wetu hazikuwa sahihi na hazikuwa na ukweli wowote na wakiri hivyo kwa kuchapisha kwenye magazeti yenye mtandao mkubwa wa usambazaji.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake juzi, Lissu alisema notisi hiyo aliipata juzi na kusema kuwa: "Kwa vile nimeiona leo (Oktoba 9, 2007) na barua yenyewe ni ya Septemba 24 ni wazi nimeshachelewa sana kutekeleza yale ambayo huyu bwana (Karamagi) anadai niyafanye. Na mpaka sasa hivi sijaletewa hati yoyote ya madai".

Walipoulizwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wanasheria wa FK Law Chambers, kila mmoja alimtupia mpira mwenzake na mwisho suala hilo wakalirudisha kwa Karamagi wakimtaka mwandishi amuulize iwapo kuna hatua zozote ambazo zimekwishachukuliwa tangu wawaandikie notisi hiyo Dk Slaa na Lissu.

Ndazi alikiri kusaini notisi hiyo, lakini akakataa kuzungumzia suala hilo na kumtaka mwandishi awasiliane na mwanasheria mwenzake wa kampuni hiyo, Profesa Luoga. Hata hivyo, Profesa Luoga alitoa udhuru kwamba, muda mrefu hayuko ofisini, hivyo, hafahamu kinachoendelea na kumtaka mwandishi awasiliane na mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Danka, akisema kwamba ndiye anayeshughulikia suala hilo.

Danka alipoulizwa alikataa badala yake alimtaka mwandishi akamuulize Waziri Karamagi kwa kuwa ndiye mhusika mkuu wa suala hilo. Naye Waziri Karamagi alipoulizwa alikataa kuzungumzia suala hilo, akisema kwamba yeye si mwanasheria na kusema kwamba wanaopaswa kuulizwa suala hilo ni wanasheria wanaoshughulikia suala hilo.

"Waulize wao wenyewe, mimi siyo lawyer (mwanasheria), wao ndio wanaojua" alisema Karamagi ambaye alipoelezwa na mwandishi kuwa wanasheria hao ndio walioelekeza aulizwe yeye, alimtaka awaambie wanasheria hao kuwa wamweleze kinachoendelea. Kwa upande wake, Dk Slaa, ametoa msimamo akisema hawezi kuomba radhi wala kulipa fidia na kuwataka watuhumiwa kwenda mahakamani. Akizungumza juzi usiku kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA), Dk Slaa alisema hawezi kufanya hivyo na kwamba ni vema watuhumiwa waende mahakamani.

Dk Slaa alifafanua kwamba, kabla ya kuibua tuhuma hizo walikaa wakazifanyia kazi kwa kina na mapana na kusisitiza kwamba wana ushahidi. "Kabla ya kuibua tuhuma hizi, nilikaa na wenzangu tukazifanyia kazi kwa kina, sasa kama kuna watu wamekwenda mahakamani ni vizuri, suala sijui la kuomba radhi, hilo kamwe siwezi kulifanya," alisisitiza msimamo wake.

Alisema kama ni kuomba radhi yeye anaweza kufanya hivyo kwa wananchi tu, lakini si mtu ambaye anajua ana tuhuma ambazo zina ushahidi. "Kama ni kuomba radhi labda kwa wananchi tu, lakini siwezi kumwomba radhi mtu ambaye najua ana tuhuma," alisema.
Dk Slaa akitoa msimamo huo wa kupinga kuomba radhi kwa Karamagi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Gray Mgonja, naye amezidi kumng'ang'ania akisema mawakili wake wako katika hatua za kukamilisha taratibu kuona namna ya kufungua kesi hiyo.

Mgonja aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kwamba, kamwe hawezi kubadili msimamo huo na kwamba lazima amburuze Dk Slaa mahakamani. Alisema mawakili wake wanapaswa kupitia kwa kina tuhuma hizo, ili waone namna watakavyoweza kufungua kesi itakayokuwa na mafanikio. Mgonja alipoulizwa vipi mawakili hao wanachukua muda mrefu wakati yeye ana uhakika tuhuma hizo ni za uongo, alijibu: "Mimi ndiyo nina uhakika ni tuhuma za uongo, lakini wao wanapaswa kujiridhisha kwa kupitia kwa makini tuhuma zenyewe".

Alipoulizwa tena kuhusu ushauri wa Jaji Mark Bomani, kutaka tuhuma hizo ziishie nje ya mahakama, alisema: "Huo ni ushauri, hata upande wa kwanza (yaani wa Dk Slaa), aliutoa kwamba zilikuwa ni za jumla mno, nimeupokea lakini msimamo wangu uko pale pale". Dk Slaa ambaye yuko Marekani alitoa msimamo wake wa kwamba watuhumiwa wanapaswa kuendelea na kesi mahakamani, leo usiku Dk Slaa anatarajiwa kufanya mahojiano maalumu katika kipindi maalum cha Sauti ya Amerika ambayo yatatangazwa moja kwa moja.

Source:Mwananchi 10/10/07
 
Mwaka huu tutaona na kusikia mengi . Wao waende tu Mahakamani tujue ukweli kwa upande wao maana kwa Slaa kila kitu kiko wazi .
 
Hawa MAFISADI wamefikia wapi na kwenda mahakamani? Jamani walioko karibu na hao wanasheria tunaomba waendelee kuuliza kulikoni miezi inakwenda bila kumaliza kuandaa mashitaka?
 
HILI NI GAZETI LA SIKU MINGI SANA. Naona Muhibu hakuona majadiliano yaliyokwisha fanyika humu ndani ya JF kuhusiana na hii mada!
 
Back
Top Bottom