Kanuni za msingi kuelekea uandikaji wa Katiba Mpya ya Tanzania tuitakayo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kanuni za msingi kuelekea uandikaji wa Katiba Mpya ya Tanzania tuitakayo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Apr 6, 2011.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Apr 6, 2011
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  KANUNI ZA MSINGI KUELEKEA KATIBA MPYA

  Na. M. M. Mwanakijiji

  Ili kuweza kufikia Katiba Mpya itakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya vizazi vya Watanzania ni lazima kuhakikisha kuwa mchakato wa kufikia katiba huo unakuwa huru, wa wazi na ambao una uhalali wa kutosha kuweza kufikia kusema kuwa Katiba itakayopatikana kweli imetokana na watu.

  Ni muhimu basi kuweka bayana mambo ya msingi ambayo yanaendana na mchakato mzima utakaosababisha Watanzania wafikie katiba Mpya. Ni mambo haya ndio yanahitajika kuonekana kwenye sheria itakayosimamia mchakato wa kufikia Katiba Mpya.

  LENGO: Kupatikana kwa Katiba Mpya ya Taifa la Tanzania itakayokidhi mahitaji mbalimbali ya kisiasa na kiutawala na ambayo itatokana na utashi, nia, matamanio, kiu, njozi na matarajio ya Watanzania. Katiba hiyo inatakiwa ipatikane kabla ya kufika mwaka 2015 ili kuhakikisha kuwa chaguzi za serikali za Mitaa za Mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa 2015 vyote vinafanyika chini ya Katiba Mpya.

  UTOFAUTI WA MCHAKATO WA TANZANIA KUJIANDIKIA KATIBA MPYA
  Jambo la kwanza la msingi ambalo tunahitaji kulitambua ni kuwa kwa Tanzania kuamua kuandika Katiba Mpya wakati huu ni jambo ambalo ni tofauti sana na nchi au jamii nyingine za watu ambazo zimewahi kufanya hivyo. Nchi nyingi zimelazimika kuandika Katiba Mpya kutokana na sababu ambazo kwa Tanzania hazipo kwa kiasi kikubwa. Kimsingi baadhi ya mabadiliko tunayoyataka yangeweza kabisa kufanyika kwa kufanya mabadiliko ya Katiba kama tulivyowahi kufanya huko nyuma lakini tumeamua kuandika Katiba mpya kwa namna ambayo naweza kusema ni ya kipekee sana duniani.

  Hatuanzii kutoka kwenye sifuri.
  Taifa letu linapoamua kuandika Katiba Mpya hatuanzii kwenye sifuri. Si kwamba hatujawahi kuwa na Katiba au hata kuwa na Katiba yetu. Kwa miaka karibu hamsini serikali zote mbili zimekuwa zikiongozwa na Katiba na hivyo suala la "katiba" siyo jambo geni. Jambo hili ni muhimu kulizamisha moyoni kwa sababu kwa vile hatuanzii kwenye sifuri ina maana ya kuwa mchakato wenyewe kimsingi hauitaji muda mrefu sana.

  Ndio maana kinyume na watu wengine wanaotaka elimu ya muda mrefu ya "katiba" ifanyika wanachukulia kana kwamba Watanzania hawajawahi kabisa kusikia Katiba au hawajui umuhimu wa Katiba. Wanafunzi wetu katika ngazi mbalimbali wamejifunza kuhusu Katiba na wanajua umuhimu wake. Kufikiria kwamba tunaenda kwa Watanzania wakiwa hawaelewi lolote ni dharau kwa Watanzania.

  Watu ambao wamekuwa wakipiga kura, wakishiriki nafasi za uongozi na wakiandika katiba za taasisi zao mbalimbali hadi vijijini kuchukuliwa kuwa hawaelewi maana ya "katiba" au "umuhimu wa Katiba" ni kejeli dhidi ya uelewa wa Watanzania na tunaweza kuona kama ni dharau ya wazi. Watanznaia wanafahamu maana ya Katiba na wamekuwa tayari kwa miaka karibu ishirini kuanza mchakato huu.

  Hatuanzii kutoka kwenye vurugu
  Nchi nyingi ambazo zimelazimika kuandika Katiba Mpya zimejikuta zikiffanya hivyo zikiwa zinatoka kwenye vurugu za kisiasa na hasa vita na udhalimu. Nchi kama Eritrea na nchi kama Marekani zilijikuta zinaandika Katiba zao zikiwa zinatoka katika vurugu na vita. Hili ni kweli pia kwa baadhi ya nchi ambazo zimekuwa katika mazingira hayo.

  Hatuanzii kama tunaotoka katika ukoloni au utawala usio halali
  Nchi kama Afrika ya Kusini au nchi nyingi ambazo zimetoka kwenye utawala usio halali zimejikuta zikilazimika kuandika Katiba Mpya ili kuakisi ukweli mpya wa kihistoria katika nchi hizo.

  Kwa msingi huo ni wazi kutambua kuwa tunapotaka kuandika Katiba Hii mpya tunakuja kama Taifa ambalo limefikia mahali pa kukomaa. Kama ni kuchukulia mfano wa familia ni kuwa katiba zetu za awali za tangu baada ya Uhuru na Muungano ni katiba ambazo zilikuwa za kutusaidia kuweza kupita katika maisha ya utoto na ujana na hivyo hata makosa yaliyofanyika wakati huo ni sehemu ya makuzi kama taifa.

  Sasa hivi taifa letu limefikia ujana na sasa liko tayari kutoka nyumbani kwa wazazi na kuwa taifa huru zaidi na lenye kuwajibika zaidi na ambalo liko tayari kushika majukumu makubwa zaidi. Hivyo, Katiba yetu mpya tunayotaka kuiandika ni sehemu ya kujieleza kwetu (self expression) kama taifa miaka ya kuelekea utu uzima. Hivyo, basi ni lazima mfumo mzima wa kuelekea uandishi huo wa Katiba Mpya uwe unaakisi ukweli huu kuwa Watanzania wanataka Katiba Mpya ambayo itawakilisha maisha ya Taifa kuelekea mbele zaidi na kuweza kuacha urithi mzuri wa kizazi kijacho.

  Kutokana na hilo basi mchakato wa kufikia Katiba Mpya unapaswa kuongozwa na

  • Kanuni za Msingi za Kuandika Katiba Mpya
  • Mgawanyo wa Mchakato ili kuhakikisha mawazo na mipango inatekelezwa ipasavyo.
  • Vyombo huru vitakavyosimamia mchakato huo

  KANUNI ZA MSINGI ZA KUANDIKA KATIBA MPYA
  Ili kuweza kufikia Katiba Mpya ni muhimu kuongozwa na kanuni za msingi ambazo zitaanishwa na kuonekana vizuri katika sheria itakayosimamia mchakato huo wa kuandika Katiba Mpya. Pasipo kuwa na kanuni za msingi ambazo zitaongoza mchakato mzima ni vigumu kuwa na sheria itakayosimamia mchakato huo vizuri.

  KANUNI YA KWANZA MCHAKATO UHUSISHE WOTE
  Mchakato wa kufikia Katiba Mpya usipoweka msingi ambao utahakikisha wananchi wote wana nafasi sawa ya kuchangia mawazo yao juu ya yale wanayoyataka kwenye Katiba Mpya basi basi utakuwa ni mchakato mbovu. Utaona sijasema "kukusanya maoni". Ninachozungumzia ni kuwa ni jambo moja kutoa maoni na ni jambo jingine kufanya mawazo yako yasikike. Kwa wale tunaokumbuka mchakato wa kurudisha vyama vingi tunakumbuka jinsi kina Marmo walivyopita na "kukusanya maoni".

  Japo wenyewe walijivunia kuwa walifanya kazi nzuri ukweli ni kwamba mfumo uliotumiwa ulihakikisha wenye kutoa maoni ni wasomi, wenye sauti na zaidi watu ambao katika maisha yao walikuwa na nafasi fulani za kuweza kusikika. Hata katika maeneo ambayo wananchi wa kawaida walitoa maoni hakukuwa na mjadala wa kutosha kati ya watu na watu kabla ya kufika kwenye tume ya maoni.

  Yaani, kwa masaa machache watu walitakiwa kutoa maoni yao kwenye kikao cha masaa machache kabla hawajaondoka hao wanakamati kwenda mji mwingine "kukusanya maoni". Kama vipepeo tume ya kukusanya maoni iliruka ruka na kupokea mshiko wa nguvu toka serikali ikikusanya maoni na baadaye kutoa ripoti yake. Matokeo yake asilimia 80 ya waliohojiwa walitaka tuendelee kuwa na mfumo wa chama kimoja. Wao wenyewe waliamini ni kwa sababu "CCM inapendwa" lakini hawakutaka kuangalia kuwa wananchi hawakuwa na muda wa kugonganisha mawazo yao ya kutosha.

  Mbinu hii ya kukusanya "maoni" kwa mtindo ambao umewekwa kwenye mswada (ambao hauna tofauti na ule wa kina Marmo chini ya Tume ya Nyalali). Mbinu ya kukusanya maoni hairuhusu mjadala huru wa watu kuweza kushawishiana kubadala maoni. Sasa tukikubali tume ya "maoni" kama ilivyo tujue mapema kabisa kuwa hawa watu watapita, wanakijiji wataitwa, kutakuwa na maelezo ya hapa na pale, maswali yataruhusiwa na wajumbe wataonekana wanaandika andika kwenye makaratasi yao na baadaye kikao kitaisha na watu watarudi makwao wakiwa "wametoa maoni"yao.

  Lakini mfumo bora ni ule wa kuhakikisha kuwa watu wote wanahusishwa siyo tu watu wachache wanatoa maoni lakini watu wote wanahusishwa katika Mjadala wa Katiba Mpya. Kwa hiyo sheria itakayosimamia mchakato wa kufikia katiba Mpya ni lazima iweke mfumo mzuri wa kuendesha mjadala kwa watu wengi zaidi KABLA ya kuanza kukusanya Maoni. Maana yake ni kwamba kabla wananchi hawajaanza kuulizwa kutoa maoni yao ni lazima yawepo mazingira ya kiasi cha juu kabisa (optimal environment) ambapo wananchi watashiriki mjadala wa katiba katika mashule, makanisa, misikiti, maofisini, mitaani, kwenye vyama vya siasa n.k. Kabla ya kuanza kuratibu maoni tufanye mjadala kwanza ambao utahusisha Watanzania katika ngazi zao zote.

  KANUNI YA PILI: MJADALA URUHUSU YOTE KUZUNGUMZIKA
  Hatuwezi kufikia Katiba Mpya inayotokana na wananchi wenyewe na inayowastahili wananchi wenyewe kama hatuwezi kujadili na kuzungumza yote yanayotuhusu kama raia na kama binadamu. Ibara ya 9:2 ya mswada huu ambao umependekezwa kusimamia mchakato unatuambia kuwa tunaweza kuzungumza mambo mengine yote lakini tusije kugusa mambo 10 ya msingi. Mambo hayo wataalamu wetu waliotuandikia mswada (sijui walikuwa watu wangapi) wametuambia kuwa mambo hayo kumi hatayakiwi kuguswa au kubadilishwa.

  Sasa hawa watu sijui nani kawapa uwezo wa kuwaambia wananchi milioni 43 na ushee kuwa wasizungumzia mambo fulani fulani au hata kuyafuta. Ndugu zangu tunapotaka kuandika Katiba Mpya ni LAZIMA mambo yote yaletwe mezani hakuna "mambo matakatifu yasiyogusika". Katika mjadala wa Katiba Mpya hata mambo ambayo hayako mezani na yamewekwa pembeni ni lazima tuyatafuta na kuyaleta pembeni hata yale ambao labda tulishayatupa inabidi tukayachukue huko na kuyaleta mezani.

  Huu ni mjadala wa Katiba Mpya yaani nyaraka kuu itakayosimamia maisha ya Watanzania. Ndio maana kwenye nchi nyingine Katiba ina nguvu kuliko maandiko matakatifu na hii si kufuru. Kama Maandiko Matakatifu tuliletewa na watu na kuambiwa kuwa ni neno la Mungu kwa sababu kuna watu walitokewa na Mungu, malaika au walivuviwa na wakatupatia neno la Mungu na wengi wetu tumejikuta tukiamini. Hata leo utaona watu wanapigana na kuumizana kwa sababu ya maandiko hayo. Lakini Katiba (kwa maoni ya baadhi ya watu) ni juu ya vitabu hivyo vitukufu! Kwa sababu katiba ni sauti ya watu ambayo ina nguvu kama sauti ya Mungu. Yaani, kama kungekuwa hakuna vitabu vitakatifu vya kutuamulia maisha yetu ya kiroho basi binadamu tungetakiwa kuwa na mfumo fulani wa kujiongoza na mfumo huo ungekuwa ni mtakatifu kwa sababu unatokana na sisi wenyewe.

  Vivyo hivyo Katiba. Kuna msemo wa Kilatini kuwa Vox Populi, Vox Dei yaani sauti ya watu (ni) Sauti ya Mungu. Katiba basi inatakiwa kuwa ni nyaraka ambayo inaakisi sauti ya watu kuhusu maisha yao na mfumo wanaotaka uwaongoze na watu hao wakiwa na taarifa sahihi, wakibadilishana mawazo na kushawishiana kwa hoja mbalimbali huweza kufikia kitu kilicho bora zaidi. Sisi binadamu tumepewa uwezo na Mwenyezi Mungu kufikiria na kutambua kitu ambacho hatukitaki hata kama hatuna uhakika wa kile tunachokitaka. Kwa mfano hakuna mwanadamu anayependa kudhulumiwa na mtu mwingine, au anayependa kufanya mtumwa na mtu mwingine. Hii hata hivyo haituzuii kuwadhulumu wengine! Kumbe Katiba ikiruhusu kuzungumzwa kwa yote inatusaidia kuona ni kitu gani hatukitaki na ni kitu gani tunaelekea kukikata au tunajua tunakitaka.

  Ni kwa sababu hiyo basi YOTE LAZIMA yaruhusiwe kuzungumzwa na kujadiliwa. Kusiwe na mada ambazo ni MWIKO. Hivyo sheria yoyote itakayosimamia mchakato wa Katiba ihakikishe kuwa wananchi wanashiriki kutoa mawazo yao kwa kila jambo. Ili hili lifanikiwe ni lazima kwanza kabisa kufanyia mabadiliko sheria ya Usalama wa Taifa ya 1970 pamoja na Sheria ya Magazeti ya 1976 kwani sheria hizo mbili ni kizuizi kikubwa cha uhuru wa mawazo na maoni kuliko kitu kingine chochote.

  Hivyo, katika mjadala huu ni lazima wanaotaka Muungano uvunjwe waruhusiwe kuzungumza mawazo yao bila ya kuogopa kutiwa pingu; wanaotaka muda wa kikomo cha Urais uondolewe ili Rais aweza kugombea bila kikomo kama wabunge waruhusiwe bila ya kuonekana "si wana demokrasia", wanaotaka Tanzania iwe Ufalme wa Kikwete na tuondokane na mfumo wa Urais waruhusiwe kutoa mawazo hayo. Naam, hata kama kuna watu wanataka kuzungumzia kuwa Tanzania iwe na Sharia za Kiislamu au iongozwe kwa Sheria za Kanisa watoe maoni yao vile vile. Tunapozungumzia Katiba Mpya ni lazima tuweke utaratibu utakaoruhusu mawao YOTE kutolewa hata yale ambayo hatuyapendi au yale ambayo yanatugusa vibaya.

  Ninaposema YOTE nina maana kusiwepo na watu ambao watasema "hilo halizungumziki". Kwa mfano wakati wapo wanaoweza kutaka tusema kwenye Katiba kuwa Tanzania inamuamini Mungu tujue wapo ambao pia wangependa tutambue haki za mashoga na wapo ambao wanaweza wakataka tutambue kuwa wanawake nao wanahaki ya kuolewa na mume zaidi ya mmoja!

  Kwa hiyo, tunaporuhusu mjadala wa mambo yote maana yake ni kuwa tutakapofika wakati hasa wa kuanza kukusanya maoni na hatimaye kuanza mchakato wa kuandika Katiba tutakuwa tumesikia hoja karibu zote zenye kugusa wananchi karibu wote na hasa zile hoja ambazo pasipo mjadala kama huu zisingeweza kutolewa. Matokeo yake ni kuwa baada ya mjadala huru wenye kuhusisha watu wote na wenye kuzungumzia mambo yote basi mawazo yaliyo BORA ZAIDI na yenye kuvutia WATU WENGI ZAIDI ndio yatakuwa msingi wa Katiba.

  KANUNI YA NNE: MCHAKATO UONESHE KUWA NI WANANCHI WANATUNGA KATIBA YAO

  Demokrasia ni utawala wa watu. Neno Demokrasia linatoka kwenye Kigiriki likiunganisha maneno mawili 'demo' yaani watu na 'kratia' yaani madaraka au nguvu au utawala. Kimsingi demokrasia ni madaraka au utawala wa watu. Ni kinyume na Theokrasia (utawala wa Mungu) au utawala wa watu mashuhuri yaani Aristokrasia. Kwenye demokrasia wananchi ndio hutawala.

  Hakuna wakati ambao wananchi wanaweza kuonesha nguvu yao ya kutawala kama katika kuandika katiba wanayoitaka. Kwa vile tunataka kuishi katika demokrasia basi hatuna budi kuhakikisha kuwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya unawapa wananchi wetu nafasi ya kuandika Katiba yao – siyo nafasi ya kutoa maoni tu kuhusu Katiba yao.

  Kanuni hii ya tatu inatokana moja kwa moja na hizo mbili za kwanza. Ukisoma mswada ulioandaliwa na "wataalam" wetu utaona ni jinsi gani kama nilivyosema awali waandishi wetu hawajapata ujumbe wa kwanini tunataka Katiba Mpya. Ushahidi ni matumizi ya neno Rais na Wananchi. Neno "Rais" linatokea mara 12 katika mswada huo, neno "mwananchi" linatoka mara mbili na moja kati ya hizo ni "asiye-mwananchi) na neno "watu" linatokea mara nne tu. Kwa maneno mengine, hawa watu watu walioandika mswada huu walikuwa wakiongozwa na fikra za kutekeleza na kulinda maslahi ya Rais.

  Katiba Mpya siyo zao la Rais aliyeko madarakani. Kutokana na hilo mchakato wowote ambao unampa nguvu kubwa Rais (kana kwamba ni mfalme wa Tanzania) ni mchakato mbovu unaohitaji kukataliwa. Walioandika inaonekana ni watu walioamua kufuata njia yenye vikwazo vidogo zaidi (a path of least resistance). Kwa maneno mengine hawakutaka kufikiria zaidi ya namna nyingine ya kufanya kitu hata kama ni bora zaidi na hivyo wakaamua tu kumrundikia Rais majukumu mengi na yasiyo na sababu. Kimsingi wanachopendekeza hawa walioandika ni TUME YA RAIS YA KUPITIA KATIBA.

  Sasa kama watu wangetaka Rais aunde tume tungeomba Rais aunde tume! Hakuna aliyemuomba Rais aunde tume na wala hakikuhitajika kibali chake kwenye suala la Katiba Mpya. Katiba Mpya ni zao la Watanzania na hasa ni zao la wanamageuzi nchini. Sasa kuandaa mswada wa kusimamia mchakato huo bila kuwashirikisha wanamageuzi siyo kutendea haki kwa sababu baada ya kuiteka hoja ya "katiba mpya" sasa wameenda mbele zaidi na wameamua kuteka mchakato wa kufikia Katiba Mpya na tukiwakubalia watateka na katiba mpya.

  Ninachosema kwa maoni yangu ni kuwa sheria itakayosimamia mchakato wa kufikia Katiba Mpya ni lazima itambue kuwa katiba ni lazima itokane na wananchi, kufikiwa kwake ni lazima kuoneshe kuwa ni Katiba ya Wananchi na hivyo hata muundo wa mfumo wa kuifikia uwe ni ule wenye kuheshimu hilo. Bila ya Wananchi kushiriki katika kuandika Katiba hiyo basi Katiba itakayopatikana haiwezi kuwa halali.

  Pamona na ukweli wa kanuni hizo hapo juu nina uhakika kuwa mswada huu unaweza kupita ukiwa na mabadiliko machache tu. Ninachojua ni kuwa endapo mswada utapita jinsi ulivyo au ukiwa na mabadiliko machache tu tutakuwa tumerasimisha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa CCM. Hivyo, huu utakuwa ni utaratibu wa CCM kufikia Katiba Mpya. Yaani, wao ndio wataamua Katiba Iweje na kwa maoni yangu itakuwa ni dhambi kwa dhamira zetu kutoa ushirikiano wowote kwa tume hiyo ya Rais.

  Kutokana na hilo ninaamini ni wajibu wa kila anayoengozwa na dhamira ambayo inamsuta kutoa ushirikiano kutofanya hivyo. CCM na serikali yake waendeshe mchakato wao na wafikie kwenye Katiba Mpya wanayoitaka wao. Sisi wengine tutaanza mchakato huru na wawazi zaidi baadaye wa kuweza kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia madaraka yao (kratia) ya kuweza kuandika Katiba wanayoitaka.

  KANUNI YA TANO: KUTAMBUA UZITO NA UNYETI WA ZOEZI ZIMA
  Tukitoka kwenye kanuni hizo tatu za juu ni wazi kuwa suala hili ni suala zito na nyeti. Ni suala ambalo matokeo yake yatabakia miaka mingi ijayo wakati sisi sote (tunaibishana leo) tukiwa tumeshageuka mifupa iliyosagika mavumbini. Ni lazima tujiulize TUNATAKA KUWAACHIA WATOTO WETU KITU GANI CHEMA KATIKA UTAWALA?

  Tukifikiria kuwa tunataka kuandika Katiba Mpya kwa ajili ya kushinda uchaguzi ujao au kwa ajili ya kuiondoa CCM madarakani tutakuwa tumekosea. Tukifikiria kuwa tunaandika Katiba Mpya ili kumpunguzia Rais madaraka au kwa ajili ya kuimarisha Muungano tutakuwa tumekosea. Tunataka kuandika Katiba Mpya ili kuweza kukiachia kizazi kijacho mfumo mzuri wa utawala ambao utawapa nafasi ya kufanikiwa katika maisha na mkipango yao na ambao utawahakikishia mtiririko mzuri wa mahusiano na kuwajibishana kati yao na watawala wao.

  Hivyo, ni lazima tutambue "utakatifu" wa mpango mzima wa kuandika Katiba Mpya. Tunachotaka kukifanya ni sawasawa na kujaribu kuandika kitabu kitakatifu kutoka katika mioyo yetu na ambacho tutaapa kukilinda kwa maisha yetu. Tujue kuwa tunaposema "Katiba Mpya" maana yake kama kuna watu watakuja kuivunja au kuichezea wajue kabisa kuwa watapata hasira ya Watanzania wote.

  Hivyo mchakato mzima ni lazima utambue ukuu, utukufu na upekee wa zoezi zima. Hili litaonekana katika mfumo na utaratibu utakaoewekwa. Hadi hivi sasa inasikitisha kuona kuwa watu wanafikiria zoezi la kuandika Katiba Mpya ni kama zoezi jingine lolote nchini; la hasha. Haliwezi kufuata taratibu tulizozizoea na kamwe halipaswi kuchukuliwa kama jambo la kawaida.

  Ni kwa sababu hiyo naamini kuwa kikao cha sasa kifupishwe ili mambo mengine tu yajadiliwe lakini Bunge liurudishe mswada huu kwa serikali na kukusanya maoni bora zaidi (nami nitakuwa tayari kutoa maoni ya kumchakato bora ambao utaakisi kanuni hizo hapo juu). Ila kifanyike kikao maalum cha Bunge ambacho kwa kuitwa kwake kitakuwa kinaonesha watawala wetu wanatambua uzito wa tukio lililo mbele yetu.

  Badala ya kufanya haya mazingaombwe ya "vikao vya Kamati ya Katiba" ambavyo vitakutana na wananchi Dodoma, Dar, na Zanzibar kama wawakilishi tu wa mawazo ili waweze kusema "tulikusanya maoni" ni bora tuvute pumzi na tujipange vizuri ili kuweza kuonesha kuwa tunaelewa uzito wa kitu ambacho kama taifa tunataka kukifanya.

  Binafsi ninaamini watawala wetu bado hawajelewa uzito wa jambo hili. Yaani kuliweka kama sehemu ya kikao cha kawaida ni kutolipa jambo hili uzito wake. Ninaamini suala la Katiba Mpya ni sawasawa na Musa alipopanda mlimani ili apewe Amri Kumi za Mungu – Katiba ya Wanaizraeli wa enzi hizo. Ilikuwa ni jambo la kuogofya. Sisi hatuendi milimani bali tunaenda kwa wananchi ambao ndio asili ya madaraka yote. Ni lazima tutetemeke na kuogopa kwa sababu watakuja na amri gani hatujui.

  Ninaamini
  Kikao Maalum cha Bunge cha kujadili Mswada wa Sheria ya Kuongoza Mchakato wa Katiba Mpya kiitwe hata kama kitakuwa ni cha siku tatu tu. Kikao hicho kisiwe sehemu, ya kikao cha kawaida (kama cha sasa) au kile cha Bunge la Bajeti. Kiwe ni kikao maalum. Ni kwa namna hii tutaweka heshima ya jambo ambalo tunataka kulifanya.

  Na tukifanya hivyo tutatoa muda kwa pande nyingine kutolea maoni sheria hizo na hata kwa upinzani kuja na mapendekezo ya mswada wao ili hatimaye miswada hiyo miwili (au zaidi) iweze kujadiliwa na hatimaye upatikane mswada ulio mzuri zaidi. Kama tulivyokosoa mswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi na watu walidhani tunawaonea wivu lakini tulikuwa sahihi nina uhakika tuko sahihi wakati huu tena.

  Mswada huu ukipitisha kama ulivyo utachangia ujio wa sheria nyingine mbovu zaidi ambao katika dhamira safi baadhi yetu tutashindwa kuitii. Sasa kama tunataka kweli kufikia katiba Mpya ni lazima kwanza tubadili fikra. Watawala wasidhani wanatutendea hisani na wananchi tusifikirie tunabembeleza watawala wetu. Ni bora tusubiri miaka mitano tuweze kuleta timu itakayotuongoza kufikia katiba mpya kuliko tuharakishwe ndani ya miaka hii mitano kuongozwa kuelekea kwenye machozi. Katiba mpya itokane na fikra mpya.

  * * *

  Itaendelea sehemu ya pili kesho – inshallah, ambayo itaangalia kile ambacho nakiita "mapendekezo ya Mgawanyo wa mchakato wa kuelekea Katiba Mpya". Huko nitaangalia kwa undani kidogo aina ya mchakato ambao utazingatia kanuni hizo tano na kwanini mswada unaopendekezwa na serikali na kujadiliwa kwa haraka haraka ni jaribio dhaifu la utawala wa CCM kuendelea utekeaji wa ajenda ya Katiba mpya na ambalo endapo halitapiingwa na kukataliwa litatuletea "katiba mpya ya Taifa inayotokana na CCM". Endapo hilo litafanikiwa tujiandae kusahihisha kosa hilo la kihistoria miaka michache baadaye kwa kuwa na mchato wa kweli wa kuandika Katiba Mpya.


  * Makala hii ina tofauti kidogo na makala inayotoka kwenye Gazeti la Tanzania Daima leo.
   
 2. Shalom

  Shalom JF-Expert Member

  #2
  Apr 6, 2011
  Joined: Jun 17, 2007
  Messages: 1,315
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Imetulia sana mkuu!
   
 3. Selous

  Selous JF-Expert Member

  #3
  Apr 6, 2011
  Joined: Jan 13, 2008
  Messages: 1,322
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Mwanakiji.

  Nitaiprint, nisome niache kwenye dala-dala wengine wasome. I will print many copies.
   
 4. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #4
  Apr 6, 2011
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  vizuri ni mchango kidogo tu katika kubadilishana mawazo.
   
 5. Edson

  Edson JF-Expert Member

  #5
  Apr 6, 2011
  Joined: Mar 7, 2009
  Messages: 9,202
  Likes Received: 722
  Trophy Points: 280
  haya ndio mawazo tunayotaka juu ya mchakato huu wa katiba mpya......
   
 6. AMARIDONG

  AMARIDONG JF-Expert Member

  #6
  Apr 6, 2011
  Joined: Jun 24, 2010
  Messages: 2,506
  Likes Received: 48
  Trophy Points: 0
  We Mwanakijiji unaishi nje ya nchi unakula upepo mwanana na hewa yenye amani huwezi kutuandikia huu utumbo hapa erti unasema unatufundisha nonsense, wewe uko ughaibuni kwa muda sasa huwezi kutuambia kitu kwanza hujui chochote kinachoendelea hapa hata kama unafuatilia huna habari kamili na hali halisi tuliyonayo na tunayoifahamu sisi tunaosaga soli hapa Kariakoo na Manzese acha utani kabisa usituseemee haisaidii kabisa na wala haibadilishi kitu

  Haisaidii Mwanakijiji, hata ukiandika na kubandika kwenye kuta zote za ikulu wala usifikiri JK atasoma, hata ukiandika na kuweka kwenye kila kona ya bunge pale Dodoma wala hamna mbunge hata mmoja wa CCM atakaeelewa, hata ukiandika na kuweka kwenye magazeti yote ya leo hakuna mtanzania atakaechukua hatua yoyote zaidi ya wote tutasoma kama hapa JF na kisha kusema ni kweli aiseee Mwanakijiji kasema ukweli kabisaaa aiaseeee ila mwisho wa yote hakuna hata moja litakalotekelezwa,

  Ngoja nifafanue kitu;

  Hii nchi imejaa ubinafsi na choyo, utapeli na tamaa na hili sio kwa CCM tuu hata vyama vya upinzani, hakuna mtanzania ambaye yuko tayari kwa ajili ya mwingine hata kama ni kufa na afe tuu lakini hakuna aliye tayari kumsaidia chadema wanapiga kelele sana lakini hebu tuwaangalie hao CHADEMA ni usaliti mara ngapi wamewafanyia watanzania, tumewachagua kwa wingi unaotosha kufanya jambo likaonekana lakini wapi ndio wa kwanza kupokea posho kubwa za bunge na mishahara mikubwa wao ndio wanaogombana kwenye vikao wakitaka maslahi ya mbunge yaongezwe, wao ndio wakwanza kuchukua milioni tisini kwa ajili ya starehe, wao ndio walevi wakubwa pale Dodoma wikiend hii wabunge zaidi ya nane wa CDM walikuwa 84 club Dodoma wakinywa pombe na kufanya uhuni sasa unategemea nini kwa watu hawa??

  Kuhusu katiba, kweli JK kaamua kuziba masikio na ataendelea kufanya hivyo kwani anajua hakuna tunachoweza kumfanya, atatunga katiba mpya ambayo itakuwa mbaya zaidi kuliko hii tuliyo nayo sasa.

  Naamini itafikia wakati CHADEMA wataanza kudai katiba hii irudishwe kwani hiyo itakayotungwa itakuwa balaa kuliko hii, dalili zimeshaonekana na mimi nakubali kabisa kwani kila kinachotokea hapa ni upuuzi na ujinga wa wananchi.

  Wananchi ndio wanaolala njaa na kufa ka magonjwa ya kipuuzi kwa kukosa dawa hata essentials tuu, lakini ndio wanaovaa tishet za kijana na manjano na kofia za kuipongeza CCM wao ndio wanaopiga kura tena kifua mbele kuichaguz ccm na wanajisifu kuwa ccm itadumu madarakani kila uozo unaokuja sasa ni wa wananchi wa tanzania wapuuzi walioichagua CCM na wanaoendelea kuipa chapuo ccm chama kilichooza na ambacho hakiko tayari kumsaidia mtanzania
   
 7. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #7
  Apr 6, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Inavyoonekana lengo la serikali kuleta muswada huu siyo kujibu kiu ya watanzania kupata katiba mpya bari ni kulinda masilahi ya CCM. Haiigii akilini katika dhama hizi za ukweli na uwazi tuwe na sheria inayokataza wananchi kutoa maoni yao. Kama misingi ya katiba hii ni pamoja na kuwanyima wananchi haki yao ya kuzaliwa ya kutoa maoni na kusikilizwa basi bora tuendelee na katiba iliyopo hadi pale tutakapokuwa tayari kwa mabadiriko
   
 8. g

  guta Senior Member

  #8
  Apr 6, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 179
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Ni mchango kidogo lakini ni mkubwa sana. Hebu fikiria sentensi hizi mara mbilimbili:

  KANUNI YA PILI: MJADALA URUHUSU YOTE KUZUNGUMZIKA
  Hatuwezi kufikia Katiba Mpya inayotokana na wananchi wenyewe na inayowastahili wananchi wenyewe kama hatuwezi kujadili na kuzungumza yote yanayotuhusu kama raia na kama binadamu. Ibara ya 9:2 ya mswada huu ambao umependekezwa kusimamia mchakato unatuambia kuwa tunaweza kuzungumza mambo mengine yote lakini tusije kugusa mambo 10 ya msingi. Mambo hayo wataalamu wetu waliotuandikia mswada (sijui walikuwa watu wangapi) wametuambia kuwa mambo hayo kumi hatayakiwi kuguswa au kubadilishwa.


  Sasa hawa watu sijui nani kawapa uwezo wa kuwaambia wananchi milioni 43 na ushee kuwa wasizungumzia mambo fulani fulani au hata kuyafuta. Ndugu zangu tunapotaka kuandika Katiba Mpya ni LAZIMA mambo yote yaletwe mezani hakuna "mambo matakatifu yasiyogusika". Katika mjadala wa Katiba Mpya hata mambo ambayo hayako mezani na yamewekwa pembeni ni lazima tuyatafuta na kuyaleta pembeni hata yale ambao labda tulishayatupa inabidi tukayachukue huko na kuyaleta mezani.

  Huu ni mjadala wa Katiba Mpya yaani nyaraka kuu itakayosimamia maisha ya Watanzania.
   
 9. AMARIDONG

  AMARIDONG JF-Expert Member

  #9
  Apr 6, 2011
  Joined: Jun 24, 2010
  Messages: 2,506
  Likes Received: 48
  Trophy Points: 0

  UNAKURUPUKA WEWE NANI AMEKATAZWA KUTOA MAONI??ISUUE NI MSWADA MBOVU YAANI MSWAADA TAKATAKA SASA TUTOE MAONI KWENYE MSAADA TAKATAKA TUNATOA MAONI GANI KAMA SIO MAONI TAKATAKA

  anza upya
   
 10. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #10
  Apr 6, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Ahsante
   
 11. G

  Gurtu JF-Expert Member

  #11
  Apr 6, 2011
  Joined: May 15, 2010
  Messages: 1,202
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Hakika sasa ninakubaliana na hisia za watu kwamba katika uchaguzi wa mwaka jana 2010 CCM walituibia kura za urais. Kama katiba hawataki iwe ya wananchi si zaidi kutokuheshimu kura za wananchi?

  CCM wanapeleka Muswada kwa hati ya dharura matokeo yake yatakuwa mchakato wa dharura ikiwa pamoja na mjadala wa dharura na hatimaye kura ya maoni ya dharura. Mwisho tutakuwa na katiba mpya iliyoandaliwa kwa dharura na kumbe katiba ni ile ile ya zamani au ni mbaya kuliko ile ya dharura.

  Mwanakijiji nakushukuru kwamba umeona jinsi CCM wanavyotaka kuwahujumu Watanzania katika suala la Katiba wakidhani kuwa Watanzani ni majuha. Iweje mchakato uwe na kasoro na hatimaye tuwe sahihi katika kufikia lengo la kuwa na katiba mpya/
   
 12. AMARIDONG

  AMARIDONG JF-Expert Member

  #12
  Apr 6, 2011
  Joined: Jun 24, 2010
  Messages: 2,506
  Likes Received: 48
  Trophy Points: 0
  UMEKULA MSUBA THIS MORNING AU??
  SOMA HAPo UNDERLINED
   
 13. g

  guta Senior Member

  #13
  Apr 6, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 179
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Nadhani hapa hamjaelewana msome mwenzio vizuri.
   
 14. I

  Igembe Nsabo Member

  #14
  Apr 6, 2011
  Joined: Jun 4, 2010
  Messages: 87
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Wasiwasi wangu ni ile tabia ya Watanzania wengi kutopenda kusoma! kwani tabia ya Watanzania wengi wamezoea kusomea MTIHANI! hii ndio imekua desturi yetu tangu utoto. Kwa maana hiyo nawasiwasi kuwa hata ukiwapa kwenye daladala wanaweza wasisome hiyo document nzuri ya Mwanakijiji.
   
 15. g

  guta Senior Member

  #15
  Apr 6, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 179
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  wanaweza wasisome, lakini kuna watakao soma. zingine zitaangukia kwenye udongo mzuri zitamea na kukua .
   
 16. lukindo

  lukindo JF-Expert Member

  #16
  Apr 6, 2011
  Joined: Mar 20, 2010
  Messages: 7,892
  Likes Received: 6,086
  Trophy Points: 280
  ubatili wa muswada huu wa sasa unaanzia pale waziri SELINA (Celine) Kombani anapokuwa mwakilishaji bungeni wakati yeye alisha declare publicly kuwa katiba mpya haiwezekani. Haiwezekani binadamu akafanya nakufanikisha kitu tofauti na dhamira yake.
  My take:
  (...Baba, ikiwezekana kikombe hiki kinipite ila si kwa mapenzi yangu ila mapenzi Yako") PEOPLES POWER!!!!!!
   
 17. m

  mwananyiha JF-Expert Member

  #17
  Apr 6, 2011
  Joined: Mar 11, 2008
  Messages: 244
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33


  Umeanza vibaya umeendelea vizuri na umemaliza vizuri sana.
   
 18. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #18
  Apr 6, 2011
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 30
  Trophy Points: 0
  Mwanakijiji,

  Ingawa siku hizi nimekuwa si mchangiaji katika barza yenu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuchoshwa na kuboreka na watu au wachangiaji wengi kupenda ms'khara na kutoa majibu rahisi katika mada nzito na useful kwa jamii lakini hapa nimelazimika kuandika japo kwa ufupi sana .

  Maneno ulioandika ni sawia kabisa lakini haya yameanzia kwenye jamii ya juu na sio watanzania. Naomba ujue kuwa zaidi ya 90% ya watanzania hawaijui na wala hawajawahi kuiona katiba ya nchi. Na naamini zaidi ya 80 % ya wachangiaji humu hawajawahi kuiona na hawaijui katiba ya Tanzania na ile ya Zanzibar ila wamelewa ushabiki kwa kutumiwa na maneno ya wanasiasa.

  Kabla kufika huko kuna umuhimu sana kutolewa Elimu ya katiba katika jamii yote ili watu waweze kujua umuhimu wa katiba . Kisha kuelezwa mazuri na upungufu wa katiba ya sasa ya muungano ndipo tuje kwenye maamuzi au mapendekezo ya kuandika katiba mpya au kutia vilaka katiba tulionayo.

  Ni vizuri kuwashirikisha wananchi wote wa rika mbalimbali na makundi yote katika kufanya maamuzi hayo wakati tukukumbuka Toka uhuru Tanzania haijawahi kuandika katiba yake zaidi ya copy and paste kutoka kwenye ile ya wakoloni.

  Nimeipenda sana article yako lakini muhimu elimu ya katiba kwa jamii na kushirikisha makundi yote ya jamii katika kufanya maamuzi.

  Nikipata nafasi nitaipambanua kwa kina sana Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar katika jukwaa la sheria kwa manufaa ya wasomaji.

  Nasriyah Saleh Al Nahdi
  Doha.
   
 19. Ngisibara

  Ngisibara JF-Expert Member

  #19
  Apr 6, 2011
  Joined: Jan 2, 2009
  Messages: 2,083
  Likes Received: 431
  Trophy Points: 180
  Askofu Ruzoka alishasema mswaada wao utatia HASIRA watu na hapo alipooandika.....mwaka jana 2011 ni hasira tu zimemfanya akosee
   
 20. Ronal Reagan

  Ronal Reagan JF-Expert Member

  #20
  Apr 6, 2011
  Joined: Nov 4, 2010
  Messages: 4,745
  Likes Received: 1,459
  Trophy Points: 280
  You're equally super genius. Thanks for your proactivity Selous.
   
Loading...