Kanisa liko sahihi kukataa padre wa Bukoba kugombea ubunge

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
221
190
Kwa wiki mbili sasa mitandaoni inazunguka barua inayoonyesha ni ya askofu Desiderius Rwoma wa jimbo katoliki la Bukoba. Barua hiyo inahusu padre aliyeandika barua ya kuacha upadre akaenda kusikojulikana.

1598880525416.png


Barua hiyo inaonyesha kwamba padre huyo ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Nkenge bila kuzingatia kuwa huo ni "uongozi wa kisiasa" unaokatazwa na kanuni ya 285(3) ya Sheria za Kanisa. Hivyo askofu amemsimamisha kutoa huduma za kipadre kokote duniani kuanzia Julai 24, 2020.

Kusimamishwa namna hii kwa kilatini kunaitwa suspended a divinis. Wote tunajua siku unapoiacha taasisi au ikikuachisha, kuanzia kesho yake sheria za taasisi hiyo hazina tena mamlaka kwako, yaani hazina jurisdiction.

Hivyo kama ni shule, chuo au kampuni iliyokuajiri, haiwezi tena kusema wewe ni mtoro. Haiwezi tena kukuadhibu au kukusimamisha (suspend). Kama askofu aliandikiwa na padre barua ile, sasa atamsimamishaje mtu aliyekwishaacha upadre? Swali hili ni gumu kama hufahamu muundo wa kanisa na mafundisho yake yaani Katekism ya Kanisa Katoliki.

AINA ZA WAUMINI:

Kila mkatoliki amefundishwa kwenye kifungu cha 1121 cha Katekism ya Kanisa Katoliki kwamba kuna hali tano ambazo hazifutiki maishani ukishazipata.

Hali hizo ni ubatizo, kipaimara, ushemasi, upadre na uaskofu. Kwa kuwa ushemasi, upadre, uaskofu haufutiki mtu haupewi bila ahadi za utii. Ahadi hizi zinamzuia asifanye lolote wala kwenda kokote bila ruhusa ya kanisa. Kwa mujibu wa kifungu cha 934 cha Katekism kanisa lina makundi mawili ya waumini, yaani maklero na walei.

Maklero ambao kwa kiingereza ni clergy ni watu waliopata wito wa kutoa huduma za kanisa, hivyo shemasi, padre na askofu ni maklero. Wote maklero na walei wanaweza kuunda shirika.

Shirika huundwa kwa lengo maalum linaloitwa mission, hivyo waliomo kwenye mashirika tumezoea kuwaita wamisionari. Huko shirikani wanaume wanapoitana brother huku tunawaita buruda na wanawake wanapoitana sister sisi tunawaita sista.

Je, walei ni watu gani? Kifungu cha 897 cha Katekism kinasema walei ni waumini wasioko shirikani na hawana daraja takatifu yaani hawana ushemasi, upadre, uaskofu.

PADRE NA ULEI:

Swali au hoja kuu kwenye suala kama hili ni iwapo mtu anaweza kuacha au kuachishwa upadre.

Tumeona inavyosema Katekism (897) kwamba mlei hana ushemasi, upadre, uaskofu. Tumeona pia inavyosema (1121) ushemasi, upadre au uaskofu haufutiki. Hivyo, mtu hawezi kuacha au kuachishwa au kufukuzwa upadre maana haufutiki.

Je, kinachoachwa ni nini? Kanuni ya 290 ya Sheria za Kanisa inasema kinachopotea kinaitwa loss of the clerical state kwa kiswahili tunaweza kukiita kupoteza uklero au kuondolewa uklero.

Kinachoitwa kimakosa "kuacha upadre" ni kuondolewa uklero. Baada ya "kuondolewa uklero" mtu anaweza kuoa kanisa likimruhusu. Wilbrod Slaa na Privatus Karugendo wana ndoa halali baada ya "kuondolewa uklero".

Ukishaondolewa uklero ile kanuni ya 285(3) ya Sheria za Kanisa haikuzuii tena kazi inazozikataza. Dk. Wilbrod Slaa amekuwa mbunge kwa miaka 15 na sasa hivi ni balozi wetu nchini Sweden. Hata hivyo kuna nyakati muumini anaweza kuhudumiwa na mtu aliyeondolewa uklero.

Ukiwa katika hatari ya kifo kanuni ya 976 ya Sheria za Kanisa inaruhusu kupata huduma ya maungamo kutoka kwa aliyeondolewa uklero.

KANISA LINACHOKATAZA:

Kanisa na siasa ni vitu wawili tofauti. Wanasiasa wanaweza kuukataa ukweli kama ukweli wako siyo utashi wao.

Kazi ya kanisa ni kuhubiri ukweli na haki ili watu wauchukie uongo na uovu. Tumeona kinachokatazwa na kanisa kupitia kanuni ya 285(3) ya Sheria za Kanisa ni "uongozi wa kisiasa". Je, huo uongozi wa kisiasa ni ubunge tu kama anaogombea huyo padre wa Bukoba?

Kanuni hii haina maneno "uongozi wa kisiasa" bali ina maneno "public office" na "civil power" na iko hivi Clerics are forbidden to assume public office which entails participation in the exercise of civil power.

Tuone mfano ufuatao ili kujua kazi zinazokatazwa. Wanasiasa wakiona ushoga utawaingiza madarakani watatunga sera ya ushoga. Padre anayegombea kupitia chama hicho atainadi sera hiyo kwenye kampeni.

Chama hicho kikifika bungeni kinatunga sheria ya kuhalalisha ushoga kiliounadi kwenye kampeni. Sheria hiyo ikianza kutumika watumishi serikalini wanautetea ushoga. Mapadre wa serikalini nao watautetea.

Kama mahakama ina jaji ambaye ni padre hukumu zake zitalinda haki za mashoga kwenye sheria ile.

Kama kuna mapadre bungeni, serikalini, mahakamani, wote hawa watakuwa wameuleta ushoga kwa kutumia mamlaka yao "civil power" wakiwa kwenye kazi zao "public office".

Mfano huu unaonyesha kwamba kanisa linakataza kote bungeni, serikalini na mahakamani. Huko nyuma kanisa liliwahi kusumbuliwa kabla ya kuanza kutumika sheria hizi mwaka 1983.

Swali lilikuwa ni kwamba hiyo "civil power" inayokatazwa iko wapi? Je, iko serikalini? Je, iko bungeni? Je, iko Mahakamani? Kipindi hicho wapo mapadre duniani walionekana bungeni.

Hata hapa Tanzania padre Supa wa jimbo katoliki la Dodoma alifaulu kuwa mbunge katika kipindi hicho.

Mwaka 1981 ofisi ya Papa ilitoa taarifa iitwayo "Relatio" iliyofafanua kwamba kinachokatazwa na kanisa ni kote serikalini (executive), bungeni (legislature) na mahakamani (judiciary). Sasa tuone kesi mbalimbali duniani.

NICARAGUA:

Mwaka 1979 padre Ernesto Cardenal wa shirika la Jesuits aliteuliwa na Rais Daniel Ortega wa Nicaragua kuwa Waziri wa Utamaduni.

Mwaka 1983, Papa John Paul II alipowasili ziarani Nicaragua serikali yote ilikuja kumpokea uwanja wa ndege. Rais Oterga akamuongoza Papa walikojipanga mawaziri ili awasalimie mmojammoja, akiwemo padre Cardenal.

Padre Cardenal alipofikiwa akapiga magoti kubusu pete ya Papa. Papa akakataa kumpa mkono, kinyume chake akamfokea mbele ya Rais Oterga kwamba aondoke serikalini kama kanisa linavyokataza.

Serikali ikazuia magazeti ya Nicaragua yasitoe picha ya waziri alivyofokewa akiwa amepiga magoti. Waandishi wa kimataifa wakaisambaza picha ile duniani {Witness to Hope: The Biography of Pope John Paul II, uk. 454}.

Agosti 1984, ofisi ya Papa ikamwandikia rasmi barua padre Cardenal kwamba aondoke serikalini arudi kwa majesuit wenzake kwani amevunja sheria za kanisa {uk. 457}.

Padre Cardenal akakataa, John Paul II akamsimamisha, yaani "suspended a divinis". Usimamishwaji huo ulidumu kwa miaka 35 hadi Papa Francis alipoufuta mwaka jana. Padre Cardenal amefariki mwaka huu, Machi 01, 2020.

HAITI:

Padre Jean-Bertrand Aristide wa Haiti alikuwa wa shirika la wamisionari wa Selasian.

Alipoanza kushiriki siasa wakuu wake wakamuonya lakini akakataa, hivyo wakamfukuza shirikani kwa kutotii onyo yaani "dismissed".

Baadaye akagombea urais akawa Rais wa Haiti tangu Februari 1991. Jeshi lilipompindua Oktoba 1991 akaishi ukimbizini na huko akamuomba Papa John Paul II kumuondoleaa uklero na akaondolewa mwaka 1994.

PARAGUAY:

Fernando Lugo alikuwa askofu wa jimbo la San Pedro nchini Paraguay hadi alipojiuzulu mwaka 2005. Desemba 18, 2006 aliandika barua kwa Papa akiomba aondolewe uklero ili agombee urais wa Paraguay.

Januari 20, 2007 Papa alimjibu askofu Fernando kwamba hatamuondolea uklero, ingawa anamsimamisha yaani "suspended a divinis". Wakati huo ilikuwa haijawahi kutokea askofu kuondolewa uklero kwa sababu kama hizi.

Kumuondolea padre uklero kunaweza kuliletea kanisa shida ya muda mfupi tu inayoisha akifa. Lakini kumuondolea askofu uklero kunaweza kuleta mgawanyiko utakaolisumbua kanisa kwa karne nyingi.

Uchaguzi wa rais ulipokuja April 20, 2008 askofu Fernando akashinda akawa Rais wa Paraguay. Baada ya kushinda urais ndipo Juni 11, 2008 Papa Benedict XVI alimuondolea uklero askofu Fernando.

PADRE WA BUKOBA:

Baada ya kuona mifano duniani sasa turejee kinachoendelea jimboni Bukoba kama barua ile inavyosema. Padre kufaulu kuwa kwenye mbio za ubunge bila kuzingatia aliondokaje kanisani ni kukaribisha matatizo kama kule Haiti, Paraguay na Nicaragua kama tulivyoona.

Tumeona pia mtindo wa kuandika barua kuacha upadre na kuondoka hauko popote ndani ya kanisa katoliki. Hivyo huyo bado ni padre wa jimbo la Bukoba na "hajaondolewa uklero".

Katazo la padre au askofu kwenda kusikojulikana linaanzia kwenye ahadi zake za utii. Hizi tu bila kanuni nyingine zinatosha kumwajibisha anayefanya hivyo kwani hajatumwa huko kusikojulikana.

Pamoja na ahadi za utii ipo kanuni mahsusi inayokataza maklero kutorandaranda. Hiyo ni kanuni ya 265 ya Sheria za Kanisa. Hivyo padre hata asipoenda kwenye mbio za ubunge bado kanuni hii inamzuia.

MASISTA:

Hadi hapa tumeona kanuni ya 285(3) ya Sheria za Kanisa inayotaja kuwazuia maklero tu. Je, sista akigombea ubunge hata wa viti maalumu, kanisa litamzuia?

Hata masista, wamisionari na watawa wote wanakatazwa vilevile ila wao kwa kutumia kanuni ya 672 ya Sheria za Kanisa. Hivyo sista wa kanisa katoliki huwezi kumsikia akiomba ubunge wa viti maalumu.

Imetayarishwa na: Joseph Magata, Cell: 075-4710684, Email:
josephmagata@yahoo.com
 
Kanisa linapita katika vipindi vigumu katika majira tofauti.
Ingawa yote haya yamewahi kufanyika pia hapo kabla.

Kikubwa nachopendezwa nacho ni namna kanisa linavyo hughulikia changamoto zake huku subira ikitawala.

Ukiangalia mifano hapo juu utagundua HEKIMA ya viongozi wa kanisa Katoliki.

Kila la heri kwa kila aliyechagua njia yake ilimradi njia hiyo isimtenge mbali na upendo wa Mungu
 
Ahsante kwa ufafanuzi mzuri.

Umenikumbusha Padre Supa. Mnamo mwaka 1990 wakati wa kampeni alikuja Shule ya Sekondari Mazengo akiwa mgombea wa Jimbo la Dodoma Mjini. Padre Supa alikuwa anatetea kiti chake kwa Tambo na majidai akisema ana shahada tano. Hata hivyo alipigwa chini wakati wa uchaguzi na ndugu Kusenha Mazengo ambaye alishinda.
 
Ungekuwa Na muda ukaongelea askof Makarious. Nadhani alikuwa barozi Wa nchi ya Cyprus. Mara nyingi hayati Mwl, Nyerere alikuwa anàmuongelea! Alikuwa Ni askofu na mwanasiasa?
 
Asante kwa uzi mzuri naenda kuanzisha uzi mwingine naomba maoni YAKO.
 
Ungekuwa Na muda ukaongelea askof Makarious. Nadhani alikuwa barozi Wa nchi ya Cyprus. Mara nyingi hayati Mwl, Nyerere alikuwa anàmuongelea! Alikuwa Ni askofu na mwanasiasa?
Nafikiri Askofu Makarious alikuwa wa ni dhehebu la Orthodox na sio Roman Catholic.
 
Yesu aisema huewezi kutumikia mabwana wawili lazima kuna mmoja utampendelea zaidi.

Pia alisistiza ya kaisali tumuachie kaisali na ya Mungu tumuachie Mungu.

Padre alizingua sana.
 
Back
Top Bottom