Kandoro,ubabe huu hausaidii.

Fidel80

JF-Expert Member
May 3, 2008
21,947
4,444
Kulwa Karedia-Tanzania Daima
KIONGOZI bora ni yule anayekubali kukosolewa pale anapokosea ili kurekebisha mwenendo wake, lakini kama akigoma, basi huyo si kiongozi bora.

Kauli hii iliwahi kutolewa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika moja ya hotuba zake alizotoa wakati wa uhai wake.

Maneno hayo ni mazito kwa kiongozi aliyepewa dhamana ya kuongoza nchi au kuwatumikia wananchi waliomwamini kwamba atawaletea maisha mazuri.

Nimeanza na maneno haya kutokana na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, aliyoyatoa mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya kuwapiga marufuku waandishi wa habari kumhoji kuhusu michango ya shule za sekondari iliyochangwa na wananchi.

Pole sana Kandoro kwa ‘jeuri’ hii, kwa sababu wewe umo katikati ya msitu wa wanahabari, ambao wamekuwa na mchango mkubwa wa kukusaidia kuweka jiji katika ramani ya Tanzania.

Mambo mengi yamekuwa yakifichuliwa na wanahabari hao hao unaowakataa leo kukuhoji kuhusu michango ya wavuja jasho wa taifa hili, ambao sasa wamefikia hatua ya kuzichoka kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi.

Kandoro kumbuka kwamba bila wana habari katika mkoa wako usingeweza kutambua majanga makubwa yanayotokea, yakiwemo ya ujambazi, ambao ulitia fora katika maeneo mbalimbali, watu walikabwa, kupigwa na kunyang’anywa mali zao, zikiwamo simu za mikononi.

Kandoro kumbuka jinsi wana habari hao unaowaona hawana maana jinsi walivyoshughulikia sakata la ubomoaji wa nyumba za wananchi wa eneo la Tabata Dampo na sakata la kuanguka kwa jengo la ghorofa 10 katika eneo la Kisutu, haya yote hauyaoni masikini wangu!

Ni ukweli usiopingika kwamba bila wao, ukweli wa mambo usingejulikana kama ilivyotokea hadi kufikia serikali kuamua kulipa fidia kwa wananchi hao.

Serikali hiyo kupitia chama tawala baada ya kuona haikuridhika na mwenendo wa sakata hilo, imeonyesha makucha yake kwa kumsimamisha Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Mohamed Yakub, kwamba alishiriki kwenye sakata hilo. Ukubali usikubali hii ilitokana na nguvu ya vyombo vya habari.

Sasa Kandoro jeuri hii anaitoa wapi? Wananchi wana haki kupitia vyombo vya habari kujua michango yao imefanya nini na kiasi gani kimepatikana hadi sasa.

Kitendo cha kukataa kujibu swali, ni mwendelezo wa utawala wa ukandamizaji na wala si utawala bora kama ambavyo viongozi wetu wamekuwa wakipanda majukwaani na kuhubiri kila siku.

Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye bosi wake tangu alipoingia madarakani amekuwa akihimiza viongozi kuwasomea wananchi mapato na matumizi kutokana na michango yao, lakini leo Kandoro ameshindwa kuelewa hili.

Tunasema kuwa kitendo hiki hatuwezi kukivumilia, Kandoro amka, soma mapato na matumizi yaliyopatikana katika michango hiyo bila kinyongo ili kurejesha imani yako kwa wananchi.

Kauli yake kwa wanahabari ilinitia ‘kichefuchefu’ pale aliposema wanahabari wanapaswa kutambua kuwa ana majukumu mengi ya kitaifa na si kila siku kuzungumzia michango tu.

Tena kwa ‘jeuri’ kubwa anajibu kwa kusema: “Nimechoka kusikia swali hili, iwe mwanzo na mwisho kuniuliza.” Jamani, kiongozi mstaarabu hawezi kutoa majibu kama hayo.

Naamini kwamba kila Mtanzania atakubaliana na mimi kwamba ujenzi wa shule za sekondari za kata ni jukumu la kitaifa, ambalo limekuwa likitangazwa kila siku na viongozi wetu wakuu, Rais Kikwete, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wakuu wa mikoa, sasa inakuwaje Kandoro agome kulizungumzia?

Hii inaonyesha wazi kwamba kama Kandoro amefikia hatua hii, inawezekana wazi kwamba yule mdudu anayesumbua vichwa vya Watanzania ‘ufisadi’ ameingia katika michango hii.

Viongozi wetu wamezoea kusema kwamba fedha zilizochangwa zinatumika kama ilivyokusudiwa, wakati huwa kinyume chake, na kuwa ‘maumivu’ kwa waliochanga fedha hizo.

Wiki iliyopita tulisikia ofisa mtendaji mmoja mkoani Arusha alihukumiwa miaka 10 kwenda jela, baada ya kutafuna karibu sh laki nane zilizochangwa na wananchi. Kwa hili, nasema vyombo vya dola vimefanya kazi nzuri, sasa Kandoro naye atusomee tu ukweli wa mambo.

Tunasema Kandoro, hivyo sivyo, mwaka huu kuna wanafunzi watahitimu elimu ya msingi na sekondari na mwakani wanatakiwa kuendelea, tutakuhukumu kwa kauli yao.

Mwenyewe utaanza kuwafuata hao unaowafukuza ili wakusaidie.

Napenda kumalizia kwa kusema, Kandoro iga mfano wa wenzako waliokutangulia, akiwamo Yusuf Makamba na wengine ambao hata usiku wa manane walikubali kupigiwa simu na kuulizwa maswali mbalimbali ya kitaifa.

Hivi kweli jamani, kama leo hii wana habari wakikataa kuandika habari za Dar es Salaam, Kandoro ataelewa kinachoendelea ndani ya mkoa wake? Tunasema muda wa ubabe katika karne ya 21 umepitwa na wakati, unapaswa ubadilike.

Mungu ibariki Tanzania ili siku moja tuone viongozi wanakubali kukosolewa kwa ajili ya manufaa ya Watanzania.
 
Back
Top Bottom