Kandoro akerwa wajawazito kutozwa fedha wanapojifungua | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kandoro akerwa wajawazito kutozwa fedha wanapojifungua

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kilimasera, Jan 8, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Jan 8, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  SERIKALI imesisitiza kwamba wajawazito wanatakiwa kupata huduma za kujifungua bila ya kulipia katika hospitali zote za serikali na kwamba ni makosa kuwataka wanunue baadhi ya vifaa.

  Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya afya ulioandaliwa na Bohari ya Dawa (MSD).
  Kandoro alisema vitendo vya wafanyakazi wa sekta ya afya hususan hospitalini kuwadai wajawazito fedha ama vifaa vya kujigungua vinaiabisha serikali na kwamba havina budi kukoma.

  Alisema serikali wakati wote inasisitiza suala la wajawazito kupata huduma bure , lakini cha kusikitisha ni kuona wanaendelea kuteseka na aliwataka wafanyakazi wa hospitali za umma nchini kuacha mara moja tabia hiyo.

  “Isaidieni Serikali kuitoa aibu kwa umma kwa kuwa imekuwa ikitoa maagizo, lakini hayatekelezwi, mama mjamzito anaambiwa apeleke vifaa wakati wa kujifungua kitu ambacho hakitakiwi na hii inasababisha lawama nyingi ambazo zinaelekezwa kwa Serikali, hivyo saidieni katika hili,” alisema Kandoro.

  Aidha Kandoro aliwataka watumishi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na wengine kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa wana dhamana kubwa ya kuhakikisha afya za Watanzania zinakuwa imara.
  Semina hiyo iliyoandaliwa na MSD iliwajumuisha waganga wakuu wa wilaya, wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, wafamasia na wadau wengine wa afya katika kanda ya ziwa.

  Kandoro alizungumzia tatizo la wizi wa dawa kwamba limeanza kuwa sugu huku wananchi wakikosa dawa na kuelekeza lawama zao kwa serikali kutowafikishia dawa kama wanavyohitaji.

  “Kuna malalamiko ya wizi wa dawa na kuwepo kwa malalamiko haya ina maana kuna ukweli ndani yake, tangulizeni uzalendo kwa nchi yenu kwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa kuwa Watanzania wanahitaji huduma yenu ili afya zao ziwe imara muda wote na waweze kuchangia katika kazi mbalimbali,” alisema Kandoro.

  Alisema miongoni mwa watumishi wa sekta hiyo wamesahau uzalendo na wanatumia nafasi walizonazo kwa kujinufaisha wao, hivyo akasisitiza kuwa hicho ni kitendo cha aibu na kinahitaji kukemewa.

  Aidha, alisema wadau wa sekta ya afya wanatakiwa kutoa elimu kwa jamii ili iweze kujenga utamaduni wa kuthamini kinga kabla ya tiba kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza hata ongezeko la wagonjwa katika magonjwa mbalimbali.

  Kandoro aliitaka mamlaka ya chakula na dawa TFDA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuondoa dawa zilizoko sokoni ambazo zimekwisha muda wake ama zile ambazo tayari zimezuiliwa lakini pia kubaini watoa huduma wa dawa hizo kama wana utaalamu wa kutosha.
  “Wenye dhamana ya kukagua wafanye kazi yao haiingii akilini kumwona mtu asiye na ujuzi wa dawa akiwa dukani akifanya kazi hiyo,utawaua Watanzania bila sababu ya msingi,” alisema Kandoro .

  Naye Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na shughuli za kanda wa MSD, Cosmas Mwaifwani alisema malalamiko ya kutokuwa na dawa katika baadhi ya vituo yanasababishwa na watendaji wasiokuwa waaminifu ambao pia wanashiriki katika wizi wa dawa.

  Alisema kuwa wao kama MSD wanakabiliana na tatizo hilo kwa kuimarisha ulinzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa lakini pia kuvunja mtandao ya wafanyakazi wezi.

  Kutokana na hali hiyo alitoa mwito kwa wananchi wanapokumbana na matatizo yanayoihusu MSD kuwasilisha kero zao haraka iwezekanavyo ili zishughulikiwe haraka badala ya kusubiri wanasiasa na kuwaeleza matatizo hayo.
   
Loading...