Kanal Bacar katolewa, Vip kuhusu Kony na Nkuda?

The Fixer

JF-Expert Member
Mar 3, 2008
1,365
593
Kanal Bacar katolewa, Vip kuhusu Kony na Nkuda ???

KWA wanaofuatilia kwa karibu suala la uvamizi wa kisiwa cha Anjouan, Comoro bila ya shaka watakuwa wameisikia taarifa ya redio ya Marekani (Voice of America) iliyoonyesha jinsi Tanzania inavyojiimarisha kama nchi yenye nguvu na ushawishi mkubwa katika eneo hili la Afrika.
Jumatatu iliyopita, redio hiyo ilionyesha namna rais Jakaya Kikwete anavyopanda chati katika eneo hili la Pembe ya Afrika. Kuchaguliwa kwake Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) mapema mwaka huu kuliashiria hilo.
Tayari baadhi ya watu wameanza kumtoa kasoro Kikwete kutokana na hatua ya AU kuidhinisha kupelekwa jeshi Comoro. AU imepeleka majeshi yake huko ili kuikomboa Anjouan, kisiwa kilichokuwa kinashikiliwa na Kanali Mohamed Bacar.
Tayari majeshi hayo yamekirejesha kisiwa hicho chini ya himaya ya serikali ya muungano wa Comoro.
Wapo waliopinga matumizi ya kijeshi. Hawa ni pamoja na Afrika Kusini. Binafsi, naunga mkono mtazamo huu, kutokana na ukweli kuwa daima nguvu za kijeshi hazileti mafanikio ya kudumu.
Kiongozi wa kisiasa na wa ki-imani wa India, aliyeshiriki katika kuleta uhuru kwao miaka ya 1940 aliwahi kusema: “Napinga utumiaji nguvu kwa azma yoyote ile, kwa sababu iwapo nguvu itaonekana kuleta mafanikio, basi mafanikio hayo ni ya muda tu, lakini uovu utakaofuatia ni wa kudumu.”
Kwa upande mwingine, utumiaji wa nguvu hautokani na maamuzi huru. Inajulikana wazi kuwa AU haina uwezo wa kifedha kugharamia harakati za kijeshi.
Kwa mfano, tunaambiwa vifaa na sehemu kubwa ya fedha zilizogharamia uvamizi wa Anjouan, zilitolewa na Ufaransa. Kidogo tu ndio walitoa nchi wanachama wa AU ikiwamo Libya.
Ufaransa imekuwa inajiingiza katika migogoro ya Comoro mara kwa mara tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1975. Hadi sasa, Ufaransa inakishikilia kisiwa cha Mayotte.
Wakazi wa kisiwa hiki, walipiga kura na wakaamua kubakia chini ya Wafaransa, koloni la zamani la Comoro, ingawa serikali huru ya Comoro na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), uliapa kukikomboa.
Hadi leo hii, si kwa njia ya kijeshi, wala ya mazungumzo, bado Mayotte haijakombolewa. Si Kikwete wala kiongozi mwingine yeyote aliyethubutu angalau kutamka neno “kupeleka jeshi Mayotte” ili kuiondoa Ufaransa katika ardhi ya Afrika.
Kwa hakika, nchi nyingi zilizopata uhuru barani Afrika, pamoja na utajiri lililonao bara hili, bado wananchi wake wanasumbuliwa na umasikini mkubwa. Hiyo inatokana na viongozi wengi kujilimbikizia mali. Pengine hilo ndilo lililowafanya wananchi wa Mayotte kuamua kubakia chini ya ukoloni.
Sasa swali la kujiuliza: kama Ufaransa inatoa fedha kugharamia “ukombozi” wa kisiwa cha Anjouan, nchi gani itainua mdomo kutaka ukombozi wa Mayotte?
Viongozi wa Afrika wanataka kusema kuwa wameitupilia mbali azma yao ya kuikomboa Mayotte? Ni jambo la ajabu kuwa AU inapokea fedha Ufaransa kuikomboa Anjouan, huku ikiiacha Mayotte. Sijui kama Kikwete ana ubavu wa kuhoji.
Kutokana na hali hiyo, anaonekana kama anatumiwa tu na nchi za Magharibi kwa maslahi yao. Inampasa aangalie vizuri kabla ya kuadhirika kama ilivyomtokezea Mobutu Sese Seko wa iliyokuwa Zaire.
Maana hebu fikiria. Je, iwapo Ufaransa isingegharamia uvamizi wa Anjouan, Kikwete angekuwa na ubavu wa kung’ang’ania uvamizi? Hapa pia kuna suala la undumila kuwili katika kufanya maamuzi.
Kwa mfano, kama ni kuwang’oa viongozi waasi wanaoshikilia maeneo mbalimbali barani Afrika, mbona haijafanya hivyo Sahara Magharibi ambako utawala wa Morocco unakalia. Bado Morocco si mwanachama wa AU.
Mbona haijamuondoa Joseph Kony wa Uganda? Mbona haijamgusa Laurent Nkunda wa DRC? Mbona AU imenyamaza kwa Ibrahim Coulibaly wa Ivory Coast? Mbona imeufyata kwa waasi wengine wanaoshikilia maeneo ya Ethiopia, Chad, Sudan (Darfur) na wanamgambo wa kiislam wa Somalia?
Kuna utata kuhusu mgogoro wa Darfur, kwani AU inashikilia kupeleka majeshi ya kulinda amani. Amani gani inayolindwa wakati makundi mbalimbali yangali yanapigana na serikali ya Khartoum na hayataki kusaini mkataba wa amani?
Je, hawa wana tofauti gani na Kanali Bacar?
Lakini kutokana na maamuzi ya AU kusukumwa na nje, ndiyo maana imejikuta ikikwama Darfur.
Rais Hassan Al-Bashir hakubali kufuata masharti ya Marekani kwa hivyo Marekani inawaona waasi wa Darfur ni halali na kwamba wana haki ya kupigana na serikali ya Khartoum.
Na katika kutimiza azma yao, akina George W. Bush wamebuni fitina mbaya zaidi, kwamba majeshi ya serikali ya Khartoum yanafanya mauaji makubwa jimboni Darfur yanayofanana na yale ya kimbari au yale ya Bosnia.
Kwa kuwa na ushawishi mkubwa wa maamuzi kwenye Umoja wa Mataifa (UN), hasahasa Baraza la Usalama, Marekani imefanikiwa kushinikiza vikwazo dhidi ya Sudan.
Inadai kwamba nchi hiyo inafanya “mauaji kwa raia wake Darfur.” Maazimio hayo hayataji kabisa “mauaji ya kimbari.”
Hii ni tofauti na nchi nyingine kama vile Chad au DRC, ambako Marekani huona ni halali majeshi ya serikali kupigana na waasi.
Tanzania pia imekubali kutuma vikosi kulinda amani Darfur, na bila ya shaka hili lilizungumzwa wakati Bush alipozuru Tanzania Februari mwaka huu, na kufanya mazungumo ya faragha.
Wasiwasi uliopo ni kwamba kwa kiasi gani Kikwete atakubali kutumiwa na madola tajiri, hasa Marekani?
Wakati Kikwete na Bush wanatia saini mkataba wa kuipatia Tanzania msaada wa dola 700 milioni za Marekani, baadhi ya wachunguzi wa mambo walisema fedha hizo zina jambo, maana haijatokea Marekani ikatoa fedha nyingi bila ya kuweka akiba kwa ajili ya maslahi yake baadaye. Ingali mapema kuanza kuvitambua vitakavyokuja?
Mh Kikwete anatumika vibaya sana na Mataifa ya Magharibi hasa Marekani lakini natamani siku ambayo noa yao itakapo kuwa Talaka !

Source; Mwanahalisi.
 
Now you see the very best of America in Tanzania and Africa at large !
 
Back
Top Bottom