Kamuhanda aondolewa Iringa

PISTO LERO

JF-Expert Member
Mar 8, 2011
2,819
1,454
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema amefanya mabadiliko ya makamanda na wakuu wa Upelelezi wa Jinai, huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda akirejeshwa makao makuu ya jeshi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso nafasi ya Kamuhanda, ambaye hivi karibuni alipandishwa cheo na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), inachukuliwa na Kamishna

Msaidizi wa Polisi (ACP), Ramadhani Mungi ambaye alikuwa Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa Maalumu wa Kinondoni, Charles Kenyela amehamishiwa Makao Makuu na atakuwa kwenye Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Arusha (ACP), Camilius Wambura. Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa, DCP Ally Mlege aliyekuwa Makao Makuu ya Polisi amehamishiwa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa, ACP Duwan Nyanda, ambaye yuko Makao Makuu ya Upelelezi atakuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Arusha.

Kamuhanda na Mwangosi

Wadau wa sekta ya habari na wanaharakati hawatamsahau Kamuhanda alipokuwa Kamanda wa Mkoa wa Iringa kutokana na tukio la Septemba 2, mwaka jana wakati polisi mkoani humo walipomuua Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi katika Kijiji cha Nyololo.

Mwandishi huyo alikufa hatua chache alipokuwa Kamuhanda ambaye kabla, alishuhudia polisi wake wakimshambulia kwa kipigo Marehemu Mwangosi.

Mwangosi na waandishi wengine wa habari walikuwa wakifuatilia mvutano wa polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kilikuwa kikitaka kufungua tawi lake katika Kijiji cha Nyololo, wakati polisi walikuwa wakizuia kufanyika kwa uzinduzi huo.

Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, Kamuhanda alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa Chadema wakamatwe lakini wafuasi wa chama hicho walipinga na yeye aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi.

Kamuhanda ni kati ya watu wanaotuhumiwa kusababisha kifo cha Mwangosi baada ya kutajwa na Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi na ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Kamanda huyo wa zamani anatuhumiwa kuvunja Sheria ya vyama vya siasa, kifungu cha 11 (a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za Chadema wakati yeye hakuwa na dhamana hiyo katika eneo husika.
 

Attachments

  • kamuahdan.jpg
    kamuahdan.jpg
    12.7 KB · Views: 95
Back
Top Bottom