Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,391
- 39,484

SIPENDI tena sitaki kusikia eti Rais wetu Jakaya Kikwete, alitakiwa aingie kwenye mtumbwi kuvuka Mto Ruvuma kwenda kuhudhuria sherehe za uhuru wa Msumbiji.
Tena mtumbwi wenyewe uwe wa kusukumwa na upepo. Zaidi ya yote, sitaki kusikia chaguo lake jingine siku hiyo lilikuwa ni ngalawa ya kasia!
Katika ziara yake mkoani Ruvuma, iliyomalizika siku chache zilizopita, Rais Kikwete alitakiwa kwenda kufungua daraja la Mkenda na hatimaye avuke kuelekea Msumbiji kushiriki sherehe za uhuru wa nchi hiyo.
Alipofika hapo darajani kumbe ni asilimia 35 tu ya daraja ilikuwa imekamilika na hakukuwa na dalili yoyote ya daraja hilo kukamilika ndani ya dakika chache za msafara wa rais.
Matokeo yake, Rais Kikwete, akalazimika kuuruka utepe wa ufunguzi na kwenda kungaza macho bila kufungua daraja hilo au kuvuka ngambo kwenda kwa watani zetu Msumbiji.
Baadaye alipohutubia wananchi alielezea jinsi alivyojisikia kuhusu suala la kuvuka mto kwa mtumbwi, alinukuliwa akisema: Nikakatazama kale kaboti kaupepo nikasema mmh, mimi Mkwere sijui kuogelea, afadhali Membe, maana mwenzangu kaoa huko Mbamba Bay ataogelea.
Ni kutokana na hisia zake hizo leo nimejikuta nazungumzia hili ambalo limetokana na maneno hayo. Rais Kikwete aliona mara moja kuwa yeye kwa hakika si mtu wa majini, licha ya kukaa karibu na Bahari ya Hindi, pamoja na ujanja wake wote, lakini si mwogeleaji.
Kilichonikera mwenzenu si rais kushindwa kutumia mtumbwi au kukiri kuwa hawezi kuogelea, bali ni ule uwezekano kuwa hadi leo karibu wiki mbili baadaye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, anapigiwa saluti! Kinachonikera, mkuu wa Itifaki bado ni yule yule!
Hivi hawa wawili peke yao walikuwa wanafikiria nini hata kutoa wazo kuwa rais atumie mtumbwi wa kusukumwa na upepo wakati tuna dege letu la sh bilioni 50 lililogongwa na gari la watu wa Usalama wa Taifa na hatuna hata kaboti ka umeme ka kumvusha rais?
Hivi wale watendaji waliohusika na maandalizi ya safari hiyo kwa nini wanaendelea kutesa na kulipwa mishahara kwa fedha za walipakodi wa taifa letu?
Hivi kama Rais Kikwete angeamua kujikaza kisabuni na kuingia kwenye mtumbwi halafu mtumbwi ungepinduka (mitumbwi ina kawaida ya kupinduka ikibeba marais na walinzi wao!) na rais wetu maskini wa Mungu hajui kuogelea na yule mpambe wake anayemfuata kila anakokwenda, angefanya nini, kumpigia saluti? Hivi, walikuwa na maboya ya kuogelea kweli?
Ningekuwa mimi fulani kabla sijaondoka pale kuna watu wangefungasha mizigo yao kurudi kijijini na kusahauliwa na mfumo wetu. Huu ni uzembe uliotukuka, ambao tuzo yake ni lupango kwa kuhatarisha maisha ya rais! Lakini, hii ni Tanzania, uzembe unazawadiwa na kutowajibika kunatukuzwa!
Lakini kilichotokea Mto Ruvuma ni mfano wa hali halisi ya uongozi wa taifa letu. Tanzania ipo upande mmoja wa maisha na inataka kuvuka kuelekea mafanikio, neema na heri.
Lakini viongozi wetu wanaogopa kuingia kwenye mtumbwi uitwao uongozi. Wanaogopa kufanya maamuzi magumu ambayo yanaweza kuharibu sifa zao na hata kuhatarisha maisha yao katika sanduku la kura.
Wote kama Kikwete wanabakia upande na kuishia kusema: Nikaangalia uamuzi wa kuchukua, nikaona eh, mimi mzembe, nitaweza vipi kuwaambia hawa ukweli na kuwatimua kazi? Nitawaacha kina Mwanakijiji wapige kelele kwa maana wapo kijijini!
Taifa letu linahitaji uongozi wa dhati, kwani sasa uongozi huo hauonekani. Leo hii tunaambiwa kuna mpango wa Canada kuja na mapendekezo ya kulinda makampuni yao kama Barrick Gold, ili yasikumbane na mapendekezo ya mabadiliko ya sera ya madini yanayoletwa na Kamati ya Jaji Mark Bomani. Waziri mkuu aliulizwa wiki moja iliyopita na hakujua kinachoendelea!
Leo hii watu wanasubiri ripoti ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, wakati hakuna aliyempa maagizo ya kuandika ripoti ya kuiwasilisha kwa rais!
Leo hii tunajivunia vimaendeleo vya simu za mkononi na internet, wakati maisha ya watu wetu katika takwimu mbalimbali hayajanyanyuka sana. Leo watawala wetu wanataka tuimbe sifa za maendeleo wakati walioendelea ni wao na vizazi vyao.
Lakini tukikosoa tunaambiwa tumezidi kukosoa, ukweli wao wanaufahamu. Wanataka waandishi wasomee fani hiyo wakati wao hawajajiamulia kusomea uongozi. Hivi wamesahau kuwa waliotufikisha hapa kama taifa si waandishi na wasiosoma? Waliotufikisha hapa, wamerundikana serikalini, bungeni na kwenye taasisi kibao, ni wale walio na BA, MA, PhD na kila aina ya vyeti vya sifa?
Hivi Tanzania imefikia hapa kwa sababu haina waandishi wasomi au viongozi wasiosoma? Hivi aliyesaini mkataba wa Buzwagi ana shahada gani? Je, yule aliyesimamia wizi wa Benki Kuu na watu walio chini yake wameishia darasa la nne?
Hivi waliotunga sheria ya Usalama wa Taifa na wale waliopitisha muswada wa sheria ya madini kule bungeni hakuna hata mmoja ambaye ni profesa humo?
Kujaribu kuona kuwa tatizo la Tanzania ni la waandishi ni kutafuta kisingizio. Mzigo huu mnaubeba wenyewe viongozi na kama woga wa Rais Kikwete kupanda mtumbwi wa upepo ni mfano, ni kweli kuwa viongozi wetu mna matatizo. Mnaogopa kupanda mitumbwi ya uongozi ambao unaendana na maamuzi magumu.
Mmebakia kusakizia kina Membe wenu na kuwaacha wengine wafanye yale ambayo ninyi wenyewe yamewashinda, siyo kwa sababu hamuwezi bali mnaogopa kujaribu, kwa kuwa mnaweza kupinduka!
Tanzania, nchi yetu inahitaji uongozi wa kweli; kuna kila dalili kuwa Rais Kikwete ni mwanasiasa kama wengine, na tunu ya uongozi hana. Nimefuatilia na sijaona dalili yoyote ya kuonyesha maono kwa taifa na kuliamsha kufikia linapotakiwa.
Jukumu la kuliongoza taifa linamuangukia rais kwa namna ya pekee kuliko waziri mkuu, waziri au mbunge yeyote. Baba wa Taifa alisema hivi katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: Na katika makosa makubwa ya maadili na utendaji, mwenye jukumu la wazi wazi la kuwadhibiti wahusika ni rais, na mawaziri wake wanapofanya makosa makubwa, badala ya kujiuzulu, wanaanza kufanya hila na kutafuta visingizio vya kutofanya hivyo.
Aliongezea na kusema: Ni kazi yake rais mwenyewe, asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza kumsaidia rais kumnongoneza waziri wake kujiuzulu; lakini hawezi kumsaidia kumfukuza waziri wake. Hiyo ni kazi ya rais peke yake. Asipoifanya, kosa ni lake peke yake.
Ni wazi kuwa Rais Kikwete hataki kuingia kwenye mtumbwi wa uongozi na maamuzi magumu. Katiba (Ibara 36) inasema wazi kuwa watumishi wa serikali wanafanya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa niaba ya rais na zaidi ya yote bado ana uwezo wa kusimamia nidhamu ya watumishi wa serikali yetu.
Sasa inapotokea kuna watu kama Mama Mbega kule Ruvuma, ambao wanamuandalia rais mtumbwi wa kusukumwa na upepo kwenda Msumbiji, bado wapo madarakani. Wakulaumiwa si Mbega, bali ni rais mwenyewe, kwani ni yeye aliyetoa baraka kwa mama huyo kuendelea kuwapo hapo.
Kuna watu wanasema na kurudia mara nyingi kuwa: Rais ana nia nzuri ya kwenda ngambo lakini ni hawa aliowatuma kukodisha mtumbwi ndio wana matatizo. Kuna watu wanaamini kabisa kuwa Rais Kikwete anaangushwa na watendaji.
Watu hawa wanashindwa kuelewa kuwa mwenye jukumu na uwezo wa mwisho wa kuajiri watu hawa ni rais! Wakati umefika tuite kijiko, kijiko; rais wetu pamoja na sura yake nzuri na tabasamu lake la nguvu lililotufanya tumpigie kura, kwa hakika kwenye suala la uongozi si kiongozi.
Yawezekana ana kipaji cha kuvutia watu lakini kwenye kutuongoza kuelekea mafanikio na neema, kwa hakika tukubali kuwa tumeliwa, tusubiri mwaka 2010.
Tumshukuru kwa jitihada zake zote, lakini kwa hakika kwenye mtumbwi hataingia, kwani yeye ni Mkwere, hajui kuogelea! Tuwaache wengine wakate mawimbi, naye abaki kuangalia kutoka ngambo.
Na kwa kadiri ambavyo watuhumiwa wa ubadhirifu uliofanyika kwenye akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA), wanaendelea kunata, ndivyo anavyoonekana asiyeingia kwenye mtumbwi wa uongozi; kwa kadiri serikali yake ilivyoshindwa kuitisha uchunguzi huru na kukaribisha taasisi ya kimataifa ya Scotland Yard kuchunguza mazingira ya safari, ajali na kifo cha Mbunge wa Jamhuri ya Muungano na kutegemea polisi ambao wenyewe nao wanatakiwa kuwa mashahidi, ndivyo mtumbwi wa taifa letu utakavyoendelea kuwabeba kina Membe!
Ndiyo, ukweli na usemwe. Mtumbi alioukataa Kikwete kwa hakika unapelekwa na upepo; unasukumwa na nguvu nje yake! Hakuna nguvu ndani yake isipokuwa kelele za wananchi na taasisi za nje ya nchi.
Ni mpaka pale Rais Kikwete atakapoamua kwa makusudi kabisa kukataa mtumbwi na kutaka meli ambayo yeye ni nahodha na yuko tayari kuyakata mawimbi na kuipeleka mv Mafanikio kulekelea kwenye neema.
Vinginevyo, kama nilivyowahi kusema huko nyuma, kwa mtindo huu wa kukaa ngambo na kukodolea wengine kwenye mitumbwi, kwa hakika asishangae kama atakuwa ni rais wa mhula mmoja katika historia yetu. Kwa nini?
Jibu alilitoa Baba wa Taifa na ninanukuu (kutoka kitabu kile kile): Kama uongozi ni mbovu, upo kama haupo, au upo kwa masilahi ya wenyewe, watatokea watu waujaze uwazi uliopo; hauwezi kuachwa wazi hivi hivi.
Lakini uongozi mbovu ni kama mzoga, una tabia ya kukaribisha mafisi na nzi. Na kama Mwalimu (nikiwa mwanafunzi wake), niseme kuwa: Ole wake Tanzania, Tusipoisaidia, niwezalo nimefanya, kushauri na kuonya.
Kama nahodha anaogopa kushika usukani wa mtumbwi wetu, tuangalie nahodha mwingine mwaka 2010 na kama hatumuoni, bora tutafute mtumbwi mwingine na nadhodha mpya, kwani safari bado ipo.
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com au
nipigie simu: 1 248 686 2010
Last edited by a moderator: