Kampuni ya Alibaba yaleta mapinduzi makubwa duniani katika kuendesha biashara ya mtandaoni

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
微信图片_20230530085122.jpg


Tunapozungumzia soko la biashara ya mtandao wa internet duniani, basi bila shaka nchi ya kwanza inayokuja kwenye vichwa vya watu wengi ni China. Kwa sasa China imeliteka soko hili na kuwa kinara duniani, ikizalisha karibu asilimia 50 ya miamala duniani.

Soko la biashara ya mtandaoni la China liliibuka miaka 20 iliyopita. Idadi ya watu walionunua na kuuza bidhaa kwenye mtandao wa internet ilianza kukua kutoka sifuri mwaka 2000 hadi zaidi ya milioni 400 kufikia mwaka 2015, na kulipiku soko kubwa la biashara ya mtandaoni la Marekani. Katika kipindi hiki kampuni kubwa kama vile JD.com na Alibaba ambayo majukwaa yake ya biashara yanajulikana kama Taobao.com, Tmall na Alibaba.com, ziliibuka na kuendesha biashara hii kwa ufanisi mkubwa ndani na nje ya China.

Kwa watu ambao wanatembelea na kujionea wenyewe namna kampuni hizi zinavyofanya kazi na kushuhudia jinsi teknolojia inavyoleta mapinduzi yake duniani, basi naweza kusema kuwa wana bahati kubwa sana. Katika safari yangu mjini Hangzhou, mkoani Zhejiang, ambako ndiko yalipo makao makuu ya kampuni ya Alibaba, nami nilikuwa miongoni mwa watu waliobahatika. Nilipoarifiwa kuwa tutatembelea kwenye kampuni hii, kwa kweli furaha yangu ilikuwa haina kifani. Ni muda mrefu nilikuwa na hamu sana ya kujionea kwa macho yangu utendaji kazi wa kampuni kama hizi, kwani siku zote tumezoea kufanya biashara tu kwenye mtandao bila kujua biashara hizi zinaendeshwa ama zinasimamiwa vipi na kampuni hizi kubwa.

Cha kuvutia zaidi ni kwamba mbali na kuona mchakato mzima yaani tangu bidhaa zinapohifadhiwa, kupokea oda, kusafirishwa na kufikisha mahali husika, pia tumepata kuelezewa hadithi ya mwaanzilishi wa kampuni hii ambayo inatoa msukumo hasa kwa wajasiriamali ambao wanaanza biashara zao kutoka chini kabisa.

Mwanzoni mwa mwaka 1999, Jack Ma aliyekuwa mwalimu pamoja na wenzake, wakiwa katika ukuta mkuu, waliapa kwamba watajenga kampuni ambayo siku moja dunia itajivunia nayo. Ni kweli wahenga hawakukosea waliposema “Penye nia, pana njia”, kwani wakiwa na ari na azma kubwa ya kutimiza ahadi yao, walifanikiwa kuifikisha kampuni ya Alibaba kimataifa, na kutoa mchango mkubwa kwa kubadilisha namna tunavyonunua na kuuza bidhaa ama hata kutoa huduma kwa ujumla.

Awali maendeleo ya biashara ya mtandaoni yalionekana zaidi katika maeneo ya mijini tu, lakini baada ya serikali ya China kutoa sera ya kuunganisha vijiji na biashara ya mtandao wa internet, maendeleo haya kwa sasa yanaonekana hadi maeneo ya vijijini. Lengo kubwa la kuanzisha sera hii ni kukuza maendeleo ya uchumi wa vijijini na kupunguza pengo la kiuchumi la vijijini na mijini.

Akituelezea namna kampuni ya Alibaba ilivyofanyia kazi sera hii, muelekezaji wetu alisema kampuni hii ilishiriki kwa kiasi kikubwa kutoa mafunzo ya kuendesha biashara mtandaoni, ikiwafunza wanavijiji kufanya matangazo ya biashara zao ama mazao yao moja kwa moja mtandaoni. Wakulima na wajasiriamali wa vijiji mbalimbali vya China sasa wamefaidika na matunda ya sera ya kuunganisha vijiji na biashara ya mtandao wa internet, na wengi wao kutajirika kupitia kuendesha biashara zao kwenye jukwaa maarufu sana hapa China la taobao.

Kwa sisi ambao tunatoka Afrika, pia tulipashwa habari njema kwamba juhudi za Alibaba hazikuishia China tu, bali zilivuka mipaka na kuwafikia hadi wajasiriamali wa Afrika. Wakati mwanzilishi wa Alibaba, Jack Ma, alipotembelea Afrika kwa mara ya kwanza miaka kadhaa iliyopita, aligundua mambo mengi yanayofanana kati ya Afrika ya sasa na China ya kipindi alipoanzisha Alibaba. Akihamasishwa na shauku na hamu ya wajasiriamali wachanga wa Afrika, aliona atumie fursa hiyo kuifunza Afrika kile alichojifunza katika kujenga uchumi mkubwa zaidi kupitia biashara ya mtandaoni.

Kwa mawazo yake, kile kinachoonekana kama hasara, ukosefu wa ajira kwa vijana, ukosefu wa miundombinu n.k, zilikuwa fursa muhimu katika zama za dijitali. Hivyo mwaka 2018, kwa mara ya kwanza wajasiriamali 29 kutoka nchi 11 za Afrika walikuja China na kupokewa na wenyeji wao kampuni ya Alibaba, ambapo walishiriki kozi ijulikanayo kama “eFounders Fellowship” na baadaye kuwa chachu ya mabadiliko ya kidijitali.

Aidha kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19, mafunzo ya awamu ya pili yaliyoendeshwa na Kampuni ya Alibaba kwenye mtandao wa internet kuanzia Oktoba 11 hadi Novemba 10 mwaka 2022, yalishirikisha zaidi ya wajasiriamali 360 kutoka Afrika. Mwamko huu wa kuunganisha vijiji na biashara ya mtandao wa interenet, umezipa hamasa hata nchi nyingine zinazoendelea zenye wakazi wengi wa vijijini, kama vile Misri, India na Vietnam, ambazo hivi karibuni zilitangaza mipango kama hiyo ya upanuzi wa biashara ya mtandaoni.

Alibaba imekuwa ikiongeza juhudi maradufu kwa vijana wa Afrika. Hii ndiyo sababu Mfuko wa Jack Ma ulianzisha Tuzo ya “Africa Netpreneur” na mpango wa “Alibaba eFounders”. Katika kipindi cha miaka kumi ijayo, mfuko huu utatambua na kusaidia wajasiriamali 100 wa Afrika kwa kutoa ushauri, mafunzo na kuwekeza jumla ya $ 10 milioni.
 
Back
Top Bottom