Kambi Maalum ya Uchunguzi na Matibabu ya Moyo yafanyika Iringa

BigTall

JF-Expert Member
Mar 9, 2022
422
1,049
Picha 1.JPG
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Elizabeth Meli akimpima shinikizo la damu mwilini (BP) raia wa Switzerland Lans Sottwals aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) leo kwa ajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano inayofanywa na wataalam hao kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.

Wananchi wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kutumie fursa ya uwepo wa madaktari bingwa wa moyo kujitokeza kwa wingi kuchunguza moyo kupitia kambi maalum inayofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Dkt. Alfred Mwakalebela wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo inayofanyika kwa siku tano lengo likiwa ni kufikisha huduma karibu kwa wananchi.

Dkt. Mwakalebela alisema kupitia kambi hiyo wananchi watapata fursa ya kupimwa vipimo vyote vikubwa vya moyo, kupata dawa kwa wale watakaokutwa na magonjwa ya moyo na wengine watakaohitaji uchunguzi zaidi watapewa rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Picha 3.JPG
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimwelezea mwananchi wa Iringa Imelda Harrison namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) kwa ajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo leo katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa IRRH.

“Tukipata wataalamu kama hawa katika Hospitali yetu kunasaidia kuwachunguza kwa kina zaidi wagonjwa na baada ya hapo wataalam hawa watatuachia wagonjwa hao kwa ajili ya kuendelea na kliniki hapa kwetu hivyo kupunguza tatizo kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa awali”, alisema Mwakalebela

Dkt. Mwakalebela alisema kupitia wataalam waliotoka JKCI wanaenda kuwaonyesha njia wataalam wa IRRH ya namna ya kuwachunguza wagonjwa wa moyo pamoja na kuwafuatilia mara kwa mara ili kwapamoja waweze kuwafuatilia kwa karibu na kuwapa huduma stahiki.

“JKCI imekuwa na utaratibu wa kupeleka huduma karibu na wananchi ili waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi na sasa ni zamu yetu wananchi wa Mkoa wa Iringa, tunaahidi kushirikiana nao kuwasaidia wananchi wetu”, alisema Mwakalebela.

Kwa upande wake Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallagyo alisema magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio yanayoongoza kwa kusababisha vifo vingi ulimwenguni na katika mazingira ya Tanzania magonjwa hayo yanaonekana yakiongezeka kwa kasi.

“Wataalam wa JKCI tupo Iringa kwa ajili ya kufanya vipimo na huduma za kibingwa za moyo hivyo tukiwa na utaratibu wa kuchunguza afya zetu na kugundua mapema inakuwa rahisi kutibu na kuwa na matokeo mazuri zaidi”, alisema Dkt. Pedro.

Dkt. Pedro alisema mwamko wa wananchi kuchunguza afya zao bado uko chini lakini kupita kambi maalum za matibabu ya moyo wanazofanya toka wameanza mwitikio umekuwa ukiongezeka huku lengo likiwa kuwasaidia wagonjwa na kujenga desturi kwa watu kuwa wanachunguza afya zao mara kwa mara.

Picha 4.JPG
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akimfanyia mgonjwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) leo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku tano inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).

Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Gerald Isambo alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kifua mara kwa mara na kutokupata utatuzi nini kinachomsumbua hivyo kupitia kambi hiyo amepata fursa ya kupima moyo wake.

Isambo alisema kuwa hakuwahi kupima moyo tangu kuzaliwa kwake hivyo fursa hiyo aliyoipata imempa mwamko wa kufanya uchunguzi wa afya yake mara kwa mara na kuacha tabia ya kuchuguza afya yake pale tu anapoumwa.

“Naomba kupitia Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa huduma kama hizi na nyingine za kibingwa ziendelee kutolewa mara kwa mara kutupa nafasi sisi wananchi ambao hatuwezi kuzifuata mahali zilipo kuchunguza afya zetu na kuwa na desturi ya kujichunguza”, alisema Isambo
 
Back
Top Bottom