Kambayuwayu ka Kikwete kalikotaka kuwa tetere! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kambayuwayu ka Kikwete kalikotaka kuwa tetere!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, May 4, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  May 4, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  bird270_std.jpg
  Na. M. M. Mwanakijiji

  Nilisimuliwa kisa cha mbayuwayu ambaye alikuwa anaishi katika shamba la Mkulima mmoja huko Ukwereni. Mbayuwayu huyo aliishi na wenzake katika maisha ya kutegemea nafaka na mbegu mbalimbali zinazopatikana katika shamba la mkulima huyo. Pamoja naye walikuwepo ndege wengine wengi ambao nao walipata afueni ya maisha yao katika shamba hilo zuri la Mkwere. Miongoni mwa ndege hao walikuwepo tetere ambao walionekana kama ndio ndege wapendwa wa mwenye shamba.

  Mkulima huyo alikuwa anahakikisha kuwa tetere wanakula na kunenepa pamoja na ndege wengine kama vile kwale na kukumaji. Na walikuwepo pia dudumizi, vigong'ota, zokoyogo na kurumbiza. Ndege wengine wote hawa walifurahia maisha yao katika shamba la Mkwere isipokuwa mbayuwayu.

  Mbayuwayu alikuwa analalamika mara kwa mara kuwa maslahi yake hayaangaliwi na kulindwa kama ya kina tetere. Mara kwa mara mbayuwayu amejikuta akijitafutia riziki yake hata nje ya shamba, amekuwa akikwepa mitego yeye mwenyewe na hata anapowindwa na paka ilimbidi atafute mbenu endelevu za kujilinda. Katika maisha hayo mbayuwayu alijikuta anaishi maisha ya "kiujanja ujanja" ilimradi mdomo uende kinywani.

  Mbayuwayu walikuwa wanalalamika kuwa tetere walikuwa wameachwa kula kwa uhuru wote na wamefikia kula hata vile vidogo vya mbayuwayu. Walilalamika kuwa hata wakionda kuna punje zimedongoka ilikuwa ni vigumu kwani tetere walifika mara moja na kwa kutumia mabavu waliweza hata kuwatimua mbayuwayu hao kwa kuwatishia kuwadonyoa.

  Kwa vile waliona kuwa maslahi yao na maisha yao yanatishiwa na tetere na mwenye shamba inaonekana hajali basi mbayuwayu kwa kutumia umoja wao wa Mbayuwayu (UMBA), waliamua kuitisha mgomo wakidai maslahi zaidi na nafasi zaidi za kutambuliwa na mwenye shamba na kupewa maslahi ambayo yanakaribiana na yale ya tetere. Tetere waliachwa kunawiri, na hata kujengewa matundu ya kisasa ili wao na makinda yao waishi maisha ya raha na amani wakati mbayuwayu wakiachwa kujijengea viota vyao kwenye kona za nyumba na majengo mbalimbali humo shambani. Tetere walikuwa wanaruhusiwa kukaa pamoja na kuimba kwa pamoja huku wakitamba kwa mwenye shamba kuwa;

  Kuku mfupa mtupu
  Mimi nyama tupu!

  Hivyo mbayuwayu wakaamua kutangaza mgomo ili kumshinikiza mwenye shamba kuangalia maslahi yao. Zikiwa zimebakia siku chache za mgomo kufika mbayuwayu walijikuta wameweza kuwashawishi mbayuwayu wa jamii tofauti kuweza kushiriki mgomo huo na kwa pamoja wakaanza kutangaza juu ya ujio wa mgomo wa mbayuwayu wote shambani. Na hata siku ya sherehe ya ndege wote wafanyao kazi zilipofika mbayuwayu waliandamana wakiwa na mabango yaliyosomeka:

  Mwenye shamba tukumbuke
  Mbayuwayu na sisi tuna haki
  Kwanini tetere peke yao?

  Walipita siku hiyo kwa umoja mkubwa japo mwenye shamba na yeye aliamua kufanya sherehe ya ndege wengine ambapo tetere, dudumizi, kurumbiza na wenzake walihudhuria kwa furaha wakiburudishwa na miziki mbalimbali. Katika sherehe ya mbayuwayu msimamo uliendelea kutolewa kuwa ni lazima wagome kwani japo wao ni vindege vidogo na ambavyo vinaonekana havina maana ukilinganisha na Mbayuwayu lakini vina sehemu katika maisha ya shamba, kwani ndio vinatafuna vijidudu vidogovidogo vya hatari, huchangamsha ndege wengine na husaidia sana katika kuhakikisha usalama wa shamba kwani vina uwezo wa kwenda sehemu mbalimbali hata zilizondogo na vina mwendo kasi sana kuweza kuwakwepa adui.

  Hata hivyo, mwenye shamba alikasirika alipoona kuwa mbayuwayu kweli wamedhamiria kuitisha mgomo. Yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya mgomo huo mkubwa kuanza mwenye shamba akaitisha mkutano wa ndege wazee na kuanza kuwahutubia kwa ukali akielezea ni kwanini mbayuwayu hawastahili maisha ya tetere!

  Akizungumza kwa ukali na akifoka hadi mapovu yakimtoka mdomoni mwenye shamba aliwaambia mbayuwayu kuwa yeyote atakayegoma atakiona cha moto kwani wawindaji wote wameruhusiwa kutumia bunduki, manati na hata mizingi ili kuhakikisha kuwa mbayuwayu hawaleti madhara katika shamba kwa kugoma kwao. Aliwahakikishia kuwa shamba lake haliwezi kuwapa maslahi kama ya tetere! Aliwahakikishia kuwa serikali yake ya shamba lake haina uwezo wa kutoa maslahi kwa mbayuwayu kwani uwezo uliopo hadi hivi sasa ni kuweza kuhakikisha tetere, dudumizi na kwale wanaendelea kuishi maisha ambayo wanastahili.

  Aliwaambia wazi kuwa hata wakigoma hatokuwa na uwezo wa kuwapa maisha ya kitetere kwani wao ni mbayuwayu! Na akawaambia kuwa endapo watagoma basi paka wote wa shamba watapewa leseni ya "kuwaleta wakibisha walipuliwe". Huku akishangiliwa na ndege wazee ambao wengine hata manyoya walikuwa hawana tena na macho yao yakisinzia kwa uchovu, mwenye shamba aliapa kuwa kama anahitaji kura basi hizo za mbayuwayu siyo za lazima kwani tetere na wengine wako tayari kumpatia kura zao!

  Ndege wote shambani walishangaza na ukali wa mwenye shamba. Walishangaa kwanini hajawahi kuwa mkali hivyo kwa dudumizi na mwewe ambao wamekuwa wakila hadi vifaranga vya mbayuwayu? Walishangaa ilikuwaje mwenye shamba awe mkali kwa mbayuwayu ambao walitaka tu wakumbukwe kama tetere na wapewe maisha yanayokaribiana na kitetere wakati ndege wakubwa na wenye nguvu wakiwa wanatambaa shambani na kula mbegu na matunda yote mtini huku wakiwafukizia mbali mbayuwayu?

  UMBA ilishangazwa na ukali wa mwenye shamba kwa mbayuwayu; ukali ambao hawajawahi kuuonesha dhidi ya ndege waharibifu wa mazao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakienda na kuchimbua hata mbegu zilizopandwa na kula na kugawana? Ilikuwaje mwenye shamba awe mkali hivyo kwa mbayuwayu?

  Hata hivyo, baada ya tafakari mbayuwayu wakaamua kusitisha mgomo wao; walijua kuwa kwa kadiri ya kwamba ndege wamegawanyika kwenye shamba la mkulima, ndege hawawezi kupata haki zao. Mbayuwayu walijua kuwa kwa kadiri ya kwamba bado hawajaweza kuungana na kuonesha umoja wa kudai maisha kama ya tetere na kurumbiza basi hawawezi kufurahia maisha ya shamba hilo. Kutokana na uelewa huo mbayuwayu walidhamiria kuona kuwa shamba hilo linaenda kwa mtu mwingine au apewe mkulima mwingine mwenye kujali maslahi ya ndege wote siyo wale tu wenye sauti nzuri na rangi za kuvutia kama tetere!

  Mbayuwayu waliamua kurudisha majeshi yao nyuma huku wakiruka ruka kivyao wakiimbiana na kupeana pole kwa sauti za chini ambazo mwenye shamba hakuweza kuzisikia;

  Pole mbayuwayu
  Maskini mbayuwayu
  Laiti ungelikuwa tetere!
  Labda angekujali Mkwere!
   
 2. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #2
  May 4, 2010
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  umesomeka babu!
  TUPEANE POLE
   
 3. Aza

  Aza JF-Expert Member

  #3
  May 4, 2010
  Joined: Feb 23, 2010
  Messages: 1,672
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 145
  mh kweli kazi ipo
   
 4. Junius

  Junius JF-Expert Member

  #4
  May 4, 2010
  Joined: Mar 11, 2009
  Messages: 3,183
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 133
  He was right.
   
 5. Tusker Bariiiidi

  Tusker Bariiiidi JF-Expert Member

  #5
  May 4, 2010
  Joined: Jul 3, 2007
  Messages: 4,757
  Likes Received: 181
  Trophy Points: 160
  Maskini Mbayuwayu... Wakati huo huo Mkwere aliwaalika Ma-bundi,Ma-tai,Ma-mbuni na Ma-Jongwe kuja shambani kwake kufanya Mkutano mkubwa ambao baadhi ya sehemu chache warukiazo Mbayuwayu hao zitafungwa kwa masaa 6 kwa siku...
   
 6. B

  Boramaisha JF-Expert Member

  #6
  May 4, 2010
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 820
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Mzee, ukiona kobe katulia kimya ujue anatunga sheria. Pamoja na machungu ya 'mbayuwayu' imebidi nicheke hadi mbavu kukaribia kukatika! Udumu Mzee wewe, sio kama wale waliokuwa wakipiga makofi kwa kulazimishwa/kulazimika!
   
 7. N

  Natasha Ismail JF-Expert Member

  #7
  May 4, 2010
  Joined: Jul 14, 2008
  Messages: 511
  Likes Received: 153
  Trophy Points: 60
  MKJJ U A ARE A PHILOSOPHER,Tumekusoma mkuu.
  Anasema atatuua,Tulimchagua atuue.
   
 8. SMU

  SMU JF-Expert Member

  #8
  May 4, 2010
  Joined: Feb 14, 2008
  Messages: 7,933
  Likes Received: 2,085
  Trophy Points: 280
  Who?
   
 9. MANI

  MANI Platinum Member

  #9
  May 4, 2010
  Joined: Feb 22, 2010
  Messages: 6,412
  Likes Received: 1,871
  Trophy Points: 280
  Mbayuwayu hana thamani kwa mwenye shamba kama hao Matai,Mabundi na Majongwe kwani hukutana nao huko kwenye misele yake ya ughaibuni.
   
 10. c

  cerezo Senior Member

  #10
  May 4, 2010
  Joined: Sep 14, 2008
  Messages: 155
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 33
  Mmh...how appropriate at this time
   
 11. Mzizi wa Mbuyu

  Mzizi wa Mbuyu JF-Expert Member

  #11
  May 4, 2010
  Joined: May 15, 2009
  Messages: 5,499
  Likes Received: 1,080
  Trophy Points: 280
  Inasikitisha, lakini ndiyo hivyo Mkwere ameahidi kutumia shortgun kumuua mbayuwayu akigoma. Bora uhai kwanza, Mbayuwayu atapata tu njia nyingine ya kumkomesha Vasco...
   
 12. The Dreamer

  The Dreamer JF-Expert Member

  #12
  May 4, 2010
  Joined: Feb 2, 2009
  Messages: 1,280
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Mbayuwayu mie sina thamani...nitamwoa mkwere niwe tetere!
   
 13. Masanilo

  Masanilo JF-Expert Member

  #13
  May 4, 2010
  Joined: Oct 2, 2007
  Messages: 22,303
  Likes Received: 168
  Trophy Points: 160
  Mimi shorwe Kibwenzi jamii ya Mbayuwayu, acha niepusha ubawa wangu!
   
 14. B

  Boramaisha JF-Expert Member

  #14
  May 4, 2010
  Joined: Apr 29, 2009
  Messages: 820
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  Unajua Mkwere huyo mwenye shamba siku zote anapenda sana sifa kutoka kwa hao Ma-bundi na Ma-tai etc kiasi kwamba aliona itakuwa fedheha kubwa hao aliowaalika wakija shambani kwake na kukuta mbayumbayu wamecharuka mitaani na mabango mikononi. Wakati akifoka na kila alipokuwa akipigiwa makofi alidhani kwamba wale wote walikuwa wakimshangilia kwa dhati lakini kumbe hata miongoni mwa hao washangiliaji walikuwemo mbayuwayu ambao walikuwa hawana jinsi ila kufuata mkumbo wasijeonekana wasaliti!
  Jambo jingine la kushangaza, mbayuwayu walikuwa na malalamiko yao na madai ya msingi ambayo wala mwenye shamba hakutaka kuyagusia, kuyazungumzia wala kutoa majibu akawa ameng'ang'ania kwenye kipengele kimoja tu ambacho alikiona ndicho kitaweza kuwaumbua mbayuwayu waonekana hawana sababu yoyote ya kunung'unika!
  Hata hivyo, cha msingi ni kwamba ujumbe kutoka kwa mbayuwayu umeishamfikia mwenye shamba kwa kishindo ndio maana aliamua kuwa mbogo na kutoa vitisho kwa mbayumbayu wasio na hatia yoyote ile. Hilo nalo la ujumbe wa madukuduku ya mbayuwayu kumfikia mwenyeshamba yapaswa liwe la faraja kwa mbayuwayu.
   
 15. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #15
  May 4, 2010
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,844
  Likes Received: 1,110
  Trophy Points: 280
  ukali huo angekuwa ameuonyesha kwa mafisadi wa EPA, Richmond, Rada, Meremeta et al., kwenye madini, uvuvi nk rasilimali zetu zingepona.
   
 16. H

  Hofstede JF-Expert Member

  #16
  May 4, 2010
  Joined: Jul 15, 2007
  Messages: 3,584
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 0
  Tatizo la wawindaji ni kama la mbayuwayu, kwani wao pia wanaruhusiwa kuwinda vindege vidogovidogo tu ambavyo vinakula punje moja ama mbili ila tetere na kurumbiza ambao wao hufakamia na kurundika katika viota vyao vya shambani na hata kupeleka nje ya shamba hawaruhisiwi kuwindwa. Laiti kama wangejua kuwa wawindaji nao ni jamii ya mbayuwayu basi wasingekubali kuwinda mbayuwayu wenzao.
   
 17. M

  Mundu JF-Expert Member

  #17
  May 4, 2010
  Joined: Sep 26, 2008
  Messages: 2,719
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 145
  waliyasema wakale
  wanyuma hakai mbele
  wanyingi hupewa tele
  wakidogo hunyang'anywa

  masikini mbayuwayu
  mkwere hajali huyu
  mbayuwayu si mbuyu
  nani anayekujali?

  labda kwa wenu umoja
  wabara na waunguja
  vinginevyo mtavuja
  mtakuja donyolewa

  mbayuwayu kaza kamba
  ivute bila kuremba
  kwa baraka za muumba
  vita mtakujashinda
   
 18. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #18
  May 4, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  yaani, ile jazba aliyoinoesha jana sijawahi kumuona akiwa nayo kwenye suala lolote nyeti la kitaifa..!!
   
 19. nkosikazi

  nkosikazi JF-Expert Member

  #19
  May 4, 2010
  Joined: Mar 11, 2010
  Messages: 354
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 35
  This time JK alikuja na nguvu kubwa ya hoja na data. Aliwaanika pabaya hao viongozi wa mbayuwayu na kuwaita waongo (whichis a bit too strong and undiplomatic)lakini hoja ilifika mahali pake. Viongozi wa wafanyakazi wanatakiwa kukaa na kujiangalia kama wanazo hoja zinazoweza kukubaliwa na kupambwa na data. Haiwezekani wafanyakazi wakala mapato yote ya nchi na kuacha hamna hela ya maendeleo mengine. tatizo ninaloliona ni kwamba wakati hizo hela za kuwapa hazipo lakini mbayuwayu wanawaona wateule wakiendelea kununua mashangingi na kujilipa posho nono. JK angefaulu zaidi kama angesema maneno yote hayo lakini akaonyesha mfano kwa kubana matumizi kwa watendaje wake vile vile. Inaumiza sana kuona kiongozi ananunua landcruiser V8 bila aibu yoyote.
   
 20. Tusker Bariiiidi

  Tusker Bariiiidi JF-Expert Member

  #20
  May 4, 2010
  Joined: Jul 3, 2007
  Messages: 4,757
  Likes Received: 181
  Trophy Points: 160
  Aliionyesha hasira kama hizo pale Airport wakati jamaa wa itifaki waliposhindwa kuandaa gari la Mapokezi kwa ajili ya First Lady wa mgeni wake,Pia pale alipokuja mkurugenzi wa wilaya ya Ngorongoro... Basi...
   
Loading...