Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,802
- 11,961
Kamati ya Maudhui ya TCRA ikiongozwa na Makamu Menyekiti wake, Ndugu Joseph Mapunda, imetembelea ofisi za Jamii Forums ikiwa na lengo la kujifunza mambo kadha wa kadha kuhusu Taasisi na kujionea namna huduma inavyotolewa kwa wananchi. Kamati hiyo ilipokelewa na watendaji wa Jamii Forums wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Ndugu Maxence Melo.
Wakiwa katika ofisi za Jamii Forums, Wajumbe wa Kamati ya Maudhui wamepata fursa ya kujifunza kuhusu utendaji wa Taasisi ya Jamii Forums inayofanya kazi kama Taasisi isiyo ya Kiserikali (NGO), na kupata uelewa wa namna inavyofanya uchechemuzi wa masuala anuai ikiwemo Haki za Kidijitali, Uhuru wa Kujieleza, Demokrasia, Uwajibikaji, Utawala Bora nk.
Katika kikao cha pamoja na watendaji wa Jamii Forums, Kamati ya Maudhui ilipata fursa ya kueleweshwa mambo yafuatayo:-
- Historia ya Jamii Forums (Taasisi) na mahusiano kati ya Taasisi na JamiiForums.com (tovuti)
- Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Taasisi (2020-2024)
- Sera ya Uhariri na jinsi inayotumiwa na Wasimamizi wa Maudhui wa JamiiForums
- Muongozo wa Uendeshaji wa Mijadala ndani ya JamiiForums.
Watendaji wa Jamii Forums waliweza kutoa mapendekezo ya uboreshaji kwa Kamati ya Maudhui hususani katika usimamizi wa watoa huduma na utoaji wa elimu kuhusu kanuni na taratibu za mawasiliano.
Akizungumza wakati wa kikao na Kamati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji, Maxence Melo alisisitiza kuangaliwa upya Kanuni za Maudhui Mtandaoni (2020) na kurekebishwa ili zisiue ubunifu nchini. Kamati imesema imepokea mapendekezo hayo na yatafikishwa sehemu husika.