Kamati ya madini yageuka kama maigizo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Posted Date::11/28/2007
Kamati ya madini yageuka kama maigizo


*Mwingine aandika barua ya kujitoa
*Aliyejitoa wa kwanza, wa pili wahudhuria

* Iddi Simba ahamaki waandishi kuwako ndani

* Bomani awataka wajumbe kuweka maslahi ya taifa mbele

Muhibu Said na Mwanaid Omary
Mwananchi

KAMATI ya Kuangalia Upya Mikataba ya Uchimbaji Madini nchini, imeanza rasmi kazi zake jana, huku wajumbe wake wawili walioomba kwa Rais Jakaya Kikwete kujitoa , wakishiriki.

Wajumbe hao, ni Peter Machunde kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mkaguzi wa Mahesabu kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Mahesabu ya PriceWaterhouse Coopers, David Tarimo.

Hata hivyo, wakati hayo yakijiri, katika moja ya kazi zake, kamati hiyo imepanga kukutana na wenyeviti wa kamati zilizoteuliwa katika siku za nyuma kuchunguza kuhusu madini ili kupata uzoefu wao katika suala hilo, kuanzia Jumatatu na Jumanne wiki ijayo.

Kamati hizo, ni ile ya Jenerali Robert Mboma iliyoundwa mwaka 2001, ya Brigedia Mang'enya ( 2003), ya Dk Kipokola (2004) na ya Masha (2006).

Machunde alitangaza kujiuzulu wiki iliyopita kwa madai ya kukerwa na maneno ya baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kumtaka ajitoe katika kamati hiyo kwa madai ya kuwa na urafiki wa karibu na mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya nne.

Taarifa za Tarimo kuomba kujitoa , zilitangazwa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo , Jaji Mark Bomani wakati akifungua kikao chao cha kwanza katika Ofisi za Bunge, jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa hiyo, Jaji Bomani, alisema Tarimo aliwasilisha barua ya kujitoa katika kamati hiyo kama mjumbe kwa madai kwamba kampuni yake inatumiwa na baadhi ya makampuni ya madini, hivyo, ana wasiwasi ushiriki wake unaweza kuleta mgongano wa maslahi, lakini alisisitiza kuwa, atakuwa tayari kutoa ushauri utakapohitajika.

Hata hivyo, Jaji Bomani alishindwa kusoma barua ya Tarimo, baada ya mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Iddi Simba kumzuia asifanye hivyo mbele ya waandishi wa habari kwa madai kwamba, iwapo jambo hilo litawafikia wananchi, linaweza kuibua malumbano mitaani.

" Watupishe kwanza waandishi wa habari, tujadili sisi wenyewe, pengine baadhi yetu tunataka (Tarimo) asijitoe," alisema Iddi Simba na kuungwa mkono na Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige.

Kutokana na ushauri huo, Jaji Bomani aliwataka waandishi wa habari wasitangaze habari hizo kwa muda huo na badala yake wasubiri hadi kamati imalize majadiliano kuhusiana na jambo hilo, kisha mchana watapewa taarifa.

Maelekezo hayo ya Jaji Bomani, yalipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, aliyesema kuwa, haoni ni busara kuwaita waandishi wa habari kila baada ya kikao na kuishauri kamati iwaruhusu wakaripoti yale waliyokwishayapata kwa muda ule.

Mapema, Tarimo alikataa kuzungumza chochote alipoulizwa na Jaji Bomani kama ana jambo la kuzungumza kuhusiana na hilo na kumuomba mwenyewe (Bomani) azungumze badala yake.

Awali, akieleza sababu za kuendelea kushiriki kwenye kamati, Machunde alikiambia kikao cha kamati kuwa, amelazimika kufanya hivyo kwa kuwa hadi kufikia jana alikuwa hajapokea majibu kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ya kuomba kujitoa katika kamati hiyo.

" Mpaka sasa sijapata jibu la ombi langu kwa Rais. Hivyo, nitakuwa mkosefu wa heshima kama sitashiriki katika vikao vya kamati kabla sijapata jibu kutoka kwa Rais," alisema Machunde.

Baadaye mchana, Jaji Bomani alikutana na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa, wajumbe walioomba kujitoa kwenye kamati hiyo, walishiriki kikao cha jana na kuongeza kuwa ana matumaini kuwa wataendelea kushiriki.

Hata hivyo, tofauti na alivyosema awali, alikanusha Tarimo kuwasilisha barua ya kuomba kujitoa, bali barua hiyo inahusu wasiwasi wa kushiriki kwake kwenye kamati.

" Tunatumai wasiwasi hautakuwapo, atafanya kazi vizuri na hakutakuwa na mgongano wa maslahi, " alisema.

Kuhusu wajumbe wengine waliotakiwa na Chadema kujitoa kwenye kamati hiyo kutokana na kutuhumiwa kwa ufisadi au mgongano wa maslahi, alisema katika kikao cha jana, hakukuwapo na majadiliano kuhusu wajumbe wengine zaidi ya Mchunde na Tarimo.

Jaji Bomani, alisema kikao cha jana ambacho kilihudhuriwa na wajumbe wake wote, isipokuwa wawili kutokana na kupatwa na udhuru, kili panga ratiba na kuafikiana namna kamati itakavyotekeleza majukumu yake.

Alisema mbali na kukutana na wenyeviti au wawakilishi wa kamati zilizoteuliwa katika siku za nyuma kuchunguza kuhusu madini, pia watakutana na wadau mbalimbali pamoja na umoja wa wachimbaji madini na kutembelea kwenye maeneo yenye shughuli za machimbo.

Jaji Bomani , alisema katika ratiba hiyo, pia watembelea nchi zenye sekta ya madini ili kujifunza namna wanavyoedesha shughuli za madini na kutoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni kabla ya kamati kukaa na kutafakari waliyoyapata na kuandaa ripoti watakayoiwasilisha serikalini katika muda muafaka.

Hata hivyo, alisema kutokana na muda na gharama kuwa finyu, watachagua nchi chache ambazo zimepata mafanikio katika shughuli za madini na kwamba, hadi kufikia jana walikuwa bado hawajakamilisha orodha ya nchi hizo na tarehe ya kuanza ziara hiyo.

Awali, akifungua kikao hicho, Jaji Bomani aliwapongeza wajumbe kwa kuteuliwa kwenye kamati, lakini akawapa pole kwa maelezo kwamba, jukumu walilopewa ni nyeti na zito.

Hata hivyo, alisema watafanya kazi kwa bidii, uaminifu wa hali ya juu ili mapendekezo yatakayotolewa na kamati yawe na maslahi mazito kwa taifa.

Aliwataka wajumbe wawe huru kutoa maoni yao wenyewe, na siyo ya kutumwa na chombo au taasisi au chama, kwani wameteuliwa kwa sifa binafsi.

" Tutoe fikra zetu na mependekezo yetu, tusiwe na ubinafsi, tutapelekea kupishana katika kutoa mapendekezo ya kamati. Tutoe mapendekezo ya kamati ili kazi yetu ifanyike kwa uwazi, siyo kwa siri siri. Pia katika ratiba yetu tutoe nafasi watu watoe mawazo yao hadharani na wakaribishwe wasomi watoe mawazo yao ili yafanyiwe kazi, " alisema Jaji Bomani.

Alisema kabla ya kutangaza mapendekezo yao, watashauriana na Rais Kikwete kwamba, wayatangaze au wampe ayapitie kwanza.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, alisema kazi iliyo mbele yao ni nzito, hivyo, akawataka Watanzania wawaombee kwa Mwenyezi Mungu wapate hekima ya kutoa maamuzi mazuri kwa kuwa, nia yao ni moja ya kujaribu kusaidia taifa kupata maslahi kutokana na utajiri wa madini uliopo nchini.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishina wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi Wizara ya Ardhi, Edward Kihundwa, Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe na mtaalamu wa masuala ya kodi na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo.

Kamati hiyo iliundwa na Rais Kikwete Novemba 13, mwaka huu na itatekeleza kazi yake kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo ni pamoja na kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta ya madini na kupitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali.

Mengine ni kukutana na taasisi zinazosimamia madini na wadau wengine na kutakiwa kutoa taarifa yenye mapendekezo na kupitia mikataba ya madini na nyaraka nyingine zitakazohusu migodi ya mikubwa nchini..
 
Back
Top Bottom