Elections 2010 Kamati ya kura ya maoni Z`bar yakwama kuanza kazi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Mwinyi%20makame%20Z%286%29.jpg

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.



Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia utekelezaji wa kura ya maoni itakayoamua kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, imekwama kuanza kufanya kazi kutokana na ukosefu wa fedha.
Kamati hiyo yenye wajumbe sita kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF), inahitaji Sh. milioni 300 ili iweze kutekeleza majukumu yake kabla ya kufanyika kura ya maoni mwaka huu.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alisema kamati hiyo imekwama kuanza kufanya kazi kutokana na matatizo ya ukosefu wa fedha na kulazimika kuomba msaada kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Kificho alisema EU imeonyesha nia ya kusaidia na ujumbe mzito kutoka umoja huo unatarajia kukutana leo naye mjini Zanzibar.
“Kikao chetu kitatawaliwa na ajenda kubwa kuhusu tatizo la fedha lililojitokeza na kukwamisha kamati yetu isiweze kufanya kazi zake haraka,” alisema Spika Kificho.
Alisema bajeti ya matumizi ya kamati hiyo, tayari imewasilishwa serikalini tangu ilipoundwa Machi, mwaka huu.
Spika huyo alisema miongoni mwa mambo yaliyopangwa kutekelezwa na kamati hiyo, ni pamoja na wajumbe wake kusafiri nje ya nchi kupata uzoefu kwa mataifa yanayotumia mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Aidha, alisema kamati hiyo itaangalia utaratibu utakaotumika katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu kura ya maoni, ambayo ndiyo itakayoamua hatima ya Zanzibar na serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema serikali inalishughulikia suala hilo.
“Siyo vizuri masuala ya Baraza na serikali kuzungumziwa kupitia vyombo vya habari, lakini suala hilo linashughulikiwa kwa utaratibu uliopo kati ya Baraza na serikali,” alisema waziri huyo alipozungumza na gazeti hili jana.Wajumbe wa kamati hiyo kutoka CUF, ni Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni, Abubakar Khamis Bakary, Zakia Omar Juma (Viti Maalum ) na Ahmed Nassor Mazrui wa kuteuliwa na Rais.
Wakati wajumbe kutoka CCM, ni Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheir, Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Ali Abdallah Ali na Ali Mzee Ali wa kuteuliwa na Rais.
Hata hivyo, CUF imesema haiamini kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) haina fedha za kuiwezesha kamati hiyo kuanza kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utekelezaji wa kura ya maoni.
Tayari Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesaini muswada wa sheria ya kuweka masharti ya kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu, lakini hadi sasa hajatangaza siku ya kufanyika kura hiyo.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom