Kamati Kuu ya CHADEMA ilikuwa wapi?

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
KAMA Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ina nguvu kweli ya kutoa uongozi wa chama kama ilivyofanya na kuchukua misimamo ya masuala mbalimbali hivi juzi ninaamini inahitaji kujibiwa walikuwa wapi hadi imefika leo hii?

Maswali ninayouliza hayana maana ya kwamba siungi mkono CHADEMA au nimebadilisha mawazo bali ninaamini kuna mambo ambayo yanahitaji majibu kwani tukiyaachilia hivi hivi yataendelea kujirudia.

Kuanzia Novemba 1 hadi Novemba 5 hii Kamati Kuu ilikuwa wapi wakati CHADEMA kilikuwa kinahitaji uongozi hasa wa kuamua nini cha kufanya wakati hali ya wasiwasi imeligubika Taifa?

Hawa ambao leo wameweza kupata muda wa kukaa, kujadiliana na kutoa maamuzi ambayo yanagusa chama katika nafasi mbalimbali walikuwa wapi wakati wanaCHADEMA, mashabiki na wananchi walipokuwa wanajiuliza nini kifanyike?

Wakati matokeo ya uchaguzi yameanza kutoka na ikaonekana kuna ucheleweshaji wa kimkakati hii Kamati Kuu ilikuwa wapi ili kuchukua msimamo?

Wakati ule jambo moja lilikuwa wazi sana kuwa hakukuwa na uongozi wa kitaifa wa chama uliokuwa kazini. Mtu pekee ambaye alikuwa na muda wa kufuatilia kinachoendelea kwa karibu alikuwa ni Dk. Willibrod Slaa ambaye alikuwa ni mgombea wa Urais!

Kwa siku tano, CHADEMA kilikuwa kama hakina uongozi wa kitaifa; siku tano muhimu na siku tano ambazo ziliamua matokeo ya uchaguzi. Wakati Dk. Slaa amejitokeza na kutaka tume isitishe kutangaza matokeo ya uchaguzi viongozi wengine wa CHADEMA walikuwa wapi na wajumbe wa Kamati Kuu walikuwa wapi?

Tatizo kubwa lililotokea wakati ule ni kukosekana kwa uongozi wa pamoja; Kabwe Zitto alikuwa kabanwa Kigoma, Freeman Mbowe alikuwa kabanwa Hai, Tundu Lissu kabanwa Singida Mashariki, John Mnyika kabanwa Ubungo n.k Lakini wazee wengine walikuwa wapi na walikuwa na uwezo gani wa kufanya kazi za Kamati Kuu?

Maana yake nini; wakati vita inaendelea na adui anashambulia hakukuwa na majemedari wa kujibu mashambulizi au kupanga mkakati wa kurudisha mashambulizi. Ninauliza hili kwa sababu kuna watu wanaanza kushangilia maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati Kuu ya CHADEMA na kuyaona kuwa ni muafaka. Yawezekana ndivyo yalivyo lakini ninaamini ni maamuzi ambayo hayakuwa ya lazima kwani yamecheleweshwa.

Kamati Kuu ilitakiwa itoe msimamo na uongozi wake kabla ya matokeo kutangazwa au mara tu baada ya kuonekana kuna matatizo. Kusubiri mwezi mmoja na nusu kutoa baraka ya msimamo ni ukosefu mkubwa wa kiuongozi.

Nimesema hivi kwa sababu sipendi tena sitaki ati Kamati Kuu ya chama kikuu cha Upinzani ifanye kazi kama Kamati Kuu ya chama tawala. Hasa baada ya kusikia kuwa KK ya CHADEMA nayo imeunda Tume ili kuleta umoja ndani ya chama. Yaani, CHADEMA wamenakili (kama kwa kuigizia) kile walichofanya CCM walipounda kamati ya Mzee Mwinyi ili kutafuta muafaka. Hivi kweli kulikuwa na ulazima huu au hawa watu wa Kamati Kuu bado wana mawazo ya kiCCM CCM hivi?

Kama kuna mgongano ndani ya CHADEMA ni mgongano ambao aidha unatokana na mfumo mbovu wa kushughulikia nidhamu au mgongano ambao ni matokeo ya uongozi wenye matatizo.

Hili la uongozi nitaligusa siku nyingine lakini ninachokiona ni kuwa badala ya kufanya haya mambo ya kiCCM, CHADEMA inahitaji kufikiria njia zake za kutatua kabisa matatizo ya aina ya ambayo yametokea.

Haiwezekani wabunge wachukue uamuzi halafu uamuzi huo ufutwe na KK kwa sababu ndicho chenye nguvu. KK kama ingekuwa ina nguvu hizo isingesubiri hadi hali ifikie wabunge wanapigiana kura ya kutokuwa na imani! Hii KK ingetakiwa kushughulikia matatizo na kuyamaliza badala ya kuyaahirisha.

Ninachosema ni kuwa Kamati Kuu ya Chadedma itajikuta inajitega kama CCM endapo itaendelea kufikiria ki CCM. Ni lazima waanze kufikiria namna mpya ya kutoa uongozi. Kama kuna kitu cha kujifunza ni kuwa huwezi kuwa na timu ya uongozi mzima wa taifa wote wanagombea huko mikoani na kusababisha kupwaya kwa uongozi wa kitaifa kama tulivyoona mara baada ya uchaguzi.

Wote ambao sasa wako mbele kuzungumza kama “viongozi” hawakuwapo wakati historia ilipowaita! Sasa leo wanapoketi kwenye viti vya enzi na kutoa uongozi sisi wengine tunawashangaa.

Walikuwa wapi wakati hasa walipohitajika?
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom