Kamanda Mambosasa awataka Polisi wasitafute makosa, na wale wa Pikipiki marufuku kutoza faini za makosa barabarani

dubu

JF-Expert Member
Oct 18, 2011
3,496
3,461
Polisi yasema askari wa pikipiki marufuku kutoza faini

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema askari wanaotembea na pikipiki maarufu kama ‘tigo’ hawana mamlaka ya kutoza faini kwa mtu aliyevunja sheria za barabarani.

Amesema jukumu lao ni kumkamata aliyevunja sheria na kumpeleka kwa askari wa usalama barabarani.

“Niwasihi wananchi, msikubali kutoa hela kwa hao askari hiyo itakuwa ni rushwa. Fedha unayompa inamfaidisha askari husika na familia yake. Jambo hili tunalipinga mno,” amesema Mambosasa leo Januari 18, 2018 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Redio Clouds.

Amesema kikosi hicho cha pikipiki hakikuanzishwa kwa ajili ya kukamata wanaovunja sheria barabarani na kuwatoza faini, kwamba askari wa usalama barabarani ndio wenye jukumu la kutoza faini na kutoa risiti.

“Kikosi cha pikipiki kilianzishwa kwa ajili ya kuangalia usalama na inapotokea kosa wanawajibika kumfikisha mhusika kwenye mamlaka inayosimamia usalama barabarani,” amesema.

Ametoa wito kwa askari wa usalama barabarani kutumia busara wakati wa kuteleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

“Tunaelekeza polisi asitafute makosa, asikusimamishe bila kujua kwanini amekusimamisha halafu anaanza kuhangaika kutafuta kosa. Tunaendelea kuwaeleza wenzetu kuwa busara inahitajika wakati wa kusimamia sheria,” amesema na kuongeza,

“Hawapaswi kuwaumiza watu. Askari unatakiwa kufikiria tu unamtoza faini mtu mchana kwa kuwa taa zake haziwaki sasa hapo anakuwa amefanya kosa gani maana ametembea mchana, labda ingekuwa usiku halafu taa haziwaki hapo sawa

======

Kama ulikuwa unaudhika kila ukiona askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, angalau sasa unaweza kuwa na ujasiri wa kukabiliana nao kisheria.

Ni kwa kutumia elimu iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambaye jana alitoa ufafanuzi wa jinsi askari hao, maarufu kwa jina la Trafiki, wanavyotakiwa kufanya kazi.

Amezungumzia jinsi trafiki anavyotakiwa kufanya iwapo atasimamisha gari yako, makosa anayotakiwa kuyahoji na hatimaye kukutoza faini kulingana na wakati na hata utendaji wa polisi wanaozunguka na pikipiki, maarufu kwa jina la tigo.

Na faraja zaidi ni kauli yake kwamba si kila kosa linastahili faini na kuwataka trafiki kuwa makini ili kuondoa malalamiko ya uonevu na kuwakandamiza raia.

Mambosasa alitoa kauli hiyo jana katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM na baadaye kuzungumza na Mwananchi kufafanua maelezo yake.

Alishangazwa na askari wanaokamata gari mchana kwa kosa la kutowaka taa na kutoza faini.

Alitaja makosa mengine kuwa ni askari kukamata gari bila kujua kosa la msingi na kulazimika kuanza kulikagua kwa lengo la kubaini kosa.

Pia alieleza kwamba askari wanaotumia pikipiki maarufu kama ‘tigo’, hawaruhusiwi kutoza faini baada ya kukamata gari.



Trafiki aeleze sababu

“Akisimamisha gari ni lazima akueleza sababu za kukusimamisha; kwamba anataka kukagua nini katika gari lako,” alisema Kamanda Mambosasa baada ya kuombwa na Mwananchi kufafanua kauli yake jana jioni.

“Nilichokimaanisha ni ile kusimamisha gari na kuanza kutafuta makosa bila kueleza sababu ya kukusimamisha.”

Trafiki wamekuwa na tabia ya kusimamisha gari, kuomba leseni na baadaye kuanza kukagua vitu kama stika ya bima, taa, gurudumu, mtungi wa kemikali za kuzimia moto na viakisi mwanga kwa ajili ya kuashiria gari bovu lililosimama barabarani.

Akipata kosa, askari huandika kuanzia Sh30,000 kwa kosa, jambo ambalo limesababisha madereva wengi kuingiwa na hofu kila wanapoona askari hao barabarani.

“Akisimamisha gari ni lazima aeleze sababu za kulisimamisha,” alisema Kamanda Mambosasa kujibu swali “trafiki atatambuaje kama gari lina bima au vitu vingine vya lazima katika gari.



Trafiki atumie busara

Mambosasa pia alisema trafiki pia anatakiwa kutumia busara kumtoza faini mtu ambaye gari lake lina matatizo ya taa kwa kuwa huenda hatumii gari hilo usiku unapoingia.

“Yapo makosa ambayo askari yeyote wa usalama barabarani anayesimamia sheria anaweza kujitathmini mwenyewe na kuona haina ulazima wa kumtoza mtu faini,” alisema.

“Kwa mfano gari langu nimeamua kutembelea mchana tu, ikifika usiku naliegesha. Kuna sababu gani ya kuwa na taa?

“Kwa hiyo ukinikamata kwa kosa la kutokuwa na taa mchana, nitakushangaa kwa kuwa sijavunja sheria. Wakati mwingine askari anapaswa kufikiria uamuzi wa kumtoza faini mchana kwa sababu ya taa.”

Alisema kama ni usiku ni wazi kuwa mhusika atakuwa amefanya kosa.

“Ili tusiingie kwenye malumbano, tunaomba wananchi watii sheria na pale inapotokea udhaifu wa askari kumbambikia kosa mhusika, (mwananchi) anatakiwa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo ili hatua zichukuliwe,” alisema.

Aliwataka askari kuacha kutafuta makosa kwa madereva kwa kusimamisha magari na kuanza kuyakagua.

“Unakamata gari halafu unaanza; mara washa taa; mara zima. Tunaendelea kuwaeleza wenzetu kuwa busara inahitajika wakati wa kusimamia sheria,” alisema.

Askari wa pikipiki

Kuhusu polisi kikosi cha pikipiki, Kamanda Mambosasa alisema wana haki ya kukamata gari au chombo chochote barabarani na kukikagua, lakini kuhusu utozaji wa faini jukumu hilo si lao, bali ni la trafiki.

“Anaweza kukukagua lakini linapokuja suala la kutoza faini, hana kitabu. Lazima akupeleke kwa wahusika ambao ni trafiki,” alisema.

Katika maelezo yake Clouds, Mambosasa alisema Jeshi la Polisi ni kwa ajili ya kulinda raia na mali zao, kusimamia sheria na si kukandamiza wananchi.

“Hawana mamlaka ya kutoza faini kwa mtu aliyevunja sheria za barabarani. Jukumu lao ni kumfikisha mtu huyo kwa askari wa usalama barabarani,” alisema.

Alisema kikosi hicho hakikuanzishwa kwa ajili ya kukamata na kutoza faini, bali kupambana na uhalifu. “Kutokana na foleni za Dar es Salaam, polisi ikaona busara kuwaweka askari hao tayari kwa ajili ya kuwahi kwenye matukio ya uhalifu na sio kukamata magari kama wanavyofanya sasa ingawa wanawajibika kushughulikia uvunjaji sheria unapotokea mbele yao,” alisema.

Aliwataka wananchi kutokubali kutoa fedha bila kupatiwa risiti kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kutoa rushwa.

Alisema jeshi hilo linaendelea kuwaelimisha askari wake kusimamia sheria na si kuwaonea watu.

Kauli yake imepokewa vizuri na wadau wa vyombo vya moto.

“Binafsi naona askari wa usalama barabarani wana haki ya kukagua magari kwa kuwa hilo ndilo jukumu lao,” alisema mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alipoulizwa na gazeti hili kuhusu kauli ya Mambosasa.

“Lakini nasisitiza kuwe na busara. Lengo si kuumizana, bali ni kuhakikisha sheria zinazingatiwa. Nitoe wito kwa wamiliki kuhakikisha magari yao yapo katika hali nzuri na madereva nao wasiingize magari mabovu barabarani.”

Kamanda Mambosasa pia alifafanua kuhusu tamko la kuzuia nguo fupi, akisema hilo ni kosa la kimaadili na si kisheria na hivyo Jeshi la Polisi haliwezi kulishughulikia kwa kuwa hakuna sheria inayozuia mavazi hayo.

~ Mwananchi
 
Duh huyu si ndie alisema kazi ya polisi ni kukamata tu na sio kumueleza mtu kosa derevaakajifunze shuleni makosa ni yapi hivyo wao wakikushika ni faini tu. .. leo kashashiba anasema polisi watumie busara.. nadhani account yake ni nene hana tena pa kuhifadhi minoti maana atatumbuliwa tu
 
Tigo sahv wanapita hadi mitaani kukamata watu wasiyovaa helmet ama kukaa mshikaki a kuwatoa fedha waliyowakamata

Ova
 
mi namshukuru mambosasa kwa kutuelimisha, hayo mengine sijui. kuanzia leo trafic akiniambia washa taa mchana nakataa au namwambia haziwaki, nione atanitoza faini kwa kosa gani. yaani halafu akinipiga mkono akaanza kuchungulia mara tairi mara bima mara kioo, ntamfundisha sheria maana mambosasa katuilimisha.HONGERA MAMBOSASA, SEBA AKULINDE
 
Sasa angejiongezea muda atuambie majukumu yao hasa ni yapi, kazi ya polisi nizijuazo mimi ni (to protect and serve) kulinda raia na mali zao.
 
“Niwasihi wananchi, msikubali kutoa hela kwa hao askari hiyo itakuwa ni rushwa. Fedha unayompa inamfaidisha askari husika na familia yake. Jambo hili tunalipinga mno,” amesema Mambosasa leo Januari 18, 2018 katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Redio Clouds.

“Hawapaswi kuwaumiza watu. Askari unatakiwa kufikiria tu unamtoza faini mtu mchana kwa kuwa taa zake haziwaki sasa hapo anakuwa amefanya kosa gani maana ametembea mchana, labda ingekuwa usiku halafu taa haziwaki hapo sawa

Mheshimiwa Rais alisema Askari kuchukua pesa kidogo ya kununulia Kiwi siyo vibaya.
 
Katika watu ninaowaheshimu Na kuwa karibu nao Ni maofisa wa polisi wengi Wao wapo polite. Lakini hawa askari wa vyeo vya chini Ni washenzi sana
 
Katika watu ninaowaheshimu Na kuwa karibu nao Ni maofisa wa polisi wengi Wao wapo polite. Lakini hawa askari wa vyeo vya chini Ni washenzi sana
Sio polisi tu hata jeshi, askari wa vyeo vya chini huwa wana mambo ya ajabu ajabu lakini maafisa huwa ni watu safi sana nahisi issue kubwa huwa ni Elimu.
 
Sio polisi tu hata jeshi, askari wa vyeo vya chini huwa wana mambo ya ajabu ajabu lakini maafisa huwa ni watu safi sana nahisi issue kubwa huwa ni Elimu.
elimu Ni kwa kiasi Fulani ila kikubwa Ni kutokana Na kitu kinaitwa chain of commands yaani askari wa chini wanapokea amri Na kutekeleza ila wale wa juu Wao ndo watoa amri kwa hiyo hawana haja ya kuwa Na hofu wanafanya mambo kwa weledi
 
Back
Top Bottom