Kama Zitto katumwa na Rais Kikwete; Jakaya Kikwete katumwa na nani? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kama Zitto katumwa na Rais Kikwete; Jakaya Kikwete katumwa na nani?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Apr 26, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 26, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Msomaji Raia

  Toleo la236
  25 Apr 2012

  MKUTANO wa nane wa Bunge umemalizika wiki hii mjini Dodoma ukiwa umeweka historia katika Taifa.

  Orodha ya matukio ni ndefu. Mimi nimechagua kujadili uamuzi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), kuamua kukusanya sahihi za theruthi moja ya wabunge, ili kumpigia Waziri Mkuu Mizengo Pinga, kura ya kukosa imani naye.


  Akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto alipendekeza njia ya kumpigia kura ya kukosa imani Waziri Mkuu ili ama kuwafanya mawaziri wajiuzulu wenyewe ili kumwokoa, au kukosa imani na Waziri Mkuu ili serikali nzima iwajibike.


  Baada ya kupata sahihi za wabunge zaidi ya theruthi moja, wakitoka vyama vyote vilivyo na wabunge isipokuwa UDP, Zitto Kabwe na wenzake wameiita hatua hiyo kwa jina la "Operesheni Uwajibikaji".


  Hatua ya Zitto Kabwe imeungwa mkono na wabunge wengi, kwa uwazi na kwa kificho. Hatua hiyo imeungwa mkono na Watanzania wengi mitaani na Serikali itafanya kosa kubwa sana kuidharau au kuibeza hatua hiyo.


  Umaarufu wa hatua ya Zitto na wote waliotia sahihi pendekezo hili lenye baraka za kikatiba na kanuni za Bunge, umeimarishwa zaidi na uzembe wa wazi wa Serikali na uamuzi wa hatari wa ama Waziri Mkuu au Rais kuahirisha Bunge bila kulitolea tamko suala la wabunge kukusanya sahihi ili kupiga kura ya imani kwa Waziri Mkuu Pinda.


  Hadi naandika makala hii, hapakuwa na dalili za Serikali kuchukua hatua yoyote kushughulikia malalamiko ya wabunge dhidi ya ufisadi na uzembe uliokithiri wa mawaziri wa Serikali ya Kikwete.


  Wakati watanzania wengi wameshuhudia wenyewe wabunge wa CCM wakichachamaa bungeni kulaani ufisadi unaofanywa na mawaziri; wakashuhudia "mshikamano wa muda" kati ya wabunge wa CCM na wale wa Upinzani katika suala hili, hapahitajiki akili za ziada kubaini mambo kadhaa yasiyopendeza mbele ya safari.


  Kwanza, Rais ajue anayepigiwa kura ya kukosa imani si Pinda bali ni yeye aliyemteua. Pinda alikuwa ni boya tu la kupitishia ujumbe ili umfikie Rais. Siamini kama ni uhaini kutabiri kuwa urais wa Kikwete uko mnadani. Pili, mawaziri waliotajwa hadharani kwa njia ya ripoti za wenyeviti wa kamati mbalimbali na kushutumiwa vikali na wabunge wa CCM, wamejeruhiwa na kupoteza kabisa madaraka ya kuongoza wizara zao. Ikiwa walishindwa kuongoza kabla ya kuvulia nguo hadharani, itakuwaje baada ya kuvuliwa nguo?


  Kujiuzulu kwa hiari yao au kwa Rais kutengua uwaziri wao haraka iwezekanavyo ingekuwa ni zawadi kubwa kwao kwa sasa. Hawa wamepoteza mamlaka na madaraka na daima watamkumbuka Zitto baada ya kupoteza hivihivi fursa aliyowapa.


  Tatu, Spika Anna Makinda aanze kutia maji ili anyolewe pale atakapodiriki kuwa kisiki cha kuzuia mabadiliko katika Serikali na jamii kwa ujumla. Umungu-mtu wa Spika ukiunganishwa na Umungu-mtu wa Rais kwa sasa unachochea hasira za wananchi na kutumika kurutubisha cheche za machafuko hapa nchini.


  Ilikuwa rahisi kwa Polisi kupambana na maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya Upinzani, lakini ni vigumu sana kupambana na maandamano yaliyoandaliwa na wananchi wenyewe! Kumwondoa Spika katika nafasi yake ni kumuepusha na aibu inayoweza kuufanya uzee wake uwe wa majuto.


  Nne, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwa mara nyingine amepoteza fursa ya kufanya jambo la kihistoria. Baada ya kudhalilishwa mara kadhaa na Rais wake, wabunge wa chama chake, mawaziri wake na Spika, angejiuzulu mwenyewe kuonyesha utii kwa Watanzania na waumini wa amani na mshikamano.


  Kilichobakia ni ama Rais amtose katika mabadiliko yanayokuja, au atoswe na wabunge katika kura ya kukosa imani naye. Hata kama yote mawili yatashindikana, historia itamhukumu kwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza kupigiwa kura ya kukosa imani na Bunge.


  Kama anabisha amuangalie Edward Lowassa. Pamoja na zigo la ufisadi alilobwagiwa na swahiba wake, bado kwa rekodi ya utendaji anamfunika Pinda na zaidi sana, atakumbukwa kwa kujiuzulu ili kuwajibika kumlinda Rais na chama chake. Uzembe wa Pinda na Kikwete unamsafisha Lowassa bila gharama za Lowassa mwenyewe.


  Sambamba na tafakuri yangu hapo juu, lipo suala limeibuka kutoka Ikulu kwa njia za ajabu. Watu wameeneza uvumi kuwa hatua ya mbunge Zitto Kabwe ina baraka za Rais Kikwete. Kwamba, kumekuwapo na mawasiliano ya mara kwa mara na ya karibu kati ya Zitto Kabwe na Rais Kikwete, na kwamba watu hao wanamlaumu Zitto Kabwe kuwa amechukua kazi yao.


  Tetesi hizo zinaendelea kudai kuwa kampeini ya Zitto inaweza kufanikiwa. Baada ya kung'olewa kwa Pinda, baraza litaundwa upya na Zitto atateuliwa kuwa Waziri mmoja "muhimu" katika baraza lijalo. Kwa mujibu wa mpango huo, Zitto baadaye atajiondoa CHADEMA na kuingia CCMna kwamba huu ni mkakati wa kuisambaratisha CHADEMA inayoonekana kushika kasi ya ajabu hapa nchini.


  Tetesi hizi zinafanana na nyingine zinazoenezwa na watu hao hao kuwa CCM inahujumiwa ndani kwa nia kukabidhi hatamu kwa CHADEMA pale muda wa Rais Kikwete utakapokoma.


  Pale baadhi ya makada maarufu wa CCM wanapohama na kujiunga na CHADEMA, watu hao wameendelea kudai kuwa makada hao wamesoma alama za nyakati na kuamua kutangulia CHADEMA ili wapambane na viongozi wao wa sasa kwa kuwa hata hao viongozi ni "CHADEMA" katika nyoyo zao!


  Wanachojaribu kusema watu hawa wachovu ni kuwa umaarufu wa CHADEMA umechangiwa na njama za chini chini za vigogo ndani ya CCM.


  Haichukui muda mrefu kugundua udhaifu wa tetesi hizi. Kwanza, ni upofu kudhani kuwa umaarufu wa CHADEMA unatokana tu na udhaifu wa uongozi ndani ya CCM, au hata wa Mwenyekiti Kikwete. Upofu huu utathibitika baada ya Kikwete kuondoka Ikulu. Ikiwa CCM haitafanya uamuzi wa kufa kwanza ili ifufuke kwa upya katika mioyo ya Watanzania, awepo Kikwete au mwingine, chini ya CCM hii, mambo yatazidi kuwa magumu.


  Pili, ni kujidanganya kwa kufikiri kuwa umaarufu wa CCM unaweza kuibuka kwa kupandikiza mgogoro ndani ya CHADEMA. Ufisadi wa CCM na Serikali yake ambao sasa unapigiwa kelele na wana CCM wenyewe, hauwezi kufunikwa kwa kupandikiza mgogoro wa kufikirika ndani ya CHADEMA.


  Ufisadi ni kigezo kimoja, na cha pekee kitakachoipeleka CCM kuwa chama cha Upinzani hata kama CHADEMA hakitakuwa maarufu.


  Hizi nadharia za "kutumwa" zimekuwa maarufu sana siku za karibuni. Wabunge wakichachamaa kukemea uzembe wa mawaziri-wametumwa au wamenunuliwa; Rais akishindwa kushughulikia matatizo ya Taifa na kupenda kusafirisafiri wakati Serikali inashikishwa adabu na wabunge – ametumwa au anaipenda CHADEMA.


  Zitto Kabwe akifanya hatua ya kizalendo kukusanya sahihi za kuungwa mkono ili Waziri Mkuu apigiwe kura ya kutokuwa na imani kwa kushindwa kuisimamia serikali–Katumwa na Kikwete.


  Wabunge wa CCM wakivutwa na uzalendo na kuamua kutanguliza maslahi ya Taifa badala ya maslahi binafsi au chama chao – wametumwa au wamenunuliwa na wanaoutaka urais wa Kikwete au wa mwaka 2015.


  Spika anapokariri kanuni badala ya kuzitafsiri kwa manufaa ya Bunge na Taifa –katumwa au kanunuliwa na waliomuweka. Kununuliwa na kutumwa umekuwa ni utaratibu mpya unaotumika kuficha uzembe hatari wa kufikiri na kuwajibika.


  Hatuhitaji muujiza kutambua kuwa matatizo ya Taifa letu ni makubwa kuliko uwezo wa Serikali na kiongozi wake. Pale kiongozi wetu anaposhindwa kushughulikia matatizo ya Taifa letu na kuyaita kuwa ni "upepo mbaya" si suala la kutumwa bali ni hukumu kwa Watanzania waliomchagua kiongozi huyo aliyeamua kuwa mganga wa kienyeji kuamini katika "upepo mbaya" badala ya kuwa kiongozi anayewajibika na kuwajibisha.


  Uongozi wa namna hii ndiyo maana unazidi kuhukumiwa kwa viwango vya chini kabisa kiuongozi pale vigezo kama dini, mkoa wa mtu na kundi lake vinapokuwa vigezo rasmi vya kuteuliwa kwa nafasi ya uongozi.


  Katika sakata hili nimeshuhudia kundi la wanasiasa muflisi katika korido za Dodoma wakihaha kuwabembeleza baadhi ya wabunge na kuwapigia simu kuwa wawalinde mawaziri fulani kwa kuwa ni wa dini yao.


  Aidha, nimeshuhudia wabunge fulani wakishutumiwa na wenzao kwa kile kilichoitwa kukosa uzalendo kwa kuwashutumu mawaziri wenye dini sawa na zao. Hawa nao wanatumwa na nani? Nabii gani? Mtume gani? Ni mtume na nabii gani anayebariki ufisadi wa kula damu na jasho la Watanzania?   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Apr 26, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Sasa nani ni mkombozi?
   
 3. AdvocateFi

  AdvocateFi JF-Expert Member

  #3
  Apr 26, 2012
  Joined: Jan 15, 2012
  Messages: 10,703
  Likes Received: 590
  Trophy Points: 280
  Tanx mleta mada kwani imeongea reality kuhusu haka ka kichaka ka kutumwa kwani watu wengi wamekuwa wakiwatetea mawaziri wachafu kwa kigezo cha dini mpaka juzi nimesikia kuna wazee fulani wakimlaani kabwe zitto kwa kitendo cha kumshinikiza mawaziri wajiuzuru kwani eti kitendo hicho nikumuungamiza muislamu mwenzie omary nundu na pia eti anashirikiana na wakristo kuiangusha serkali ya muslamu mwenzake Jk.
  My take
  kama watz tutaendelea na hiz hisia kahawa za udini kila muda, tutafika kweli?
   
 4. N

  Ndinani JF-Expert Member

  #4
  Apr 26, 2012
  Joined: Aug 29, 2010
  Messages: 5,413
  Likes Received: 734
  Trophy Points: 280
  Fisadi ni fisadi tu awe mkristo au muisilamu na madhara ya ufisadi wao ni machungu kwa wananchi wote wawe waislamu au wakristo!! Upumbavu huu wa kuwagawa watu kwa misingi ya dini au kabila ni sumu mbaya sana kwa maendeleo ya nchi yetu!
   
Loading...