Kama Rais john Magufuli angekubali kunisikiliza…

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
221
190
Kama Rais john Magufuli angekubali kunisikiliza…
Na Padre Privatus Karugendo,
Mwananchi
Toleo la 20 Julai 2016.

Chama cha Mapinduzi (CCM), kitakuwa na mkutano mkuu maalumu hivi karibu na kazi kubwa ni mwenyekiti wa sasa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuachia kiti hicho na bila shaka kitakaliwa na Rais John Magufuli.

Umekuwa ni utamaduni wa kuachiana nafasi hiyo ndani ya chama tawala. Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alimwachia Benjamin Mkapa, naye akamwachia Kikwete.

Hata hivyo, mwaka huu si wa uchaguzi ndani ya chama hicho.Si lazima rais wa nchi kuwa ndiye mwenyekiti wa chama. Hata Katiba yetu haisemi kwamba rais wa nchi lazima awe mwenyekiti wa chama.

Rais anaweza kuwa mwingine na mwenyekiti mwingine.Kule tunakoelekea inawezekana rais akawa mgombea binafsi ambaye hatakuwa na chama cha siasa.

Ni matumaini yangu kwamba suala hili la msingi litajitokeza kwenye Katiba Mpya tunayoitarajia hivi karibuni.Kama Rais Magufuli angekubali kunisikiliza, angekataa kiti hicho.

Kuna sababu nyingi, nyingine ni za wazi, lakini nyingine ni za ndani ya chama chao. Kwa vile, mimi si mwanachama wa CCM niseme sababu ambazo ziko wazi.

Labda nidokeze tu kwamba wadadisi wa masuala ya kisiasa hapa Tanzania wanaiona nafasi ya mwenyekiti kama mtego kwa Rais Magufuli wa kupunguza kasi yake ya mabadiliko katika Taifa letu.

Tanzania tulihitaji mabadiliko kila mtu alikuwa anayalilia. Kwa kiasi kikubwa Rais Magufuli amekuja na sehemu ya mabadiliko haya.

Hadi sasa amefanya mengi kuelekea mabadiliko tuyatakayo.Mbali na ufisadi, kutowajibika, udini na ukabila, Tanzania tuna ugonjwa wa ‘uchama’. Huu ni ugonjwa mbaya kuliko magonjwa yote nchini.

Vyama vyote vya siasa bila tofauti yoyote ile vinafikiri viko juu ya uraia na utaifa.Kuna watu wamefikia hatua ya kuwaona wale wasiokuwa kwenye vyama vyao vya siasa kama wasaliti au watu kutoka nje ya Tanzania.Ushabiki wa vyamaUshabiki wa vyama vya siasa uko kwenye hatua ya juu na ya kutisha.

Mwalimu Nyerere, alikipenda chama chake cha CCM, lakini hakuwa na ushabiki kama tunaoshuhudia leo hii. Sote ni mashahidi, Mwalimu Nyerere hakuvaa sare za CCM, hakuna picha yoyote ile ikimwonyesha kuvaa shati la kijani.

Leo hii sare za vyama umekuwa ni ushabiki wa kutishia, kufikia watu kushambuliwa na kuumizwa kwa kuvaa sare za vyama vya siasa.

Mwalimu Nyerere hakuteua watu kwenye nafasi zao za uongozi kwa kuangalia mapenzi yao kwenye chama, bali aliangalia uwezo na mchango wa mtu katika Taifa.Mwalimu Nyerere aliangalia uwezo wa mtu na uzalendo zaidi.

Maana kuwa mzalendo wa Tanzania, si lazima kuwa mwanachama wa CCM, kuna watu wengi hawako kwenye vyama vya siasa, lakini ni wazalendo wakubwa wa Taifa letu.

Mabadiliko ya kweli ambayo tunayalilia ni yale ya kuutukuza utaifa wetu zaidi ya chama. Pamoja na kazi nzuri ambayo Rais Magufuli amefanya hadi sasa, bado na yeye amefungwa na ugonjwa huu wa uchama.

Kama tukio la hivi karibuni la ‘kumtumbua’ mkurugenzi aliyeteuliwa kwa kisingizio kwamba alikuwa mwanachama wa ACT Wazalendo, kama ni kweli, basi Rais Magufuli bado ana ugonjwa wa uchama ambao hauwezi kulisaidia Taifa letu kukua, bali kudumaa.

Taifa litapiga hatua kuelekea maendeleo ya kweli, pale tutakapofikiri na kupanga pamoja kama Taifa.Nimemsikia Rais akisema : “Ukisifiwa na adui ni lazima uchunguze umekosea wapi, lakini ukisemwa na adui, ujue umewatwanga”.

Tunaweza kujiuliza, adui hapa ni nani? Nchi jirani? Wazungu au vyama vya upinzani? Kila mtu atakuwa na jibu lake.Hata hivyo, ukiangalia uteuzi aliofanya Rais Magufuli bado haujazingatia utaifa, unazingatia uchama.

Hilo neno ‘umewatwanga’ ni akina nani? Utawatwanga raia unaowaongoza au unawatwanga nani?Rais ni baba na mlinzi wa maisha ya Watanzania, akianza kuwatwanga baadhi na kuwakumbatia wachache ni hatari kubwa kwa Taifa letu.

Hoja yangu hapa ni kwamba ikiwa Rais Magufuli atakuwa mwenyekiti wa chama basi hali itakuwa mbaya zaidi. Hata akitaka kufanya jitihada za kusimamia utaifa, chama chake kitamvuta miguu.

Asema ‘hapana’Kama kweli Rais wetu anataka kuleta mabadiliko na kuhakikisha Tanzania inapiga hatua ya maendeleo akatae nafasi ya uenyekiti wa chama tawala. Akatae kuwatwanga baadhi na kuwakumbatia wachache.

Aendelee na nafasi yake ya urais, uenyekiti wa chama uchukuliwe na mtu mwingine au Kikwete aendelee na nafasi hiyo. Chama kifanye siasa na Serikali iliongoze Taifa.

Ni vigumu, kufuatana na hali ya sasa ya nchi yetu, kuleta mabadiliko wakati mtu anashika nafasi mbili: Rais wa nchi na mwenyekiti wa chama cha siasa.

Huu ni wakati wa kumwachia Rais wa nchi akaiongoza nchi kwa kufutata Katiba na kuviachia vyama vya siasa kufanya siasa.Majipu yatatumbuliwa?

Ni bahati mbaya, kwamba majipu makubwa na ya hatari yako ndani ya CCM. Au tuseme wote ambao wametumbuliwa hadi sasa ni wanachama wa CCM.

Bado kuna majipu mengi ya kutumbua ndani ya chama hicho kikongwe.Je, mwenyekiti atakubali kutumbua hadi roho ya chama chake? Rais wa nchi, ambaye analindwa na Katiba anaweza kutumbua mtu yeyote yule kwa uhuru na bila kuogopa.

Lakini ndani ya chama atahojiwa na wakati mwingine hata nafsi yake itamsuta na hilo likitokea ni lazima kasi ya Rais Magufuli itapungua.Wengi wetu tusingependa kasi hii ya Rais Magufuli ipungue.

Tunamtaka aendelee na kasi ile ile isipokuwa aheshimu Katiba, demokrasia na uhuru wa kujieleza.Watu tutoe maoni yetu kwa vile tunalipenda Taifa letu na tunampenda Rais wetu.

Ukimpenda mtu ni lazima umwambie ukweli ili aweze kuona kama anatembea kwenye njia sahihi. Ukimya, uoga na unafiki si dalili za upendo.

Wasi wasi wetu ni kwamba Rais Magufuli akikubali kuwa mwenyekiti wa chama tawala, chama kikongwe, chama dume na chama kina wenyewe, atake asitake ni lazima kasi yake itapungua tu, maana kama tunavyoambiwa ni kwamba CCM ina wenyewe.

Kwa maoni yangu ni kwamba Rais Magufuli anaweza kuisaidia CCM ijisahihishe na kuendelea kukomaa kama chama cha kisiasa na kulisaidia Taifa kwa ujumla, akibaki nje ya uongozi wa chama hicho, kuliko kukubali kuingia kwenye uongozi wa chama.

Hapana shaka kasi yake imekitikisa chama hicho kikongwe, na wajanja wachache ndani ya chama hicho wanatafuta mbinu za kupunguza kasi hiyo.

Vyovyote vile kasi hiyo ni lazima ipunguzwe na nafasi ya uenyekiti. Ni kama mtego, ambao akikubali kuingia, kutoka itakuwa mbinde. Akipenda kusikiliza maoni haya na kutafakari ni juu yake.

Lakini anaweza kutupilia mbali maoni haya au asiyasome kabisa, maana hayajaanza na salaam ya kidumu Chama cha Mapinduzi. Ukweli utabaki pale pale kwamba yanatolewa na mzalendo wa taifa letu la Tanzania.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii anapatikana kupitia:
Email: pkarugendo@yahoo.com
Simu: 0754 633122.
 
Akusilize wewe, Mweeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee aheeeee,
hebu nipite mie
 
Back
Top Bottom