Kama ni kuchukua mithali kutoka Qur'an, basi Maalim Seif anapita njia aliyopita Nabii Nuh

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
Kinachoendelea hivi sasa katika siasa za Tanzania kwa ujumla hasa kwa upande wa Zanzibar na hususan katika Chama Cha Wananchi - CUF kimenifanya nikumbuke tarekhe za visa vya Mitume na kwa muktadha wa makala hii fupi nitaangalia kazi kubwa ya kiutume iliyofanywa na Nabii Nuh (AS), upinzani aliokumbana nao na mwisho kulitazama Jahazi la Uokozi lililochongwa na Nabii Nuh kwa Amri ya Mola wake na kuyaakisi mafunzo yatokanayo na kisa hiki na hali ya siasa nchini kwetu. Nafanya hivi kwa kufuata maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'an kwamba visa hivi anavyotusimulia ni kwa ajili ya kuchukua mfano na mafunzo ndani yake na kutuongoza.

Nabii Nuh (AS) ni katika Mitume wa mwanzo na alifanya kazi kubwa ya kuwalingania watu wake kutaka kuabudiwa kwa Mungu mmoja. Kazi hii ilimchukua Nabii Nuh zaidi ya miaka 900 kwa ustahamilivu mkubwa. Hata hivyo Nabii Nuh hakukubalika na watu wake; wengi walimkataa kama ilivyo desturi za Mitume kukataliwa na jamaa zao wa karibu. Nabii Nuh alikataliwa hata na mwanawe wa kumzaa.

Si tu jamaa zake walimkataa lakini pia walishtadi katika kumfanyia vitimbi na maudhi ya kila aina hata pale alipoamrishwa na Mola wake atengeneze jahazi basi waliamua kulifanya ndio pahala pa kuweka haja zao kubwa. Mungu akawatia adabu kwa kuwapa ugonjwa mbaya ambao dawa yake ikawa ni kinyesi kile kile walichokipaka katika jahazi la Nabii Nuh.

Mambo yalipofurutu ada, Mwenyezi Mungu Mtukufu Akamuamrisha Nuh apande kwenye jahazi yeye na wafuasi wake waliomuamini kama njia ya kumtoa Nuh na watu wake kwenye vitimbi hivi na kuwaacha wale wafanya vitimbi katika gharika itokayo kwa Mola wao. Miongoni mwa waliogharikishwa ni mtoto wake Nuh ambaye alikataa kupanda jahazi pamoja na Baba yake.

Maalim Seif si Mtume na katu hatuwezi kumfananisha hata kidogo na kazi ya Mitume, hapokei wahyi na wala hakuna miujiza kutoka kwake. Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, nimekianza kisa cha Nabii Nuh kwani kina mazingatio muhimu kwa muktadha wa makala hii.

Maalim Seif amekuwa kwenye siasa kwa zaidi ya nusu ya umri wake sasa. Ni kiongozi wa pekee aliyedumu kwa muda mrefu anayekubalika na watu wa rika lake na kizazi hata cha wajukuu zake.

Maalim Seif tokea siku aliyokula kiapo mbele ya maelfu ya wananchi pale Tibirinzi, Pemba Desemba 1987 baada ya mapokezi makubwa ya kihistoria ambayo yalifanyika kwanza Unguja na baadaye Pemba muda mfupi kabla ya kufukuzwa ndani ya CCM; aliwaahidi Wazanzibari kuwa atakuwa nao akiwa ndani ya Serikali au nje ya Serikali na atakuwa nao akiwa ndani ya Chama au nje ya Chama. Naam, mpaka leo Maalim Seif huwezi kumtenganisha na umma kwa namna yoyote ile.

Kazi kubwa aliyoifanya Maalim Seif ya kuwatumikia Wanzanzibari na Watanzania kwa ujumla imemjengea heshima ya kipekee, ni Kiongozi pekee aliyetembea karibu katika Wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar kuonana na wananchi na kulala nao vijijini katika hali ambayo sio viongozi wengi tulio nao wanaweza kufanya hivyo. Hali hii ya mahusiano kati ya Maalim Seif na Wananchi ndio iliyopelekea Wananchi kumpenda, kumthamini na kumuamini. Anaishi katika mioyo ya Wananchi walio wengi. Hata maadui zake wa kisiasa haiwezi kupita siku bila kumuwaza mtu huyu.

Ni imani hii ya Wananchi kwa Maalim Seif ndio imekuwa kosa kubwa kwake; kila uchao maadui zake wanahangaika kufikiria namna ya kummaliza. Bahati nzuri kazi ya kummaliza Maalim Seif nayo imekuwa si rahisi hata kidogo. Kazi hii imeanza tokea wakati wa Mwalimu Nyerere hadi leo zama za Rais Magufuli lakini kila uchao Maalim ndivyo anavyowatazama maadui zake wakimalizika kisiasa nao wakimuacha Maalim Seif akizidi kung'ara kisiasa.

Wengi wanaweza kudhani kuwa kilichotekea juzi ndani ya CUF ndio mwisho wa Maalim Seif; kwamba CUF aliyoiunda yeye mwenyewe na kuijenga kwa nguvu zake zote leo inatumika kumkomoa. Wale aliowajenga kisiasa akiwemo Lipumba mwenyewe aliyepokelewa katika chama na kupewa nafasi ya kugombea Urais wa Muungano mwaka 1995 na baadaye Uenyekiti wa Chama 1999 eti ndio wanammaliza Maalim Seif. Huku ni kuota mchana.

Khofu imetanda kila pahala hivi sasa. Dhoruba hii sio ndogo kwa kukiri ukweli hasa linapohusika jabali la kisiasa kama Maalim Seif. Wakati wafuasi wa Maalim ambao ndio majivuno yake wapo kimya wakisubiri kauli ya Maalim itoe mwelekeo na matumaini mapya ya kisiasa, cha kustaajabisha hata wale wapishi wa njama hizi za kuihujumu CUF unapowaona imekuwa hamkani si shwari tena. Kwanza, wanastaajabishwa na uvumilivu wa Maalim unaofanana na Nuh. Pili, hivi sasa ndio wanagundua kuwa CUF kama itikadi na imani iliyowajumuisha kina Maalim Seif na wafuasi wao bado haijatetereka, ipo madhubuti na sasa inawatia khofu sana hasa juu ya mwelekeo wanaoweza kuuchukua hasa ukiongozwa na Maalim Seif mwenyewe.

Magazeti yanayotumikia watawala (system) na makala za uchambuzi zote hivi sasa zinaelekezwa kwa Maalim Seif zikijaa kila aina ya propaganda. Hii ni dalili ya khofu kubwa kutawala katika nyoyo zao. Kama Maalim Seif amekwisha, wamefanikiwa kummaliza kama wanavyodai si wamuache tu wasubiri kumshindikiza katika kaburi la kisiasa?

Bila shaka khofu zote zinakuja kwa sababu dalili zote zinaonesha kuwa " they have played with a sleeping lion" (wamemchezea simba aliyelala). Sasa Simba kaamka khofu ya kujeruhiwa imeshawajaa.

Na naam, wenye macho wanaona kuwa huu ni wakati muwafaka ambao kama Nabii Nuh alivyotakiwa kutengeneza jahazi na kuwaamrisha wale wafuasi watiifu kwake kupanda jahazi pamoja naye ili kukwepa gharika itokayo kwa mola wao basi na Maalim naye achonge jahazi watu waingie.

Kwa mazingira ya siasa za Tanzania hivi leo, mfano wa aliyoyapitia Nabii Nuh anayapitia au anapotishwa Maalim Seif. Tuna imani vitimbi hivi havitotukatisha tamaa ya kuendeleza mapambano yetu. Tunajua pia kama walivyokuwepo watoto wa Nabii Nuh waloasi basi watakuwepo pia kina Muhunzi, Khalifa, Mnyaa, Nassor Seif, Rukia, Mussa Haji na wenziwao katika zama zetu. Watachupa kwenye jahazi na kudhani wataokoka kwa kupanda juu ya jabali wakati hakuna jabali la kupanda likawanusuru. Gharika hii ni kubwa. Kusalimika ni kuwa pamoja katika Jahazi la Nuh tu. Tunamsubiri Nuh wetu atuongoze kwenye Jahazi maridhawa la kutuvusha katika gharika hii hadi kufikia malengo yetu.

Kama alivyowahi kusema Maalim Seif kuwa wakimpa Chama Lipumba watajuta kitakachotokea. Naona majuto yameshaanza. Nyoyo zinawasuta wasaliti, dola inataharuki kwa kuiona nguvu mpya ya umma itakayosimama pamoja na Nuh wao (Maalim Seif) kupinga dhulma hii na kupigania haki na demokrasia ya kweli.

Mwandishi, Mtumbatu.
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom