Kama mwandishi, sema wazi, taja jina lako, onyesha sura yako | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kama mwandishi, sema wazi, taja jina lako, onyesha sura yako

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Yona F. Maro, Oct 28, 2010.

 1. Yona F. Maro

  Yona F. Maro R I P

  #1
  Oct 28, 2010
  Joined: Nov 2, 2006
  Messages: 4,237
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 0
  Jenerali Ulimwengu​
  Oktoba 20, 2010 [​IMG]
  MIONGONI mwa mambo yaliyojitokeza katika kampeni za mwaka huu ni ukubwa wa hamasa na ushabiki wa kisiasa miongoni mwa Watanzania.
  Wananchi wengi wamechangamkia kampeni hizi kwa kiasi ambacho mimi binafsi sikutarajia.
  Sikutaraji kuona hamasa ya kiwango hiki kwa sababu huu ni uchaguzi unaohusu ngazi tatu: udiwani, ubunge na urais. Katika ngazi za udiwani na ubunge ni jambo la kutarajiwa kwamba hamasa ya chaguzi nyingine zote ingejionyesha, kwa sababu bila shaka wapo watu ambao wangependa kuwang’oa madiwani na wabunge waliomo katika halmashauri na Bunge, nao wangetarajia siku zote kuzitetea nafasi zao.
  Katika ngazi ya urais nilitaraji kuona hamasa iliyopoa kidogo, hususan kwa sababu yupo rais anayeomba kura kwa mara ya pili akiwa amemaliza muhula wake wa kwanza. Mara nyingi katika nchi za Kiafrika, rais aliye madarakani hapati changamoto kubwa kutoka kwa wapinzani wake. Hii ni kutokana na sababu kadhaa ambazo zinaeleweka.
  Lakini mwaka huu hamasa kubwa imejitokeza katika ngazi zote tatu, na hakuna kiti kinachohesabika kama kilichokwisha kuchukuliwa na mtu au chama isipokuwa vile tu ambavyo vina wagombea waliopita bila kupingwa. Inaelekea sasa tutakuwa na mshikemshike moja kwa moja hadi siku ya uchaguzi.
  Hili ni jambo jema, hasa kama hamasa iliyoumuka safari hii itajiepusha na shari ya mapigano na vurugu. Najiunga na wale wote wanaowatanabahisha Watanzania kujiepusha na vurugu za aina yo yote. Tunatakiwa tujue, kwa kuwaangalia wenzetu waliotetereka, kwamba amani ikivunjika katika nchi, ni kama maji yaliyomwagika, ambayo hayazoleki.
  Ndiyo maana naamini kwamba wote ambao wanatoa matamko ya kutishana au kuzuliana mambo yasiyo na ushahidi wanastahili kuchukuliwa hatua zinazopasa. Zimeandikwa taarifa za ajabu, yamesambazwa maandiko ya hovyo ambayo siamini kwamba wahusika wa usalama wa nchi yetu hawajakumbana nayo, lakini naona kimya.
  Kwa mfano, iwapo chapisho lo lote linachapisha taarifa za ‘uchunguzi’ kwamba mtu fulani kutoka asasi fulani anakusudia kutenda jambo ambalo ni kosa la jinai, tungetaraji angalau mambo mawili au matatu yafuate taarifa hizo:
  Kwanza tungetaraji kwamba yule aliyetajwa kama anayeandaa kutenda matendo ya jinai angekanusha taarifa hiyo, na hata kutishia kumpeleka mahakamani ye yote aliyehusika na taarifa hiyo. Angemtaka aombe radhi kwa kumkashifu raia na asasi yake.
  Kama asipochukua hatua ya kusafisha jina lake, asasi zinazohusika na uzuiaji wa jinai na utoaji wa adhabu kwa wanaotenda jinai zingejitokeza na kumhoji huyo aliyeshutumiwa kwamba anapanga kutenda kosa la jinai.
  Katika hali kadhaa uchunguzi unaweza kuanza mara moja inapotolewa taarifa kama hiyo, hata bila kusubiri kuona kama mshutumiwa atakanusha au la.
  Iwapo uchunguzi na mahojiano na mshutumiwa yangedhihirisha kwamba kuna chembe ya ukweli katika madai yaliyomo ndani ya taarifa husika, uchunguzi rasmi ungeanzishwa, nia ikiwa ni kuingia katika undani wa shutunma hizo na kuona kiwango cha uhalifu unaokusudiwa kufanywa, lengo likiwa ni kuzuia tendo hilo linalohofiwa, na kuwatia mbaroni wote wanaohusika na mpango mzima.
  Iwapo ingedhihirika kwamba taarifa zilizochapishwa hazikuwa na ukweli wo wote na kwamba ni uzushi wa shari, asasi husika zingetarajiwa kuchukua hatua kali dhidi ya ye yote ambaye angebainika kuwa ni chanzo cha uzushi huo. Sheria zetu zimeainisha kinaganaga adhabu zinazotakiwa kutolewa kwa kosa kama hilo ninalolijadili.
  Najiuliza ni kwa nini taarifa kama hizi zinaachiwa bila kujibiwa na bila kufanyiwa uchunguzi? Tumesikia wakuu waandamizi wakionya dhidi ya watu watakaokataa kukubali matokeo ya uchaguzi. Tumesoma tahariri zinazosema kwamba mgombea fulani hatakuwa rais, mwezi mzima kabla ya kura kupigwa. Lakini hatusikii sauti zinazokemea shutuma kama hizi ambazo sina shaka kwamba zinaweza kuzua shari kubwa.
  Naelewa kwamba zipo taarifa nyingi zinazosambaa kila kona lakini ambazo ni ngumu kuzifuatilia kwa sababu hazina saini ya mtu. Hiyo ni mojawapo ya faida na hasara ya mtandao wa inteneti.
  Hata hivyo wakati asasi zetu za ukachero zinapodhamiria kuwapata wachapishaji ‘maruhani’ zimekuwa zikifanikiwa kuwafuatilia na kuwagundua walikojificha. Mbona ukali huo wa makachero wetu haujitokezi katika muktadha wa sasa?
  Tunatakiwa kujenga utamaduni wa uwazi unaothibitisha kwamba tunalolisema tunaliamini, na kwamba tuko tayari kusimama inapobidi na kulitetea bila kuogopa kuchukiwa na wanafiki. Najua hili ni gumu katika jamii iliyozoea kukaa kimya wakati mambo yanaharibika kwa kuogopa kuadhibiwa na watu waovu lakini wenye nguvu. Si rahisi katika hali ya nchi nyingi za Kiafrika kuwa na watu wenye ujasiri wa kusimama na kumwambia mwenye nguvu kwamba amekosea.
  Wenzetu wana kitu kinaitwa Speak Truth to Power, maana yake waambie watawala ( na wengine wenye nguvu) ukweli. Nimeongeza “wenye nguvu” kwa sababu si watawala pekee wanaoweza kufanya mambo ya hovyo katika jamii. Wenye nguvu wanaopaswa kuambiwa ukweli wanaweza kuwa wafanyabiashara wakubwa; wanaweza kuwa wakulima wakubwa wenye maslahi mahsusi; wanaweza kuwa ni asasi za kisomi zenye ushawishi mkubwa ndani ya jamii; wanaweza kuwa viongozi wa asasi za kidini.
  Sasa, sikiliza na hili: Wanaweza kuwa hata wananchi waliopotoshwa na kurubuniwa na wajanja wenye nia mbaya, wakakubali kuhadaika. Hii inaweza kuwa hali ngumu kweli kweli, kwa sababu sisi tumefundishwa kwamba wananchi ndio mabosi wetu; sasa inakuwaje kwamba tuwaambie kwamba wamekosea, na nguvu hiyo tunaipata kutoka wapi?
  Hapa ndipo tunapata ufafanuzi wa dhima ya uandishi wa habari. Zipo asasi chache ndani ya jamii ambazo zimejikuta, kupitia historia ya maendeleo ya binadamu, zikibeba jukumu ‘takatifu’ la kuiarifu, kuielimisha na kuiburudisha jamii.
  Mojawapo ya asasi hizo ni vyombo vya habari, ambavyo vimeelezwa kwingineko kama muhimili wa nne wa dola (baada ya Utawala, Bunge na Mahakama).
  Wasimamizi wa vyombo ndani ya asasi hii wanatakiwa kuwa watu makini, wenye akili zilizotulia, wenye uadilifu mkubwa na wenye kujiheshimu na kuheshimu taaluma yao, kwa sababu madhara yanayotokana na shughuli za watu wanaojiita waandishi wa habari lakini ni waajiriwa wa miradi ya uporaji, wanaweza kusababisha madhara makubwa, hasa kama wanazua na kuchochea malumbano yenye shari yanayotokana na chokochoko za kikabila au za kidini. Hatuna haja ya kukumbushana juu ya maafa yaliyowapata wenzetu kwingineko.
  Ndiyo maana naamini kwamba ye yote anayejiita ‘mwandishi’ na anayeandika makala au anayerusha matangazo yanayokosoa mtu au asasi na kutoa hoja kali kuhusu upande huu au ule, kuhusu jambo hili au lile, na akakosa ujasiri wa kuandika jina lake, huyo anaweza kuwa mwandishi, lakini katu hawezi kuwa mwandishi wa habari. Kazi anayofanya ni ya utarishi wa maslahi fulani ambayo yamejificha nyuma ya kalamu yake.
  Hakuna ubaya wo wote katika kutamka wazi katika makala zako za gazetini au redio kwamba unaunga mkono sana upande huu au unaupinga kwa nguvu zako zote upande ule. Ubaya unakuja pale unapojificha, usiseme wewe ni nani na uko wapi, halafu ukatoa matamko makali ajabu.
  Kama unataka kuwa mkali, kwa sababu unadhani ukali ndio unadhihirisha kwamba wewe ni mwanamume au mwanamke wa kweli, basi taja jina lako, weka picha yako na elekeza anwani yako. La sivyo kaa kimya.
  Inafaa jamii ijihadhari na taarifa za chuki zinazoenezwa na watu wasiotaka kufungua shungi zilizofunika nyuso zao. Jema ninaloweza kusema juu yao ni kwamba hata wao wanajua kwamba wanalofanya ni jambo ovu, ila tu wamelipwa kufanya hivyo, na ndiyo maana hawathubutu kuonyesha sura zao hadharani.
  Si waandishi wa habari, wala wachambuzi: nyenzo yao ni kalamu, lakini kazi yao ni ukuwadi.
   
 2. ghumpi

  ghumpi Senior Member

  #2
  Oct 28, 2010
  Joined: Nov 10, 2009
  Messages: 187
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 33
  kama mtu an uhakika na anachokisema na tuko tayari kukitetea, kwa nini ujifiche??
   
 3. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #3
  Oct 28, 2010
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 9,227
  Likes Received: 1,414
  Trophy Points: 280
  Too long for a blog
   
Loading...