Kama muungano pekee unatutoa jasho, shirikisho je? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kama muungano pekee unatutoa jasho, shirikisho je?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by sulphadoxine, Jan 9, 2012.

 1. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #1
  Jan 9, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  KAMA Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana huru [1957] na Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania huru [1961], kwa pamoja wangefufuka leo na kuona jinsi Afrika inavyoyumba kufikia muungano wa kisiasa na kiuchumi, wangetazama; kwanza kimya kimya, kasha wangeulizana, kila mmoja akitupa lawama kwa mwenzake akisema: “Kwa msimamo wako, wewe ndiye umesababisha Afrika isiungane mpaka leo”.

  Tunaamini, zogo hilo lisingeweza kupata mshindi kati ya majabali hao wa enzi za uhuru wa Afrika, lakini umma ungekuwepo kuwahukumu, kila mmoja kwa matendo yake.

  Wote wawili, Nkrumah na Nyerere walikuwa watetezi wakubwa wa Shirikisho la Afrika, ila walitofautiana kuhusu njia za kuufikia muungano huo.

  Ni tofauti zao za mahesabu zilizotufikisha hapa tulipo, kwa maana ya hesabu za moja kutoa moja kubakia sufuri, kwa maana ya kushindwa kufikia Shirikisho kabisa, zaidi ya miaka 40 ya uhuru. Ilianza hivi:

  Miaka ya 1960 ulikuwa muongo wa uhuru wa Afrika nyeusi, yaani, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kilikuwa ni kipindi cha matumaini na kujiamini kwa Mwafrika, kwamba uhuru na umoja ungetatua matatizo yake ya umasikini, ujinga na maradhi.

  Ingawa muongo huo ulibeba mamba ya ushindi kwa Uafrika na Mwafrika katika kumiliki maisha na hatima yake, kilikuwa kipindi pia cha kusikitisha kutokana na kuibuka kwa utamaduni mpya wa mapinduzi ya kijeshi, kuanzia na kupinduliwa na kuuawa kwa Rais wa Togo, Sylivanus Olympio, mwaka 1963

  Kilikuwa kikwazo kikubwa mno kwa maendeleo tarajiwa kwa Afrika, na kilionyesha jinsi Serikali za Kiafrika zilivyokuwa tete, legelege na “katope”.

  Kwa sababu hii, kile kibwagizo cha Nkrumah, kwamba “utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa”, ulikuwa mwangwi usiokita kutokana na uhuru wa kisiasa kutoka kwa wakoloni kutoweza kutafsiriwa kumaanisha amani na maendeleo kwa Afrika na Waafrika.

  Na kadri miongo ilivyopiga hatua mbele kuingia miaka ya 1970 na 1980, ndivyo Waafrika walivyozidi kushuhudia makali ya uhasama wa soko la dunia iliyogawanyika kwa misingi ya vita baridi, kati ya nchi za kibepari za Magharibi na zile za Kisoshalisti za Mashariki.

  Kwa mgawanyiko huo, uliotema cheche za kuunguza, mapinduzi, mauaji na mizengwe ya kisiasa na usalama duni wa kijamii na kiuchumi vilitawala Afrika.

  Kwa kifupi, kilichoibuka sasa ni kile ambacho mwanafasihi mahiri barani Afrika, Wole Soyinka wa Nigeria alikiita Sander – yaani Utamaduni wa mapinduzi ya kijeshi usiojua demokrasia, amani na utulivu.

  Ni Kwame Nkrumah aliyebuni mbiu ya Shirikisho la Afrika wakati Viongozi wengine wangali wakihangaika na viugomvi na tofauti ndogondogo ndani ya nchi zao.

  Nkrumah alikuwa mmoja wa Viongozi wachache wa Kiafrika walioamini kwamba “hakuna nchi moja ya Kiafrika inayoweza kujiita huru na salama kama nchi zingine za Kiafrika zitabakia chini ya utawala wa kikoloni au ukoloni mamboleo”. Vitabu vyake vya kwanza, “Africa Must Unite” na “I Speak of Freedom”, vilisisitiza jambo hili.

  Nkrumah alitumia kila nafasi kuhakikisha kwamba Viongozi wenzake wanaielewa dhana hii na ambayo baadaye ilizaa harakati za vyama vya ukombozi barani Afrika; na Makao Makuu yakawa Dar es Salaam.

  Hatua ya kwanza ya Nkrumah baada ya uhuru wa Ghana ilikuwa kuitisha Mkutano wa mataifa ya Kiafrika [All-African Peoples’ Conference] mjini Accra, 1958 na kuhudhuriwa na Wajumbe zaidi ya 300.

  Katika mkutano huo, iliazimiwa kuwa vyama vya siasa vya kupigania uhuru viache malumbano katika nchi zao na kuelekeza kwa pamoja nguvu na mapambano dhidi ya ukoloni mkongwe.

  Kati ya waliohudhuria mkutano huo ni mahasimu wawili wa kisiasa Zanzibar, Abeid Amani Karume wa Chama cha Afro-Shiraz Party [ASP], na Ali Muhsini, wa chama cha Zanzibar Nationalist Party [ZNP], waliokabana koo visiwani kuhusu chama kipi kitawale Zanzibar, kiasi cha kuwa “vita vya panzi furaha ya kunguru” kwa Sultani wa Zanzibar.

  Ni Nkrumah aliyewasulubisha Karume na Muhsini, wakaelewana kwa lengo la kufanya kazi kwa pamoja na nguvu moja katika kuutafuta uhuru wa Zanzibar.

  Huu ndio ulikuwa “mwafaka” wa kwanza kwa siasa za Zanzibar zinazoendelea kuwa kero hadi leo, ambapo Chama cha Wananchi [CUF] kimechukua nafasi ya ZNP na CCM Zanzibar nafasi ya ASP. Uhasama huu unatema sumu ya kuyumbisha, kama sio kutishia kuua Muungano wa Tanzania.

  Ingawa Nkrumah na Nyerere walikuwa waumini wakubwa wa Muungano wa Afrika na vita dhidi ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo, lakini walitofautiana kuhusu njia na jinsi ya kufikia Muungano huo, kiasi cha miamba hao wawili kutoweza kupikwa chungu kimoja wakaiva.

  Ni tofauti za viongozi hao wawili juu ya Muungano wa Afrika umelifanya bara hili lisiweze kuungana hadi leo mpaka limekutwa na ukoloni mpya wa karne ya 21 [utandawazi] na kufifisha kabisa matumaini ya kuungana.

  Nkrumah aliwakilisha mawazo na mtazamo uliotaka mabadiliko ya haraka kufikia Muungano, akihofu kwamba azima ya kuungana ingepotea kama kungepita muda mrefu bila Afrika yote kushinikizwa kuungana sawia, kabla viongozi hawajanogewa utamu wa madaraka wakajenga ubinafsi na ubwana katika nchi zao kiasi cha kukataa kuyaachia. Nkrumah alitaka “Afrika iungane sasa”, bila ya visingizio vyovyote.

  Ukweli, Nkrumah alifikia hatua ya kujenga hoja kwa wakoloni kwamba, iwe sharti la kwanza kwa nchi ya Kiafrika kukubali kujiunga na Shirikisho la Afrika kabla ya kupewa uhuru, kama lilivyokuwa kwa nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Waingereza kutakiwa kujiunga na Jumuiya ya Madola [Commonwealth], kama sharti la kupewa uhuru.

  Nyerere, kwa upande wake hakukubaliana na mtazamo wa Nkrumah. Yeye alitaka Muungano hatua kwa hatua, kwa nchi moja moja kuelewana kabla ya kufikia Shirikisho la Afrika nzima.

  Kwa kuanza na yeye mwenyewe, alitetea Ushirikiano wa kiuchumi Afrika Mashariki [EAC] na Shirikisho la kisiasa la nchi hizo [EAF], kama hatua kuelekea Muungano wa Afrika.

  Nkrumah aliamini kwamba jumuiya za uchumi za kikanda zingejenga ubaguzi wa kikanda na kuidhoofisha Afrika kwa utengano kuliko hata ilivyokuwa wakati wa ukoloni na hivyo kusaidia mabeberu “wavue samaki bila shida katika bahari ya mabwege”.

  Vivyo hivyo, aliona wazo la kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki kama aina moja ya mbinu za wakoloni kuigawa na kuipunguzia nguvu Afrika huru isiweze kupambana na ukoloni mamboleo kiwango cha kimataifa.

  Misimamo ya Viongozi hao wawili ilikuwa haisuluhishiki, na Afrika iliwatazama tu kimya wakikabana koo na kupigana kwa pembe za vichwa vyao.

  Ilifika mahali kwa Nkrumah kutamka kwamba haikuwa sahihi kwa Makao Makuu ya Ukombozi wa Afrika kuwa Dar es Salaam, kwa sababu Nyerere alikuwa kibaraka wa wakoloni, ukoloni mamboleo na mpinzani wa Shirikisho la Afrika.

  Tofauti na mawazo kati ya Viongozi hao wawili juu ya Muungano wa Afrika zilifika mahali zikakithiri kiasi cha kuonekana kuwa ni uhasama na ugomvi binafsi kati yao, kama ilivyodhihirika katika mpambano wao wakati wa mkutano wa Cairo, Julai 1964.

  Nyerere alimchokoza Nkrumah kwa kusema kwamba hapakuwa na njia mbadala kufikia muungano wa Afrika isipokuwa kwa kuanza na nchi moja moja, “wanaopinga njia hii ni watu hohe hahe, muflisi wa fikra, na waliopungukiwa hekima na busara,” alisema Mwalimu.

  Akijibu hoja ya Nkrumah kwamba wanaopendelea kuanza na miungano ya kikanda walikuwa “mawakala wa ubeberu”, Nyerere alisema: “Kudai kwamba mfumo huu umeundwa na mabeberu ni kufikia ukomo wa uhayawani.”
   
 2. sulphadoxine

  sulphadoxine JF-Expert Member

  #2
  Jan 9, 2012
  Joined: Nov 1, 2010
  Messages: 2,264
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Hadi Nkruma akipinduliwa mwaka 1966, Afrika ilikuwa [hadi sasa] haijaungana ama kwa mfumo wa mtazamo wake, au kwa mfumo wa mtazamo wa Nyerere; Afrika inazidi kugawanyika, kila mtawala na lwake, "kwake na watu wake"

  Jumuiya za uchumi za kikanda kwa mtazamo wa Nyerere, kama vile ECOWAS, Mano-River Basin, CCAM [Afrika Magharibi] na Jumuiya ya Afrika Mashariki [EAC] na Kusini mwa Afrika [SADC], ziliundwa na kuvunjika haraka bila kutoa mwelekeo wala matumaini ya Muungano wa kisiasa.

  Shirikisho la kisiasa Afrika Magharibi kama lile kati ya Senegal na Gambia [Senegambia] nalo lilisimama na kuvunjika, likafa.

  Naye Nyerere, kwa mbiu yake ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki mwaka 1963, alijikuta akitelekezwa na wenzake – Marais Jomo Kenyatta [Kenya] na Milton Obote [Uganda], akaambulia Muungano mdogo na dhaifu, kati ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964; tena kwa shinikizo la agenda ya siri la nchi za Magharibi katika kulinda maslahi ya nchi hizo wakati huo.

  Kuhusu juhudi za kuunda Shirikisho la kisiasa la Afrika [kwa mtazamo wa Nyerere], kuelekea Shirikisho la Afrika, tuna mengi ya kuuliza: Kama Shirikisho hilo lilishindwa mwaka 1963 wakati moyo wa Afrika Mashariki ulikuwa ungali moto juu ya kujikomboa kisiasa na kiuchumi kabla haijagawanyika kwa misingi ya kiitikadi, ni kipi leo kipya, tofauti na sababu zilizofanya hatua hiyo isifanikiwe huko nyuma?

  Kama Muungano tu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara unaendelea kututoa jasho, na Jumuiya za kiuchumi zinaundwa na kuvunjika, Shirikisho la kisiasa je? Kama tumeshangaa kuona la Mussa, la Firauni je?

  Kuna ukweli gani Shirikisho la Afrika Mashariki litafanikiwa, ikizingatiwa pia kwamba Burundi na Rwanda zimejiunga, ambazo ni nchi zenye utamaduni, mfumo wa Sheria, siasa na miundombinu tofauti na waasisi wa wazo hilo – Tanzania, Kenya na Uganda? Tuna hakika gani kwamba kuharakishwa kwa Shirikisho hili kwamba liwe limeundwa kufikia au kabla ya 2013, si agenda nyingine ya siri ya ubeberu mpya kwa nchi zetu?

  Nyerere na Nkrumah hatunao tena na kizazi cha leo hakionyeshi kutaka kuyafanyia kazi mawazo yao kwa dhati kwa ukweli na uaminifu ili kufikia muungano wa kweli.

  Swali litakaloendelea kugonga vichwa vyetu ni hili: Ni mtazamo wa nani kati ya Nyerere na Nkrumah unaweza au ungeweza kuleta muungano makini wa Afrika? Je, tunaweza kuufuata leo na kufanikiwa?

  Inawezekana Nyerere alikuwa sahihi, lakini tunadhani Nkrumah alikuwa sahihi zaidi kwa misingi kwamba "Mchuzi wa mbwa hunywewa ungali moto moto", au kwamba "Samaki mkunje angali mbichi". Viongozi wa Afrika sasa hawakunjiki, wamejaa uchu wa madaraka kiasi cha kuona kwamba muungano kwao ni kuwapokonya maslahi ya kiutawala. Ni sababu hizi hizi zinazowafanya baadhi ya Wazanzibari wadai Zanzibar ni nchi.

  Tutarajie "Shirikisho" gani wakati watawala wetu, kama asemavyo Ngungi wa Thiong'o [Ngugi Detained – uk. 62], wanaabudu kwenye madhahabu ya ukoloni mamboleo? Sala yao sasa inakwenda hivi:

  "Baba yetu uliyeko Ulaya na Amerika, Jina lako litukuzwe,
  Ufalme wako uje, Utakalo lifanyike, katika Afrika yetu tajiri,
  Kama ilivyokuwa enzi za ukoloni; Utupe leo dola [fedha] yetu
  ya kila siku. Utusamehe udhaifu wetu, Tusaidie kuwaangamiza
  Wanaokuchukia na kukutukana; Utupe baraka na misaada tele;
  Tupe nguvu ya kuwa wapole, wenye shukrani na unyenyekevu;
  Milele na milele, Amina.

  Ni ukweli usiopingika kwamba katika mazingira ya zama zetu, agenda ya Muungano huru na wa kweli kwa nchi zetu imefika njia panda. Hatua yoyote kuelekea Muungano wowote ule haina budi kupimwa kwa vigezo vyote, kwa mapana na marefu ili kuepuka historia ya ukoloni kujirudia.
   
Loading...