Kama Kweli Tuna Nia Ya Kujenga Demokrasia... ( Makala, Raia Mwema) | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kama Kweli Tuna Nia Ya Kujenga Demokrasia... ( Makala, Raia Mwema)

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by maggid, Mar 21, 2012.

 1. m

  maggid Verified User

  #1
  Mar 21, 2012
  Joined: Dec 3, 2006
  Messages: 1,084
  Likes Received: 397
  Trophy Points: 180
  Na Maggid Mjengwa,

  JUZI hapa mtoto wangu wa miaka kumi na miwili aliniuliza; “ Hivi baba, kwanini uchaguzi hapa Tanzania ni kila wakati. Mara utasikia Igunga na sasa ni Arumeru. Na kila uchaguzi kuna habari za vurugu?
  Kwangu swali hili linatutaka, kama watu wazima, tutafakari kwa kina. Na katika wakati huu tukielekea kuanza mchakato wa Katiba Mpya lina umhimu sana.

  Umefika wakati wa kuubadili mfumo wetu wa uchaguzi ambao kimsingi unachochea rushwa. Unaongeza umasikini wa nchi na hata kutishia usalama na amani ya nchi. Uchaguzi una gharama kubwa. Inakuwaje basi, hata baada ya kufanya Uchaguzi Mkuu, hatuna taratibu zitakazofanya kusiwe na chaguzi ndogo za wabunge na madiwani pindi wanapofariki dunia au kuondolewa kwenye nafasi zao na vyama vyao au vyombo vya sheria kama mahakama.


  Kwamba ingependekezwa kwenye Katiba Mpya, tuwe na utaratibu ambapo pale inapotokea mbunge amefariki dunia, basi, kwa vile vyama vyote vitatakiwa kuwapata wagombea wao wa udiwani na ubunge kupitia kura za maoni miongoni mwa wanachama wao wasiopungua elfu tatu katika kila jimbo kama ni ubunge, na wanachama wasiopungua mia mbili katika kila kata kwa nafasi ya udiwani.


  Katika mazingira hayo, walioshika nafasi ya pili mpaka ya nne kwenye kura za maoni majina yao yapelekwe na chama husika kwenye Tume ya Uchaguzi ili yatumike kupata mrithi wa kiti cha ubunge au udiwani pindi diwani au mbunge wa jimbo au kata husika anapofariki dunia au kuondolewa kwenye wadhifa wake kwa sababu nyinginezo.


  Na ili kusiwepo na hofu ya diwani au mbunge aliyechaguliwa kuhujumiwa na aliyeshika nafasi ya pili, ili akifa au kuondolewa madarakani, huyo wa pili achukue nafasi yake, basi, Tume ya Uchaguzi ipewe jukumu la kuyapigia kura ya wazi majina ya washindi wa pili hadi wa nne kwenye kura za maoni ya chama husika kwenye jimbo au kata husika. Ni majina yatakayotokana na kura za maoni za chama husika katika uchaguzi mkuu uliopita, chama ambacho mgombea wake ndiye aliyeshinda nafasi ya ubunge au udiwani kwenye uchaguzi huo.


  Kwa vile majina hayo matatu yatakuwa ni ya watu waliopitishwa na chama husika kuwa wana sifa za kugombea ubunge au udiwani, basi, Tume Huru ya Uchaguzi itayapigia kura ya wazi na kutoka na jina moja la mrithi wa kiti cha diwani au mbunge aliyefariki au kuvuliwa nyadhifa zake kwa sababu nyingine.


  Utaratibu kama huo.unaopendekezwa hapa unaweza kuifanya nchi ipunguze gharama zisizo za lazima kama ambazo nchi inaingia kwa sasa kwa wagombea, vyama na hata Serikali kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo. Tumeona hata helikopta zenye gharama nyingi zikiruka kilomita nyingi angani eti kwenye harakati za kusaka kura kwenye chaguzi ndogo huku wananchi wengi wa jimbo husika wakitembea kilomita nyingi kusaka maji ya kunywa na kupikia.

  Wiki kama hii ya Maji inayoendelea sasa ilipaswa kuwa wiki ya kuomboleza uhaba wa maji unaochangiwa pia na matumizi mabaya ya rasilimali za wananchi kama haya ya kuendesha chaguzi ndogo kule Arumeru Mashariki.

  Ndio, inasikitisha kuwa muda mwingi unatumika, railisimali nyingi zinatumika, lakini, kinachopatikana s i tu ni haba, bali, kimsingi tunavuna hasarakubwa ikiwamo hata ya watu wetu kupoteza maisha au kutiwa ulemavu.

  Tunaona leo wabunge wengi na viongozi waandamizi Serikalini wanashiriki kwenye kampeni za chaguzi ndogo kuwasaidia wagombea wa vyama vyao. Hawa ni viongozi wanaoacha vituo vyao vya kazi. Wanaoacha majukumu yao ya msingi. Wanaoacha majimbo yao. Wanaoacha familia zao na kwenda kulundikana kwenye jimbo moja la uchaguzi, eti, kufanikisha ushindi wa mwakilishi mmoja wa watu wasiozidi laki mbili kwenye nchi yenye watu milioni arobaini na mbili. Huu ni uwendawazimu.

  Na kwanini chaguzi zetu zimekuwa ni za hovyo hovyo na hata kututia hasara kama taifa?

  Nimepata kuainisha hili huko nyuma, kuwa, kuna taasisi tatu ambazo zaweza kuwa chimbuko la kuzifanya chaguzi zetu kuwa za hovyo hovyo na hata kuhatarisha amani ya nchi. Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Vyombo vya habari.

  Siku zote nimesisitiza, kuwa historia ni mwalimu mzuri. Katika nchi zetu hizi, taasisi hizo tatu ndio zimekuwa chanzo cha maafa ya nchi nyingi za Kiafrika. Wahenga walisema; kujifunza kuanzie kwa jirani yako.

  Ndio, tumeona hata kwa jirani zetu wa Kenya. Kwamba Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Vyombo vya habari vilichangia vurugu, mauaji na hasara kubwa kuafuatia matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya uliopita.

  Leo WaKenya wamepata Katiba mpya na kuanza kusonga mbele, lakini, wakiwa na makovu na hata machungu yaliyobaki kwa yaliyotokea huko nyuma. WaKenya walikuwa na uwezo wa kuzuia kilichotokea. Lakini, nao pia, walikuwa na viongozi wa hovyo hovyo waliodhani WaKenya wote ni watu wa hovyo hovyo. Na matokeo ya dhania hiyo dunia nzima imeyaona.


  Hivyo basi, kule Igunga na kwingineko tulishaziona ishara, kuwa kama nchi yetu itakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 bila kuufanyia mabadiliko ya kimsingi mfumo wetu wa uchaguzi ikiwamo uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, bila kuwa na Katiba itakayolifanya Jeshi la Polisi kutenda haki kwa raia na vyama vyote vya siasa kwa wakati wote na bila kuwa na vyombo huru vya habari , basi , sihitaji kuwa na maarifa ya elimu ya nyota kuweza kutabiri machafuko ya kisiasa huko twendako. Machafuko yakayopelekea madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa nchi yetu.


  Maana, WaTanzania kwa asili ni watu watulivu na wenye kupenda amani. WaTanzania hawa kwa kawaida watakwenda kwenye mikutano ya siasa na watawasikiliza wanasiasa. Na siku ya kupiga kura watakwenda kupiga kura kwa amani.


  Ni vyama vya siasa na baadhi ya wanasiasa ndio wenye kutumia hila , ghilba na hata , kwa kutumia fedha, hutokea wakagharamia vurugu ili baadae kwa kuvilipa vyombo vya habari na hata baadhi ya wana habari, watajenga taswira ya uongo juu ya uwepo wa vurugu na hata kusukuma lawama kwa wapinzani wao wa kisiasa.

  Kisha , jeshi la polisi nalo, kwa ama kutojiamini kwa baadhi ya viongozi wa jeshi hilo au kusukumwa kisiasa, nao wataingia kwenye mapambano na wafuasi wa vyama na hata viongozi wa vyama. Na hapo ndipo chuki inapozaa chuki na silaha inapozaa silaha. Ni balaa.

  Na uwepo wa Tume ya Uchaguzi isiyo huru unapelekea Tume kuwa na viongozi wasiojiamini, hivyo basi, kuendesha shughuli za uchaguzi katika hali ya mashaka na hata kuegemea upande mmoja. Na katika nchi zetu hizi, siku zote, tabu inakuja kwenye shughuli ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo. Joseph Stalin wa Urusi ya zamani alipata kutamka; Katika uchaguzi wowote ule, mpiga kura si anayeamua matokeo, bali mhesabu kura!


  Tunachojifunza kwenye kauli hiyo ya Jeseph Stalini ni ukweli, kuwa kikubwa katika mchakato wa uchaguzi ni uwepo wa imani kwa wanaondesha mchakato huo. Kama vyama vya siasa na hata wapiga kura watakosa imani na aliyeteuliwa kuendesha mchakato na hata kuhesabu kura zao, basi, matokeo ya chaguzi yanaweza kuwa chanzo cha vurugu za kisiasa.


  Na hapo ndipo tulipofikia WaTanzania, kwamba chaguzi zetu zimekuwa chanzo cha mashaka badala ya kutupa matumaini ya kwenda mbele. Na sasa ni kuanzia ngazi ya udiwani. Haya ndio mambo ya hovyo hovyo yanayotufanya tuonekane kuwa ni watu wa hovyo hovyo. Tuna uwezo na kila sababu ya kuandaa taratibu za kuendesha mambo yetu kistaarabu. Kama tuna nia ya dhati ya kujenga demokrasia.Nahitimisha. ( Makala hii imechapwa leo kwenye Raia Mwema)

  0788 111 765

  Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo
   
 2. S

  Shembago JF-Expert Member

  #2
  Mar 21, 2012
  Joined: Aug 20, 2011
  Messages: 332
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi na Vyombo vya habari ni muhimu sana kufanyiwa marekebisho,hawa watawala wasiogope marekebisho maana ni kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote
   
Loading...