Kalenda ya Papa Gregory XIII

Paschal Matubi

JF-Expert Member
Sep 15, 2008
235
302
Source: TANZANIA DAIMA, JANUARY 03, 2010

Heri ya mwaka mpya ndugu msomaji. Naanza kwa kukumbusha maswali ya shuleni. Moja liliuliza kwamba dunia hutumia siku ngapi kulizunguka jua. Tulijibu ni siku 365.25 yaani 365 na robo. Jingine liliuliza mwaka una siku ngapi. Tulijibu ni siku 365.

Hivyo, tofauti ni robo-siku. Kila miaka minne zile robo zinakuwa siku kamili. Ndicho kisa cha kuipata Februari yenye siku 29 kila baada ya miaka minne na kuufanya uwe mwaka mrefu au Leap Year.

Miaka mirefu au Leap Years ni kama 2000, 2004, 2008, 2012. Inaonekana rahisi kuutambua mwaka mrefu, kwani ni suala la kuhakikisha kama unagawanyika kwa nne bila baki.

Msomaji , naomba ushiriki kitendawili kifupi kujipima. Itafakari kwa makini miaka minne ifuatayo: 1700, 1800, 1900, 2100. Upi ni mrefu na upi ni mfupi? Weka majibu yako pembeni, tutayarejea kuona kama umepata au umekosa.

Msingi wa kuielewa kalenda ya sasa ni kuielewa kwanza kalenda ya Roma (Roman Calender) iliyotumiwa na warumi. Ilizinduliwa mwaka 738 KK ikiwa na miezi kumi huku ikiuanza mwaka kwenye mwezi Martius (Machi) au mwezi wa tatu. Mwezi ambao jua huwa kwenye mstari wa ikweta (Equinox) hivyo ni rahisi wataalamu kuutambua.

Mzunguko wa dunia uliodhaniwa kuwa ni mzunguko wa jua ulifahamika kuchukua siku 365. Kalenda haikulingana na mzunguko huo kwani ilikuwa na siku 304 na hivyo lilibaki pengo la siku 61.

Pengo hili hawakulipa jina la mwezi wowote, wakakiita hiki ni kipindi cha baridi (winter) wakisubiri kuuanza mwaka mpya kwenye ule mwezi Martius.

Mwaka 452KK , Numa Pompilius aliziba pengo lile kwa kuongeza mwezi Januarius (Januari) mwanzoni ukifuatiwa na mwezi Februarius (Februari). Kalenda mpya ikawa na siku 355 na pengo likabaki siku 10 tu.

Hizo siku kumi si haba. Zisiposhughulikiwa bado kalenda haitakidhi lengo la kulingana na mzunguko wa dunia. Mfano, jua litafika kwenye ikweta tarehe 31 badala ya tarehe 21 Martius (Machi) kwa mwaka wa kwanza na siku kumi zaidi mwaka wa pili.

Warumi walibuni mbinu ili tatizo lijiondoe kila baada ya miaka 24. Ndani ya miaka hiyo waliamua kuwe na miaka kadhaa mirefu (Leap years). Mwaka mrefu utaongezewa mwezi mwingine baada ya Februarius (Februari), mwezi ulioitwa Mercedonius.

Ndani ya ile miaka 24 kukawa na jumla ya siku 8,766 zilizofanya wastani uwe siku 365.25 kwa mwaka.

Jukumu la kuuongeza mwezi (Mercedonius) kila ulipofika mwaka mrefu, halikufanyika kwa umakini. Lilitawaliwa na uzembe uliosababisha mwezi usiongezwe kwenye baadhi ya miaka mirefu.

Uzembe ule ulileta athari gani? Mzunguko wa dunia hausubiri uzembe. Ilifika wakati matukio hayakuwa sambamba na tarehe zilizotarajiwa. Mwaka 50KK tarehe ya uzinduzi wa mavuno ilitofautiana miezi mitatu na siku halisi mavuno yalipoanza kuvunwa mashambani. Marekebisho yalihitajika.

Ndipo mwaka 45KK, mtawala Julius Caesar alitangaza kalenda mpya iliyoandaliwa na mtaalamu (astonomer) aliyeitwa Sosigenes. Ikaitwa Kalenda ya Julius (Julian Calendar) kwa ajili ya heshima ya mtawala, ikawa kama tunavyoiona kalenda yetu ya sasa.

Ndani ya kila miaka minne, kalenda itakuwa na siku 1,461. Hivyo wastani utakuwa ni siku 365.25 kwa kila mwaka kwani hiyo ndiyo iliyodhaniwa kuwa ni muda wa mzunguko. Pia mwaka mmoja mrefu utakuwa na siku 366 na utakuwa unagawanyika kwa nne. Miaka mitatu inayobaki itakuwa ni mifupi ikiwa na siku 365 lakini haigawanyiki kwa nne.

Siku moja zaidi inayofanya mwaka uwe mrefu itaongezwa baada ya mwezi Februari ili uwe na siku 29 badala ya 28.

Je, hii Kalenda ya Julius ilidumu? Kama haikudumu, kutodumu huko kulisababishwa na nini? Maswali haya yatatufanya tudadisi kisa cha kuwa na kalenda ya sasa. Lakini tujadili kwanza maendeleo ya utaalamu duniani

Usahihi wa mzunguko wa dunia ulizidi kujulikana. Hata leo bado wapo wanaojua kwamba mzunguko ule ni siku 365.25 kama ulivyokadiriwa kwenye Kalenda ya Julius. Lakini iligundulika kwamba mzunguko ule hutumia siku 365.24218967 na huitwa Tropical year.

Hapa ndiyo chanzo cha tatizo jipya, kwani 365.24218967 ni ndogo kuliko 365.25 kwa tofauti ndogo. Tofauti hii ni sawa na dakika 11 na sekunde 14.812512. Hivyo kasi ya mzunguko wa dunia (Tropical year) inazidi makadirio ya Kalenda ya Julius kwa dakika hizo chache.

Je, ni nini athari za tofauti hiyo ndogo? Tuijadili tofauti hii kwa hesabu za uwiano. Kama kwa mwaka tofauti ni dakika 11 na sekunde 14.812512 basi tofauti ya siku nzima itapatikana baada ya miaka miaka 128.0355.

Karne ya 16 wakatoliki walishaligundua tatizo hili. Walikumbuka mtaguso wa Nicaea uliofanyika mwaka 325BK wakati mtaguso wa Trent ulianza mwaka 1545BK. Hivyo mitaguso hii miwili ilipishana kwa miaka1,220.

Kwa yale mahesabu utaona kwamba hiyo miaka 1,220 italeta tofauti ya siku 9 na masaa sita. Kama jambo lilihusu tarehe na liliamuliwa na Mtaguso wa Nicaea, basi wakati wa Mtaguso wa Trent liliathirika kwa hizo siku tisa.

Je, kulikuwa na jambo la aina hiyo? Ndiyo. Mtaguso wa Nicaea ulipanga tarehe ya Pasaka iwe ni Jumapili baada ya mwezi mng’avu (Full moon) unaojitokeza baada ya Machi 21. Hii Machi 21 ni siku ambayo jua huwa juu ya ikweta yaani Vernal Equinox. Kumbe si rahisi kukuta Pasaka inaangukia Machi 21au kabla ya hapo.

Kwa tatizo lile la kalenda, Machi 21 iliwasili wakati tayari jua limeshavuka ikweta kwa siku tisa. Dalili kuwa pasaka ilianza kusherehekewa kimakosa katika siku isiyotakiwa.

Kwa nini mtaguso wa Nicaea haukuliona tatizo hili na kujikuta Kanisa Katoliki linapanga jambo litakalowaletea matatizo? Wakati wa mtaguso (325BK) tofauti ile ilikuwa masaa 2 na dakika 32. Haikuonekana madhara yake kwani hata Sosigenes aliyeunda kalenda ile aliitambua wakati anamkabidhi Julius Caesar kuizindua. Udogo wa tofauti hii ulimfanya na yeye asiizingatie.

Ukristo ulikuwa haujagawanyika kwa kiwango cha sasa, hivyo wakristo wengi ni washiriki wa maamuzi yale ya Nicaea hasa hili la siku ya Pasaka.

Kanisa Katoliki halitasahau lilivyohangaika kwa miaka mingi kutafuta utatuzi wa kitaalamu. Dr. Nicolaus Copernicus ni mmoja wa wataalamu (astronomer) walioitwa Roma kwa Papa kupeleka mapendekezo ya kuunda kalenda mpya itakayolingana na mwendo wa jua na mwezi.

Mapendekezo ya wataalamu yalijadiliwa kwenye Mtaguso wa Trent ulioanza mwaka 1545. Hakuna mapendekezo yaliyofaulu mtihani ule hivyo mtaguso ulimshauri Papa aunde tume itakayotayarisha kalenda mpya ili siku ya Pasaka irudi kuwa kama ilivyopangwa kwenye mtaguso wa Nicaea. Pia kalenda mpya itatue tatizo hilo lisijirudie tena.

Papa Pius IV alifunga mtaguso mwaka 1563 lakini alifariki kabla hajarekebisha kalenda. Papa aliyefuata (Pius V) alijaribu lakini akajikuta amerekebisha kalenda ya sala za Kanisa iitwayo Breviary ambayo haikusaidia. Alifariki mwaka 1572 na kurithiwa na Papa Gregory XIII.

Huyu Papa Gregory XIII ndiye aliyefaulu suala zima la Kalenda hadi iwe ilivyo leo. Je, alitumia mbinu gani?

Papa Gregory XIII aliunda tume ya kalenda iliyojumuisha wataalamu. Mfano, mmoja ni Profesa Carolus Laurus, mhadhiri wa hesabu katika Chuo Kikuu (Sapienza University of Rome) ambacho hadi leo ni chuo kikubwa barani Ulaya.

Tume ilijadili na kupitisha mapendekezo ya Profesa Aloysius Lilius aliyefariki wakati tayari ameshatengeneza kalenda yake lakini hakuna aliyekuwa akiijua isipokuwa mdogo wake Dr. Antonius aliyebahatika kuwa mjumbe wa tume ile pia.

Tume ilimkabidhi kalenda Papa Gregory XIII naye akatangaza kwamba Alhamis Oktoba 04, 1582 ni siku ya mwisho kutumika Kalenda ya Julius. Siku itakayofuata kalenda mpya itaanza huku ikiziba lile pengo ambalo lilishafika siku kumi wakati huo. Hiyo iliitwa Gregorian Calender (Kalenda ya Gregory).

Kwa mujibu wa Kalenda ya Julius, kalenda mpya ingeanza kutumika Ijumaa, Oktoba 05, 1582. Kwa Kalenda ya Gregory, iliyosogea siku kumi mbele, Ijumaa hii ilikuwa Oktoba 15, 1582.

Hii ndiyo sababu katika historia ya Kanisa Katoliki hutazikuta tarehe za Oktoba 05, 1582 hadi Oktoba 14, 1582, kwani hizo siku kumi ndizo zilizorukwa ili kuziba pengo lile.

Kalenda ya Gregory iliacha miaka mirefu iendelee kuwa ni ile inayogawanyika kwa nne. Miaka yote inayofunga karne hugawanyika kwa nne, mfano 1600, 1700, 1800, 1900 na 2000. Kalenda ya Gregory ilifanya mabadiliko kwa miaka hii. Kwamba ili miaka inayofunga karne itambulike kuwa ni mirefu, basi haitoshi kugawanyika kwa nne tu, bali pia igawanyike kwa mia nne (400).

Hivyo mwaka 1600 na 2000 ilikuwa miaka mirefu yenye siku 366. Lakini miaka ya 1700, 1800 na 1900 haigawanyiki kwa mia nne na hivyo ilikuwa mifupi yenye siku 365. Vivyohivyo mwaka 2100 hautakuwa mrefu.

Msomaji, turejee majibu ya kitendawili changu nilipouliza miaka 1700, 1800, 1900 na 2100. Usipoijua Kalenda ya Gregory ni rahisi kujiamini kwamba kitendawili kilikuwa rahisi na kudhani kwamba miaka yote ile ilikuwa ni mirefu. Kumbe yote ile kwenye kitendawili ni mifupi. Mpendwa msomaji, je, umepata swali lile?

Hatukuwepo mwaka 1900 na bila shaka hatutakuwepo mwaka 2100 kushuhudia ufupi wa miaka hiyo. Lakini wanaotumia program za kompyuta kama Microsoft Outlook 2007 wanaweza kuhakikisha kwani ina uwezo wa kukupa kalenda kuanzia Januari 01, 1601 hadi Agosti 31, 4500.

Je, hii kalenda ya Papa ilileta usahihi unaotakiwa? Ndani ya kila miaka mia nne (400) ilileta wastani mpya wa siku 365.2425 kwa mwaka. Ni mdogo kuliko ule wa siku 365.25 kwenye Kalenda ya Julius. Hivyo tofauti ya mzunguko wa dunia na kalenda mpya imekuwa ni sekunde 26.81 tu badala ya dakika 11 kama zamani kwenye Kalenda ya Julius.

Tumeona kwamba tofauti ya zamani ilitumia miaka 128 kuwa siku nzima. Kwa Kalenda ya Gregory tofauti ya siku nzima itafikiwa baada ya miaka 3,222.

Je, kalenda hii ya Papa Gregory XIII ambaye ni mkatoliki, iliwezaje kuwashawishi hata kwa wasio wakatoliki?

Kalenda mpya haikuwa na mamlaka yoyote nje ya nchi alizotawala Papa yaani Papal States. Hata hivyo kupokelewa kwake Ulaya kulikuwa kwa mgawanyiko. Nchi zilizojaa wakatoliki kama Italia, Hispania na Ureno ziliipokea mara moja toka siku ya kwanza.

Kwingine ambako Ukatoliki haukutawala, kalenda haikukubalika haraka kama vile ni jambo la kupigwa kunakoitwa “protest” kulikozaa neno “Protestant”.

Ujerumani walidhani kalenda hii ni mbinu ya kijanja ya kuwarudisha walutheri kwenye Ukatoliki iliyobuniwa kwenye mtaguso wa Trent. Hivyo wajerumani walichelewa kuikubali hadi mwaka 1700 tena baada ya kushauriwa na wataalamu wao.

Hatimaye dunia ikakiri kwamba ujio wa Kalenda ya Gregory ni wa kitaalamu zaidi na si suala la imani. Utaalamu wenye upeo wa kutatua tatizo kwa zaidi ya miaka 3,000 mbele.

Wafuatao waliikubali Kalenda ya Gregory kwenye miaka iliyowekwa kwenye mabano: Ubelgiji (1583), Denmark (1700), Uingereza (1752), Sweden (1753), Wasovieti (191, Ugiriki (1923).

Waliochelewa mabadiliko walizidi kuathirika kwani pengo la siku tumeona huongezeka kila baada ya miaka 128. Uingereza ilikuta pengo limeshakuwa siku 11 wakati Ugiriki na Wasovieti wamekuta pengo ni siku 13.

Watunzi wawili wa riwaya yaani William Shakespeare na Miguel de Cervantes ni mfano kwa tatizo la kuchelewa mabadiliko. Tarehe ya vifo vyao ni moja yaani Aprili 23, 1616.

Lakini ni kifo cha Shakespeare kilichelewa siku kumi zaidi, kwani Uingereza ilikuwa bado inatumia Kalenda ya Julius wakati Hispania ilikuwa inatumia Kalenda ya Gregory.

Umoja wa Mataifa haukupata shida au ulalamishi kuwaenzi watunzi hawa kwa kuitangaza hiyo Aprili 23 kuwa “Siku ya Kimataifa ya Vitabu na Hatimiliki au “World Book and Copyright Day” iliyozinduliwa mwaka 1995.

Nchini Uingereza kama kawaida kalenda mpya ililiziba pengo kwa kuziruka siku ambazo tayari zilishafika 11. Baadhi waliandamana wakidai kurudishiwa siku zao 11 zilizoonekana kama zimefutwa katika historia.

Nchini Ugiriki badiliko la kalenda mwaka 1935 lilitosha kuwakosanisha wakristo wa humo wa Makanisa ya Mashariki (Eastern Churches). Ulizuka mzozo kama huu wa askofu Emmanuel Milingo na Vatican. Wakati Milingo anakataa dhana ya mapadri kutooa kule Ugiriki wale maaskofu walitengana (schism) kwa ajili ya kuikubali au kuikataa Kalenda ya Gregory.

Hadi leo wapo wakristo wa Mashariki (Eastern Churches) wanaotumia Kalenda ya Julius hata kama nchi walizomo zimeshabadili na kutumia Kalenda ya Gregory. Pengo lile limeshakuwa siku 13 hivyo tunawatangulia kwa siku 13. Wao wataishangilia Krismas yao Januari 07, 2010 yaani siku nne zijazo.

Zifuatazo ni nchi zinazoitambua Januari 07 kuwa ni Krismas: Ethiopia, Misri, Russia, Serbia, Macedonia, Montenegro, Ukraine, Georgia, Moldova, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan.

Baadhi ya nchi hizo huzifanya Krismas zote mbili Desemba 25 na Januari 07 kama siku za mapumziko.

Nchini Misri, sikukuu pekee ya Kikristo iliyopewa mapumziko ni hii Januari 07 ambayo ni Krismas kwani Kanisa la Coptic Orthodox la Alexandria ndilo lenye wakristo wengi nchini humo.
 
Ndugu Paschal

Asante sana kwa kutoa somo hilo; ni mambo mazuri kuyafahamu ingawa baadhi yetu tunapenda sana tunaridhika kufuata mambo mbalimbali tuliyokuta duninai hapa bila kujua background zake.

Vile vile kuna sababu za kwa nini kalenda hii ina miezi 12 badala ya miezi 13 inayolingana na idadi ya mizunguko ya mwezi kuizunguka dunia katika mwaka mmoja. Mwezi mmoja huzunguka dunia kwa siku 28 kwa hiyo katika hizo siku 365.25 mwaka, mwezi utakuwa umezunguka dunia mara 13.04; haitakuwa vibaya kama utatoa somo hilo pia.
 
Kwa nini waliibadilisha Kalenda ya Kibiblia kama ilivyotabiriwa katika Kitabu cha Daniel sura ya pili?
 
Ndugu Paschal

Asante sana kwa kutoa somo hilo; ni mambo mazuri kuyafahamu ingawa baadhi yetu tunapenda sana tunaridhika kufuata mambo mbalimbali tuliyokuta duninai hapa bila kujua background zake.

Vile vile kuna sababu za kwa nini kalenda hii ina miezi 12 badala ya miezi 13 inayolingana na idadi ya mizunguko ya mwezi kuizunguka dunia katika mwaka mmoja. Mwezi mmoja huzunguka dunia kwa siku 28 kwa hiyo katika hizo siku 365.25 mwaka, mwezi utakuwa umezunguka dunia mara 13.04; haitakuwa vibaya kama utatoa somo hilo pia.

Thanks for knowledge. Nilivyoelewa ni kwamba mzunguko wa muhimu ni ule wa dunia kulizunguka jua ambao ndiyo unaoleta hiyo equinox. Nilivyosoma ni kwamba mzunguko wa mwezi haukuwahi kufikiriwa isipokuwa kwa kukadiria siku ya Pasaka ipatikane vipi ikiwa na uhusiano na equinox ya Machi 21.

Neno mwezi wa kalenda linafanana na mwezi unaozunguka dunia. Lakini mwezi wa kalenda kwa kiingereza si moon bali ni month.
 
Kwa nini waliibadilisha Kalenda ya Kibiblia kama ilivyotabiriwa katika Kitabu cha Daniel sura ya pili?

Mkuu, wewe unayeuliza ni mkristo gani ambaye hukushiriki uamuzi ule? Soma kipande cha article hapa chini kwamba na wewe ulishiriki.

Ukristo ulikuwa haujagawanyika kwa kiwango cha sasa, hivyo wakristo wengi ni washiriki wa maamuzi yale ya Nicaea hasa hili la siku ya Pasaka.
 
Thanks for knowledge. Nilivyoelewa ni kwamba mzunguko wa muhimu ni ule wa dunia kulizunguka jua ambao ndiyo unaoleta hiyo equinox. Nilivyosoma ni kwamba mzunguko wa mwezi haukuwahi kufikiriwa isipokuwa kwa kukadiria siku ya Pasaka ipatikane vipi ikiwa na uhusiano na equinox ya Machi 21.

Neno mwezi wa kalenda linafanana na mwezi unaozunguka dunia. Lakini mwezi wa kalenda kwa kiingereza si moon bali ni month.

Nashukuru kwa hiyo paragraph ya kwanza lakini, da!! kwenye hii paragraph ya pili umeni-paint kama kwamba sijui tofauti kati ya moon na month ambayo katika kiswahili yanatumia jina moja tu la mwezi. Nadhani umenionea bure tu, I know more than that.

Sasa turudi katika ile paragraph yako ya kwanza; siyo kweli kuwa kwenye upangaji wa kalenda walifuata mzunguko wa jua tu, hapana, walifuata pia muda utumikao kwa mwezi kuzunguka dunia ujulikanao kama lunar month ambao ni kati ya siku 28 na 29, ndiyo maana mwaka mmoja katika kalenda za awali ulikuwa na miezi 13 (lunar months) wakiwa na imani kuwa mwezi mmoja ni siku 28 kamili. Kuna mambo yaliyosababisha usitishwaji wa matumizi hayo ya lunar months kwenye calendar hizo na kuanzisha hizi zinazoitwa calendar months ambamo idadi ya siku hubadilika badilika. Sababu Mojawapo lilikuwa ni ukweli kuwa siku zitumikazo katika kukamilisha mzunguko mmoja wa mwezi hazikuwa 28 kamili kama ilivyokuwa imeaminika hapo mwanzo bali zilikuwa zinabidilika badilika kati ya siku 28 hadi siku 29.5, sababu nyingine lilkitokana na kalenda hizo kuwa zinapredict kwa karibu sana siku za akina mama wengi; yaani iwapo siku za mwanamke katika mwezi mmoja zikishajulikana basi ilikuwa ni rahisi kupredict siku zake katika maisha yake yote.
 
Paschal,

Asante kwa elimu hii ambayo si rahisi sana kuipata darasani!
 
Du kumbe kuindaa kalenda hii haikuwa kazi rahisi. Asante sana kwa elimu hii Paschal.
 
Ndugu Paschal

Asante sana kwa kutoa somo hilo; ni mambo mazuri kuyafahamu ingawa baadhi yetu tunapenda sana tunaridhika kufuata mambo mbalimbali tuliyokuta duninai hapa bila kujua background zake.

Vile vile kuna sababu za kwa nini kalenda hii ina miezi 12 badala ya miezi 13 inayolingana na idadi ya mizunguko ya mwezi kuizunguka dunia katika mwaka mmoja. Mwezi mmoja huzunguka dunia kwa siku 28 kwa hiyo katika hizo siku 365.25 mwaka, mwezi utakuwa umezunguka dunia mara 13.04; haitakuwa vibaya kama utatoa somo hilo pia.

Mkuu,

Warumi walikuwa tayari wameshakuwa scientific kuliko taifa lolote na ndiyo mana wakati huo waliweza kueneza kalenda zao kokote walikotawala.

Kumbuka science ndiyo iliyofanya Roman Empire kuvunja rekodi ya kuwa superpower kwa zaidi ya millenium.

Technology ya lunar calender hawakuitumia warumi kwani kwao solar calender ilikuwa more advanced na hivyo mambo ya kuhesabu kwa mzunguko wa mwezi waliwaachia wengine ten kule ambako hawakufika kutawala kama vile uarabuni.
 
PASCHAL MATUBI ARE YOU JOURNALIST?

This is good article to be found in Tanzanian news papers!!!

you rock
 
Kumbe kuna watu waliumiza akili eeeh!! Ingekua kipindi hiki. Ingekua ngumu sana kuset calenda
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom