Kalamu Yenye Siri ya Damu

NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269
SEHEMU YA 06

Ilikuwa ni lazima Chilo aangalie ni kwa namna gani biashara ya kitabu alichopanga kukiweka kwenye Mtandao wa Amazon kinakuwa na mvuto na hata kusomwa na watu wengi.
Haraka sana akawasiliana na Kindo Emmanuel ambaye alikuwa mbunifu wa makava na kuanza kuzungumza naye, ilikuwa ni lazima atengenezewe kavaa ambalo litamvutia kila mtu ambaye angekiona.
Hakutaka kubaki na jambo hilo kichwani mwake, haraka sana akampigia simu na kuanza kumwambia kuhusu kitabu hicho, alikipa jina la There is No God At All yaani Hakuna Mungu kabisa.
Mara ya kwanza Kindo kusikia jina la kitabu hicho akashtuka, hakuamini kama kungekuwa na mwandishi ambaye angediriki kuandika kitabu cha namna hiyo. Alikuwa na maswali mengi ya kuulizwa, kwa mtu kama Chilo, Mwafrika ambaye alimpenda Mungu na kumuabudu lisingekuwa jambo jepesi kuwa na kitabu chenye jina kama hilo.
“Sasa Chilo ndugu yangu wewe si mtoto wa mchungaji?” aliuliza Kindo huku sauti yake tu ilivyokuwa ikisikika ilionyesha alikuwa na hofu.
“Ndiyo!”
“Na si ulisoma Seminary?”
“Ndiyo!”
“Na kanisani ukawa unakwenda?”
“Tena sana tu! Ile shule hatari, asubuhi kanisani, mchana kanisani na usiku kanisani!” alimjibu.
“Na unamwabudu Mungu kwa asilimia mia moja?” aliuliza Kindo.
“Maswali yamekuwa mengi sana, mengine bakiza utaniambia siku nyingine. Hilo kava linatengenezwa lini?” aliuliza Chilo, aliona maswali yanakuwa mengi sana.
“Umekengeuka mshikaji wangu!” alisema Kindo.
“Hapana! Hebu niambie, inawezekana ama?”
“Itawezekana! Ngoja niingie Google kutafuta picha,” alisema Kindo.
“Hapana! Hiki kitabu kitauzwa kimataifa, kama ni picha, nitamtafuta msichana kwa lengo la kupiga picha ambayo tutaitumia,” alisema Chilo.
“Sawa. Mkishapiga nitumie!”
“Haina shida.”
Kazi ikabaki kwa Chilo, ilikuwa ni lazima kutafuta msichana ambaye angekwenda kupigwa picha kwa lengo la kutumika kwenye kava la kitabu hicho. Haraka sana akaingia Facebook na kuangalia picha kadhaa za msichana aliyekuwa akimtaka.
Kwa sifa ya msichana aliyemwandika kwenye kitabu hicho alikuwa mwembamba, mweusi kidogo lakini aliyekuwa na uzuri wa kumvutia kila mtu ambaye angemwangalia, kwenye kuangalia huko macho yake yakatua kwa msichana aliyekuwa akijiita kwa jina la Pearl Mk.
“Huyu atafaa! Ila atakubali?” alijiuliza.
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akamtumia meseji na kuanza kuwasiliana naye, alichomwambia ni kwamba alihitaji kuonana naye kwa lengo la kuzungumza kidogo.
Msichana huyo hakujiamini, hakuwahi kuongea na Chilo, alimuogopa, mawazo yake yalifikiria ni mwanaume mtu mzima, mwenye mwili mkubwa, simulizi alizokuwa akiziandika zilimtisha na kuhisi alikuwa mtu ambaye hakustahili kuonana naye.
“Uonane na mimi?” aliuliza msichana huyo kwenye simu.
“Ndiyo! Ninahitaji kuzungumza na wewe!” alimwambia.
“Kuhusu nini?”
“Labda nakutaka!” alisema na kuanza kucheka.
“Unanitaka mimi?”
“Hahaha! Mbona hujiamini bhana! Una nafasi kwa kesho?” aliuliza.
“Mh!”
“Mh nini sasa na wewe!”
“Yaani! Jamani! Sasa mbo...”
“Pearl acha masihara bhasi!”
“Wewe ndiyo umeanza masihara, yaani uonane na mimi! Kuna shida gani?”
“Jambo dogo tu! Halafu jepesi sana! Naomba kuonana nawe kwa kesho. Unatoka chuo saa ngapi?” aliuliza.
“Saa kumi.”
“Saa kumi na mbili nitakuwa Pizza Hut hapo pembeni ya Serena Hotel!” alimwambia.
“Pembeni ya Serena Hotel?”
“Yaani umesikia hoteli ushaanza kuogopa. Basi acha niseme pembeni ya Jengo la Uhuru Heights! Naomba kuonana nawe. Saa kumi na mbili, usikose, ukishindwa niambie nimwambie msichana mwingine!” alimwambia.
“Nitajitahidi!”
Pearl, msichana mrembo hakuwa akijiamini, aliiangalia simu yake mara mbilimbili, hakuamini kama alipigiwa simu na Chilo. Alizoea kumuona mwanaume huyo kwenye mitandao, hakuamini kama kuna siku angempigia simu na kuomba kuonana naye.
Aliwahi kuzungumza naye mara moja tu, tena zamani alipohitaji kitabu, na bahati mbaya kwake, Chilo akamwagiza mtu ampelekee kitabu hicho huku yeye akidai kuwa bize. Ilimuuma lakini hakutaka kumwambia.
Leo hii mwanaume huyo alimwambia alihitaji kuonana naye, hakujua alitaka kitu gani kutoka kwake. Aliingia kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali kwa kuhisi labda kulikuwa na picha chafu zake ambazo mwanaume huyo alizinasa, hakufanikiwa kuziona, na hakuwahi kupiga picha za namna hiyo. Sasa alikuwa akimuhitajia nini?
Hakutaka kuwaza sana, kwa kuwa alimwambia walitakiwa kuonana Posta, hakuwa na jinsi, siku iliyofuata mapema sana akatoka Kigamboni na kuelekea huko huku akionekana kutokujiamini hata kidogo.
Alipofika hapo akatulia na kuagiza chakula na kula mdogo mdogo huku akimsubiri Chilo mahali hapo. Baada ya dakika kadhaa macho yake yakatua kwenye gari ndogo aina ya Vitz ambayo ilisimama na mwanaume huyo kuteremka.
Kitendo cha kumuona tu akahisi mapigo yake ya moyo yakiwa juu, hakuamini, alikuwa akitetemeka na kwa mbali kijasho chembamba kikaanza kumtoka, akatamani kukimbia mahali hapo.
Chilo akaingia na kuanza kuangalia huku na kule, macho yake yalipotua kwa msichana huyo, akamsogelea, akamsalimia na kuanza kuzungumza naye.
Pearl alitamani kutoa kamera yake na kumpiga picha, alitamani kumkumbatia, alitamani kufanya kitu chochote kile kuonyesha furaha aliyokuwanayo mara baada ya kumuona mtu ambaye alitamani sana angekuwa na uwezo kama wake, kuandika vitu vikubwa kama alivyokuwa akiviandika.
“Najaribu kuyatafakari hayo macho yako!” alisema Chilo baada ya mazungumzo marefu kidogo.
“Yamefanyaje?”
“Ni kwamba unanionea aibu ama unaniogopa?” alimuuliza.
“Kawaida tu!”
“Kwamba?”
“Wala sikuogopi!”
“Kumbe?”
“Basi tu!”
Chilo hakuzungumza kitu, akaachia tabasamu na kumkazia macho msichana huyo, Pearl alihofu, alitamani kumwambia alitaka kuondoka lakini akavuta subira na kusubiri alichoitiwa mahali hapo.
“Kuna kitabu nimeandika!” alimwambia.
“Kitabu gani?”
“Cha hadithi!”
“Unauza shilingi ngapi ninunue?” aliuliza kwa bashasha.
“Dola kumi!”
“Dola tena?”
“Yeah! Ila nitahitaji unisaidie kitu kimoja!”
“Kipi?”
“Nahitaji nikutumie kwenye kava la kitabu hicho!”
Ni kama Pearl hakuamini, alimwangalia Chilo mara mbilimbili, ni kweli alimaanisha kile alichokisema ama alikuwa akitania. Yeye kukaa kwenye kava, kila mtu amuone lilikuwa ni kama ndoto machoni mwake, hakuamini kama kuna siku picha yake ingetumika kwenye kava la kitabu.
Kukataa lingekuwa jambo jepesi sana lakini hakutaka kufanya hivyo. Hakutaka kujua sababu ya Chilo kumchagua yeye, kuwa kwenye kava hilo, tena kwa mbele kwake ilikuwa ni fahari kubwa mno. Akamkubalia.
“Gharama yako?”
“Yaani jamani! Mimi hata bure!”
“Hahaha! Hapana! Mjini cha bure ni salamu tu! Na unaponiambia bure, unanitia hofu!” alisema Chilo.
“Mh! Sasa jamani mimi nitasema kiasi gani?”
“Chochote kile!”
“Mh! Yaani hata sijui!”
“Basi nitakulipa. Sipendi nifanyiwe kazi bure, hasa kazi ambayo inakwenda kuniingizia pesa. Nitakutafuta kwa ajili ya kupiga picha. Umelipia chakula?” alisema na kumuuliza.
“Bado!”
“Basi shika hiyo utalipia. Naomba nikutakie jioni njema!” alisema Chilo na kusimama huku akimpa kiasi cha shilingi elfu ishirini.
“Asante!”
Chilo hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka na kuendelea na mambo mengine. Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza kilikuwa ni kufuatilia kwa kina kuhusu mtandao wa Amazon, ilikuwa ni lazima ajue namna ambazo kitabu chake kilitakiwa kuwa na kuingizwa humo.
Aliangalia kila kitu na kukubali kwamba ni lazima atumie jina la Williams McCannon. Alitaka kufanya hivyo kwa sababu alihitaji sana kitabu hicho kisomwe na watu wengi, hasa Wazungu ambao walipenda sana kusoma vitabu.
Kama angeliweka jina la Juma Hiza ingekuwa ni vigumu sana kitabu hicho kupakuliwa na kusomwa na ndiyo maana alihitaji kuweka jina lililoendana na majina yao ili iwe rahisi kununuliwa.
Alijifunza zaidi usiku huo na alipomaliza, akampigia simu Juma Hiza, wakaonana na kumwambia alitakiwa kujiandaa ilikuwa ni lazima kwenda kufungua akaunti kwenye Benki ya Barclays.
“Kufungua akaunti haina shida!” alisema Juma.
“Ila subiri kwanza! Hapa inabidi tucheze mchezo mmoja mkubwa sana, hutakiwi kufungulia akaunti nchini Tanzania, ni lazima iwe Afrika Magharibi!” alisema Chilo.
“Kwa maana ya Ghana, Cameroon, Nigeria, ama unataka wapi?” aliuliza Juma Hiza.
“Nigeria!”
“Sasa huko tutakwendaje?” aliuliza, Chilo akaanza kucheka.
“Vipi tena?”
“Tutafunguliwa akaunti huko!”
“Na nani?”
“Unawajua watu wanaitwa Yahoo Boys?” aliuliza Chilo huku akimwangalia Juma.
“Yahoo Boys? Ndiyo akina nani?”
“Hawa ni vijana kama sisi tu, wao wanadili na utapeli wa mitandaoni yaani Scammers, ni vijana wanaokaa na laptop vyumbani, wanakutapeli kupitia mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. Ushawahi kutumiwa meseji Facebook msichana akajitambulisha yeye ni Christina ameachiwa pesa na baba yake tajiri, alihitaji kuja kuweka kwenye akaunti yako, sijui anakuamini, analelewa na mchungaji mmoja huko mbele?” aliuliza Chilo.
“Nishatumiwa mnooo!”
“Sasa waliokutumia hao ndiyo wanaitwa Yahoo Boys! Hao watu hatari, wanaongozwa na jamaa anayeitwa Ray Hushpuppi, ukipata muda utamcheki Instagram uone mwamba anavyokula bata,” alisema Chilo.
“Duuh!”
“Ninajua mambo mengi sana, ila nikwambie kitu kimoja usichokijua, mimi pia ni Yahoo Boy!” alisema Chilo huku uso wake ukiwa kwenye usiriazi na kile alichokuwa akikizungumza.
“Sijakuelewa!”
“Najua hujaelewa. Kwenye hii sekta unatakiwa kuwa makini sana, niliamua kuwa mmoja wa vijana wa Yahoo Boy miaka kama mitatu iliyopita, niliamua kuwa hivyo kwa sababu ya kufanikisha huu mpango wetu. Juma, huu ni mpango ambao niliupanga kabla ya kuonana nawe, ulikuwa kichwani mwangu na nilihitaji sana siku moja nije kupata mabilioni ya pesa,” alisema Chilo.
“Kwa hiyo na wewe ni Yahoo?”
“Yeah! Ongezea Boy kwa mbele ila sijawahi kutapeli! Niliamua kujiunga nao kwa ajili ya huu mchongo tu, kwenye mtandao huo nilifahamiana na washikaji wengi, wa kwanza anaitwa Usman Umar. Kuna stori nyingi sana kuhusu huyu jamaa, nisingependa kupoteza muda sana ila jua mchizi amemuoa manzi fulani anaitwa Lisa kutoka nchini Marekani. Huyu jamaa nilikuwa naye beneti mitandaoni na kitu nilichomwambia anifungulie akaunti kwenye Benki ya Barclays nchini Nigeria ikiwa na jina la Williams McCannon. Kazi hiyo itafanyika haraka sana endapo tutatuma picha yako,” alisema Chilo.
“Mh! Unamwamini jamaa? Sasa atanifunguliaje akaunti? Saini yangu vipi?” aliuliza Juma.
“Juma! Kuna matatizo mengi sana duniani, ila hakuna tatizo linaloitwa saini! Wadau wanasema ukienda pale Posta hata saini ya ikulu unaipata! Andika saini yako, nitatuma kwa jamaa na kila kitu kitafanyika!” alisema.
“Unamwamini mchizi?”
“Yeah! Hakuna tatizo lolote lile!”
Juma hakuwa akijiamini hata kidogo kufanya alichoambiwa na Chilo akifanye lakini hakuwa na jinsi, alikifanya na kila kitu kutumwa nchini Nigeria. Suala hilo lifanyika, hakujua Usman alilifanyaje lakini alifanikiwa na baada ya siku kadhaa alipokwenda kuangalia akaunti yake na namba ya siri aliyopewa, alishangaa kuona imekubali.
Yahoo Boys hawakuwa watu wa mchezo, walijua kufanya vitu kwa utalaamu mkubwa, duniani kulikuwa na watu wengi walikuwa wakilizwa, kuna wengine waliibiwa mpaka dola milioni mia moja na vijana hao ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kula bata tu.
Walinunua magari ya kifahari na majumba makubwa kwa pesa ndefu, walilala na wanawake waliokuwa wakiwataka, walifanya kila aina ya ujinga mpaka pale CIA walipoamua kuingilia kati na kuanza kumkamata mmoja baada ya mwingine.
Baada ya kukamilisha kila kitu, Pearl akapiga picha, kava likatengenezwa, kitabu kikapangwa na hatimaye kuingizwa sokoni huku namba ya malipo ikiwa ya akaunti ambayo ilifunguliwa nchini Nigeria.
Kwa siku ya kwanza tu kitabu kilipowekwa katika Mtandao wa Amazon kila mtu alishtuka, hapakuwa na mtu aliyeamini kama kungeandikwa kitabu kilichokuwa na jina kama lile lililokuwa mbele ya kava hilo ambalo kulionekana picha ya msichana mrembo aliyekuwa ameshika mkoba ambapo ule mkono ulioshikilia mkoba ule begani ukiwa na simu na kwa mbali yalionekana majengo ya WTC yaani World Trade Center yaliyokuwa jijini New York nchini Marekani.
Kava lilivutia machoni, jina lake ndilo lilikuwa chachu ya watu kutaka kufahamu hasa kilichokuwa kimeandikwa humo. Walipoanza kusoma tu, kila mmoja hakuamini, ilikuwa ni simulizi iliyoandikwa kwa mtindo wa flashback, yaani kuanza mwisho na kuja mwanzoni.
Ni ndani ya kurasa hamsini za mwanzo tu, kulikuwa na jumbe mbalimbali, maneno ambayo kwa namna moja yalionyesha ni kwa namna gani majengo hayo yalilipuliwa huku chanzo kikiwa ni msichana mmoja aliyejulikana kwa jina la Esta kutoka barani Afrika kuingia ndani ya jengo moja akiwa na simu ambayo iliweza kupeleka taarifa kwa Waarabu waliokuwa uwanja wa ndege wakisubiri kufanya safari zao za humohumo, simu ile iliweza kunasa sauti ya kila floo aliyokuwa akipita msichana huyo mpaka alipofika floo ya juu kabisa.
“Hiki kitabu..mh! Hebu subiri niendelee kusoma zaidi, nadhani kuna mambo nayaona kabisa yalijulikana kabla, nadhani kutakuwa na mengi ambayo mwandishi anajaribu kutuambiwa kwa mafumbo na kwa undani zaidi juu ya kile kilichokuwa kimetokea,” alisema Peter O’Brain, mwanaume aliyekuwa msimamizi wa maofisa wa CIA hapo Marekani.

Je, nini kitaendelea?
 
NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269
SEHEMU YA 07.

Gumzo kubwa duniani kwa kipindi hicho lilikuwa ni kitabu hicho kilichokuwa kimeandikwa na kuwekwa katika Mtandao wa Amazon. Kilikuwa kinaelezea vitu vingi vilivyokuwa vimefungwa ambavyo hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akivijua kabla.
Hilo likawachanganya watu wengi, hawakuamini kama kweli kulikuwa na mwandishi aliyekuwa akiandika simulizi nzuri na iliyojaa mafumbo kama hiyo iliyokuwa imeandikwa.
Williams McCannon akawa mtu aliyekuwa akisikika zaidi sehemu mbalimbali kwa sababu ya kitabu chake. Kwa siku saba za mwanzo tu jina lake likawa linaongoza kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wametafutwa sana kwenye Tovuti ya Google.
Watu mbalimbali walipoingia kwenye Mtandao wa Wikipedia kwa lengo la kumsoma zidi na kumfahamu, au hata kuvifahamu vitabu vingine alivyokuwa ameviandika, hawakufanikiwa kumuona, yaani ilionyesha hicho ndicho kilikuwa kitabu chake cha kwanza kuandika.
Wengi walisikika, mtu makini kama huyo hakutakiwa kuandika kitabu kimoja tu, ilitakiwa kuwa na vitabu vingi kwa lengo la kuwafundisha watu jinsi dunia ilivyokuwa ikienda kwa wakati huo kwani alionekana kufahamu mambo mengi mno.
Akaunti ya mwanaume huyo ilizidi kujazwa pesa, watu walikinunua kitabu hicho kwa gharama ya dola kumi tu na pesa hizo kuchukuliwa na Chilo, Juma Hiza nchini Tanzania na kuendelea na mambo yao.
Taratibu watu hao wakaanza kuwa matajiri, walikula bata, wakanunua majumba na magari ya kifahari, maisha yao yalibadilika lakini kila siku Chilo alimwambia Juma kuwa alitakiwa kujiandaa kwani muda wowote ule mambo yangebadilika na kuanza kutafutwa.
“Sasa wakinitafuta watanipata?” aliuliza Juma huku akimwangalia Chilo.
“Juma! Unaposikia CIA sio watu wa kawaida ukadhani wale ni Waafrika. Mule kuna watu wanaongea Kichaga kama wamezaliwa Kilimanjaro! Wakitaka kupeleleza kwetu Dodoma, utaletewa watu wanapiga Kigogo kama Wagogo kumbe ni watu weusi waliozaliwa na kukulia nchini Marekani,” alisema Chilo huku akimwangalia Juma aliyeonekana kushangaa.
“Duh! Basi hao watu ni hatari!”
“Ndiyo hivyo! Cha msingi kuwa makini na mambo mawili. Kwanza usipokee simu kwa namba ngeni inayokutafuta,” alisema Chilo.
“Kwa sababu gani?”
“Ni rahisi sana kukudaka na kujua mahali ulipo,” alimwambia.
“Basi nibadilishe namba!”
“Pia hakuna tatizo! Ila la pili sasa!” alimwambia.
“Lipi?”
“Mademu!”
“Hahaha! Wamefanyaje sasa?”
“Hao ni watu hatari sana, ni hatari zaidi ya simba!”
“Mh!”
“Wakati wa Vita Baridi kati ya Marekani na Urusi, watu hao walitumika sana, na walifanikiwa kwenye kila ishu waliyokuwa wakitumwa, watu wakiona wewe ni mwanaume, wanakuletea mwanamke, mrembo kama malaika, ana saa sita, kiwowowo cha kizushi, ndugu yangu unatokaje hapo? Hahahaha!” alisema Chilo.
“Jamani jamani jamani!” alisema Juma.
“Hawa ni watu wa kuwa nao makini sana!”
“Sawa.”
“Najua umenielewa, cha ajabu baadaye nasikia Juma kadakwa kisa kaona saa sita sehemu, kaitamani, watu wakamuwahi,” alisema Chilo na kuanza kucheka.
Maisha yalikuwa ya mafanikio makubwa, ni ndani ya mwezi mmoja kila kitu kilibadilika, hawakuwa vijana wale waliopigika, walikuwa wengine waliokuwa na pesa ndefu. Walifanya walichotaka huku kitabu walichokiweka kwenye Mtandao wa Amazon kikiendelea kuingiza pesa kila siku.
Walifungua biashara zilizowapa pesa zaidi na zaidi kiasi cha kila mmoja kuona huo ndiyo ungekuwa mwisho wa umasikini, yaani wasingekula tena chakula wanacholetewa bali wangekula chakula wanachokitaka, watoto wao hapo baadaye wangekuwa na maisha mazuri, wasingekuwa masikini tena.
***
“Huyu mwanamke ndiyo chanzo,” alisema Peter huku akionekana kuwa makini na kitabu hicho.
Kilikuwa ni kikao cha tatu tangu kuanza kwa uuzaji wa kitabu hicho katika Mtandao wa Amazon, maofisa wa CIA walikutana kwa lengo la kukijadili na kuyajadili mambo yote yaliyokuwa ndani ya kitabu kile.
Sababu kubwa ilionekana kuwa ni mwanamke, yaani yeye ndiye aliwapa uelekeo magaidi wale waliokuwa uwanja wa ndege, aliwapa ishara kwamba kila kitu kilikuwa tayari na walitakiwa kuyalipua majengo hayo.
“Waliingiaje ndani ya ndege kirahisi sana?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hilo ndilo swali lililokuwa limetusumbua kwa miaka yote hiyo, ila amini usiamini, kitabu hiki kimekuja na majibu. Kimeeleza wanaume hao waliingia kwa kujifanya wabeba mizigo ambao walikuwa na jukumu la kupeleka mizigo ndani ya ndege, walikuwa na bastola zao, visu, hawakupekuliwa kwa kuwa tayari wabeba mizigo huwa hawakaguliwi,” alijibu Peter huku akiwaangalia wenzake.
“Halafu? Ila si kama walipeleka mizigo walitakiwa kurudi mjengoni, ikawaje wakazamia?” aliuliza mwanaume mwingine.
“Napo kitabu kimetupa majibu yake.”
“Kwamba kinasemaje?”
“Mwandishi anasema kulikuwa na watu sita ambao ndiyo waliokuwa wakibeba mizigo hiyo, wakati wameipeleka, wawili wakazamia humo na kurudi wanne, kwa hiyo ilikuwa vigumu sana kuwagundua kama walikuwa sita kutokana na ile idadi ya watu waliorudi ilikuwa nyingi,” alijibu.
“Sawa. Kwa hiyo lilifanyika hilo kwenye ndege zote mbili?” aliuliza.
“Ndiyo!”
“Na vipi yule mwanamke wa kule kwenye jengo aliyekwenda na simu. Kwa mujibu wa kitabu ni kwamba alikuwa Mwafrika, na kwa mujibu wa kitabu hichohicho na uchunguzi wetu, watu waliokuwa ndani ya ndege ambao waliwaambia marubani kwenda kugonga majengo yale walikuwa Waarabu, hawa watu walikutana vipi?” aliuliza jamaa mwingine huku akiumauma kalamu aliyokuwa ameishika.
“Huyu msichana wazazi wake walitekwa, alikuwa ni mtu wa Nigeria, akaambiwa ili wazazi wake waachwe basi ilikuwa ni lazima kufanya hicho alichokifanya, na kweli akafanikiwa,” alisema Peter.
“Kwa hiyo akafariki?”
“Yeah!”
“Ukawa mwisho wa kitabu ama?”
“Hapana! Sasa kuna huyu mwanaume aliyekuja Marekani kutoka nchini Nigeria, nadhani tufuatilieni kuhusu huyu mwandishi, nitakuwa nawaambia kila kitu klichozungumziwa humu, huyu ndiye aliyeleta balaa sasa, na ndiye mtu anayetufanya tumtafute huyu mwandishi, aliyajuaje haya yote?” alisema Peter huku akionekana kuwa na mawazo tele.
“Inabidi atafutwe!”
“Kabisa. Mkianza kufanya hivyo, suala hili nitalipeleka kwa bosi, Todd tuone tunafanyaje kwani naye anaonekana kuwa bize sana kipindi hiki, kuna mambo mengi yanamuweka kwenye wakati mgumu!” alisema Peter, kitengo cha upelelezi cha CIA kiligawanyika katika vipengele kama kumi na mbili, kila mmoja alikuwa akishughulika na chake.
“Anahangaikia suala gani tena?”
“Kuhusu Donavan Skull. Mnamkumbuka?”
“Yule mtekaji na muuaji?”
“Ndiye huyohuyo.”
“Kitengo cha Secure 44 kimejitahidi sana kumtafuta mtu huyo na hawakumpata kwa kuwa anabadilisha sana sura, inawezekana vipi akaendelea kumtafuta na wakati hii ni miaka mingi na bado hajafanikiwa?” aliuliza.
“Inashangaza ila anahitaji kuwapata watu watatu ambao anaamini watamsaidia!” alijibu.
“Akina nani?”
“Robert, Richard na Robinson! Acha awatafute hao, akiwapata ndipo nitamfikishia kuhusu hili suala, ni jambo muhimu sana, na kwa maelezo ya kitabu, kinasema inawezekana kukaibuka mlipuko mwingine ama siri za kambi za kijeshi za Marekani zikatoka na kwenda kwa maadui zetu! Huyu mwandishi ni lazima apatikane kwanza,” alisema Peter.
“Kwa hiyo Todd anaamini hao vijana wataweza kumpata Skull?” aliuliza mwanaume huyo.
“Wale vijana achana nao, wasikie tu. Ni wasumbufu na wabunifu, unakumbuka kuna kazi tulipewa kuhusu neno la Angelica? Yaani sehemu walipokuwa vijana hao! Mnakumbuka?” aliuliza Peter huku akiwaangalia wenzake.
“Ndiyo! Halafu sikufuatilia ilimaanisha nini!”
“Ndiyo maana nilisema wale vijana ni hatari sana. Yaani sisi tulidhani ni eneo linaitwa Angelica kumbe siyo. Yaani jina hilo lilitokana na mahali fulani huko Peru panapoitwa Ica, huo ni mji ambao ni maarufu sana kwa kutengeneza pombe ziitwazo Angel, hivyo neno Angelica lilikuwa ni muunganiko wa mji wa Ica na pombe ya Angel, huoni hadi hapo hao watu walikuwa hatari sana kiasi cha kutusumbua CIA? Kwanza acha watafutwe, si kwa ubaya, wanatakiwa kuja kufanya kazi ya kuhakikisha Skull anapatikana kwa udi na uvumba!” alisema Peter.
“Bila shaka watakubali, hakuna anayethubutu kuacha kufanya kazi na Marekani,” alisema mwanaume mwingine.
“Inaweza kuwa ngumu!”
“Kwa sababu gani?”
“Unamkumbuka yule gaidi aitwaye Omar Al Fadhuu?” aliuliza Peter.
“Yupi? Kuna Omar wawili ambao wote ni hatari! Kuna yule Omar aliyeuawa na CIA lakini hatukubahatika kuupata mwili wake lakini pia kuna Omar Bin Sharif, unamzungumzia yupi?” aliuliza jamaa mwingine.
“Sikilizeni! Kuna huyu Omar Bin Sharif anayeongoza kundi la kigaidi la Al Qaida ambaye ndiye tunahangaika kumpata lakini kulikuwa na Omar Al Fadhuu ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Mujaideen. Mnamkumbuka?” alitoa maelezo na kuuliza.
“Yeah! Nimemkumbuka!”
“Yule gaidi alikamatwa, mchoro mzima ulichorwa na vijana hao watatu, ni watu hatari sana, kinachonisikitisha, waliahidiwa pesa, hawakulipwa na ndiyo maana wakaichezea helkopta na kuanguka majini, na ndiyo maana mpaka leo hii sisi Wamarekani tunasema tulimuua Omar Al Fadhuu lakini hakuna mwili wake ulioonyeshwa, na dunia haiamini mpaka leo hii,” alisema Peter.
“Mh! Kama ni hivyo hao watu hatari sana!”
“Ndiyo maana anawahitaji sana! Wakikubali kufanya kazi na sisi, tutamshukuru Mungu. Sasa hilo ni suala la kitengo kingine, sisi ktengo chetu tuendeleeni na huyu Chilo na Juma Hiza,” aliwaambia.
Historia ya Omar Al Fadhuu na Angelica vyote kwa pamoja vimeandikwa katika kitabu cha Dili la Dola Bilioni Nne kuanzia kuanzisha kundi la kigaidi mpaka alipokamatwa na CIA kwa msaada wa Robert, Richard na Robinson.
Hicho ndicho kipindi ambacho maofisa wa upelelezi walitumwa mpaka Nigeria na baadaye kutumwa kuelekea nchini Tanzania, walifanya upelelezi wao na kukutana na mwandishi Chilo ambaye aliwadanganya kuhusu Juma Hiza kitu kilichowafanya kuanza kumtafuta tena na yeye kwani tayari alionekana kufahamu mambo mengi kuhusu Juma.
Kama aliamua kuwadanganya kwamba alifariki dunia na walipokwenda kufukua kaburi hawakukutana na mwili wake, waliamini kabisa kila kitu kilichokuwa kimetokea kilipangwa, vijana hao walishirikiana kwenye hilo, hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanawapata na kuwahoji zaidi, ila mtu wa muhimu kuliko yeyote yule alikuwa huyo Juma Hiza.

Je, nini kitaendelea?
Kumbuka kitabu cha Dili la Dola Bilioni Nne kinaendelea kupatikana. Nicheki 0718069269.
 
NYEMO CHILONGANI
KALAMU YENYE SIRI YA DAMU
0718069269

Sehemu ya 08.

Chris na Jericho walikuwa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, hawakutakiwa kuondoka mpaka pale ambapo wangehakikisha Chilo ama Juma wamepatikana. Waliwasiliana na bosi wao, Peter na kumwambia kilichotokea na kitu pekee ambacho aliwasisitiza ni kuhakikisha vijana hao wanapatikana.
Hawakujua Juma alikuwa akitumia namba gani, ingekuwa ni rahisi kwao kuhakikisha wanampata na kuzungumza naye, wamchukue na hata kuondoka naye kuelekea huko Marekani kwa lengo la kuwaambia ni kwa namna gani aliyajua mambo hayo yote na kuyaandika kwenye kitabu chake.
Wakati wakifikiria hivyo ndipo wakakumbuka kuhusu akaunti yake ya Facebook. Walichokiamini ni kwamba Waafrika wengi walipenda kuweka mambo yao binafsi kwenye mitandao hivyo waliamini ili kuifahamu familia ya Juma kwa undani zaidi ilikuwa ni lazima waingie humo na kuangalia.
Hilo likafanyika haraka sana, wakazikuta picha nyingi alizokuwa ameziweka, wakagundua mwanaume huyo alikuwa na mtoto mmoja wa kike aliyeitwa kwa jina la Ilham, alikuwa kwa mama yake huko Moshi, Kilimanjaro.
Hilo likaonekana kuwasaidia sana, ilikuwa ni lazima kwenda huko na kuonana na mke wake, hawakutaka kusubiri jijini Dar es Salaam, wakachukua ndege na kuelekea huko.
Walipofika, wakadukua barua pepe yake ya Gmail kwa lengo la kupata mawasiliano yake yote yaliyokuwa humo kwani mara nyingi kwenye simu zenye mfumo wa Android hupenda kuhifadhi namba kwenye barua pepe zao, hivyo wakapata namba ya wazazi wake na mkewe.
Haraka sana wakawasiliana na mke wake na kuomba kuonana naye kwa kisingizio cha kuwa rafiki wa Juma aliyeitwa kwa jina la Chilo, na alifika kilimanjaro kwa lengo la kumuona mtoto wake, Ilham na wazazi wake.
Mkewe hakuwa na hofu, aliwahi kuzungumza na Chilo mara chache, hakuwa ameikariri sauti yake, kubwa zaidi mtu aliyempigia alizungumza Kiswahili safi kabisa kiasi cha kutokugundua kama alikuwa Mzungu.
Akamuelekeza na watu hao kufika katika Mtaa wa Old Moshi alipokuwa akiishi. Walipowaona, mkewe alishangaa, hakutegemea kuwaona Wazungu mahali hapo, aliambiwa alikuwa Chilo, sasa iweje watu waliofika mahali hapo wawe Wazungu?
Kidogo akawa na wasiwasi, hakujua kuhusu ishu ya kile kitabu kilichokuwa kimewekwa katika Mtandao wa Amazon na mbaya zaidi mpaka muda huo Juma hakumwambia kuhusu pesa alizokuwa ameziingiza kupitia kitabu hicho.
Alifanya hivyo kwa kuwa hakutaka kuonekana mwizi, ashindwe kuaminika, hakumshirikisha mkewe kwa lolote lile na ndiyo maana hakutaka kumwambia kitu chochote kile.
“Tunahitaji kuonana na Juma,” alisema Chris huku akimwangalia mke wa Juma aliyeitwa kwa jina la Halima.
“Nyie ni akina nani?” aliuliza mama yake.
“Marafiki zake!”
“Wazungu?” aliuliza. Watu hao wakatoa tabasamu.
Hawakuwa na jinsi, Juma hakuwa akitumia namba ya zamani, alibadilisha na kutumia namba mpya, hivyo haraka sana akapigiwa na Jericho kuhitaji kuongea naye, akapewa na kwenda pembeni.
Alichomwambia ni kwamba walikuwa na familia yake, walikuwa na uwezo wa kufanya lolote lile ambalo wangehitaji kulifanya kama tu asingekwenda Kilimanjaro na kuonana nao.
Juma alishtuka, hakuamini alichokuwa ameambiwa, ni kama alikuwa akiota. Kwa maneno madogo tu aliyokuwa akiambiwa na Chilo kuhusu hao maofisa wa CIA walionekana kuwa si watu wa kawaida, walikuwa katili pale ambapo walihitaji kufanya ukatili, walikuwa watu waliokuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile, hata walipoamua kuua, walifanya hivyo bila kupepesa macho.
Huko Dar es Salaam alipokuwa alibaki akitetemeka, alijificha maeneo ya Mwananyamala Komakoma, alipanga chumba kwa muda ili kuendelea kufanya mambo yake, alipopigiwa simu hiyo, moyo wake ukafa ganzi, akahisi kama kulikuwa na kitu kilichoufanya mwili wake kupooza kwa sekunde kadhaa.
Aliipenda familia yake, aliijali kuliko kitu chochote kile, kwake, alikuwa tayari kupoteza kitu chochote kile lakini si familia yake ambayo ilikuwa muhimu kuliko kitu chochote kile. Haraka sana akampigia simu Chilo kwa lengo la kuonana naye.
“Wameifikia familia yangu!” alisema Juma huku akionekana kuwa na hofu tele.
“Hutakiwi kuhofu kwa lolote lile, bado nina akili ya ziada kucheza na watu hawa,” alisema Chilo.
“Ninaogopa! Wanaweza kuimaliza familia yangu!” alisema Juma huku akionekana kuogopa.
“Hilo usijali! Hawawezi kuimaliza familia yako, wanakuhitaji sana, bila wewe, hawawezi kujibiwa maswali waliyokuwanayo,” alisema chilo.
“Kwa hiyo?”
“Nenda Kilimanjaro kama wanavyotaka!”
“Ila watanichukua!”
“Hutakiwi kuogopa. Juma nisikilize kwa makini. Tumekuwa mabilionea wakubwa wa siri, wewe kwenda Marekani kutatufanya kuwa mabilionea zaidi,” alisema Chilo.
“Kivipi?”
“Utajua kila kitu, usihofu kuhusu hilo. Huu mchezo wote niliuandikia script, na uzuri zaidi CIA wanatembea kwenye script ileile,” alisema Chilo.
“Unanichanganya!”
“Nenda Kilimanjaro kwanza, hakikisha unawaambia kila neno nililowahi kukwambia,” alisema Chilo.
Juma aliona kama anasalitiwa lakini hakutaka kuwa na wasiwasi, alimwamini Chilo zaidi ya mtu yeyote yule, alichokifanya ni kuchukua ndege siku iliyofuata na kuelekea mkoani Kilimanjaro.
Alipofika huko akaonana na familia yake, walikuwa wakilia, walichohisi ni kwamba alifanya kosa hivyo alikuwa akitafutwa. Hakuwaambia kuhusu kitabu hicho hicho, hawakuwa wakifahamu kitu chochote kile.
“Hao Wazungu ni akina nani?” aliuliza mama yake kwa sauti ya chini.
“Marafiki zangu!”
“Wamekujaje? Imekuwajekuwaje? Uliwapata wapi?” aliuliza maswali matatu mfululizo.
“Facebook!”
“Jamani hiyo Facebook imekuletea Wazungu, watakuua...” alisema mama yake huku akionekana kuwa na hofu nzito.
“Hamna! Kuna kitu tunataka tufanye, kitatuingizia pesa sana,” alisema Juma huku akitoa tabasamu pana, alifanya hivyo ili kumuondoa hofu mama yake.
“Sawa mwanangu!” alisema mama yake.
Baada ya kuzungumza naye kwa dakika kadhaa akamuita mke wake, Halima na kuanza kuzungumza naye. Mwanamke huyo alikuwa na hofu tele, kile alichokuwa akikiona hakutaka kuamini, alihisi kulikuwa na tatizo kubwa hivyo alihitaji kujua kwa undani zaidi.
“Umefanya nini?” alimuuliza.
“Na wewe pia una hofu?”
“Sana! Hawa Wazungu ni akina nani?” aliuliza.
“Ni washikaji zangu, nilikuwa nawasiliana nao, kuna dili la kuandika muvi, wamenichagua bwana!” alisema Juma huku akicheka.
“Unanidanganya!”
“Ili iweje mke wangu? Siwezi!” alimwambia.
Alimuondoa hofu aliyokuwanayo, alimwambia kuhusu mpango wa kwenda kuandika filamu nchini Marekani. Mwanamke huyo hakumwamini lakini kwa sababu alitoa tabasamu pana, hakuwa na jinsi, akamuamini mume wake kwa asilimia mia moja.
“Kuna jingine!” alisema Juma.
“lipi?”
“Mtafute Chilo! Kuna kitu atakupa! Nimeshindwa kuja nacho!” alimwambia.
“Kitu gani?”
“Wewe mtafute tu! Namba zake hizi hapa,” alisema Juma huku akimwandikia namba za mwanaume huyo, baadaye wakaondoka zao.
Jericho akawasiliana na Peter na kumwambia walifanikiwa kumpata Juma Hiza na walikuwa wakifanya kila liwezekanalo kuhakikisha mwanaume huyo anafikishwa nchini Marekani haraka sana.
Peter alifurahi, hakuamini kama jambo hilo lilikuwa jepesi namna hiyo, akajiona mshindi, alifurahi mno, wakati mwingine aliwaangalia wafanyakazi wenzake na kugongesheana mikono kwani kwa kumpata Juma ilimaanisha kungekuwa na vitu vingi ambavyo wangevifahamu na zuri zaidi ni kuwa walimpata wao kabla ya Waarabu ama Warusi ambao waliamini nao ilikuwa ni lazima kumtafuta mtu huyo.
Siku iliyofuata Juma akapandishwa ndani ya ndege na kuanza kuelekea nchini Marekani. Njiani alikuwa na mawazo mengi, kitu kilichokuwa kikimsumbua ni Chilo tu, kwa nini alimwambia aende Kilimanjaro kuonana na wanaume hao, wamchukue na kuelekea naye nchini Marekani?
Aliamini aligeukwa na inawezekana Chilo alifanya hivyo ili pesa zote alizokuwa ameingiza azitumie, yaani pesa zilimfanya kusalitiwa, zilimfanya kuonekana mjinga, hapo akamuona Chilo kutokuwa rafiki tena, alikuwa msaliti kama Yuda tu alivyomsaliti Yesu Kristo.
“Pesa....pesa....pesa.....!” alisema Juma huku akiwa amejiinamia, moyo wake ulikuwa na majonzi mazito.

Je, nini kitaendelea?

Vitabu vya Dili la Dola Bilioni Nne vinaendelea kupatikana kwa 0718069269.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom