Kakobe, Tanesco Wazichapa Live

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,870
155,829
MTAFARUKU mkubwa ulizuka jana kati ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) baada ya walokole wa kanisa hilo kudaiwa kuvamia na kuwapiga wafanyakazi wa Kampuni ya TAKAOKA kutoka Japan na kujeruhi baadhi yao.
Wakati TANESCO wakidai walokole hao waliwapiga wafanyakazi hao wa Kijapani ambao baadhi yao walilazwa hospitali, waandishi wa habari waliokuwapo na Askofu wa kanisa hilo, Zachary Kakobe walikanusha kipigo hicho.
Meneja Uhusiano wa TANESCO, Badra Masoud, aliliambia Tanzania Daima kuwa tukio hilo lilitokea mita chache kabla ya wafanyakazi hao kufika kwenye kanisa hilo ambako kulikuwa na waumini zaidi ya 200 waliokuwa wametanda.
“Ni kweli mafundi wa Kampuni ya TAKAOKA walikwenda eneo hilo kwa ajili ya kusafisha eneo la kuweka nyaya, lakini kabla ya kuanza zoezi lao walivamiwa na kundi la waumini wa kanisa hilo ambao walihisi kuwa wanataka kuanza kazi ya kutandaza nyaya…wakaanza kuwapiga na kuwarushia kila kilichokuwa mbele yao.
“Bahati nzuri wale mafundi walikuwa wamevaa kofia maalumu za kulinda kichwa (helmet) ambazo ziliwasaidia kupata matatizo zaidi,” alisema.
Alisema katika vurumai hiyo, wafanyakazi watatu walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Palestina iliyoko Sinza kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Wafanyakazi wetu walipigwa kwa nondo, lakini bahati nzuri polisi wakiwa na magari matano walifika kwenye eneo la tukio kutuliza hali hiyo,” alisema Masoud.
Alisema kutokana na tukio, wafanyakazi hao waliamua kwenda kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi Mabatini kilichoko Mwananyamala.
Hata hivyo, Kakobe aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya wafanyakazi wa TANESCO kufika katika eneo hilo, waumini wake waliwatimua ili kuzuia upitishaji wa nyaya hizo.
TANESCO inapanga kupitisha nyaya za umeme wa kilovolti 132 katika eneo hilo.
Kakobe alisema waumini wa kanisa hilo wamechukizwa na hatua hiyo ya serikali kwa kuwa wameshachanga sh milioni 800 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha Televisheni ya Holiness ambacho wanadai kimeota mbawa kutokana na upitishwaji wa nyaya hizo.
“Ni kweli waumini waliwatimua, lakini hawakuwa na silaha zozote za kuwapiga wafanyakazi hao…sasa nashangaa kusikia kuna watu eti wamepigwa,” alisema Askofu Kakobe.
Alisema kilichotokea ni wafanyakazi hao kuingia ndani ya gari lao lenye namba za usajili T 346 ARR na kisha kuondoka katika eneo hilo baada ya kusikia ving’ora vya magari ya polisi yaliyosheheni askari kwa ajili ya kukabiliana na hali yoyote ya vurugu kama ingetokea.
Askari hao walifika katika eneo hilo na kisha baadhi yao kuelekea ndani ya ofisi za Askofu Kakobe ili kupata maelekezo kuhusiana na mgogoro huo.
Mnamo saa tano asubuhi, wafanyakazi hao walifika eneo hilo wakiwa kwenye gari maalum kwa ajili ya kupakia na kushusha vitu vizito. Waumini walihisi kuwa limepelekwa pale kwa ajili ya kuchomeka nguzo kubwa za umeme.
Wakati wafanyakazi wakiendelea na kazi ya kushusha nguzo hizo, waumini walianza kupigiana simu na kutaarifiana kuhusu tukio hilo. Ghafla waumini kwa mamia walimiminika katika eneo hilo na kusababisha vurugu kubwa kati yao na wafanyakazi wa kampuni hiyo ya TAKAOKA.
Muda mfupi baadaye magari ya polisi yaliwasili katika eneo hilo huku yakipiga ving’ora, hali iliyosababisha wafanyakazi hao kuamua kupakia nguzo zao na kisha kutoweka.
Askofu Kakobe alisema askari hao waliingia ndani ya ofisi za kanisa hilo ili kupata ufafanuzi wa hali iliyokuwa ikiendelea katika eneo hilo bila ya kukamata hata muumini mmoja.
“Tuliwapa polisi maelezo kuhusu hali ya mambo iliyokuwa ikiendelea hapa,” alisema Askofu Kakobe.
Hata hivyo, waandishi wa habari waliokuwa eneo hilo, walisema hawakuona tukio lolote la watu kupigwa.
Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hadi jana jioni ofisi yake haikuwa na taarifa yoyote kuhusiana na vurugu hizo. Alimtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na mtu aliyemtaja kwa jina la Masinde aliyeko katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kwa ajili ya ufafanuzi zaidi wa tukio hilo, lakini simu yake ya kiganjani iliita bila kupokewa.
 
Mathayo 5:39-40; Lakini mimi nawaambia, mshishindane kwa uovu. Mtu akupigae shavu la kuume, mgeuzie na la kushoto; na mtu atakaye kushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia!!
 
Back
Top Bottom