Kahangwa alipokerwa na uchafu wa jiji | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kahangwa alipokerwa na uchafu wa jiji

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Charuka, Oct 24, 2009.

 1. C

  Charuka Member

  #1
  Oct 24, 2009
  Joined: Oct 20, 2009
  Messages: 56
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Kabla ya kutimkia huko yanakobebwa maboksi, huyu Bwana aliliachia taifa maneno haya;
  WITO KWA WANANCHI KUHUSU KUKABILIANA NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA, HUSUSAN AIBU YA UCHAFU

  02 AGOSTI, 2009

  UTANGULIZI
  Tumekuwa tukitafakari kwa muda mrefu sasa kuhusu suala la utunzaji wa mazingira na usafi hapa nchini na kwingineko duniani. Tumegundua kwamba taifa letu lipo hatarini kutokana na uharibifu wa mazingira, na kukithiri kwa uchafu hususan mijini.

  Kama tunavyoelewa, Utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa uhai na afya ya jamii. Wataalam katika tafiti zao mbalimbali wamethibitisha kuwa gharama zitumikazo katika utunzaji wa mazingira huokoa maisha ya wanadamu na viumbe vingine. Tena utunzaji wa mazingira ni hatua inyoweza kuhesabika kuwa kinga au tahadhari muhafaka kiafya. Tukichukulia mfano wa matokeo ya utafiti uliofanywa na shirika la Water Aid (la Uingereza) kwamba shilingi moja ikitumika katika kutunza mazingira/kuhakikisha uwepo wa usafi, inaokoa shilingi tisa ambazo zingetumika katika matibabu ya magonjwa mbalimbali, hususan yatokanayo na hewa chafu, maji machafu na taka zinazozagaa.

  Suala la usafi na utunzaji wa mazingira ni miongoni mwa ajenda nyeti duniani, likiwa ni mojawapo ya changamoto zinazoukabili ulimwengu kwa sasa. Tumesikia mara nyingi juu ya ongezeko la joto duniani, upungufu wa hewa safi na maji safi, na kadhalika. Ni jambo la kutia matumaini kwamba zipo jitihada za kimataifa za kukabiliana na changamoto hii, ili kudumisha ustawi wa mwanadamu hapa duniani kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

  UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA UCHAFU KATIKA TAIFA LETU
  Wakati mataifa ya wenzetu yakifanya kila linalowezekana dhidi ya changamoto hii, hivi leo, sisi watanzania katika nchi yetu, tumekuwa wachafu kupindukia na waharibifu wa mazingira katika namna isiyo ya kibinadamu kabisa.
  Mifano ya haya si ya kutafuta;
  Sote ni mashahidi wa mlundikano mkubwa wa takataka katika masoko barabara za hapa nchini. Zipo habari kuwa baadhi ya watu wamefikia kujisaidia katika mifuko ya plastiki kwa sababu ya kukosa vyoo wanapo kuwa masokoni (matharani soko la Ilala). Kadhalika siku hizi mtu kula muwa au kitu kingine chochote na kurusha mabaki ovyo tu barabarani/njiani.
  Kana kwamba haitoshi, imekuwa ni tabia ya kawaida kwa baadhi ya wananchi kutapakaza vinyesi barabarani, almaarufu ‘kutapisha chemba’ pindi mvua zinaponyesha. Hili linaendelea bila watanzania kuonekana kujali na viongozi wetu katika ngazi zote kutolikemea.

  Aidha, miji ya Tanzania imekithiri kwa ujenzi holela, yaani usiofuata mipango miji wala viwango, kiasi kwamba mitaa haipitiki na mfumo wa usafishaji mitaa hiyo unakuwa mgumu kabisa.
  Kadhalika kana kwamba hatujaelewa, watanzania tumeendela na matumizi ya mifuko ya plastiki, licha ya kuambiwa madhara ya mifuko hiyo, tunauziana michicha inayoooteshwa kando ya barabara bila kujali kwamba michicha hiyo ni myepesi kunyonya madini ya Lead yasababishayo kansa. Haishangazi kwamba wagonjwa wa kansa wameongezeka nchini.
  Matatizo haya yakujumlisha na uwepo wa kelele za bar katika maeneo ya makazi ya watu, uwepo wa karakana ‘Gereji-bubu’ katika makazi ya watu, uvuvi haramu, uchomaji misitu na mbuga, uharibifu wa vyanzo vya maji, kutapakazwa ovyo kwa sumu za viwandani na migodini, yanaifanya nchi yetu isiwe mahali bora pa kuishi.

  Ndugu wananchi, leo hii jiji la Dar es Salaam linapigiwa mfano wa majiji yanayongoza kwa uchafu duniani. Kwa mujibu wa Takwimu za mwaka jana (2008), Dar es salaam ni jiji la 12 kwa uchafu duniani (mwaka huu 2009, ni la 10), na la tatu Afrika Mashariki na kati. Na wala halisingiziwi, sijui tunaweza kukanushaje sifa hii katikati ya uwepo wa harufu mbaya ya Ocean Road, na milipuko ya mara kwa mara ya gonjwa la kipindupindu katika mitaa ya jiji. Katika karne ya 21, ni aibu kubwa kwa mji kama Dar es Salaam kukithiri kwa uchafu namna hii .

  Kwa ujumla katika maeneo ya miji, takataka zinazotoka katika viwada zina metali kama vile zebaki (Mercury), Chromium, lead, Cadmium, chumvi ya cyanide, nitrite na natrate, organic matter, na sumu za kemikali zinazotokana na bidhaa zinazotengenezwa na viwanda hivi, zinaenda moja kwa moja katika vyanzo vya maji. Tatizo hili liko katika maeneo mbalimbali ya nchi, ilikwa ni pamoja na; Tukuyu, Korogwe, Chunya, Singida, Arusha, Tanga, Dar es Salaam, mto Msimbazi, mto Ngerengere Morogoro, Themi Arusha, ziwa Victoria, mto Karanga, Njoro, Rau- Moshi na mto Kiwira ( Wilaya ya Tukuyu)

  Vilevile takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni nchi ya 4 Afrika katika ukataji miti, hukata zaidi ya hekta 500,000 kwa mwaka. Zaidi 60%ya ardhi ya Tanzania inakabiliwa na hatari ya kuwa jangwa.


  Hapo ndipo tulipo kwa nchi ambayo, wakati wa Serikali ya awamu ya tatu, tulipewa heshima ya kuongoza dunia katika suala la utunzaji mazingira, pale Mhe. Arcado Mtagazwa, aliyekuwa waziri katika ofisi ya makamu wa rais inayoshughulikia mazingira alipopewa dhamana na ulimwengu kuwa rais wa baraza la mazingira duniani.

  Tanzania ni chafu isivyomithirika, licha katiba ya nchi kuzingatia haki za watu kuishi, na licha ya kuwepo kwa sheria mbali mbali za kudhibiti uharibifu wa mazingira.
  Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania katika ibara ya 14 inatamka jambo ambalo undani wake una uhusiano na suala la usafi na usalama wa mazingira. Katiba inatambua haki ya mtu kuishi, haki hii inafungamanisha hifadhi yak maisha yak mtu, haki ya kuishi katika mazingira safi na salama, katika nyumba bora, kupata huduma bora za afya, kuishi katika makazi yenye heshima (sio kwenye nyumba za maboksi na uchafu) ni wajibu wa serikali kuhakikisha upatiukanaji wa haki hii.
  Matharani, hata serikali inapobomoa nyumba za watu, jukumu lake la maana halipaswi kuwa kuwalipa fidia bali kujenga nyumba mbadala, katika eneo mbadala la kuishi. Serikali inatakiwa kujenga nyumba za kisasa za kuishi, lakini badala ya serikali kufanya hivyo imewaachia watu binafsi kujenga na kuendesha kwa ufisadi nyumba za kupanga mijini hata kwa ajili ya watumishi wa umma. Wakati tunayo sheria yak sheria ya pango (the rent restriction act of 1971) inayokataza kuchukua kodi ya nyumba kabla yak mpangaji kukaa katika nyumba kwa kipindi husika, imekuwa kana kwamba sheria hiyo haipo na serikali iko likizo wakati wenye nyumba binafsi wakiendelea kuwatoza kodi kwa miezi 6 hadi mwaka mzima kabla kwakipindi ambacho mpangaji hajakaa katika nyumba.
  Tunasema hivi, licha ya kwamba nyumba nyingi mijini hazina hadhi ya kulinda haki ya mtu kuishi katika mazingira safi na salama, si halali kisheria kwa wenye nyumba kutoza kodi kwa kipindi cha zaidi yak mwezi mmoja kwa mara moja tena kabla yak mpangaji hajakaa kwenye nyumba.

  Vile vile haki ya kuishi inabeba ndani yake suala zima la afya. Kwa maana hiyo kila mtu ana haki ya kulindwa afya yake.
  Wakati wa serikali ya awamu ya kwanza, serikali ilikuwa na sera ya afya iliyokuwa na mtazamo wa preventive medicine (kinga dhidi ya magonjwa). Chini ya sera hiyo serikali iliwajibika kuweka mazingira mazingira anamoishi mtu kuwa katika hali ya usafi na usalama. Enzi za mwalimu mabwana afya na wasaidizi wao walipita mitaani wakifukiza madawa kwenye madimbi ili kuharibu mazalia ya wadudu wasababishao magonjwa, hususan mbu. Zoezi hili lilifanyika kila wiki kwa sababu za kitaalam kwamba kuzaliana kwa mbu huchukua takribani siku saba.
  Bahati mbaya serikali ya sasa haina habari na wajibu huo. Badala yake imegeukia sera au mtazamo wa curative medicine (tiba tu dhidi yak magonjwa) mtazamo ambao ni aghali sana, na mara nyingi hauna matunda mazuri. Vile vile mtazamo huu umetoa fursa kwa mafisadi kuchezea maisha ya watu, kwa kuingiza nchini madawa yaliyo chini ya viwango, ndio maana leo hii kila uchao tuaambiwa dawa hii na hii hazifai tena katika matibabu ya malaria n.k. yamkini viongozi wan chi hawajali maana wanajua kutibiwa kwao ni nchi za nje.
  Suala la mzingira na haki ya kuishi linaathiriwa kwa kiasi kikubwa na sera ya uwekezaji. Sera hii kwa jinsi inavyotekelezwa na serikali ya CCM, haizingatii usafi na usalama wa mazingira. CCM inaruhusu uwekezaji katika miradi chafuzi yak mazingira, inayozalisha taka mbali mbali za sumu. Matharani Uwekezaji katika Asbestos uliokataliwa katika bara la Ulaya hapa Tanzania unakumbatiwa; Kampuni yak Barrick Gold ambayo haizingatii viwango vilivyowekwa kimataifa vinavyokubaliwa na World health Organization, kwa mfano inapotumia Zebaki kusafisha dhahabu na kutililisha mabaki yake katika mito, imefanya uharibifu katika nchi nyingi, nasi ilihali tukijua hilo tumeipokea nchini.
  Migodi mingi nchini yenye uwekezaji wa kigeni, licha ya kwamba taifa halipati faida ya maana kutokana na migodi hiyo, migodi hii haizingatii kanuni za kutunza usalama na usafi wa mazingira.
  Yamesemwa mengi kuhusu jinsi uwekezaji katika migodi ulivyoleta madhara kwa wananchi kiafya, cha kushangaza badala ya serikali kutafuta ufumbuzi ilikimbilia kukanusha yanayosemwa. Hatuelewi kwa nini serikali ihamue kuchukua hatua ambazo zinausaliti umma kwa kiasi hicho.

  Japo sheria za mazingira na usafi zipo, serikali imeshindwa kuzitekeleza. Tatizo jingine ni kwamba japo sheria ya mazingira inazungumzia kufanyika tathmini ya madhara ya miradi kwenye mazingira, sheria hiyo haitoi fursa ya kufanyika kwa tathmini kwa njia huru/independent assessment, matharani inayoweza kufanya na asasi za kiraia

  Sheria na sera tulizo nazo nchini kuhusu usafi na usalama wa mazingira, ni pamoja na; National Environmental Action Plan ( NEAP - 1994), National Environmental Policy (NEP- 1997), National Action Plan ( 1999/2004, Sheria ya machimbo ya mwaka 1998, Sheria ya mazingira ( Environmental Management Act 2004 ( EMA 2004), iliyoambatana na mkakati wa ukombozi wa mazingira wa mwaka 2004.
  Ni dhahiri sheria hizo hazifuatwi na yamkini hazifahamiki miongoni mwa Watanzania walio wengi

  Serikali kuu badala ya kuchukua hatua, inabaki kulalamika kuwa kuna uhaba mkubwa wa watendaji na vitendea kazi, uhaba mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya, ujenzi holela usiozigatia mipango miji, biashara holela, ongezeko la watu mjini.

  Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya, tunaambiwa kuna maafisa afya na wasaidizi wao ambao hufanya kazi za ukaguzi wa mazingira katika Halmashauri za jiji, manispaa, miji, wilaya, kata na vijiji na wanapobaini chukizo huchukua hatua kwa kutumia sheria za afya. Katika Serikali za mitaa/vijiji kamati za afya zinapaswa hushiriki kupanga na kusimamia mipango ya usafi wa mazingira, kuelimisha jamii na kuandaa sheria ndogo ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Bahati mbaya haya hayafanyiki hata kidogo.

  Suala la uchafu mijini lina hata harufu ya ufisadi, matharani hapa Dar es Salaaam, kuna habari kuwa Kampuni ya MJENT(mali ya Mhe. Kingunge), imeiondoa kinyemela Kampuni ya SINCLON, iliyokuwa na tenda ya kuzoa taka. Sinclon imekwenda Mahakamani kuweka pingamizi dhidi ya hatua hiyo. Hii ni sababu mojawapo ya kufurika kwa taka katika maeneo ya jiji.


  NINI KIFANYIKE KWA SASA
  ninatoa wito kwamba yafuatayo yafanyike mara moja;
  • Watanzania wote tuchukue kila aina ya tahadhari ya kutuhepusha na madhara ya uchafu. Tunawaomba wananchi waongeze biidi katika kushiriki kikamilifu kutunza usafi wa maeneo wayoishi.

  • Serikali iwajibike moja kwa moja kutunza mzingira katika kila mtaa kupitia mtazamo wa awali wa Kinga kuliko tiba

  • Serikali itoe ushirikiano wa kutosha kwa taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wanaharakati, katika zoezi zima la kuhifadhi mazingira.

  · Serikali itoe elimu ya Sheria za mazingira hadi ngazi za vijiji na vitongoji kwa wananchi na kuhakikisha sheria hizi zinafundishwa hata mashuleni kuanzia shule za msingi

  • Baraza la Mazingira la Taifa NEMC lichukue hatua thabiti za nguvu kukomesha balaa la uharibifu japo kwa kutumia sheria zilizopo.

  • Halmashauri za miji/serikali za mitaa zitumie ipasavyo sheria ndogo ndogo za kudhibiti vitendo vya uchafu, zinunue magari ya kutosha na kisasa ya kubebea taka, ziwapatie watendaji vitendea kazi bora ili kuleta ufanisi wa kazi na kuepuka magonjwa ya kuambukizwa, zihakikishe uwepo wa mapipa ya kuhifadhia taka katika vituo vya mabasi na maeneo ya hadhara.

  Mungu ibariki Tanzania!
  Ahsanteni kwa kutusikiliza,

   
 2. Waridi

  Waridi JF-Expert Member

  #2
  Oct 24, 2009
  Joined: Mar 30, 2008
  Messages: 1,027
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 135
  du! Mitaa yenyewe kama naiona vile. Ngoja tusikie kama katika chaguzi za serikali za mitaa itakuwa mojawapo ya agenda za kampeni
   
 3. WomanOfSubstance

  WomanOfSubstance JF-Expert Member

  #3
  Oct 24, 2009
  Joined: May 30, 2008
  Messages: 5,465
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 0
  usafi ni hulka, Kuna watu hata wasome vipi, hata waende kwenye ustaarabu ni vigumu ku adapt.Utamwona mtu mtanashati, nenda kwake utashangaa anapolala, jikoni, maliwatoni achilia mbali mazingira yake.Huyu hata akikupa maji ya kunywa hutakunywa.Pata picha kuwa ndio anapewa madaraka ya mipango miji, nakadhalika... unategemea nini?
  Watu kama hawa wala hawaoni kuna tatizo.... haoni uchafu wa miji wala nini... wao mradi kumekuchwa ni poa tu.
   
 4. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #4
  Oct 24, 2009
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  usafi unaanza at individual level at infancy stage ili tuwe wasafi tuanza lei kuwafundisha watoto kuwa kutoweka kitu mahali pasipotakiwa ndio defination ya uchafu. That is kila kitu kiwe na sehemu yake, na sisi watu wazima tukumbuke hilo. halafu at institutional level manispaa zitekeleze wajibu wake wana by laws nyingi za kufanya miji iwe misafi lakini hawazitumii kwani hazina maslahi kwao.
   
 5. C

  Charuka Member

  #5
  Oct 24, 2009
  Joined: Oct 20, 2009
  Messages: 56
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  kama unaelekeza jukumu hili kwa wazazi, ndio hao hao walioshindwa kuwa wasafi, watawafundishaje watoto wao?
  kama unalielekeza kwa walimu, ndio hao hao tumewanyima morali wa kufanya kazi zao ipasavyo.
  Mi bado narudi kule kule, intervention ya serikali ni lazima, maana wao ndio viongozi wa jamii ati. Sheria zipo wazisimamie, wizara husika zipo zifanye kazi yake, n.k
   
Loading...