JWTZ yazima jaribio la utekaji wa meli; Maharamia saba wakamatwa, sasa wahojiwa polisi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,781
[h=3][/h]

*Risasi zarindima mashariki mwa Kisiwa cha Mafia
*Maharamia saba wakamatwa, sasa wahojiwa polisi


Na Edmund Mihale

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linawashikilia watu saba kwa tuhuma za
kufanya uharamia katika umbali wa kilometa 40 Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Mafia katika Bahari ya Hindi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari Dar es Slaam jana, ilieleza kuwa watu hao walikamatwa baada ya kuvamia Meli ya Utafiti wa Mafuta ya Sams Allgood juzi saa mbili usiku.

Baada ya kuvamiwa meli hiyo ilitoa wito kwa nyingine kwa nia ya kuomba msaada na kuashirika kuwa kuna hatari, na hivyo meli ya Monck na Froshiber ambazo zipo kwenye eneo hilo zilisikia kilio cha mwenzao na kujipanga kutoa msaada.

"Kwa kuwa meli hizo zinalindwa na vikundi kutoka JWTZ askari walipo kwenye meli iitwayo Froshiber walijipanga kivita na kuisogelea meli hiyo baada ya kuwasiliana kwa redio na meli ya Sams Allgood," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Askari hao walipofika katika eneo hilo waliwasha taa kuimulika meli hiyo na kuwaona watu wakitembea melini, ndipo walipiga risasi hewani kuwataka kujisalimishe, badala yake walianza kuwarushia risasi askari hao.

Kutokana na kitendo hicho, askari hao walijibu mapigo kwa kutumia risasi za moto.

Alieleza kuwa meli nyingine iitwayo Monk iliwasili katika eneo hilo nayo ikiwa na Askari wa JWTZ waliotoa msaada wa kukabilina na watu hao.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hali ilitulia na askari wa JWTZ kwa kutumia kipaza sauti na kuwatangazia watekaji nyara hao kujisalimisha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo ilichukua takribani saa mbili hadi wapoamua kujisaliamisha kwa kutupa silaha baharini na kuinua mikono juu.

Ilieleza kuwa baadhi ya askari hao walipanda katika meli hiyo na kuwaweka chini ya ulinzi kwa kuwafunga na kamba na hatimaye kuikagua meli nzima.

Mmoja wa maharamia hao aliyekuwa ameumizwa katika paja la kulia wakati wamajibizano ya risasi, alipatiwa huduma ya kwanza na wote wakahamishiwa katika Meli ya Froshiber.

Taarifa hiyo ilieleza askari waliokuwa katika opresheni hiyo wote ni salama na Meli ya JWTZ iliondoka Kigamboni jana kwenda katika Kisiwa cha Mafia kuwachukuwa watu hao kwa ajili ya kuwafikisha mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa mahojiano.

Mazoezi ya kijeshi

Wakatu huo huo, Mwandishi Wetu Anneth Kagenda anaripoti kuwa kuna umuhimu mkubwa wa nchi wanachama za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutenga rasilimali za kutosha ili kukabiliana na wimbi la maharamia wa majini kwa kuimarisha ulinzi.

Meja Jenerali wa Jeshi la Nchi Kavu kutoka nchini Afrika Kusini, Karl Wieswer aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya zoezi la kupambana na maharamia majini.

Alisema zoezi hilo limetokana na makubaliano yaliyofikiwa na nchi hizo ili kuhakikisha masuala ya ulinzi yanasimamiwa vyema hasa katika upande wa ardhi na maji.

“Hili ni zoezi la kwanza kufanywa na nchi zote za SADC hivyo nchi hizi zinapaswa kushirikiana vizuri na kutenga rasilimali za kutosha kwani kuna vikosi vya wazamiaji ambavyo vitakuwa vikizama majini.

“Ikumbukwe kuwa raslimali maji ni muhimu katika nchi hizi, zipo rasilimali nyingine ila maji ni muhimu zaidi, nchi za SADC zinapaswa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto walizonazo ikiwemo ya uharamia,” alisema.

Aliongeza kuwa, suala la uharamia majini ni tatizo kubwa hivyo ni muhimu nchi husika zikashirikiana ili kuondokana na tatizo hilo.

Meja Jenerali Wieswer alisema upande wa Tanzania ili iweze kupata mafanikio inapaswa kuonesha ushirikiano kwa nchi zingine, kufanya kazi kwa bidii kuwa na raslimali za kutosha na SADC kuwa na fedha za uwekezaji katika viwanda.

“Baadhi ya nchi zimeonekana kuwa na raslimali za kutosha hivyo nawaomba kuzitumia vizuri rasilimali zilizipo ili kuleta maendeleo ya wananchi,” alisema.
 
0 Reactions
Reply
Top Bottom