Juzi Bunge liliwachagua wabunge tisa watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Juzi Bunge liliwachagua wabunge tisa watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Apr 20, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Apr 20, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Juzi Bunge liliwachagua wabunge tisa watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, wagombea hao pia walipata fursa ya kujieleza na kuulizwa maswali.
  Kwa kuwa lugha rasmi ya Bunge la Afrika Mashariki ni Kiingereza, wagombea walitakiwa kujieleza, kuomba kura na kujibu maswali kwa lugha hiyo.
  Wapo waliofanya vizuri sana na wapo waliotokwa na kijasho chembamba kutokana na kile kinachodhaniwa kuwa ni kikwazo cha lugha.
  Hata hivyo, kwa ujumla wagombea walijieleza vizuri na tunaungana na matokeo yaliyotangazwa kwamba waliochaguliwa ni kweli wanastahili kwa kuwa walionyesha umahiri mkubwa wa kujieleza pamoja na kuyajua mambo kwa mapana yake.

  Wabunge hawa sasa wataungana na wenzao kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi kuunda chombo cha kutunga sheria na kupitisha bajeti ya Jumuiya. Wataiwakilisha nchi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.

  Tunachukua fursa hii kuwapongeza wote waliochaguliwa kwamba wamechakuliwa miongoni mwa kundi la wengi wenye sifa na kwa maana hiyo wana wajibu wa kuthibitisha kwa vitendo halisi kwamba wabunge hawakukosea kuwachagua.
  Pamoja na pongezi hizi, ni vema tukaweka wazi pia rai na angalizo letu. Kabla ya kazi ya kujieleza na kuomba kura haijaanza, zilizuka hoja za lugha ya kutumika.
  Hoja hii haikuwa ya bahati mbaya. Ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya Kiingereza kwa Watanzania wengi ni ya kiwango cha chini.
  Tanzania ni nyumbani kwa lugha ya Kiswahili, ndiyo lugha ya taifa na kwa kweli ndiyo inatumika kuendesha mambo yetu mengi, iwe mahakamani, bungeni na hata ndani ya ofisi za serikali.
  Ni kweli pia kuwa Kiingereza ni lugha rasmi pia nchini. Ndiyo maana bado inatumika katika uendeshaji wa serikali, utungaji wa sheria zetu bado unatumia lugha hiyo na kwa ujumla ni vigumu kukiweka pembeni Kiingereza katika mazingira ya mahusiano ya sasa ya kidunia.
  Kiingereza ni Kiswahili cha dunia.
  Kutokana na umuhimu wa Kiingereza ndiyo maana hoja ya kutaka wagombea wajieleze kwa lugha hiyo iliwekewa msisitizo kwa kuwa hata shughuli za Jumuiya hiyo ndiyo lugha rasmi.
  Tunajua kuna mjadala na maoni tofauti juu ya umuhimu wa lugha ya Kiswahili kuwa iwe ndiyo lugha rasmi ya kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu. Kwa mantiki ya hoja hii, hata ndani ya Bunge la Afrika Mashariki hoja hii bado inapigiwa chapuo.
  Tunasema kwa kauli ya dhati kabisa kuwa kuna kila sababu ya kupiga kampeni kwa ajili ya kukikuza, kukienzi na kukitumia Kiswahili kadri iwezekanavyo, si ndani ya Tanzania na kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki tu, bali barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.
  Hata hivyo, si vema kukikuza Kiswahili kwa njia ya kukibeza Kiingereza kwa sababu mbali ya ukweli kuwa hii ni lugha kubwa duniani na ambayo inatumika ulimwenguni kote, bado ni muhimu kwa ajili ya ustawi wetu kama taifa na kama sehemu ya jumuiya kimataifa.
  Pengine ni kwa sababu hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, alitoa angalizo muhimu wakati wa mjadala wa ni utaratibu upi ungestahili kutumiwa na wagombea.
  Alisema ni vema muda wa kujieleza upunguzwe kutoka dakika tano hadi tatu ili kupata muda wa kuwauliza wagombea wote kila mmoja maswali matatu kwa nia ya kuwapima.
  Naibu Waziri huyo alisema kuwa kumekuwa na tabia ya watu kuomba nafasi hiyo, hufika mbele ya Bunge wakiwa wamejiandaa kwa kukariri mambo, lakini kwa kweli wamekuwa ni mzigo mkubwa kwa taifa kwa sababu hawashiriki katika mijadala ya Bunge la Afrika Mashariki.

  Naibu Waziri huyo ambaye alipata kuwa mbunge wa Bunge hilo kabla ya mwaka 2005, alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa baadhi ya wabunge hao hujificha chini ya meza wakati mijadala mikali ikiendelea ndani vikao vya Bunge la Afrika Mashariki.

  Maana ya kauli hii ni kwamba uwakilishi wao unakosa nguvu hivyo kutokuitendea haki nchi ambayo imewatuma kuiwakilisha.

  Tunajua ndani ya Bunge hili ndiko zinaibuka sheria zinazohusu uendeshaji wa Jumuiya, kwa hali hiyo ni matarajio yetu kuwa hawa wabunge waliochaguliwa safari hii watakuwa wawakilishi mahiri na makini katika kuitetea nchi, kadhalika tunaamini wanakwenda kama kundi moja la wawakilishi wa Tanzania na si wa vyama vya siasa kwa ajili ya kuiwezesha nchi hii inufaike zaidi na Jumuiya hii. Ni kwa sababu ya kazi hii adhimu tunawatakia kila la kheri wabunge wa Afrika Mashariki.

  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...