Jumuiya ya Afrika Mashariki yatii agizo la Magufuli kubana matumizi

Bilionea Asigwa

JF-Expert Member
Sep 21, 2011
16,515
28,487
Magu.jpg


Staili ya Rais John Magufuli ya kubana matumizi nchini sasa imepanua wigo baada Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuanza kutekeleza agizo lake kwa kupunguza matumizi.

Sekretarieti hiyo imepunguza matumizi ya uendeshaji katika idadi ya wajumbe wanaogharimiwa na Jumuiya, idadi ya vikao na gharama nyingine.
Wakati bajeti ya EAC kwa mwaka ujao ikipunguzwa, wajumbe wa sekretarieti hiyo wametakiwa kutumia zaidi mawasiliano ya mtandao ya video kuendesha mikutano na vikao vyao ili kuokoa fedha ambazo zingetumika kuwasafirisha maofisa wa Serikali kutoka nchi wanachama.

Miezi miwili iliyopita, Rais Magufuli ambaye sasa ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alisema uongozi wake utajikita zaidi katika kubana matumizi na kuwaagiza watendaji wakuu kuangalia namna ya kupunguza gharama za uendeshaji, huku akiwakumbusha kuwa nchi wanachama zina wananchi maskini wa kipato.

Aliwataka kutazama upya gharama za vikao vyao, usafiri, pamoja na posho wanazolipwa wanaohudhuria mikutano, sambamba na zile za kuwatumia washauri waelekezi kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na jumuiya.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk Liberat Mfumukeko alitangaza utekelezaji huo na kubainisha kuwa wataalamu wasiozidi wawili kutoka kila nchi ndio watagharamiwa na jumuiya hiyo wakati wowote watakapotakiwa kuhudhuria mkutano wa kitaalamu baina ya nchi wanachama.

Idadi hiyo pia haitazidi watumishi watatu wa sekretarieti na mikutano haitapaswa kuendeshwa kwa zaidi ya siku nne kama moja ya kanuni za uendeshwaji wa EAC zinavyodai.

Akionyesha kuunga mkono matumizi ya teknolojia ya video kuendesha mikutano hiyo, Dk Mfumukeko alikaririwa akisema:

"Walau asilimia 25 ya mikutano yote itaendeshwa kwa njia ya video na iliyosalia itafanyika kwenye kumbi za bure za Serikali husika ili kupunguza gharama."

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa mfumo huo wa kuendesha majadiliano ya jumuiya hiyo mwaka jana, zaidi ya Sh8 bilioni zimeokolewa kwenye gharama za mikutano takribani 800 inayofanywa na sekretarieti pamoja na taasisi zake kila mwaka ambayo ilikuwa inalipiwa zaidi ya Sh24 bilioni.

Jana jumuiya hiyo imetangaza bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha, ambayo imepungua kwa takribani asilimia 10. Pamoja na utekelezaji wa agizo la kufunga mkanda, mishahara ya watendaji waandamizi wa Sekretarieti haijaguswa.

Watendaji wa jumuiya hiyo hawajafanya kama kile ambacho Rais Magufuli ametangaza kukifanya nchini; kushusha mishahara ya wakurugenzi na maofisa waandamizi wanaolipwa fedha nyingi kila mwezi.

Miongoni mwa watumishi wanaolipwa mishahara mikubwa ndani ya EAC ni katibu mkuu na manaibu wake ambao hulipwa hadi zaidi ya Sh40 milioni wakifuatiwa na wabunge wanaochukua zaidi ya Sh30 milioni, zinazotokana na michango ya kodi za raia wa nchi wanachama.

Bajeti hiyo imepungua kutoka Dola 110.66 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh221 bilioni) mpaka 101.37 milioni (zaidi ya Sh202 bilioni), jambo linaloilazimu kuchukua hatua za makusudi kupanga matumizi muhimu na kuyapunguza yasiyo na tija.

"Jumuiya inakabiliwa na changamoto ya ukata kutokana na kucheleweshwa kwa fedha za michango kutoka kwa wanachama na misaada ya wafadhili," alisema katibu huyo mkuu.

Mabadiliko haya yanatokea wakati mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais Magufuli akiwa amechukua hatua kadhaa za kubana matumizi nchini kiasi cha kuigwa na mataifa mengine ya Afrika.

Siku chache baada ya kuzuia safari za viongozi wa Serikali nje ya nchi isipokuwa kwa kibali cha Ikulu, Rais wa Rwanda, Paul Kagame naye alifuata nyayo, huku akiwatuhumu mawaziri wake kutojali maslahi ya taifa.
Aliwatuhumu mawaziri wake wasiopungua watano kuwa wanasafiri mara tatu kwa wiki kushiriki mikutano ya EAC popote inapotokea na kwamba ziara hizo zinaigharimu Serikali yake fedha nyingi na kuahidi kwamba suala hilo litaachwa kwa waziri husika.

Hata Dk Magufuli alipochukua hatua dhidi ya wafanyakazi hewa, Rais wa Nigeria, Mohammed Buhari naye alifanya hivyo. Wakati Tanzania ikiwa imewabaini zaidi ya watumishi hewa 10,000, Buhari anao zaidi ya 40,000 waliokuwa wanalipwa na hazina ya taifa hilo kubwa kiuchumi Afrika.

Source: Mwananchi
 
Mbona Tanzania yenyewe 'haijatii' agizo la jumuiya la kulipa ada!? Au kitakachopatikana kwenye hii 'saving' ndio itakuwa ada.
 
Back
Top Bottom